WAAFRIKA TUNA MATATIZO MENGI,
TUSIPIGANE!
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, ambaye ndiye amiri jeshi mkuu wa taifa letu la Tanzania, ametoa tamko
kali kwamba atakayeichokoza Tanzania, tutamchapa. Inafurahisha kujua kwamba
jeshi letu liko imara. Hapana shaka kwamba tuna jeshi zuri la kizalendo na
Jeshi letu ni Jeshi la Wananchi. Pamoja na pongezi hizi kwa Rais wetu na jeshi
letu, ni lazima tuwe wazi kabisa kwamba vita si kitu kizuri. Vita ni kumwaga
damu, vita ni kupoteza maisha, vita ni kuzalisha wakimbizi na mahangaiko ya
watu na hasa watoto na wanawake, vita ni kuvuruga uchumi. Na vita si mpango wa
Mungu! Kama kuna njia nyingine ya kumaliza tatizo, bila kuingia kwenye vita, ni
busara kuifuata njia hiyo.
La pili, ni je hawa
wanaotuchokoza, na tunataka kuwachapa ni watu gani? Ni Wachina, Wajapani, Wamarekani
au Waafrika wenzetu? Kama ni Waafrika, tuseme hapana: Waafrika tuna matatizo
mengi, tusipigane! Tunahitaji kuungana zaidi ya kupigana; hatuna chakula cha
kutosha, hatuna maji, hatuna makazi bora kwa kila mwananchi, tunakufa kwa
magonjwa yanayotibika kama malaria na mengine, watoto wengi bado wanakufa
wakiwa chini ya umri wa miaka mitano, hatuna elimu ya kutosha na matatizo
mengine mengi yanayotufanya kujuliana kama “Masikini” wa dunia hii au watu wa
dunia ya tatu. Tuna maadui wengi, na maadui wetu wanafanana, hivyo ni lazima
kuungana ili kupambana nao. Wale wanaotuchukia wanatukejeli kwamba Afrika
hatuna la kutufanya kuungana: tunaunganisha umasikini wetu? Tunaunganisha
ufisadi wetu? Tunaunganisha nini? Kama tumeshindwa kujenga utaifa,
tutaweza kujenga Afrika moja iliyoungana? Kama makabila bado yanatengana na
kubaguana ndani ya nchi mmoja, itawezekana kuunganisha bara zima la Afrika? Ingawa utaifa ni kitu kilichopandikizwa
vichwani mwetu na wakoloni, lakini sasa hivi ndiyo ukweli uliopo kwamba tuna
nchi za Afrika, zina mipaka na uhuru wake. Hata tukifanikiwa kuondoa mipaka hii
siku moja, swali ni je watu wa nchi hizi ni wamoja? Watu wa nchi hizi wana
mshikamano? Maana huwezi kuwa na mshikamano na wengine kama wewe huna
mshikamano nyumbani kwako. mbona hadi leo hii hakuna sauti moja ya Afrika?
Mbona Afrika inashindwa kutatua matatizo yake yenyewe?
Afrika inahitaji mshikamano
kupambana na utandawazi na matatizo mengine mengi. Tukumbuke utandawazi hauna
rangi. Afrika inahitaji mshikamano kupambana na Ubeberu unaosambaa kwa kasi na
kutishia uhai na ustawi wa Waafrika. Vita nyingi kwenye bara la Afrika inakuwa
na msukumo wa nje; inakuwa na msukumo wa wale wanaotaka tupigane ili watutawale
tena kwa njia za kisasa zenye kubeba maneno ya kinafiki “ dunia ni kijiji
kimoja”. Ubeberu hauna rangi. Tulizoea ubeberu wa Wazungu, lakini sasa hivi
kuna tishio la ubeberu wa Kichina na hata ubeberu wa Kiafrika; maana kuna nchi
za Afrika ambazo zinaanza kuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi na nyingine
zinatumiwa na nchi za magharibi kuzinyanyasa nchi changa za Afrika. Je sababu
zilizowasukuma wazee wetu kusimama na kupinga ukoloni bado zipo? Ni kiasi gani
Mwafrika amejikomboa kifikira baada ya Uhuru? Ni kiasi gani Mwafrika ametambua
kwamba mipaka ya nchi za Afrika iliwekwa na wakoloni?
Mshikamano wa Waafrika, ni
tofauti na muungano wa nchi za Afrika. Wakati muungano wa nchi za Afrika
unatengenezwa na viongozi, mshikamano unachipuka kwa njia nyingine tofauti;
Maana mshikamano unatengenezwa na watu wenyewe; vuguvugu hili linajenga
mazingira ya kwamba Mwafrika popote alipo akishikwa sote tumeshikwa. Mshikamano
unaweza kuzaa muungano imara kuliko muungano unaoshinikizwa na viongozi wa
Afrika.
Mfano, mshikamano wa
Watanganyika na Wazanzibari; unaweza kuunda muungano wa nchi hizi mbili ulio
imara. Watu wakihusiana kwenye mambo ya kijamii ya kuoana, kufanya
biashara kwa pamoja, kutembeleana, kuabudu pamoja na kuibua uzalendo imara wa
nchi hizi mbili, swala la muungano linakuja lenyewe. Leo hii watu wameanza
kuhoji Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, maana kuna ushahidi kwamba muungano
huu ulizaliwa au ulitengenezwa na urafiki wa watu wawili; inawezekana pia
kwamba watu hawa walisukumwa na hekima, busara na mapenzi ya nchi zao, lakini
ukweli unabaki pale pale, kwamba Marehemu Mwalimu Nyerere na Marehemu Abed
Karume, hawakuwashirikisha wananchi juu ya swala la muungano.
Na kuziunganisha nchi za Afrika
ni wazo ambalo mpaka sasa limekuwa likishughulikiwa na viongozi wa Afrika bila
ya kuwashirikisha wananchi wa Afrika. Kwa kifupi ni kwamba umoja wa nchi uhuru
za Afrika ni umoja wa viongozi wa nchi za Afrika. Viongozi wanafanya mikutano
na kutafuta namna ya kuunganisha nchi zao. Lakini hatujasikia viongozi hawa
wakitafuta maoni ya wananchi juu ya kuziunganisha nchi hizi za Afrika. Muungano
wa Tanganyika na Zanzibar ni mfano mzuri wa umoja wa nchi za Afrika. Vingozi wa
nchi hizi mbili walikutana na kukubaliana juu ya muungano wa nchi zao mbili
bila kuuliza maoni ya watu. Historia imetufundisha kwamba muungano huu
umeendelea kuwa na matatizo hadi leo hii. Ni wazi waanzilishi wa muungano
walikuwa na nia njema kwa watu wao. Lakini leo hii mambo yamegeuka; huwezi kumwakilisha
mtu bila kusikia matakwa yake.
La kujifunza hapa ni kwamba tunahitaji sauti moja ya
Afrika. Na sauti moja hii haiwezi kujengwa na viongozi wa nchi hizi za Afrika.
Sauti moja ya Afrika italetwa na wananchi wa Afrika. Mshikamano wa Waafrika, ndio
chombo pekee cha kuleta sauti moja na kusukuma kasi ya maendeleo ya nchi
za Afrika. Marais wetu wakitupiana maneno, haina maana kwamba wananchi wa nchi
hizo wana magomvi miongoni mwao. Marais wetu wakichukiana, haina maana kwamba
nyuma yao kuna wananchi wanaochukiana pia.
Kuna watu wana utata juu ya
Umajumui (Pan Africanism) na Umoja wa Afrika, ingawa maneno haya yanafanana, yana maana
mbili tofauti. Umajumui unamaanisha zaidi Mshikamano wa Waafrika; au Mshikamano
wa watu weusi popote walipo duniani. Na Umoja wa Afrika unamaanisha zaidi
kuunganisha nchi zote za Afrika. Na kuna ndoto kwamba siku moja Afrika itakuwa
na rais mmoja na kuwa na fedha moja ya Afrika.
La msingi, na lenye maana kubwa
kwetu ni mshikamano wa Waafrika. Hili likifanikiwa, hatuwezi kuwa na vita katika Bara letu la Afrika. Mara
nyingi wanaoleta vita, si wananchi bali ni viongozi. Ni wakati wa kusimama
kidete na kuwaambia viongozi wetu kwamba hatutaki vita. Kama kuna matatizo, ni
muhimu kukaa kwenye meza ya majadiliano. La muhimu ni ushirikishwaji. Viongozi
wasijadili peke yao na kugombana hadi kufikia hatua ya “Kutishiana” kwa
kupigana, bali viongozi wetu watushirikishe mabishano ili na sisi tuchangie na
mjadala wetu uanze na hitimisho kwamba tutajadiliana, tutatofautiana,
tutachukiana hata kwa sura, lakini hatutoani uhai!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122.
2 comments:
I do not know whether it's just me or if everyone else experiencing issues with your blog. It appears as though some of the text on your content are running off the screen. Can someone else please comment and let me know if this is happening to them too? This may be a issue with my web browser because I've had this happen previously. Many thanks itunes login
The TD Mortgage Payment Calculator may help you better understand what your repayments may look like once you borrow to get a home. mortgage payment calculator You accept to use Third Party Content only at your own risk. canadian mortgage calculator
Post a Comment