UHAKIKI WA KITABU: HAKI ZA MADEREVA, ABIRIA
NA POLISI BARABARANI.
1.
Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu
kinachohahikiwa hapa ni Haki za Madereva, Abiria na Polisi Barabarani. ,
Kimeandikwa na Al-Muswadiku K.Chamani . Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania
Educational Publishera LTD(TEPU) na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia
ya vitabu duniani (ISBN): 978 9987 07 048 0 Kitabu kina kurasa 85 . Na
anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Jina refu la kitabu hiki linastahili liwe “
Haki na Wajibu wa Madereva, Abiria na Polisi Barabarani kwa mujibu wa sheria na
kanuni”. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Oxford
University Press, maana ya neno dereva ni mwendeshaji wa vyombo vinavyosafiri
nchi kavu, kama vile trekta, treni, motokaa, pikipiki na baiskeli; neno abiria
lina maana ya mtu anayesafiri kwa chombo chochote cha usafiri na neno polisi
lina maana ya askari mwenye dhamana ya kuona kuwa sheria na usalama wa nchi
hauvunjwi. Kwa upande mwingine, hakuna mtu mzima ambaye hajawahi kuwa abiria au
anayeweza kusema kuwa hatakuwa abiria maishani mwake.
Ili shughuli za usafiri
na usafirishaji ziendeshwe kwa usalama, sheria kadhaa zimetungwa kuongoza
wadau, na makundi matatu, yaani Madereva, Abiria na Polisi hayaepukiki
kukutana. Wajibu wa polisi ni kuhakikisha kuwa sheria hizo zinazingatiwa kwa
usalama wa abiria na wadau wengine na wajibu wa madereva ni kuzizingatia.
Katika kufanya kazi hii,
baadhi ya polisi wa barabarani na wakubwa wao, hawana sifa nzuri. Wanatuhumiwa
na madereva kuwa hudai na kupokea rusha. Lakini, si polisi wote wanabebeshwa
tuhuma hii. Hata hivyo, mara nyingi madereva au/na vyombo vyao kweli huwa na
makosa. Lakini ni si wote huyakubali. Wao wanadai wameonewa, hata makosa
yanapokuwa dhahiri.
Lakini, sheria za
usalama barabarani zinasema nini katika kulinda usalama wa madereva, abiria na watumiaji
wengine wa barabara? Je, kwa mujibu wa sheria hizo, haki na wajibu wa Madereva,
Abiria na Polisi ni upi? Katika kitabu hiki, mwandishi, anayajibu maswali hayo
kwa utaalamu na umakini. Katika kurasa zinazofuata nitafanya uhakiki wa kitabu
hiki baada ya kukaangalia mazingira yanayokizunguka.
III. Mazingira
yanayokizunguka kitabu
Tanzania, tuna tatizo
kubwa kutofuata sheria. Kwa maneno mengine hatupendi kufuata utaratibu. Unaweza
kutaja mambo mengi ambayo mara nyingi watanzania wanapenda njia za mkato. Na
kufuata njia za mkato ni chanzo cha rushwa katika taifa.
Lakini kwa hoja iliyo
mbele yetu, njia za mkato zinasababisha vifo. Ajali nyingi za vyombo vya
usafiri na hasa vyombo vya abiria ni matokeo ya utamaduni wa kutofuata sheria.
Vifo vinavyobabishwa na vyombo vya usafiri vinaongezeka siku hadi siku. Wakati
polisi wanalaumiwa kuwanyanyasa madereva, kwa upande wao wanajitetea kuzingatia
sheria. Bila kuwapendelea polisi, ambao nao kwa upande wao kuna ambao
wanatanguliza rushwa na maslahi binafsi kabla ya sheria, kwa kiasi kikubwa
madereva wanachochea utamaduni wa rushwa kwa kutaka kukwepa usumbufu wa
kusimamishwa muda mrefu na maswali mengi.
Pamoja na ukweli kwamba
Tanzania, ina baadhi ya sheria ambazo ni nzuri, lakini watu hawazifuati na
kuzitekeleza. Ni wazi kuna baadhi ya sheria ambazo ni kandamizi na zilitungwa
wakati wa ukoloni na zinaendelea kuwepo kwa vile zinawalinda viongozi wanaokuwa
madarakani, kwa vyovyote vile ili maisha yaende vizuri ni vyema kufuata sheria.
Serikali, mashirika
yasiyokuwa ya kiserikali na watu wengine wenye mapenzi mema wamekuwa
wakijitahidi kuhimiza utawala wa sheria na watu kufuata sheria. Mwandishi wa
kitabu hiki Bwana Al-Muswadiku K Chamani, ni mmoja wao. Ameandika vitabu vingi
juu ya sheria mbali mbali katika taifa letu, baadhi ya vitabu hivyo ni: Ufafanuzi wa Sheria ya
Kumiliki ardhi vijijini Tanzania, Mwalimu katika Sheria Tanzania, Fahamu kisheria
afisa mtendaji wa kata nchini Tanzania, Sheria ya ardhi: Umilikaji na matumizi
ya ardhi mkoani Kagera, Haki zangu mbele ya polisi, Haki za mwalimu Tanzania, Ufafanuzi
wa sheria ya kumiliki ardhi vijijini Tanzania. Na sasa kitabu hiki cha Haki za
Madereva, Abiria na Polisi Barabarani kinaongezeka kwenye orodha ya mwandishi
huyu.
Wakati sote tunalalamika kwamba watu hawafuati
sheria, na wakati mwingine hata wale wanaofanya kazi serikalini hawafuati
sheria, mwandishi amevunja utamaduni huu wa kulalamika, na kuhakikisha anatumia
elimu yake ya sheria, kuwafahamisha watu sheria mbali mbali na kuzieleza katika
lugha nyepesi, ili kila mtu azifahamu.
Mfano, alipoandika kitabu juu ya Watendaji wa
vijiji, watu wengi walifurahi kufahamu wajibu wa watendaji wa vijiji na mipaka
yao. Tabia ya watendaji wa vijiji kujifanya Miungu watu, kuwapiga watu na
kuwaweka ndani ilipungua sehemu ambazo vitabu hivi vilisambazwa. Ni wazi
watendaji ambao walitumia nafasi yao kujipatia fedha na mali kwa kuwanyanyasa
na kuwatesa wananchi, hawakukipenda kitabu cha Chamani, hata hivyo ukweli
unabaki pale pale kwamba tunahitaji utawala wa sheria.
Huyu ni miongoni mwa watu wachache wanaotumia
elimu yao kuwaelimisha watu wengine na hasa kwa kuandika vitabu. Mzee Pius
Ngeze, amefanya hivyo kwenye kilimo na kuandika vitabu vingi vya kilimo katika
lugha nyepesi. Sasa na Chamani, anafanya hivyo upande wa sheria. Watanzania
wakijijengea utamaduni wa kusoma, na kuvisoma vitabu hivi, ni lazima maendeleo
ya taifa letu yatakwenda kwa kasi kubwa.
Mwandishi wa kitabu hiki
ni wakili wa kujitegemea, aliyezaliwa wilayani Karagwe, mkoani Kagera, mwaka wa
1952. Al-Muswadiku K Chamani, maarufu kwa jina la “Kaka Alli”, alimaliza elimu
ya msingi katika shule ya Msingi Katembe iliyoko wilayani Karagwe, mwaka wa
1967 na kujinga na Shule ya Sekondari ya Nyakato, wilayani Bukoba, kuanzia
mwaka wa 1968 hadi 1971.
Baada ya hapo, alijiunga
na kozi ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Tabora,mwaka 1972 hadi 1973. Kaka
Alli alianza kufundisha mkoani Mara katika shule ya Msingi Kanyega, wilayani
Musoma, mwaka 1974 hadi 1977. Alifanya mtihani wa kidato cha sita mwaka 1975 na
akafaulu kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, kuanzia 1977 hadi 1980
alipotunukiwa shahada ya B.A. (Hons).
Aliteuliwa kuwa Mkuu wa
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi wilayani Ngara mwaka 1981 na baadaye kuhamishiwa
wilayani Biharamulo mwaka 1982. Alijiunga tena na masomo ya Stashahada ya Juu
ya Sheria kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam.
Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, akafaulu kupata shahada ya
Sheria (LLB- Hons) mwaka 2004.
Sasa hivi ni wakili wa
kujitegemea kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa akiwa katika kampuni ya Mawakili ya
Chamani And Company Advocates, makao makuu yakiwa ndani ya Manispaa ya Bukoba,
Kagera.
IV. Muhtasari wa
Kitabu
Kitabu kimegawanywa kwenye vipengele 50. Vipengele 1 – 8 vinaongelea;
Wajibu wa raia katika kulinda sheria za nchi, wajibu wa Mwanasheria wa
Serikali na Kamanda wa Takukuru katika kuhakikisha sheria zinalindwa,
Sheria zinazohusiana na usalama wa magari barabarani, Adhabu bila
kushatakiwa,, Kumkamata mtu aliyetenda kosa, Makosa ya taarifa na kuwekwa chini
ya ulinzi kwa makosa yasiyoorodheshwa katika kanuni ya taarifa ya makosa.
“Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,(Sura ya 2 R.E.2002) inampa raia wajibu wa kuhakikisha hifadhi ya
Katiba na Sheria za nchi” (Uk 1).
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mteule wa Rais, madaraka yake
yanaonyeshwa katika Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kuwa ni mshauri wa serikali juu ya mambo ya sheria na kutekeleza shughuli
zozote zenye asili au zinazohusiana na sheria zitakazopelekwa ofisini kwake au
atakapoagizwa na Rais kuzitekeleza na kutekeleza shughuli nyingine
zilizokabidhiwa kwake na Katiba hii au sheria yoyote” (Uk2)
“Sheria zinazohusu usalama barabarani ambazo ni muhimu zaidi ni ni: Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya jinai, Sheria
ya Usalama Barabarani (sura ya 168 R.E. 2002), Sheria ya Leseni za Usafirishaji
(Sura ya 317 R.E. 2002), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya
Moto na Jeshi la Uokoaji ( Sheria namba 14 ya mwaka 2007) na Sheria ya Mamlaka
ya usafirishaji wa Nchi kavu na majini (Sura ya 413 R.E. 2002)” (Uk 4).
“Fungu la 110 la Sheria ya Usalama Barabarani (Sura ya 168 R.E. 2002)
limeonyesha kosa ambalo likitendeka, basi, Ofisa wa Polisi atakuwa na madaraka
ya kumkamata mtuhumiwa” (Uk 11).
Vipengele kuanzia cha 9 hadi 25, vinajadili juu ya; Madaraka ya polisi kusimamisha gari, kupekua na kuzuia
gari, Umuhimu wa Ofisa wa Polisi kufuata sheria, Tafsiri ya “Sababu za maana”,
Watoza ushuru wa maegesho kukamata gari na kuyafunga minyororo, Utaratibu wa
kupinga Sheria ndogo inayokinzana na Sheria andishi, Kuwa na leseni wakati wa kuendesha
gari, Mtuhumiwa kutoroka, Bima ya gari, Stika ya Wiki ya Nenda kwa Usalama
Barabarani, Leseni ya barabara na Stika ya Zimamoto, Kutoa kibao cha usajili wa
gari na kunyang’anywa leseni, Muda wa kulipa faini baada ya ilani ya kosa
kutolewa, Matumizi ya pikipiki kibiashara, Utaratibu wa kufuta leseni, Makosa
ya pikipiki ya biashara, Nani hulipisha faini za pikipiki za biashara, Muda na
kiwango cha kulipa faini ya pikipiki ya biashara, Nauli ya abiria na Kuweka
petroli wakati gari lina abiria.
“ Madaraka ya Polisi kusimamisha, kupekua na kuzuia gari lisiendelee na
shughuli zake yapo katika fungu la 25 la sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Sura ya 20 R.E. 2002)” (Uk 14).
“Mtu yeyote kwa makusudi anayetumia vibaya nafasi yake katika kufanya au
kushindwa kufanya tendo kwa kukiuka sheria, wakati akitekeleza wajibu, atakuwa
ametenda kosa..” (Uk 23).
“Iwapo itaonekana ( kuwa mtu huyo) hakuamini kuwa (Mtu aliyetuhumiwa) alikuwa katenda kosa,
basi, hakuna “sababu ya maana” kwa upande wake na hawezi kusikilizwa kwa kusema
hali halisi ambayo ilikuwa haifahamiki kwake ingeweza kumfanya mtuhumiwa kuwa
na kosa” (Uk 24).
Juu ya matumizi ya Pikipiki kibiashara tunaambiwa na mwandishi kwamba:
“ Kanuni za Lezeni za Usafirishaji (Pikipiki na Pikipiki yenye magurudumu
matatu) za mwaka 2010, zilizotolewa katika Gazeti la Serikali 144 ya mwaka
2010, imeruhusu pikipiki kutumiwa katika shughuli ya biashara ya kusafirisha
abiria kwa mashati yafuatayo:
- Kuwa na leseni halali ya huduma ya barabara inayotolewa na mamlaka ya
serikali za Mitaa inayohusika, vinginevyo ukiendesha pikipiki bila leseni hii
utakuwa umetenda kosa na ukitiwa hatiani utatozwa faini isiyopungua shilingi
elfu hamsini au kifungo kisichopungua miezi sita wala kuzidi mwaka mmoja au
vyote kwa pamoja.
- Leseni hii, itatolewa kwa mwombaji mwenye pikipiki inayofaa kufanyiwa
biashara hii.
- Mwombaji awe na umri zaidi ya miaka kumi na nane
- Mwombaji atapaswa kulipa ada, faini na gharama nyinginezo kwa SUMATRA
kupitia mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuweza kupata leseni hiyo” ( UK39)
Juu ya utaratibu wa kufuta leseni,
tunaambiwa kwamba: “Kanuni ya 19 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Pikipiki
na Pikipiki za Magurudumu matatu) za mwaka 2010 inaonyesha utaratibu
utakaotumiwa katika kufuta leseni hiyo iwapo atakiuka masharti yaliyotolewa” (
Uk 41).
Vipengele vya 26 mpaka 40, vinajadili juu ya: Taarifa ya kito cha
kushukia, Gari likiharibika, abiria hurudishiwa nauli?, Ukaguzi wa gari kwa
kuwekwa chini ya ulinzi, Madaraka ya Ofisa wa Polisi Mkaguzi kukagua gari la
abiria, Wafanyakazi wa gari la abiria, Wajibu wa abiria, Uzito wa mizigo ya
abiria, Kulipia tiketi mapema na kusitisha safari, Nauli ya mtoto na
mwanafunzi, Kiwango cha nauli, Kutotoa huduma ya usafiri kwa muda uliopangwa,
Kosa la kutotoa tiketi ya nauli, Abiria kushindwa kulipa nauli nakuteremshwa.
Juu ya taarifa ya kituo cha kushukia, tunasikia kwamba: “ Anayefanya
huduma ya gari ya kusafirisha abiria atapaswa ahakikishe anawatangazia kituo
kinachofuata” (Uk 48) na hii ni kwa mujibu wa “ Kanuni ya 103 ya Kanuni za
SUMATRA (Usalama wa Kiufundi na kiwango cha huduma (Magari ya abiria) za mwaka
2008. Hivyo ni lazima kituo cha kushukia kitangazwe, ingawa mara nyingi hawafanyi
hivyo, ni vizuri kupitia kitabu hiki abiria wakatambua haki zao ambazo mara
nyingi zinakiukwa.
Je Gari likiharibika, abiria hurudishiwa na nauli? Kanu ya 11 ya Kanuni
za SUMATRA(Usalama wa Kiufundi na Kiwango cha huduma) (Magari ya abiria) za
mwaka 2008, inaonyesha kuwa; “ Iwapo gari lililoharibika linafanya shughuli
zake katika maneno ya mji, basi, mwenye gari atapaswa atoe usafiri mwingine
ndani ya dakika kuma na tano au arudishe kiasi cha nauli ambacho kitamalizia
sehemu ya safari iliyobakia kwa kila abiria. Kama gari hilo linafanya safari za
nje ya mji, basi mwenye gari atapaswa alitengeneze na kuendelea na safari ndani ya muda wa saa
mbili au atoe usafiri mwingine ndani ya saa mbili...... Kutokana na msimamo wa
kisheria ni kuwa, iwapo gari la abiria limeharibika, basi, unazo haki zako na
utapaswa utendewe kwa mujibu wa sheria” ( Uk 49)
Ni abiria wangapi wanatendewa hivyo? Au ni abiria wangapi wanafahamu
kwamba sheria inawalinda na gari likiharibika ni lazima sheria ifuate mkondo
wake?
Vipengele vya 41 mpaka 50, vinajadili juu ya: Vizuizi barabarani, Vizuizi
kwa ajili ya kutoza ushuru, Kuzuia polisi kufanya wajibu wake, Polisi
kufunguliwa madai akiwa kazini, Kutovaa helmeti ni kosa? Kukamatwa, kushtakiwa
na udhamini wa mahakamani, Pikipiki za polisi barabarani, Majedwali, marejeo na
mwisho kabisa ni wasifu wa mwandishi wa kitabu hiki.
Kwa kifupi kitabu hiki kinalenga kusaidia kupunguza ufa wa ushirikiano
uliopo kati ya madereva na wa vyombo vya usafiri vinavyotumia barabara, abiria
na Jeshi la polisi. Wananchi wakifahamu madaraka na wajibu wa polisi inakuwa
rahisi kushirikiana nao badala ya kuwaona kama maadui wake.
Mada zilizogusiwa humu zinahusu zaidi Haki na Wajibu wa madereva wa
polisi wakiwa barabarani; utaratibu wa kumaliza makosa yaliyotendwa na dereva
wa chombo cha usafiri; ukamataji wa
dereva na chombo chake; amri ya kulipeleka Kituo cha Polisi na magari ya
abiria, pikipiki za biashara, baiskeli na masharti yake.
V. Tathmini ya Kitabu
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye
tathimini ya kazi hii aliyoifanya Bwana Al-Muswadiku K Chamani.
Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa
kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi, kitabu kinasisimua, kinafundisha na
kinafikirisha kutokana na mtindo alioutumia mwandishi. Ametumia mtindo wa Maswali na Majibu
kuwasilisha ujumbe kwa msomaji, huku akinukuu vifungu vya sheria kwa makusudi
ya kuweka msisitizo na kufanya wepesi wa marejeo kwani sheria zilizo nyingi
hazipatikani kwa wadau.
Pili, mwandishi kwa kutumia vitabu vyake hivi vya
sheria mbali mbali katika jamii yetu anatufumbua macho na kutuaminisha kwamba
utawala wa sheria unapofuatwa, basi, haki na amani vitakuwapo kwa manufaa ya
maendeleo.
Tatu, kama nilivyodokeza kwenye utangulizi,
mwandishi huyu anajiunga na waandishi wengine ambao baada ya kusoma kuihitimu
wanaitumia elimu yao kuwaelimisha wengine ambao hawakupata bahati ya kufikia
hatua hiyo ya elimu. Si kila Mtanzania anapata nafasi kusomea Sheria, hivyo kwa
kutumia kitabu hiki, hata yule ambaye hakusomea sheria anaweza kutetea haki
zake.
Nne, kitabu hiki kinakuja wakati wake, ambapo
magari yakiharibika abiria wanajijua. Ni wachache wanaofahamu haki zao. Sasa
wakisoma kitabu hiki, na kufahamu haki zao, kufahamu kwamba Gari, likiharibika
ni lazima mwenye Gari kuhakikisha abiria hao wanaendelea na safari wenye vyombo
vya usafiri wa abiria wataacha kiburi chao na vitendo vya kuwanyanyasa abiria.
Tunaweza kuanza kushuhudia mabadiliko makubwa katika usafirishaji wa abiria.
Uzuri wa kitabu hiki kinaelezea vizuri haki na wajibu wa kila mdau. Ni kwamba
kinasisitiza kufuata sheria ili mahusiano ya polisi, madereva na abiria yawe
mazuri.
Tano, kitabu hiki ni msaada kwa wadau wote,
madereva, abiria na polisi. Kuna wakati polisi anawakamata madereva, kwa uonevu
tu au kwa utamaduni wa kutaka rushwa na hasa sikukuu kubwa za kidini na kufunga
na kufungua mwaka zinapokaribia, lakini kwa vile madereva hawafahamu haki zao,
wanakubali kunyanyaswa na kutoa fedha. Hivyo madereva wakisoma kitabu hiki
watafumbuka macho na kuanza kuzitetea haki zao.
Sita, kwa upande wa mijini na hasa mikubwa kama vile Dar-es-Salaam,
Mwanza, Arusha, Mbeya na mingine, ambako karibia kila siku ya Mungu, kila mtu
anapanda magari ya abiria, kitabu hiki kitakuwa msaada mkubwa.
Saba, kwa vile sasa hivi tuko kwenye siasa za
vyama vingi, ufahamu wa sheria ni muhimu sana. Ule upendeleo wa wazi, kwa watu
wanaokiunga mkono chama tawala, kiasi hata cha kuvunja sheria zote hata na zile
za barabarani utakwisha! Sheria haina vyama, sheria haina dini na sheria haina
kabila. Hivyo kitabu hiki kitawasaidia wengi na uonevu wa ovyo utapungua.
VI. Hitimisho
Kwa kuhitimisha, nawaomba watanzania
kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Kusema kweli ni kitabu cha msaada kwa wale
wanaosafiri mara nyingi na vyombo vya abiria. Pia ni muhimu kwa polisi nao
kukisoma kitabu hiki ili kupunguza mapambano yasiyokuwa ya lazima katika ya
polisi na madereva.
Lakini pia ni muhimu kuvitafuta vitabu
vingine vya Al- Muswadiku Chamani na kuvisoma, maana vyote vinaelezea utawala
wa sheria.
Mwisho kabisa, nampongeza Bwana Al-Muswadiku
Chamani kwa kujitoa kuandika vitabu vya sheria ili kuwasaidia watu wengi ambao wananyanyaswa
na kupokwa haki zao kwa vile hawana utaalamu wa sheria. Vitabu vyake vimekuwa
msaada mkubwa kwa watu wa vijijini na hasa vitabu vyake vinavyohusu sheria za
Ardhi na watendaji wa vijiji.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment