USHOGA NA USAGAJI, PAPA HANA MSIMAMO MPYA.
Papa Francis wa Kanisa Katoliki Duniani, akiwa Brazil, alitoa matamko
kuhusu ushoga na usagaji na baadhi ya watu wakafikiri amekuja na msimamo mpya
na labda kuonyesha kuunga mkono Ushoga na usagaji. Alisema: “ Kwa kuwa
watangulizi wangu walikua na msimamo mkali dhidi ya watu Mashoga na suala zima
la ushoga na mimi nasema ushoga ni dhambi na chukizo kubwa mbele ya Mungu na
Binadamu... Mimi nani hadi nitoe hukumu dhidi ya watu hao, kwani Yesu mwana wa
Mungu alifundisha ya kwamba usimhukumu mtu yeyote kwani na wewe utakuja
kuhukumiwa”.
Huu si msimamo mpya hata kidogo. Tumekuwa tukiandika na kuelezea jambo
hili. Kwamba ni wazi ushoga na usagaji ni dhambi na ni kitu kisichokubalika.
Lakini ukweli ulio mbele yetu ni kwamba watu hawa wanaishi miongoni mwetu. Tuwasikilize,
tuwashauri na kuwabadilisha kutokana na hali yao hiyo. Kuwatenga na kuwalaani
haisaidii.
Tarehe 1Oktoba 1986 Kadinali Ratzinger (Papa
Benedict wa 16 aliyestaafu), alitoa mwongozo wa Kanisa Katoliki juu ya watu
wanaovutiwa na jinsia zao (homosexuality). Mwongozo huu ilikuwa ni barua
aliyowaandikia Maaskofu wote wa Kanisa Katoliki:
“ON THE PASTORAL CARE OF HOMOSEXUALS”. Katika barua hii Kadinali Ratzinger, aliwakumbusha maaskofu juu ya
mwongozo mwingine kuhusu swala hili hili uliotolewa Desemba 1975: “
Declaration of Certain Questions Concerning Sexual Ethics” uliosisitiza
kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake ifanyiwe utafiti na ichukuliwe kwa
uangalifu na busara.
Katika barua hiyo
Kadinali Ratzinger, aliwashauri maaskofu kwamba hali ya mtu kuvutiwa na jinsia
yake inahitaji wachungaji (mapadri) wenye kufanya utafiti kwa uangalifu mkubwa,
wenye kujali, wa kweli na wenye theolojia isiyokuwa ya msimamo mkali.
Ingawa Kadinali
Ratzinger, anapinga hali hii na kuiona kama hali Fulani ya ugonjwa na kufanya mambo kinyume na
maumbile, anashauri watu wenye matatizo ya kuvutiwa na jinsia zao wasitengwe.
Wapatiwe huduma za kiroho, washauriwe na kuvumiliwa hadi pale watakapobadilika.
Anasema wachukue njia ya msalaba. Wakubali kuwekwa msalabani na kufa na
kufufuka kama alivyofanya Yesu Kristu. Wazaliwe upya na kupata maisha mapya.
Anakubali kwamba ni kitu kigumu mtu kuachana na tabia yake aliyozaliwa nayo,
lakini hiyo ndiyo njia ya msalaba. Si jinsi mtu anavyotaka yeye bali ni jinsi
anavyotaka Mwenyezi Mungu!! Ni wangapi wanaukubali ukweli huu wa maisha ya
msalaba? Huu ni wajibu wa wakristu wote si wale tu ambao miili yao
inawalazimisha kuvutiwa na jinsia zao wenyewe!
Hapa ndipo kuna
tofauti kidogo. Wakati Kadinali Ratzinger, aliuchukulia ushoga na usagaji kama
aina Fulani ya ugonjwa na ulemavu, Papa Francis, anakataa. Anasema si ugonjwa,
bali ni tabia ambazo mtu anajifunza na kuna uwezekano wa kuzikomesha tabia
hizi. Na kwa mapadri na watawa wanaojifunza tabia hizi ni kwamba: “
Wanachotakiwa ni kutubu na kusamehewa na kuacha dhambi hiyo mara moja na kurudi
kwenye maisha ya tawa waliokuwa nayo na kutimiza viapo walivyoapa katia kufanya
kazi yao ya kumtumikia Mungu maisha yao yote”
Matendo ya ushogo na
usagaji si matatizo ya wakristu peke yao. Haya ni matatizo ya dunia nzima.
Hivyo kuyapinga ni lazima tuwe na misingi inayokubalika kwa watu wote. Ikibidi
na sayansi itumike. Kuipinga sayansi, ni sawa na uwenda wazimu – waliokataa
kwamba dunia haizunguki, sasa hivi wanajionea aibu kule kuzimu waliko. Si watu
wote wanaoamini kuumbwa kwa mwanamke na mwanaume kama kunavyoelezwa kwenye
Biblia. Hata hivyo si watu wote wanaoiamini Biblia. Dunia hii ina watu wangapi,
na ni kiasi gani imani yao imesimikwa kwenye biblia?
Watu ambao imani yao
haiongozwi na biblia wanasema nini kuhusiana na ushoga na usagaji. Je sisi
Waafrika, kabla ya ujio wa hizi dini za
kigeni, tulikuwa na maadili gani juu ya hali mtu kuvutiwa na jinsia yake
mwenyewe. Kuna ushahidi wa utamaduni kama kula yamini miongoni mwa makabila
mbali mbali. Watu wa jinsia moja walikuwa wanapendana kiasi wanaamua kuungana
na kuwa kitu kimoja. Kuwa kitu kimoja maana yake nini? Ni kuunganisha mwili na
roho – jinsi mkono wako unavyozigusa sehemu zote za mwili wako, ndivyo na mkono
wa ndugu yako uliyeungana naye utakavyozishika na kuzigusa sehemu zote za mwili
wako, jinsi usivyokuwa na mipaka juu ya
mwili wako ndivyo hivyo hivyo hutakuwa na mipaka juu ya mwili wa ndugu yako
utakayeungana naye! Huu ni undugu au urafiki uliokuwa na masharti magumu kweli.
Ilikuwa ni kuungana katika taabu na katika raha, mfano rafiki wa kuchanjana,
akiugua na wewe unaugua, akifiwa na wewe umefiwa, akiwa na sherehe na wewe ni
sherehe yako, akakiugua ugonjwa wa ukoma huwezi kumtenga, akiugua ugonjwa wa
kifafa huwezi kumtenga, mke wake anakuwa mke wako, na watoto wako wanakuwa watoto
wake. Akikutembelea unahama chumbani kwako, unamwachia kitanda na mke wako! Ni
vigumu kusema kwamba katika uhusiano wa
namna hii watu walikuwa hawawakiani tamaa
ni vigumu kuwa na uhusiano mzito hivi na mtu ambaye hakusisimui kimwili
na kiroho! kuna haja ya kufanya utafiti juu ya jambo hili!
Ushoga ni aina Fulani ya
uhusiano wa mtu na mtu. Watu wa jinsia moja wanajenga uhusiano mkubwa kiasi
wanashindwa kujua ni wapi waweke mipaka katika uhusiano wao. Mfano kama mtu
anaweza kushirikiana mke wake na rafiki yake, bila kujificha kwa kukubaliana,
kama mtu akishindwa kumtenga rafiki yake akiugua kifafa na ukoma, kama mtu
anaweza kumwogesha rafiki yake hata kumsindikiza hadi chooni, kama mtu anaweza kuugusa mwili wote wa rafiki
yake ni kitu gani hawawezi kufanya pamoja? Ni wapi waweke mpaka? Wao peke yao
hawawezi hadi wapate msaada wa jamii inayowazunguka. Swali linakuwa je, hiyo
inakuwa ni tabia ya baadhi ya watu katika jamii, au ni tabia inayokubalika
katika jamii nzima. Je tabia hii inaweza kuvuruga amani ya jamii kama vile
kusengenya, uchoyo, wivu na wizi? Haya ndiyo mambo ya kujadiliana.
Wakati sisi tunaishikia
bango kubwa hali ya mtu kuvutiwa na jinsia yake, wakati tunalaani matendo ya
kulawiti, kufira, usenge, ushoga na usagaji, Paulo, anazichanganya dhambi hizi
na dhambi nyinginezo kama vile uchoyo, ulevi, kusengenya na kulaghai. Na bahati
mbaya hakutofautisha ili kuonyesha ni dhambi ipi ni ndogo na ipi ni kubwa. Kama
ushoga na usagaji zingelikuwa ni dhambi kubwa kuliko nyingine, basi Paulo,
angezitaja peke yake ili kuuonyesha mkazo. Lakini yeye anaziweka kwenye ngazi
moja na dhambi nyingine. Tuna watu wangapi katika jamii zetu wanaosema uongo,
walevi, walaghai na wanaosengenya? Na je hawa tumewashikia bango mara ngapi
kama tunavyowashikia mashoga? Je, wachoyo ni wangapi? Dunia yetu imegawanyika
katika makundi ya maskini na matajiri kwa sababu uchoyo wa mali ni mkubwa sana.
Hili tumelishikia bango? Hili tunalilaani kama tunavyolaani ushoga na usagaji?
Katika hali ya kawaida uchoyo wa mali ni dhambi kubwa, maana uchoyo wa mali
unasababisha vita, mashindano na kuvuruga amani katika dunia yetu. Ushoga
umeleta vita? Umeleta matabaka katika jamii? Hili ni jambo la kujadiliana kwa
kina na wala si kulipinga kwa kufuata mkumbo.
Kazi kubwa iliyo mbele
yetu ni kufafanua uhusiano wa mtu na mtu. Ni kuwafanya watu wa kawa wazi juu ya
uhusiano wao. Walio wengi na hasa katika jamii zetu za Kiafrika, wanakuwa
wagumu kuweka wazi swala hili la uhusiano. Watu wangependa kuhusiana kwa siri, lakini
mapenzi ni kikohozi hayawezi kujificha. Yawe ni mapenzi yanayoruhusiwa au ya
kinyume na maumbile, penye mapenzi hapakosi dalili!
Hadi sasa hivi watu
wanaogopa kuutaja udhaifu wao ili wasichekwe na kutengwa. Jinsi tunavyoficha
ukweli juu ya ugonjwa wa UKIMWI, ndivyo tunavyoshindwa kusema ukweli juu ya
mambo mengine yanayozunguka uhusiano wa mtu na mtu. Tunaogopa kuchekwa,
kunyoshewa kidole na unyanyapaa. Hivyo walio wengi wanaamua kuendelea kuishi na
udhaifu wao. Msimamo huu umeleta madhara mengi katika kanisa na katika jamii
nzima. Mfano watu wanaoshindwa kumudu sheria ya mke mmoja mme mmoja,
wanashindwa kujitokeza na matokeo yake ni ndoa za mitala ambazo mara nyingi
watoto wa nje hapawapati haki kama wanazozipata watoto walio kwenye ndoa
zinazotambuliwa na kanisa na jamii nzima. Hali hii imezalisha watoto wengi wa
mitaani. Pia uhusiano wa mtu na mtu limekuwa ni jambo la kufanywa kwa siri
kiasi watu wengi wameanguka kwenye hatari ya ugonjwa wa UKIMWI, bila kupata
ushauri maana wengi wao wanakutana kisiri. Ni vigumu kumpatia mtu ushauri wa
kujikinga kama hajakueleza kwamba anatembea na mtu ambaye una hakika ana virusi
vya UKIMWI.
Hivyo tusifikiri Papa, amekuja na msimamo mpya.
Tusifikiri Papa anaunga mkono ushoga na usagaji. Ni jambo la busara na hekima
na kama anavyosema Papa Francis: “... anayestahili kuhukumu ni Mungu pekee na
si mwingine”
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22
0 comments:
Post a Comment