UKATILI WA
KJINSIA BADO NI KITENDAWILI TANZANIA
Tarehe 25.11.2013, tunaanza siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia. Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni kampeni ya
kimataifa iliyoanzia kwenye mkutano wa kwanza wa Taasisi ya Uongozi wa Wanawake
Duniani (Women’s Global Leadership Institute)
uliofadhiliwa na Kituo Cha Uongozi wa Wanawake Duniani (Center for
Women’s Global Leadership ) mwaka 1991. (. Washiriki walichagua tarehe 25 mwezi
Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake, na Desemba 10,
Siku ya Haki za Binadamu Duniani, ili kuhusianisha ukatili dhidi ya wanawake na
haki za binadamu na kuhamasisha kuwa ukatili kama huu ni ukiukaji wa haki za
binadamu. Kipindi hiki cha siku 16 pia kinaangalia siku nyingine muhimu,
ikiwemo tarehe 29 Novemba, ambayo ni Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu,
Desemba 1 Siku ya Ukimwi Duniani na Desemba 6, Kumbukumbu ya Mauaji ya Montreal.
Ukatili Dhidi ya Wanawake ni ukiukwaji ulionea wa haki za binadamu , ni janga la
kibinadamu katika jamii, na kikwazo cha kufikia usawa, maendeleo, usalama na
amani. Maneno “ukatili dhidi ya wanawake” na “ukatili wa kijinsia” yanatumika
kumaanisha mlolongo wa unyanyasaji unaofanyika dhidi ya wanawake unaotokana na kutokuwepo na usawa wa kijinsia
na hadhi ya chini wa wanawake katika jamii ukilinganisha na wanaume. Mwaka
1993, Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake uliutafsiri
ukatili dhidi ya wanawake kama:
“kitendo
chochote cha ukatili wa kijinsia kinachosababisha au kinachoweza kusababisha
maumivu au mateso ya kimwili, kingono au kiakili kwa wanawake, ikiwamo vitisho,
kulazimishwa au kunyimwa uhuru, vinavyotokea katika jamii au kwenye maisha
binafsi .” Inakadiriwa kuwa mmoja kati
ya wanawake watatu duniani atakumbana na ina Fulani za ukatili wa kijinsia
katika maisha yake. Hivyo ni wazi kabisa kwamba wanaofanyiwa ukatili wa
kijinsia ni wanawake, ingawa si lazima kwamba ukatili huu unafanywa na wanaume
peke yao.
Lengo la siku hizi 16 ni kupinga ukatili wa kijinsia,
lakini kwa wengi siku hizi zimechukuliwa kama kupinga ukatili dhidi ya
wanawake. Na kwa mtizamo finyu ni ukatili unaofanywa na wanaume kwa wanawake.
Lakini hali halisi na matukio ya siku kwa siku na hasa hapa Tanzania
yanaonyesha tofauti kabisa, kiasi cha kulifanya suala zima la ukatili wa kijinsia
kuwa ni kitendawili.
Hata ukiiangalia mikataba ya kimataifa ya haki za
binadamu na maazimio yaliyofikiwa ndani ya Umoja wa Mataifa kushughulikia
ukatili dhidi ya wanawake na inayohitaji Serikali kuchukua hatua yote imelenga
ukatili dhidi ya wanawake, ikiwemo Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ukatili
Dhidi ya Wanawake (CEDAW, 1979), Mkataba
wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake (DEVAW, 1993),Azimio la Beijing na Ulingo wa Hatua(1995), Mkataba wa
Mahakama ya Uhalifu Kimataifa (Mkataba
wa Rome , 1998), Azimio la Milenia
(2000) na Azimio la Baraza la
Usalama 1325 juu ya Wanawake, Amani na
Usalama (2000), na mengineyo.
Wimbi kubwa la kuwanyanyasa wafanyakazi wa
majumbani ambao asilimia kubwa ni wasichana linabadilisha kwa kiasi fulana
dhana nzima ya ukatili wa kijinsia. Manyanyaso haya kwa kiasi kikubwa
yanatekelezwa na wanawake. Ingawa kwa kiasi Fulani wafanyakazi hawa wa majumbani
wananyanyaswa na kudhalilishwa na wanaume, kama kuwabaka au kuwageuza nyumba ndogo,
lakini mateso makubwa dhidi ya utu wao na uhuru wao yanatendwa na wanawake.
Biashara ya ngono, kwa kiasi Fulani inaendeshwa
na wanawake. Wanawakusanya wasichana wadogo sehemu mmoja, na hasa kwenye miji
mikubwa na kuwatumikisha kingono, ni
aina Fulani ya utamaduni wa kule mkoa wa Mara, ambako wanawake wanao kwa lengo
la kuwa na wasichana wa kuwatumikisha kingono na kujipatia watoto. Utamaduni
huu unajulikana kama “Nyumbantobu”. Katika utamaduni huu, msichana anayeolewa
na mwanamke, anakuwa hana uhuru wa aina yoyote na mwili wake au na watoto
anaowazaa. Hii ni aina ya ukatili wa kijinsia, ambao ingawa wanatendewa
wanawake, lakini si ukatili wa wanaume.
“Idadi ya wanaume wanaofika kwenye kituo cha
polisi kulalamika kupigwa na wake zao imeanza kuongezeka kwa kasi katika Jiji
la Dar-es-Salaam” Hayo yalisemwa na Kaimu Kamishana wa Polisi, Adolphina Chialo,
alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia, ulioratibiwa na Shirika la wanawake katika Sheria na Maendeleo
(WiLDAF).
Utafiti uliofanywa tarehe 22.11.2013 kwenye Bar
ya Kisuma- Mwembeyanga-Temeke- Dar-es-alaam, umeongeza giza nene kwenye suala
zima la ukatili wa kijinsia. Wanawake sita ambao ni miongoni mwa wanawake wengi
wanaohudumia kwenye Bar hiyo walikuwa na maoni tofauti na yanayopingana juu ya
ukatili wa kijinsia. Wakati wanawake watatu
walikataa kushuhudia aina yoyote ile ya
ukatili na udhalilishaji wa wahudumu kwenye baa hiyo, wanawake wengine
watatu walilalamikia manyanyaso na udhalilishaji wa hali ya juu kwenye baa hiyo
ya Kisuma.
Utafiti ulifanywa Kisuma, baada ya kuwepo na
taarifa za unyanyasaji wa kijinsia kwenye baa nyingi za Dar-es-Salaam. Wahudumu
kulazimishwa kuvaa nguo fupi, kuonyesha sehemu kubwa ya matiti yao,
kulazimishwa kushikwa shikwa na wateja, kufanyishwa kazi masaa mengi kwa malipo
kidogo na matendo mengi ambayo ni
kinyume na haki za Binadamu.
Adela Joseph (jina la kubuni), mhudumu wa Baa ya
Kisuma, alilalamika “ Tunafanya kazi masaa mengi, mshahara kidogo. Tunashikwa
shikwa na wanaume, ukilalamika unafukuzwa au unaambiwa hii si hoteli ya chai,
hivyo ni lazima kuvumilia… ukibeba mimba, unakuwa umejifuta kazi, maana ukienda
kujifungua, ndo mwisho wa kazi yako… hakuna haki hapa, tunanyanyaswa na
kudhalilishwa”
Meneja wa Bar ya Kisuma, bwana Peter Jackob (jina
la kubuni), aliungana na wale wanawake watatu waliosema Kisuma hakuna
udhalilishaji. “ Mtu akimshika shika mhudumu bila ridhaa yake, sheria inachukua
mkondo wake. Tunatenda haki na kuhakikisha kila mhudumu anapata haki yake,
mishahara yetu ni mizuri na wana marupurupu mengi.
Bwana Kafana Mbyango (Jina la kubuni) mteja wa
Kisuma, aliyefuatilia maongezi yetu kwa karibu alisaidia kufumbua kitendawili cha
Kisuma; wanawake watatu na meneja wanasema mambo safi, wakati wanawake wengine
wanasema Kisuma kuna unyanyasaji wa kijinsia. “ Unajua wale wanaotetea, ni wale
wenye mishahara mikubwa, ni wale wenye mahusiano ya karibu sana na Meneja au
mwenye Bar, ni wale wakivunja gilasi, mishahara yao haikatwi. Kusema kweli hapa
Kisuma kuna unyanyasaji wa hali ya juu, nimeshuhudia mara nyingi wahudumu
wakidhalilishwa..”.
“Kisuma, kuna udhalilishaji wa hali ya juu.
Kwanza, kwa maoni yangu mimi wanawake wote wa Kisuma, ni Malaya tu! Ukifanya
kazi kwenye Baa, wewe ni Malaya..” Alichangia kijana mmoja aliyeonekana kuwa ni
mteja wa kila siku pale Kisuma.
Ina maana pale Kisuma, wahudumu wanawake wenye
hali nzuri kimaslahi, wanabariki unyanyaswaji na udhalilishwaji wa wanawake
wenzao? Kwa maneno mengine, huu ni unyanyasaji wa wanawake unaoendeshwa na
wanawake wenyewe! Hiki ndicho tunachokiita kitendawili. Kazi kubwa iliyo mbele
ya wanaharakati na wale wote wenye mapenzi mema ya kutaka kuona ukatili wa
kijinsia unakomeshwa, wajitahidi kutegua kitendawili hiki. Tusipumbazwe na
utamaduni wa wanaume kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake, tuliangalie na
kulishughulikia suala zima la unyanyasaji wa kijinsia: Wanaume wanawanyanyasa
wanawake, lakini pia kuna wanawake wanaonyanyasa na kuwadhalilisha wanawake
wenzao na wakati mwingine kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wanaume.
Ukatili wa kijinsia, uzingatie suala zima la haki
za watoto: Wasichana kwa wavulana, haki za wanawake na haki za wanaume.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment