TUJIFUNZE KUTOKA KWA MZEE MANDELA
Wakati
dunia nzima inaendelea kumwombea Mzee Mandela, apate afya njema na kupona
ugonjwa uliomlaza kitandani zaidi ya majuma mawili sasa, ni lazima watanzania tujifunze
kutoka kwake. Mzee Nelson Mandela, ni kati ya watu wachache waliofanikiwa
kuyaishi na kuyashika mafundisho magumu. Mafundisho ambayo waliowengi tunayaita
ndoto, lakini tunayafundisha na kuwahimiza watu wengine wayashike na
kuyafuata.Alipohukumiwa kifungo cha maisha,Mzee Mandela, alipokea hukumu hiyo
bila ya woga, ni kitu alichokifahamu hata kabla ya kuanza mapambano na serikali
ya makaburu. Alifahamu nguvu na uwezo wa serikali ya makaburu. Alijua
walivyokuwa wameshikilia vyombo vya dola na silaha nzito nzito, alijua
angekamatwa na kufungwa au kuuawa.Pamoja na kuyajua yote hayo aliamua kuendelea
kupambana na makaburu kwa vile alitanguliza uhai wa taifa lake na wala si uhai
wa maisha yake binafsi. Lakini pia alijua jinsi nguvu na uwezo wa makaburu vilivyokuwa
vinaishia kwenye kuutesa mwili wake bila ya kuwa na uwezo wa kuigusa roho yake
hata hivyo mafundisho magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa
yalikuwa mbele ya macho yake:
“ Msiwaogope wale wauao mwili lakini
hawawezi kuiua roho. Afadhali zaidi kumwogopa yule awezaye kuuangamiza mwili
pamoja na roho..” (Matayo 5:28).
Makaburu
waliutesa mwili wa mzee Mandela, alifanyishwa kazi za
suluba,alidhalilishwa,alipokonywa uhuru wake,alinyimwa uhuru wa kuwa na familia
yake,alinyimwa uhuru wa mawasiliano, alipofiwa na mtoto wake wa kiume,
alinyimwa ruhusa ya kuhudhuria mazishi yake. Unyama wote aliofanyiwa akiwa
gerezani uliugusa na kuutesa kwa kiasi kikubwa mwili wake tu,lakini roho yake
ilibaki madhubuti. Alipochaguliwa kuwa Rais wa kwanza mwafrika wa Afrika ya
kusini huru, Mandela, alimshangaza kila mtu pale alipowakumbatia adui zake na
kukaa nao meza moja ya chakula. Hakulipiza kisasi! Unyama aliotendewa
gerezani,haukuigusa roho yake! Mzee Mandela, amekuwa mwalimu wa kuwafundisha
watu kuishi na kuyashika mafundisho magumu, mambo ambayo tumezoea kuyaita
ndoto.Watanzania tuna utamaduni wa kuogopa mwenye nguvu na uwezo wa kuua
mwili.Pia tuna utamaduni wa kulipa kisasi, wawe ni viongozi wa dini au viongozi
wa serikali,tabia hii ipo. Tujifunze kwa Mzee Mandela: Mwili unateswa,
unanyanyaswa na kudhalilishwa na mwanadamu, lakini roho ya ukweli, amani na
wema viko juu ya uwezo wa mwandamu! Hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kuiua roho
ya wema, hata kama mtu huyo angekuwa na nguvu za kidunia kama za Amerika!Pia
tujifunze kwamba ukipambana na mtu, ukimshinda, mnashikana mikono na
kukumbatiana – si kujenga chuki wala uhasama!
Watu wanaouona mwanga huu wameanza kugundua
kwamba yale tunayoita mafundisho magumu na ndoto yanawezekana, Mzee Mandela,
ametuonyesha mfano:
“ Mmesikia
kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino’. Lakini mimi nawaambieni,
usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia
shavu la pili..” (Matayo 5:38-39).
Haya ni mafundisho magumu ambayo yamewashinda
watu wengi hata na wale walioyafundisha na kuyaeneza. Hadi leo hii hata
viongozi wa dini bado mafundisho haya yanawapatia shida. Bado wanashikilia
‘Jicho kwa jicho, na jino kwa jino’. Migogoro inayowakumba viongozi wa dini inasababishwa na kutokubali kupigwa
shavu la kulia, na kugeuza la kushoto. Wakipigwa kofi, wanarudisha. Hii
inavuruga amani na kuleta magomvi yasiyoisha. Mandela, hakurudisha kofi!
Alisamehe! Mafundisho magumu yalikuwa mbele ya macho yake na roho yake
iliyoandaliwa kwa umakini na kwa miaka mingi haikuwa na uwezo wa kuyakwepa:
“Mmesikia
kwama ilisemwa: ‘Utampenda jirani yako,
lakini utamchukukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni,wapendeni maadui wenu
na kuwaombea wale wanaowadhulumu ninyi…” ( Matayo 5:43-44).
Tunakumbuka
jinsi Mzee Mandela, alivyowashauri wamarekani:
“Tumejifunza jinsi ya kuishi na maadui zetu, nanyinyi mjifunze kuishi na
maadui zenu..”
Tume
ya maridhiano ya Afrika ya Kusini, ilifanya kazi kwa uhuru na kumsikiliza kila
mtu. Haikuwa na upendeleo wala kukikumbatia chama tawala. Haki ilitendeka kwa
kila mwanachi na watu wote walifurahia kazi yake.Hizo zilikuwa mbinu za Mzee
Mandela, za kukumbatia mafundisho magumu ya kumpenda adui.
Mzee Mandela, alipompoteza mtoto wake wa kiume
kwa ugonjwa wa UKIMWI, kwa masikitiko makubwa(maana huyu ndo mtoto pekee wa
kiume aliyekuwa amebakia) alitangaza wazi mbele ya vyombo vya habari bila aibu
kwamba mtoto wake alikufa kutokana na ugonjwa wa UKIMWI. Hapa pia mafundisho
magumu ambayo roho yake haikuwa na uwezo wa kuyakwepa yalikuwa mbele ya macho
yake:
“ Jihadharini
na chachu ya Wafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa
kitafunuliwa, na kila siri itajulikana. Kwa hiyo, kila mlichosema
gizani, watu watakisikia katika mwanga, na kila mlichonong’ona,
faraghani,milango imefungwa,kitatangazwa juu ya nyumba.” (Luka 12:1-3).
Hili
limekuwa fundisho jingine kutoka kwa Mzee Mandela, la mafundisho magumu ambayo
wengi wetu na hasa Barani Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara, tumekuwa
tukidhani ni ndoto. Tumezoea kusikia watu mashuhuri wakifa kutokana na
shinikizo la damu,kisukari, ugonjwa wa muda mrefu na ugonjwa wa ghafla nk. Ni
nadra kusikia mtu mashuhuri amekufa kwa UKIMWI. Ugonjwa huu, umezungukwa na
unafiki mkubwa.Ndo maana ugonjwa huu umekuwa wa hatari katika nchi zetu hizi
masikini. Ugonjwa unafichwa na unafiki unaendelea kutawala.Hawa watu mashuhuri
wanaokufa kwa shinikizo la damu wanatoa mwanya wa wenzi wao kuendelea kusambaza
virusi vya UKIMWI, hakuna anayeshughulika kuchukua tahadhari maana shinikizo la
damu si ugonjwa wa kutisha kama UKIMWI!! Matokeo yake ni janga kama
tunavyoendelea kushuhudia. Ni lazima tumpongeze Mzee Mandela, kwa ujasiri wake
na tuendee kujifunza kutoka kwake.
Mzee
Mandela, alipougua ugonjwa wa saratani ya kibofu cha mkojo, alitangaza wazi.
Hakuficha ugonjwa wake.Alipatiwa matibabu, na sasa anaendelea kuishi! Hapa
Tanzania, tumewapoteza watu wengi kwa ugonjwa huu kwasababu ya aibu na unafiki!
Pia watu wanakufa kwa kuficha magonjwa ya zinaa yanayotibika kwasababu ya aibu
na unafiki. Magonjwa yakigusa sehemu za siri, watu wanakuwa na aibu.Aibu hii
inatokana na mawazo ya kulichukulia tendo la ngono kama la aibu. Ingawa kuna
ukweli kwamba si magonjwa yote yanayozishambulia sehemu za siri yanasababishwa
na tendo la ngono. Baadhi ya watu wakiugua sehemu za siri, wanataja
kichwa,tumbo na mgongo. Madaktari wanatibu kichwa,tumbo na mgongo, kumbe mgojwa
ana saratani ya kibofu cha mkojo au magonjwa mengine ya zinaa. Inapotokea
bahati ya kuugundua ugonjwa,mgonjwa anakuwa amezidiwa na kufa! Aibu na unafiki
vinasababisha vifo visivyokuwa vya lazima katika taifa letu na katika nchi
nyingine za Kiafrika.
Lengo
la makala hii ni kuonyesha jinsi tulivyo na mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa
Mzee Mandela. Bahati mbaya viongozi wetu wa dini na serikali ni woga.
Hatujapata viongozi wa kuyashika na kuyaiishi mafundisho magumu kama
alivyofanya Mzee Mandela. Hatujapata viongozi wasiogopa macho na masikio ya
watu, viongozi wasiojali kudhalilishwa na ikibidi kuupoteza uhai wao katika
harakati za kutetea ukweli na kupingana na unafiki.
Tunapojifunza
kutoka kwa Mzee Mandela, ni lazima tumwangalie yeye na historia yake. Si kwamba
misimamo yake hii ya kuishi na kuyashika mafundisho magumu, ilimnyeshea kama
mvua. Ni mtu aliyefanya maandalizi, ni
mtu aliyeitafuta elimu akiwa na malengo katika maisha yake – hakusoma tu kwa
vile kusoma ni lazima – hakusoma kuishinda maitihani, bali alisoma kwa vile
alikuwa na lengo la kuikomboa nchi yake. Lengo hili lilijaa kwenye roho
yake.
Hata ungeupiga na kuumiza mwili wake, usingeliligusa lengo lililokuwa kwenye
roho yake.Alijiandaa kwa maamuzi magumu –alijua jinsi njia ya kulifikia lengo
lake ni kupitia kwenye maamuzi magumu. Alijifunza na kujiandaa kulitanguliza
taifa lake kwa kila kitu. Hakuaangalia tumbo lake,cheo chake au biashara yake
(mambo ya mwili) aliangalia uhai wa taifa zima(mambo ya kiroho) . Mungu
amsaidie, hata uhai wake ukiondoka, tutaendelea kuishi na roho yake.
Na,
0 comments:
Post a Comment