TGNP NA MPANGO WA UTAFITI SHIRIKISHI WA URAGHABISHI.
Katika jitihada zake za kupambana na mfumo dume, uliberali mamboleo na
mifumo yote kandamizi na kupambana ili rasilmali ziwanufaishe wanawake walioko
Pembezoni, TGNP imeanzisha mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi. TGNP,
imeamua kuukumbatia mpango huu kwa vile unatoa nafasi pana ya ushirikishwaji
hadi ngazi ya vijijini na kuchochea kuibua kero na changamoto nyingi ambazo
zinahitaji majibu ya jamii nzima.
Mpango huu unatumika kama mbinu muhimu ya kujifunza, kutafakari, kuchambua
na kutekeleza mikakati mbali mbali ya ujenzi wa Tapo la ukombozi wa wanawake
kimapinduzi lililokita katika ngazi za msingi ya kijamii na lenye uwezo kwa
kudai uwajibikaji katika kutoa huduma bora, kusimamia rasilimali za taifa ili
ziwanufaishe makundi yaliyoko pembezoni hususani wanawake.
Lengo kuu na mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi ni kuwezesha
ushiriki wa wanawake, wanaume, makundi na mitandao katika ngazi ya jamii
kufanya uchambuzi wa hali halisi kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake
kimapinduzi; kuibua kero na changamoto zinazokabili makundi husika na za pamoja. Mpango huu pia unalenga katika
kukuza uwezo na uelewa wa uchambuzi wa
kero zinazoikabili jamii.
Tamko la TGNP kwa vyombo vya habari lilitolewa tarehe 9.6.2013 ni la mpango
huu ulioendeshwa kwenye wilaya tatu za Mbeya vijijini, kata ya Mshewe, Morogoro
vijijini Kisaki na Kishapu – Shinyanga. Katika makala hii tutajadili mrejesho
wa utafiti huu ambao ni wa aina yake.
Changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wananchi,
ilijitokeza katika utafiti huu na mfano mzuri ni Kata ya Mshewe Mbeya vijijini.
Katika kata hii utafiti ulibaini mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wawekezaji; ardhi
nzuri na yenye rutuba imetolewa kwa wawekezaji kiasi kwamba wenyeji hawana
mashamba na wanalazimika kuwa vibarua kwenye mashamba ya wawekezaji. Mbaya zaidi
ni kwamba wawekezaji wenyewe wanawalipa kidogo. Mfano wanawake wanalipwa kati
ya shilingi 2,500 hadi elfu3 kwa siku. Pamoja na kulikwa kidogo, wanakumbana na
rushwa ya ngono na manyanyaso mengine hali inayosababisha ongezeko la magonjwa
ambukikizi yakiwemo VVU na Ukimwi.
Changamoto hii ya mgawanyo mbaya wa ardhi imejitokeza pia katika kata ya
Kisaki, Morogoro mjini, ambapo wakulima wadogo wadogo wanapambana na wafugaji.
Kwa vile wafugaji hawana maeneo ya kutosha kwa mifugo yao, wanaingiza mifugo
kwenye mashamba ya wakulima na kuleta vita mbaya. Kwa upande mwingine wafugaji
wanatumia fedha kuwahonga viongozi ili wasisumbuliwe wanapoingiza mifugo kwenye
mashamba ya wakulima. Matumizi ya fedha ni kupokonya wanyonge haki zao ni
tatizo sugu kwa wananchi waishio pembezoni.
Suala jingine muhimu lililojitokeza kwenye utafiti huu wa TGNP kwenye
wilaya tatu, ni upatikanaji wa maji safi na salama. Pamoja na sera ya taifa
kwamba maji yawe umbali wa mita 400 kutoka kwa makazi ya watu, bado maeneo
mengi hapa Tanzania yana tatizo kubwa la kupata maji safi na salama. Watu wa
Kishapu na Mshewe, ni miongoni mwa
wananchi wa Tanzania ambao bado wana tatizo hili kubwa. Kijiji cha Ilota- Mshewe, wananchi wanalazimika
kuchangia maji machafu na mifugo. Tatizo hili la maji sai na salama ni kubwa
sana katika vijiji vya Isoso na Lubaga katika kata ya Kishappu, wanawake
wanatembea mwemdo mrefu na katika mazingira hatarishi kutafuta maji; mazingira
haya yanasababisha mimba za utotoni, ubakaji na vipigo kwa wanawake wakichelewa
kutoka kuchota maji. Na nyongeza ni kwamba muda mwingi na rasilmali vinatumika
kusaka maji kitu kinachoongeza hali ya umasikini katika jamii ya watu hawa
Kishapu.
Ukosefu wa huduma bora za afya ni suala jingine lililoibuliwa na mpango wa
utafiti shirikishi wa uraghabishi. Mfano kati
ya wanawake 20 walihojiwa katika kijiji cha Ilota, Mbeya vijijini ni
mwanamke mmoja tu ndiye aliyetaja kujifungulia hospitali. Umbali wa hospitali
na vituo vya afya unawalazimisha wanawake wengi kuzalia nyumbani kwa wakunga wa
jadi. Hii ni hatari kwa mama na mtoto na kuna ukweli wa wanawake wengi kupoteza
maisha wakati wa kujifungua na watoto kutopata huduma muhimu za chanjo wakiwa
na umri chini ya miaka 5.
Kata ya Kisaki Morogoro vijijini, tatizo si hospitali wala kituo cha afya,
tatizo ni dawa na wahudumu wa afya katika vijijini vya Gomero, Station na
Nyarutanga. Vijiji hivi vina majengo mazuri, lakini hakuna dawa na wahudumu.
Mbali na tatizo hilo, pia inapobidi wananchi wanachangia gari la wagonjwa
silingi 70,000, ili kumpeleka mama mja mzito kwenye hospitali ya Mkoa Morogoro
mjini. Hali hii ni hatari, maana wanawake wengi wanaweza kupoteza maisha yao
kwa kushindwa kulipia hizo shilingi elfu 70,000.
Ukiachia masuala hayo yaliyotajwa hapo juu, utafiti huu wa TGNP, ulibaini
kwamba tatizo la msingi ni uongozi mbovu na rushwa. Hili lilitajwa kila sehemu
iliyofanyiwa utafiti. Kwamba uongozi mbovu na rushwa vinasababisha ukosefu wa
huduma za msingi kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni. Na kwamba kuna
usiri wa taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi
katika masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono
na viongozi kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.
Ni mengi yaliyojitokeza kwenye utafiti huu, ila yametajwa machache ili
kufikisha ujumbe kwa wahusika, ili wajaribu kutafuta majibu ya kuondoa unyanyasaji
wa wanawake na wasichana katika wilaya hizi zilizotembelewa na watafiti wa TGNP
pamoja na maeneo mengine ndani ya taifa letu. Mfano tatizo la maji
linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za
utotoni na ukosefu wa kipato.
Serikali kuu na serikali za mitaa zinaweza kuyatumia matokeo ya utafiti huu
kurekebisha matatizo yaliyoorodheshwa hapo juu: Mfano serikali kuirejesha ardhi
ya Kata ya Mshewe inayomilikiwa na wawekezaji wa n nje na ndani ya nchi, kwa manufaa
ya wananchi sasa na vizazi vijavyo. Pia serikali itenge maeneo ya wafugaji
katika kata ya Kisaki, ili kuepesha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.
Huduma ya kupatikana maji safi na salama ishughulikiwe katika vijiji
vilivyotajwa na ambavyo havikutajwa. Utafiti huu umeonyesha wazi kwamba maji
safi na salama ni muhimu kwa watanzania wote. Huduma ya hospitali pia nayo
iboreshwe. Pia ni muhimu kuwepo na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wote
wanaokiuka maadili ya kazi zao ili kuondokana na aina zote za rusha na ukatili
wa kijinsia hasa ukatili kwa wanawake na wasichana.
Lakini pia viongozi wawakilishi hususan madiwani na wabunge wanaweza
kutumia matokeo ya utafiti kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika
ngazi zote kupita bajeti, ripoti ya mkaguzi wa serikali, kudai sera ya haki ya
uhuru wa wananchi na mikakati mbali mbali ya maendeleo.
Vyombo vya habari, taasisi za utafiti na makundi ya kiraia yanaweza pia
kuutumia mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi kuibua masuala ya
wanajamii na kujenga uwezo wa wanajamii kuhoji na kudai uwajibikaji. Hapana
shaka kwamba mpango huu wa utafiti shirikishi na uraghabishi ndio unafaa kabisa
kubainisha chanzo cha vurugu za Mtwara. Mpango huu unamruhusu kila mshiriki kuzungumza
bila kuogopa na kwa njia hii ya uraghabishi, watu wanajifunua na kujiweka wazi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment