UHAKIKI WA KITABU: UTHIBITI WA HUDUMA ZA KIUCHUMI TANZANIA
1.
Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu
kinachohahikiwa hapa ni UTHIBITI WA HUDUMA ZA KIUCHUMI TANZANIA , Kimeandikwa
na Profesa Mark Mwandosya. Mchapishaji
wa kitabu hiki ni E&D Vision Publishin Limited na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani
(ISBN): - 978-9987-735-09-9 Kitabu kina kurasa 151 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii
ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Udhibiti ni njia
mojawapo inayotumika kusimamia uchumi wa nchi na kuendeleza ustawi wa jamii.
Udhibiti wa huduma za kiuchumi (Public utilities) unahusu kuweka mizania kati
ya kuwawezesha watoa huduma na kuwalinda watumiaji wa huduma kama vile maji,
umeme, uchukuzi na mawasiliano. Suala Udhibiti wa huduma za uchumi lilijitokeza
kwanza miaka zaidi ya 150 iliyopita, huko Marekani na Ulaya kwa madhumuni
makubwa ya kumlinda mlaji katika mazingira ya uchumi wa soko huria.
Kitabu hiki kinaelezea
chimbuko la udhibiti Tanzania katika muktadha wa mabadiliko ya uchumi duniani
pamoja na udhibiti katika nchi nyingine. Ni kitabu chenye maarifa ya msingi kwa
kila mtuamiaji wa huduma za kiuchumi, pamoja na wanafunzi, wasomi, wafanyakazi
na viongozi. Lakini pia ni kitabu kinachomsaidia mwananchi kuelewa udhibiti na
kufahamu jinsi mfumo huu unavyolenga kumtetea katika mfumo wa soko huria.
Kitabu hiki kina sura 15
ambazo zinaongelea: Sura ya kwanza ni Utangulizi, sura ya pili ni Dhana ya
Udhibiti, ambayo inajadili malengo ya udhibiti, huduma za kiuchumi, mazingira
sawa ya ushindani, uhuru wa Mdhibiti, Uteuzi wa Bodi na Ofisa Mtendaji Mkuu,
Uhai wa bodi, nidhamu ya usimamizi wake. Sura ya tatu ni juu ya Maeneo Muhimu ya Udhibiti,
ambayo inajadili kwa undani juu ya Leseni, Kudhibiti Mwenendo wa Bei na tozo Mbali mbali, mwongozo wa maadili. Sura ya
nne ni juu ya Uwezo wa kifedha wa Mdhibiti. Sura ya tano ni juu ya kuwalinda
watumiaji wa huduma na bidhaa. Sura ya sita ni juu ya Muundo wa vyombo vya
Udhibiti. Sura ya saba inajadili Udhibiti wa sekta za Kiufundi na kufafanua
zaidi juu ya Mifano ya dhibiti wa Masuala ya kiufundi, usimamizi wa Masafa ya
Redio, Muunganisho wa mawasiliano na namba za simu kama rasilimali muhimu. Sura
ya nane inajadili juu ya Uhusiano Kati ya serikali na mthibiti. Sura ya tisa inajadili
juu ya Udhibiti na ushindani wa Biashara; Utaratibu wa kumlinda mlaji na mtoa
huduma, Uhusiano wa udhibiti na huduma na wa biashara. Sura ya kumi inajadili
juu ya Sheria za Kisekta. Sura ya kumi na moja inajadili juu ya Uhusiano kati
ya Bunge na Mdhibiti. Sura ya kumi na mbili ni juu ya Udhibiti katika nchi
nyingine. Sura ya kumi na tatu inaongelea Masuala Mtambuka. Sura ya kumi na nne
inajadili Mafanikio na changamoto za udhibiti; Kusimamia utekelezaji wa sheria,
utoaji wa Leseni, sekta ya mawasiliano, sekta ya maji, sekta ya umeme, sekta ya
uchukuzi, sekta ya mafuta ya petroli na watumiaji wa hudumaza kiuchumi. Sura ya
mwisho ya kumi na tano ni hitimisho na kitabu kinafunga na orodha ya marejeo.
Mwandishi wa kitabu
hiki, Mark Mwandosya, amewahi kuwa Profesa wa Uhandisi wa Umeme Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Kamishana wa Nishati na Masuala ya Petroli, Katibu Mkuu Wizara
ya Maji, Nishati na Madini, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri
wa Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Nchi (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa
Rais, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, na waziri wa Maji. Kwa sasa yeye ni waziri
wa Nchi(Kazi Maalum), Ofisi ya Rais.
Katika aya zifuatazo nitafanya
uhakiki wa kitabu hiki, lakini kwanza kwa kudokeza mazingira yanayokizunguka
kitabu hiki.
III. Mazingira
yanayokizunguka kitabu
Kitabu hiki kimeandikwa
na msomi tena profesa. Tumekuwa tukiwalalamikia wasomi wetu kukaa kimya na
kushindwa kulielekeza taifa letu la Tanzania. Sasa mwandishi wa kitabu hiki
amekata mzizi wa fitina. Ameandika, labda sisi tushindwe kusoma. Tumekuwa tukiwalalamika
wasomi wanaojitahidi kuandika, lakini wanafanya hivyo kwa lugha za kigeni.
Mwandishi wa kitabu hiki amekata mzizi wa fitini kwa kuandika kitabu kwa lugha ya Kiswahili.
Tumekuwa tukiwalalamika wanasiasa wetu kuhubiri majukwaani na kushindwa kutuandikia
vitabu kama kumbukumbu za leo, kesho, keshokutwa na vizazi vijavyo, mwandishi
wa kitabu hiki amekata mzizi wa fitini, atakuwa ni miongoni mwa wanasiasa
wachache wa Tanzania wanaoandika vitabu. Tumekuwa tukiwalalamikia wanasiasa
kuchanganya siasa na kila kitu hata kuiingilia taaluma nyingine za kisomi,
mwandishi huyu amekata mzizi wa fitina, pamoja na kwamba anaongelea huduma za
kijamii, huduma za kiuchumi, kitabu chake kutoka sentensi ya kwanza hadi ya
mwisho hakuna neno CCM. Ingawa mwandishi ni kada, lakini amevuka ufinyo huo na
kuwa juu katika uwanja wa wanazuoni. Anaandika kwa watanzania wote bila kujali
siasa, dini wala kabila. Ni kitabu cha aina yake!
Udhibiti ni kitu kipya,
na kusema kweli ni msamiati ambao ni mgumu kueleweka kwa watu wengi ingawa tunashiriki mfumo huu siku kwa
siku. Kitabu hiki, au niseme mwandishi wa kitabu amefanya kazi ya peke kuelezea
maana ya udhibiti. Na sikuelezea tu, bali huyu ni mmoja wa watanzania
walioshiriki kiazi kikubwa uanzishwaji wa udhibiti katika taifa letu.
Tumekuwa tukisikia EWURA
– Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, TCRA – Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano, TCAA – Mamlaka ya udhibiti wa
Usafiri wa Anga, SUMATRA – Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Maji.
Lakini ni kiasi gani tumekuwa tukielewa misamiati hii? Ni kiasi gani wananchi
wamefahamu vyombo hivi vya udhibiti na jinsi wao wanavyoweza kushiriki na kutoa
maoni kwenye uendeshaji wa vyombo hivi? Mwandishi amejaribu kwa kiasi kikubwa
na lugha nyepesi kuelezea maana ya udhibiti na chimbuko lake; kipindi cha
mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi wa Tanzania kutoka mfumo wa uchumi hodhi
hadi mfumo wa uchumi wa soko. Katika uchumi hodhi, Serikali ilishikilia na
kusimamia mihimili yote ya uchumi, kuanzia mitaji, njia za uzalishaji, upangaji
wa bei na uendeshaji wa masoko kupitia mauzo ya jumla na maduka ya rejareja. Katika mfumo huo, serikali kupitia
idara zake, mashirika na kampuni zake, ilikuwa ndiye mwajiri mkubwa katika
uwanja wa ajira rasmi. Kipindi hiki ni na zama hiyo ni ile ya kabla ya mwaka
1985.
“ Kipindi cha mwaka 1985
hadi 2005 ni kipindi cha miaka 20
ambacho kimehusisha Awamu ya Pili ya uongozi wa nchi kutoka mwaka 1985 hadi 1995; na Awamu ya Tatu, mwaka 1995 2005
iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Benjamin William Mkapa. Kipindi hiki cha
miaka 20 ni kipindi ambacho kinaweza kikausishwa na zama ya mageuzi ya mfumo wa
uchumi wa nchi kutoka mfumo hodhi na kuanzisha misingi na utekelezaji wa mfumo
wa soko. Katika mifumo yote miwili, kumekuwa na udhibiti na usimamizi wa huduma
za kiuchumi na miundombinu. Katika mfumo hodhi, udhibiti na usimamizi huo
ulifanywa moja kwa moja na Serikali kupitia wizara na idara zake wakati mfumo
wa soko umehitaji uanzishaji wa vyombo huru vilivyo nje ya mfumo rasmi wa
wizara na idara za serikali. Kwa urahisi
wa uelewa, angalau kwa nadharia tu, fumo wa vyombo huru vya usimamizi wa huduma
za kiuchumi na miundombinu unafana na uhuru, udhibiti na usimamizi unaofanywa
na Benki Kuu katika sekta ya fedha nchini kupitia sera ya fedha” (Uk xv na
xvi).
Mwandishi wa kitabu hiki
hafanyi kazi ya kubahatisha, maana mwaka 1985 aliteuliwa na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa kamishna wa kwanza wa Nishati na Petroli
na hivyo kuanzisha kwa mara ya kwanza idara kamili ya huduma ya kiuchumi, Idara
ya Nishati. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya lililokuwa
Shirika la Posta na Simu Tanzania na mjumbe wa Bodi ya TANESCO, kwa nafasi hizo
aliweza kuwa na uzoefu na uelewa wa huduma tatu za kiuchumi, mawasiliano ya
posta, simu na nishati.
Mwaka 1992, mwandishi wa
kitabu hiki alihamishiwa Wizara ya
Viwanda na Biashara kama katibu mkuu, akapata nafasi ya kuhusiana moja
kwa moja na mageuzi ya kiuchumi kwa kuanzisha mfumo wa na taratibu za awali za
ubinafsishaji wa viwanda. Pia alikuwa mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya
shirika la Petroli Tanzania (TPDC) na kupata nafasi ya kusimamia huduma muhimu
ya kiuchumi.
Mwandishi wa kitabu hiki
kati ya mwaka 2000 na 2005, alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na kupata
fursa ya kipekee ya kusimamia maandalizi ya kupitisha Bungeni sheria
zilizoanzisha mamlaka tatu za udhibiti;
Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano(TCRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Anga (TCAA), Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Na mwaka 2008, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, alimteua mwandishi wa kitabu hiki
kuwa waziri wa Maji na Umwagiliaji. Waziri mwenye dhamana ya sekta ya maji kwa
sasa ndiye Waziri anayesimamia Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati ya Maji
(EWURA). Hivyo mwandishi anajua vizuri mada hii hivyo atatufumbua macho.
IV. Muhtasari wa
Kitabu
Kitabu hiki kinajadili
na kufafanua kwa kina juu ya suala la udhibiti wa huduma za uchumi; kwamba
suala hili la udhibiti lilijitokeza
kwanza miaka zaidi ya 150 iliyopita, huko Marekani na Ulaya kwa madhumuni
makubwa ya kumlinda mlaji katika mazingira ya uchumi wa soko huria. Pia kwamba
mfumo wa sasa wa udhibiti nchini Tanzania ulianza kipindi cha muongo mmoja
uliopita ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya mfumo wa uchumi, kutoka uchumi hodhi
kwenda uchumi wa mseto, mfumo ulioutambua umuhimu wa soko huru na sekta binafsi
katika kuchochea kukua kwa uchumi. Taratibu za kuanzisha mfumo wa sasa wa
udhibiti zilienda sambamba na zoezi la ubinafsishaji. Na kwamba mfumo wa sasa
wa udhibiti unafanana na mifumo katika nchi nyingi, na kwa kiwango kikubwa,
umefuata misingi mizuri ya kimataifa. Misingi hiyo imefafanuliwa katika kitabu
hiki. Mwandishi wa kitabu hiki anaweka wazi kwamba: “ Ni jambo la kujivunia
kwamba nchi nyingi hasa za Afrika kusini mwa Sahara zimekuja Tanzania kujifunza
jinsi ya kudhibiti huduma za nishati, maji na mawasiliano” (Uk 132).
Sura ya kwanza ya kitabu
hiki ni Utangulizi. Hapa mwandishi anafafanua kwamba udhibiti kwa maudhui ya
kitabu chake unahusu huduma za kiuchumi, na kwamba mfumo wa sasa wa udhibiti wa
sekta za uchumi Tanzania unatokana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka
uchumi hodhi kwenda kwenye uchumi wa kati au uchumi mchanganyiko.
Hapa ndipo mwandishi
anatuelezea na kufafanua juu ya Uchumi wa soko (Market economy): Kwamba “ huu
ni mfumo wa uchumi ambao maamuzi kuhusu uwekezaji, uzalishaji na ugawaji wa
bidhaa na huduma hutegemea upatikanaji wake na mahitaji... katika mfumo huu wa
uchumi, bei za bidhaa na huduma hupangwa na soko lililo huru..” (uk 1);
Pia juu ya Uchumi hodhi
au uchumi wa mipango (planned economy), kwamba “Mfumo huu wa uchumi unatoa
maamuzi yanayohusu uwekezaji, uzalishaji na ugawaji wa rasilimali, huduma na
bidhaa yanatokana na mpango wa Serikali. Kwenye mfumo wa aina hii, mipango ya
uzalishaji na utekelezaji wake inatakiwa kuzingatia mahitaji ya jamii na
watumiaji wa huduma...”( Uk 1-2);
Na juu ya Uchumi mseto (
mixed economy), kwamba huu ni mfumo ambao “ Serikali na sekta binafsi
hushirikiana katika kuendesha uchumi. Katika uchumi wa aina hii, uwekezaji
unaachiwa sekta binafsi wakati Serikali inauwa na wajibu wa kuweka mazingira
mazuri ya uwekezaji...” (Uk 2). Katika mfumo huu wa uchumi Serikali hutumia
vyombo vya udhibiti katika kusimamia uchumi. Mwandishi anatufahamisha kwamba
nchi nyingi duniani zina uchumi wa mfumo huu. Na Tanzania ni miongoni mwa nchi
hizo zinazofuata mfumo wa aina hii. Na kudokeza kwamba.. “... inabidi soko huria lisimamiwe na
lidhibitiwe ili kumlinda mlaji au mtumiaji wa huduma na kumhamasisha mto huduma
aongeze tija na kuleta faid katika
uchumi kwa ujumla...” (uk 3).
Baada ya ufafanuzi huo,
mwandishi anajadili juu ya Udhibiti kabla ya Sera ya ushindani na kipindi cha
mpito. Linalo elezwa hapa na mwandishi ni kwamba hata kabla ya mabadiliko au
mageuzi ya kiuchumi yaliyoletwa na kuanzishwa kwa soko huru na serikali kujitoa
katika kufanya biashara, kwa kiwango
kikubwa, usimamizi na udhibiti ulifanywa na wizara husika na idara za Serikali.
Waziri muhusika na sekta ndye aliyekuwa na mamlaka ya mwisho katika usimamizi
wa sekta husika , akisaidiwa na Mkurugenzi
wa Idara, Kamishna mhusika na Katibu mkuu wa wizara.
“ Hata hivyo, katika
sekta za kiufundi na miundombinu, kama vile uchukuzi na mawasiliano, vilikuwepo
vyombo ambavyo vilianzishwa kisheria kusimamia baadhi ya maeneo yaliyohitaji
udhibiti wa kiufundi. Kwa mfano, kabla ya mageuzi ya uchumi, sehemu kubwa ya
sekta ya mawasiliano ya simu na posta ilidhibitiwa na Shirika la Posta na Simu
la Tanzania (TPTC)...”
“ Kwa upande wa
uchukuzi, udhibiti, pamoja na kusimamiwa
na wizara yenye dhamana ya uchukuzi, kiutendaji ulikuwa chini ya vyombo
vilivyoanzishwa chini ya wizara mbali mbali...” (Uk 7).
“ Jeshi la Polisi nalo
lilikuwa ni Mdhibiti kwa minajili ya Sheria ya Usalama wa Barabarani, kupitia
Kikosi cha Usalama Barabarani. Wizara yenye dhamana na uchukuzi nayo ilikuwa na
Kitengo cha Usalama Barabarani (Road Safety Unit). Wakala wa Barabara, kupitia
sehemu ya mizani, nao ni sehemu ya udhibiti pamoja na kwamba lengo lao kuu ni
kutunza barabara na kurefusha uhai wa barabara...” (Uk 8).
Mwandishi anaendelea
kutuelimisha juu ya kipindi hiki cha udhibiti kabla ya sera ya ushindani kwamba
“... nyenzo muhimu ya udhibiti kabla ya mfumo wa sasa ilikuwa ni marekebisho ya
bei... Kwa eneo la bidhaa, kiliundwa chombo kilichofahamika sana, Tume ya Bei.
Tume ya bei ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya udhibiti wa Bei ya mwaka 1973” (Uk8).
Tukiwa bado kwenye sura
ya kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa ni utangulizi, mwandishi anaelezea juu ya
udhibiti wa Huduma za Maji Dar es salaam, Kipindi cha mpito. Kwamba “ Wazo la
kuwa na mdhibiti kwa ajili ya kusimamia sekta ya maji lilijitokeza wakati wa
zoezi la kubinafsisha shughuli za Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Dar-es-Salaam
- DAWASA au kuwe na udhibiti kupitia mkataba wa ubinafsishaji. Hatimaye,
ilikubalika kwamba awepo mdhibiti maalum” (Uk 11).
Pia katika sura hii
mwandishi anafafanua juu ya udhibiti wa Kimataifa. Kwamba kwa vile Tanzania ni
sehemu ndogo ya ulimwengu, katika masuala ya kimataifa, inaongozwa na
makubaliano ambayo kwa kiwango kikubwa yanasimamiwa na Umoja wa Mataifa na
mashirika yake. Anaelezea chanzo cha kuanzishwa Umoja wa mataifa na sheria
zinazoongoza mashirika ya umoja wa mataifa na kwamba mikataba yote ambayo
Tanzania inaingia na umoja wa mataifa ni lazima ipate nguvu za kisheria.
“ Katika maeneo ya
matumizi ya rasilimali za pamoja, makubaliano ya kimataifa yamewezesha
kuanzishwa kwa vyombo au mashirika ya usimamizi na udhibiti wa kimataifa.
Mashirika haya yamewezesha pia kuwekwa kwa sheria za kimataifa, taratibu na
kanuni za usimamizi na udhibiti wa kijumla” (Uk 15). Taasisi au vyombo hivyo
vinavyojadiliwa hapa ni pamoja na Shirika la Simu Duniani, Shirika la posta
duniani, Shirika la Kimataifa la Usalama wa usafiri wa Anga na Shirika la
Kimataifa la Usafiri Majini. Aidha, kuna mashirika ya kimataifa yasiyo chini ya
Umoja wa Mataifa moja kwa moja lakini yanadhibiti maeneo muhimu kama viwango
vya kimataifa vinavyoshughulikiwa na Shirika la Viwango Duniani.
Sura ya pili ya kitabu
hiki, mwandishi anafafanua juu ya dhana ya udhibiti. Hapa ndipo anapotuelezea
malengo ya udhibiti, huduma za kiuchumi, mazingira sawa ya ushindani, uhuru wa mdhibiti, uteuzi wa
bodi na ofisa mtendaji mkuu, uhai wa bodi, nidhamu na usimamizi wake.
“ Kwa maoni ya
mwandishi, madhumuni muhimu ya udhibiti ni kukuza uchumi wa nchi, ingawa
madhumuni haya hayajitokezi waziwazi katika kazi za udhibiti za kila siku. Bila
udhibiti wenye ufanisi, uwekezaji utalegalega na uchumi hautaweza kukua
haraka...” (Uk 17)
“Maneno ‘Huduma za
Kiuchumi’(Public Utilities) yanatumika katika kitabu hiki kumaanisha huduma
ambazo hutolewa kupitia miundombinu ambayo inakuwepo wakati wote na ambayo
inamwezesha mtumiaji wa huduma kuipata huduma hivyo wakati inapohitajika.
Huduma hizi ni kama vile umeme, mafuta ya petroli, gesi asilia, maji, uondoaji
maji taka , mawasiliano ya posta na mawasiliano ya kielektroniki kama vile
simu, intaneti, radio na televisheni.
Kwa maana hiyo pana ya huduma za kiuchumi, huduma hizo ni pamoja huduma za
uchukuzi, kama vile uchukuzi wa anga, ardhini (reli, mabasi, malori) na
uchukuzi wa majini” (Uk 18).
La kujifunza hapa ni
kwamba huduma za kiuchumi huangaliwa kwa karibu na Serikali zote duniani.
Kazi kubwa ya mthibiti
ni kuweka mazingira sawa ya ushindani ( Uwanja sawa wa ushindani) “...Kwani
inatarajiwa kwamba soko litajirekebisha lenyewe na huduma na bidhaa kuendelea
kutolewa ipasavyo. Lakini soko la namna hiyo ni ndoto tu ambayo kama ilivyo
njozi nzuri, tungependa itimie. Kwa kawaida haiwezekani. Ndipo unapokuja
umuhimu wa mdhibiti. Na moja ya majukumu yake muhimu sana ni kuweka mazingira
sawa ya ushindani, kwa lugha nyingine kuweka uwanja wa ushindani ulio sawa
(level playing field)” ( Uk 19).
Ili mdhibiti aweze
kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kusimamia ushindani kwa ufanisi na
kutenda haki ni lazima awe huru. Uhuru unamwezesha kupima katika mizania haki
za mtumiaji wa huduma au bidhaa, haki za mtoa huruma au mzalishaji na muuzaji
wa bidhaa, gharama za kutoa huduma, gharama za kuzalisha bidhaa na kuzisambaza,
kudhibiti mwenendo wa bei ya huduma hizo au bidhaa hizo kwa mtumiaji na
kuhakikisha sera za nchi zinafuatwa na sheria na taratibu zinatekelezwa.
Mwandishi anafafanua vizuri zaidi juu ya uhuru huu wa mdhibiti katika kitabu
chake. Kwa kukisoma, mtu ataelewa vizuri juu ya uhuru wa mdhibiti na kwamba: “
Katika kurekebisha hali hii ya kumpa Mdhibiti uhuru wa kutosha wa kutenda kazi
kwa misingi ya haki bila woga, sheria zote zinazoanzisha mamlaka za udhibiti
zinampa Waziri uwezo wa kusimamia mamlaka hizi kisera na kiutawala tu na sio
katika masuala yaliomo ndani ya himaya ya Mdhibiti...” ( Uk 21).
Dhana muhimu ya uhuru wa
Mdhibiti inadhihirika pale ambapo muhula wa kazi wa bodi unalindwa kisheria na
taratibu za uteuzi wa bodi na ofisa mtendaji mkuu zinatambuliwa kisheria. “Sheria zote zinazoanzisha vyombo vya
udhibiti Tanzania zinaunda Kamati ya Uteuzi (Nominations Committee). Kamati hii
si kamati ya kudumu. Inakutana pale tu inapohitajika kupendekeza majina ya
uteuzi wa mjumbe au wajumbe wa bodi pamoja na ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya
udhibiti... Kamati huwa chini ya uenyekiti wa katibu mkuu wa wizara ya kisekta
inayomsimamia Mdhibiti. Sheria pia zinafafanua sifa na aina ya wajumbe wa
kamati ya uteuzi, ikisisitizwa kuwepo kwa mwakilishi wa sekta binafsi..” (Uk
23).
Katika sehemu hii,
mwandishi ameelezea vizuri uhuru wa mdhibiti na sheria zinazompatia uhuru huo
na kuulinda. Pia, hapa anatuelezea Uhai wa Bodi, mfano kwamba “ ... kwa mujibu
wa sheria ya TCRA, sheria Na.12 ya 2003, Mwenyekiti wa bodi anateuliwa kwa
muhula wa miaka (4),Makamu wa Mwenyekiti muhula wake ni miaka mitatu na wajumbe
wengine wawili kipindi chao ni miaka mitano” (Uk 26).
“Kwa mamlaka zote,
mjumbe wa bodi akimaliza muhula wake anaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi
kingine kimoja. Hawezi akazidisha mihula miwili. Vilevile, katika mamlaka zote,
mkurugenzi mkuu ambaye ndiye ofisa mtendaji mkuu, ni mjumbe wa bodi kwa wadhifa
wake...” (26). Katika sehemu hii mwandishi anaelezea vizuri uzoefu uliopo, mfumo ulivyo juu ya
uhai wa bodi. Hivyo mtu akijisomea mwenyewe kitabu hiki atapata ujuzi na uelewa
mpana juu ya suala zima la udhibiti, uteuzi wa bodi na uhai wa bodi hizi.
Sura ya tatu ya kitabu
hiki inajadili juu ya Maeneo Muhimu ya udhibiti, Leseni, Kudhibiti
Mwenendo wa Bei na Tozo Mbalimbali na mwongozo wa maadili. “ Sheria
zilizoanzisha mamlaka za udhibiti Tanzania zimeainisha maeneo muhimu matatu
ambayo mamlaka zinatakiwa kisheria, kufanya uchunguzi wa kina, wa wazi, na
unaohusisha wadau na wananchi kwa ujumla (taftishi) . Maeneo hayo yanahusu:
Kutoa leseni, kuongeza muda wa leseni au kufuta leseni ambazo mdhibiti ana
uwezo wa kufanya hivyo; Kudhibiti mwenendo wa bei ya bidhaa na /au huduma
zinazotolewa katika sekta inayodhibitiwa; na kupitishwa kwa kanuni za maadili
(code of conduct)” (Uk 33). Hayo yote yaliyotajwa hapo juu yanajadiliwa kwa
ufasaha mkubwa katika kitabu hiki.
Sura ya nne ya kitabu
hiki inajadili Uwezo wa kifedha wa Mdhibiti: “Kutokana na yaliyoelezwa mpaka
sasa, ni dhahiri mdhibiti ana madaraka na mamlaka makubwa, na hali kadhalika
ana dhamana kubwa aliyopewa na Taifa kupitia sheria za kisekta na sheria
zinazoanzisha vyombo vya udhibiti. Ana uhuru mkubwa katika masuala na maamuzi
yanayohusu udhibiti. Mamlaka, madaraka, dhamana na uhuru huo unaweza
kudhihirika pale tu ambapo mdhibiti ana uwezo wa kujiendesha; na pale
upatikanaji wa rasilimali fedha na rasilimali watu unatabirika ili aweze
kuendesha shughuli zake. Vinginevyo atakwazwa katika utekelezaji shughuli
zake...” (Uk 39).
Katika sehemu hii
mwandishi anaelezea jinsi mdhibiti anavyopata fedha za kujiendesha na ni
kutokana na:
- Ada zinazolipwa kwa
mdhibiti ikiwa ni pamoja na ada za kudurusu au kutoa leseni;
- Tozo mbalimbali kutoka
kwa wazalishaji na/au watoa huduma; na
- Misaada ya aina
mbalimbali au michango inayoweza kutolewa kwa Mdhibiti.
Mfano: “ Mapato ya EWURA
kwa kiwango kikubwa yanatokana na tozo ya udhibiti (regulatory levy) ambayo
wadhibitiwa (regulated entities) wanatozwa kiwango kisichozidi asilimia moja
(1%) ya mapato ghafi, katika sekta za umeme, petroli, gesi asilia, maji na
uondoaji majitaka.” (45).
Mwandishi, anaelezea
mapato ya mdhibiti, matumizi na sheria zinazoongoza kukusanya na kutumia mapato
haya. Mtu akijisomea kitabu hiki ataelimishwa kwa kina juu ya jambo hili
la uwezo wa kifedha wa mdhibiti.
Sura ya tano inajadili juu ya kuwalinda watumiaji wa huduma bidhaa
zinazodhibitiwa... “Pamoja na haki za mlaji au mtumiaji wa bidhaa kuwekwa
bayana kisheria, baina ya wadau wote wa udhibiti, mlaji au mtumiaji ndiye asiye
na nguvu na anaweza akaonewa. Hii inatokana na ukweli kuwa mlaji kwa kawaida
hajajipanga kutetea maslahi yake kama ilivyo kwa watoa huduma na wazalishaji.
Jamii imelitambua hilo na kuanzisha mifumo mbalimbali ya kisheria kutambua
makundi au vikundi vya watumiaji. Katika nchi zilizoendelea, vikundi vya hiari
vya watumiaji wa huduma vina nguvu na ushawishi mkubwa. Hata katika nchi hizo
bado imewekwa mifumo rasmi ya kupokea na kushughulikia kwa haraka kero na
migogoro inayoweza kuadhiri utoaji wa huduma au inayotokana na haki kutotendeka
(Ombudsman)” (uk 49)
“Katika nchi
zinazoendelea, Tanzania ikiwa ni mfano, hakuna vyama vya hiari
vinavyounganisha watumiaji wa huduma au
bidhaa ambavyo vingeweza kutetea kundi hilo la jamii katika sekta
inayodhibitiwa. Baada ya mjadala mrefu uliohusu uanzishaji wa mamlaka za
udhibiti, ilionekana vema yakaanzishwa mabaraza ya ushauri ya watumiaji wa
huduma zinazodhibitiwa (Consumer Consultative Councils- CCC). Mabaraza haya ni
EWURA-CCC, SUMATRA-CCC, TCAA-CCC, na TCRA-CCC, Pia, chini ya Sheria ya Fair
Competition Act limeanzishwa Baraza la watumiaji linaloitwa National Advocacy
Council (NCAC)” (Uk 49)
Mwandishi anaendelea
kufafanua zaidi kuhusu kuwalinda watumiaji wa huduma na bidhaa zinazodhibitiwa.
Msomaji wa kitabu hiki atapa hayo yote na kupata majibu ya maswali mengi ambayo
watu wamekuwa wakijiuliza kuhusu dhana nzima ya udhibiti wa huduma za kiuchumi.
Sura ya sita, inajadili
muundo wa vyombo vya udhibiti. Hapa tunafahamishwa kwamba: “...mifumo ya vyombo
vya udhibiti ina mambo mengi yanayofanana. Hata hivyo, mfumo wa uchumi,
historia, ushirikiano wa kikanda, na ushirikiano wa kimataifa ni baadhi ya
vigezo vinavyotofautisha mfumo mmoja na mwingine” (Uk 54).
Hapa mwandishi anaelezea
mfumo unaotumika Tanzania. Faida na hasara zake. Na kulinganisha mfumo wetu wa
udhibiti na mifumo ya nchi nyingine. La kuzingatia hapa ni kwamba misingi ya
udhibiti inafanana na inakubalika kote duniani. Kwa mfano ukilinganisha mfumo
wa udhibiti wa Tanzania na Uingereza, tofauti
zake ni matokeo ya tofauti za mazingira ikiwa ni pamoja na historia ya
utawala, utamaduni, biashara, mazingira ya masoko, ushindani, na hali ya
uchumi.
Sura ya saba inahusu
Uthibiti wa Sekta za Kiufundi. Hapa ndipo tunafafanuliwa juu ya mifano ya
udhibiti wa Masuala ya Kiufundi, Usimamizi wa Masafa ya Redio, Muunganisho wa
Mawasiliano na Namba za simu kama Rasilimali Muhimu.
“Sekta ya mawasiliano
ina mifano mzuri inayohusu udhibiti wa masuala ya kiufundi. Ni sekta yeye
changamoto kubwa kwa wadhibiti. Kwani teknolojia katika sekta hii inabadilika
kwa kasi kubwa sana na kufanya
teknolojia ya miaka miwili au mitatu iliyopita kuwa ya kizamani” (Uk 62-63)
“Usimamizi wa masafa ya
redio unahusu kuhakikisha matumizi bora ya masafa, kupunguza mwingiliano wa
masafa kwa watumiaji mbalimbali, kuhakikisha kwamba hakuna anayetumia masafa ya
redio bila kuruhusiwa kisheria, na kwamba aliye na leseni ya kutumia masafa ya
redio anayatumia vizuri na kwa mujibu wa masharti yaliyo katika leseni...” (uk
63)
Mwandishi anaelekea kwa kirefu
juu ya muunganisho wa mawasiliano. Anaelezea jinsi muunganisho wa mawasiliano
unavyorahisisha mawasiliano ya kampuni mbali mbali za simu. Anatoa mfano
muunganisho wa mawasiliano baina ya TTCL, Vodacom, Tigo, Airtel, Zantel,
Sasatel na kampuni nyingine.
“Suala la muunganisho
linapohusu mawasiliano ya kimataifa linasimamiwa na Umoja wa Simu Duniani (ITU)
kama mdhibiti wa kimataifa wa mawasiliano. Usimamizi huo unahusu makubaliano
yavifaa, viwango vya huduma na miongozo kuhusu malipo” (65).
Pia katika sura hii ya
saba, mwandishi anaelezea juu ya namba ya simu kuwa rasilimali muhimu: “ Namba
ya simu huwezesha mteja kutambulika mahali ilipo
Kijiografia; kampuni
ambayo yeye ni mteja kujulikana; mteja kuunganishwa na mtumiaji mwingine wa
simu katika eneo lake na eneo la mbali na hata nje ya nchi. Namba ya simu kwa
mpangilio wake humwezesha mitambo kutambua chanzo cha simu na kuiwezesha
mitambo hiyo kuielekeza kwenye kituo au vituo vya mpito mpaka kumtambua na
kumfikia mlengwa” (Uk 67)
Kuhusu namba ya simu na
udhibiti, mwandishi anafafanua hivi: “ Namba za simu ni rasilimali ambayo iwepo
itahodhiwa na kampuni moja, itakuwa sirahisi kampuni hiyo kugawa rasilimali
hiyo kwa kampuni nyingine, na hivyo kuzuia ushindani na kuongeza gharama kwa m
teja wa simu. Kabla ya kufungua sekta ya mawasiliano ya simu na kuruhusu ushindani,
TTCL ilikuwa ndiyo pekee iliyopanga na kutoa namba za simu. Baada ya soko la
mawasiliano kuwa huru, jukumu la kupanga na kusimamia namba za simu limekuwa ni
jukumu halali la Mdhibiti wa mawasiliano ya simu” (Uk 68).
Mwandishi, kwenye sura
hii anaendelea kuelezea umuhimu wa namba ya simu, jinsi zinavyopangwa, namba za
kila nchi na namba ya kila mteja. Kusema kweli hapa anatupatia elimu ambayo
wengi wetu hatukuwa nayo.
Sura ya nane, mwandishi
anatuelezea uhusiano uliopo kati ya serikali na mdhibiti. “Changamoto kubwa inayomkabili
Mdhibiti yeyote hasa katika nchi zinazoendelea ni uhusiano wake na Serikali.
Katika mazingira ya kawaida, changamoto hii haipaswi kumpa shida Mdhibiti au
kuisumbua serikali. Kwanza, ili Mdhibiti awepo kisheria, ni Serikali ambayo
inamwanzisha. La, pili na la muhimu ni madhumuni ya kuanzishwa kwa Mdhibiti na
majukumu ambayo anapewa kisheria. Madhumuni makubwa ni kuhakikisha kwamba
maisha ya wananchi yanaboreshwa. Madhumuni haya ndiyo yanayoifanya Serikali
iwepo. Madhumuni haya hayawezi kuwa chanzo cha mgogoro kati ya serikali na
Mdhibiti...” (70)
Kwa maoni ya mwandishi
ni kwamba sheria zikifuatwa na kila mtu akajua mipaka yake, haiwezekani hata
kidogo pakatokea changamoto kati ya Mdhibiti na Serikali. Lakini: “ Katika nchi
kama Tanzania, mara nyingi hutokea kutokuelewana kati ya Serikali na mdhibiti
hususan pale ambapo mwekezaji, au mtoa huduma anapoona kwamba kwa kupitia
maamuzi yake mdhibiti, hataweza kuyapata yale anayoyataka na hasa katika
kipindi alichojiwekea. Anakuwa hapendi ushindani huru, na kwa hakika huyu si
mwekezaji mwenye tija...”
Mwandishi anatoa mifano
kuonyesha changamoto zinazojitokeza kati ya mdhibiti na serikali ya Tanzania: “
Mawasiliano na makubaliano kati ya
Wizara ya Nishati na Madini na Songas yalikuwa ni njia ya kujaribu
kukwepa udhibiti wa EWURA. Kama hii haitoshi, na kwa kuwa EWURA ilishikilia
msimamo wake wa kuhakikisha Songas haikiuki maagizo ya kiudhibiti, Kampuni ya
Songas ilifungua kesi kwenye Baraza la Ushindani (FCT). Katika tukio ambalo
halitarajiwi kwenye utawala bora, Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO
waliamua kuisaidia Songas katika kesi yake dhidi ya EWURA ingawaje EWURA kwa
wakati ule ilikuwa inatetea maslahi ya Taifa. Ikumbukwe pia kwamba waziri wa
Nishati na Madini ni waziri msimamizi wa sekta ya nishati kwa mujibu wa Sheria
ya EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania. TANESCO ilikwenda mbali zaidi na
kuomba kuunganisha katika kesi hiyo kama mlalamikaji, yaani ikiungana na Songa
dhidi ya EWURA katika shauri lililofunguliwa kwenye Baraza la Ushindani, ombi
hilo lilikataliwa. Hata hivyo, mwezi Desemba 2009, Songas iliondoa mashitaka
yake kabla hayajasikilizwa” (Uk 74)
Pamoja na mfumo mzuri
unaoeleweka kama huu wa udhibiti, bado kuna changamoto na mgongano. Labda ni
kwa vile mambo haya yalikuwa hayajafafanuliwa vizuri kama alivyofanya mwandishi
wa kitabu hiki. Kwa mfano, mwandishi anaelezea vizuri nafasi ya waziri na
katibu mkuu katika mfumo huu wa udhibiti na kuonyesha wazi kwamba kila mtu
akifuata wajibu wake vizuri katika mfumo huu ni vigumu kabisa kutokea mgongano.
Sura ya tisa mwandishi
anafafanua kwa kina juu ya udhibiti na ushindani wa biashara. Na hapa ndipo
tunatambua utaratibu wa kumlinda mlaji na mtoa huduma na uhusiano wa udhibiti
wa huduma na wa biashara.
Mwandishi anatoa
historia ya chanzo cha kumlinda mlaji na mwongozo wa ushindani. Mfano hapa
Tanzania “ Ili kusimamia, kukuza, na kulinda ushindani wa haki katika biashara,
na kuwalinda walaji dhidi ya mwenendo wa soko usio na haki, ilitungwa sheria ya
Ushindani wa Haki ya mwaka 2003 (Fair
Competition Act, 2003). Sheria hii imeanzisha vyombo viwili vya kutekeleza azma
ya Serikali ya kusimamia biashara ya haki vyombo hivi ni Tume ya ushindani
(FCC), na Baraza la Ushindani (FCT). FCC inashughulikia udhibiti wa mwenendo
unaokwaza au unaozuia ushindani wa kibiashara (anti-competitive conduct).” (Uk
84).
Sura ya kumi, mwandishi
anafafanua na kuelezea kwa kina juu ya sheria za kisekta, taratibu, maagizo na
miongozo ya kisheria.
Sura ya kumi na moja
inaelezea vizuri uhusiano kati ya Bunge na Mdhibiti: “ Kwa upande wa Bunge,
Mdhibiti anawajibika kwa njia moja iliyo dhahiri ambayo pamoja na uhuru alionao
hawezi kukwepa. Fedha anazokusanya na kuzitumia Mdhibiti ni fedha za umma. Kwa mantiki
hiyo, hesabu zake za mapato na matumizi hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Serikali (CAG). CAG anatakiwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu hizo
kwa Rais na baada ya hapo kupitia waziri mwenye dhamana ya fedha, ripoti hiyo huwasilishwa
Bungeni...”
Mwandishi anaendelea
kufafanua zaidi juu ya uhusiano uliopo kati ya mdhibiti na Bunge, hivyo kwa
kukisoma kitabu hiki, msomaji atajipatia elimu zaidi juu ya suala zima la udhibiti
wa huduma za kiuchumi Tanzania.
Sura ya kumi na mbili,
mwandishi anaelezea na kufafanua udhibiti katika nchi nyingine. Hapa
tunaelimishwa jinsi nchi nyingine zinavyofanya katika suala zima la udhibiti.
Changamoto na mafanikio katika nchi nyingine. Hii inatufumbua macho na kutambua
kwamba si Tanzania peke yake inatumia mfumo huu wa udhibiti wa huduma za
kiuchumi.
Sura ya kumi na tatu,
mwandishi anajadili masuala mtambuka, kama vile kupima ubora wa udhibiti,
udhibiti wa utawala bora, kupima ufanisi wa udhibiti na uthibiti wa sera za
kitaifa.
Sura ya kumi na nne,
mwandishi anaelezea juu ya mafanikio na changamoto za udhibiti katika kusimamia
utekelezaji wa sheria, utoaji wa Leseni, sekta ya mawasiliano, sekta ya maji,
sekta ya umeme, sekta ya uchukuzi, sekta ya mafuta ya petroli na watumiaji wa
huduma za kiuchumi.
Sura ya kumi na tano ni
hitimisho: “ Kwa kuhitimisha, inatarajiwa kwamba huko utendako udhibiti
hautahusika tu na fikra finyu ya udhibiti wa kiufundi. Tasnia ya udhibiti itapimwa,
pamoja na mambo mengine, kwa jinsi uwepo kwake kutakavyokuwa kumechochea kasi
ya kukua kwa uchumi wa nchi. Ili iweze kufanikisha jukumu hilo, lazima tasnia
ya udhibiti iwe wakala wa mabadiliko ya mtazamo katika jamii, mabadiliko yanayozingatia uaminifu, uwajibikaji, utawala
bora, utawala wa sheria, amani, usalama, haki za binadamu, demokrasia, na
wajibu wa kulinda kushirikisha jamii zisizojiweza katika maendeleo” ( Uk 140)
Sehemu ya mwisho ni
marejeo.
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kumpongeza Profesa
Mark Mwandosya kwa kazi hii nzuri sana
aliyoiandika. Kusema kweli kazi hii inafundisha na kufumbua macho. Tulikuwa
tukisikia EWURA, lakini hatukufahamu kwa undani hiki ni kitu gani. Wengine
walifahamu kidogo, lakini hawakuwa na uelewa mpana na elimu ya kutosha juu ya
chombo hiki. Sasa kwa kusoma kitabu hiki watafahamu zaidi. Tumekuwa tukisikia
SUMATRA, lakini hakuna aliyetambua maana yake, zaidi ya kuchukiwa na wenye
daladala na wasafiri. Kwa wengine SUMARA, ilikuwa ni kero na kuchukuliwa kwa
kusema kwamba hii ni miradi ya wakubwa. Kwa ufafanuzi uliotolewa kwenye kitabu
hiki, wale watakao soma kitabu hiki, wataelewa vizuri na hawezi hata siku moja
kuibeza na kuichukia tena SUMATRA.
Pili, nimpongeze
mwandishi wa kitabu hiki kutumia lugha ya Kiswahili kuandika kitabu hiki.
Imekuwa ni tabia ya wasomi wetu kuandika kwa lugha za kigeni na kuifanya elimu
kuwa ni faida wanayoipata wachache. Kwa
kuandika kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, watu wengi watakisoma na kuipata
elimu hii.
Tatu, ni kumshukuru kwa
kuandika. Wanasiasa wetu wanapenda kuhubiri na kupiga siasa za maneno bila
kuandika. Viongozi ambao wanapata uzoefu mkubwa kwa kutunga sera na sheria, na
baadaye kusimamia utekelezaji wa sera hizo na sheria hizo, hawafanyi kazi
kuandika ili uzoefu wao uwe na faida leo, kesho, keshokutwa na siku zijazo.
Profesa Mwadosya amefanya kazi hii kubwa kama anavyosema yeye mwenyewe: “
...wazo la kuandika kitabu hiki ni na chimbuko lake ni mazungumzo niliyoyafanya
na wenzangu wawili: Ndugu Haruna Masebu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti
wa Huduma za Nishati na Maji; na Profesa John Nkoma, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
ya Udhibiti wa Mawasiliano. Mazungumzo haya yalifanyika ofisini kwa Waziri wa
Maji na Umwagiliaji, Ubungo, Dar-es-Salaam, tarehe 7 Septemba 2009. Sote, kwa
nafasi zetu tofauti, tulikuwa tumehusika katika mijadala ya kisera, kuandaa miswada
ya sheria na kuanzisha mamlaka za udhibiti. Baada ya mjadala mrefu, tukakubaliana
kwamba njia pekee ya kuwa na mchango wa kudumu kwa Taifa, ni kwa kila mmoja
wetu katika nafasi yake kuweka katika maandishi, uelewa na uzoefu tulioupata,
tukiamini kwamba uelewa na uzoefu huo utakuwa wenye manufaa katika usimamizi wa
uchumi ,kwa zama hizi, na rejea muhimu kwa zama zinazokuja” ( xviii – xix)
Nne, ni kumshukuru
mwandishi jinsi alivyofafanua Udhibiti, historia yake, sera yake na sheria zake. Kusema ukweli, baada ya kukisoma
kitabu hiki mtu anakuwa na ufahamu mpana juu ya suala hili la udhibiti. Ni
vigumu kabisa baada ya kukisoma kitabu hiki mtu akapinga suala hili.
Tano, ni kumshukuru
mwandishi, ambaye ni mwanasiasa na kada wa chama tawala kukumbuka usomi wake,
na kuandika kitabu hiki “Kisomi” bila kutawaliwa na “upepo” wa siku hizi wa
kushabikia vyama vya siasa hata pale ambapo si nafasi yake. Mwandishi ameandika
kitabu hiki kwa watanzania wote bila kuangalia itikadi za siasa, maana ustawi
wa jamii na maendeleo ya watanzania ni ya wote na wala hakuna itikadi.
Ameandika kitabu chake, neno la kwanza hadi la mwisho bila kutaja CCM. Hii si
kawaida kwa kada wa chama kwa utamaduni
uliojengeka. Angeweza kusema kwamba udhibiti ni sera iliyoanzishwa na chama cha
mapinduzi. Angeweza kukitukaza chama chake kwa mafanikio hayo, kama tulivyozoea,
lakini Profesa Mwandosya, ameonyesha kuvuka mipaka ya “Uchama”; wakati huu
ambapo taifa letu linaelekea kuchanganyikiwa na kuingia kwenye mapambano ya
vyama vya siasa; tunawahitaji watu kama Profesa Mwandosya, ili waweze
kuturudisha kwenye njia sahihi.
VI. HITIMISHO.
Kama kawaida yangu,
ningependa kuwashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Wasiishie
kusoma uchambuzi huu kwenye gazeti. Huu ni uchambuzi mfupi na kitabu ni kikubwa
zaidi na kimesheheni mambo mengi ambayo nimeyagusia kidogo tu. Ni imani yangu
kwamba kwa kukisoma kitabu hiki watajifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki na
hasa juu ya ufafanuzi wa udhibiti na mambo mengine kama EWURA,SUMATRA na mengine kama hayo ambayo kwa kiasi kikubwa
yalikuwa ni msamiati kwa wananchi wengi.
Mwandishi ameonyesha
wazi kwamba Tanzania bado haina sera ya kumlinda mtumiaji wa huduma za kiuchumi.
Na kuonyesha wazi kwamba hakuna popote mtumiaji anaposhirikishwa katika
uanzishwaji wa vyombo hivi vya udhibiti kama vile EWURA na SUMATRA. Hivyo ni
muhimu hili kuzingatiwa ili itungwe sera ya kumlinda mtumiaji na ushirikishwaji
wa watumiaji katika mfumo mzima wa
udhibiti.
Dokezo la mwandishi
kwamba “ Katika hali ya kawaida vyombo
vya udhibiti vingeanzishwa kwanza kabla ya zoezi la ubinafsishaji. Ingekuwa
vema pia iwapo zoezi la ubinafsishaji lingekwenda sambamba na uanzishwaji wa
vyombo vya udhibiti...” (Uk 4) ni la kuzingatiwa, ingawa lilifanyika kinyume,
lakini jitihada zinaweza kufanyika, hasa kwa kuwaelimisha watu juu ya mfumo huu
wa udhibiti, kama mwandishi alivyofanya kwenye kitabu chake. Udhibiti usibaki
ni “fumbo” au chombo cha kunyanyasa pande zote mbili, watoa huduma na
watumiaji.
Pia, ni muhimu
kuzingatia maneno yanayotolewa na mwandishi kwenye kitabu chake kama vile : “
Mamlaka za Udhibiti huwajibika kwa maamuzi yake, lakini pasipo na changamoto
chanya baina ya serikali, Mamlaka za Udhibiti na watoa huduma, maendeleo
hayawezi kupaikana”(Uk 100). Na “ Pamoja na uhuru wa Mdhibiti, ili aweze
kufanikiwa ni muhimu Mdhibiti akayaelewa mazingira ya kisiasa” (Uk 100).
Kwa upande wake Profesa
Mwandosya, amefanya kazi yake. Ametuelezea umuhimu wa kuwa na mfumo wa udhibiti
na jinsi mfumo huu unavyopaswa kufanya kazi. Amedokeza changamoto na baadhi ya
mafanikio. Mtu mwingine anaweza kuanzia hapa na kuandika juu ya mafanikio ya
mfumo huu, je unafanya kazi, je ni kitu gani kinakwamisha mfumo huu? Je ni
kuingiza siasa katika utendaji au ni watu kutotambua nafasi zao au ni watu
kutofahamu mfumo wenyewe. Bado kuna kazi kubwa kwa upande wa wachambuzi, watoa
huduma na watumiaji.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment