MPANGO WA UHAMASISHAJI UWAZI KATIKA MAPATO YA MADINI,GESI ASILIA NA MAFUTA
UENDE MBALI ZAIDI!
Makala iliyopita katika safu hii, tuliwaelezea mpango wa TEITI hapa
Tanzania na faida zake. Maswali
yanayokuja kutoka kwa baadhi ya wasomaji wa gazeti hili, yanaonyesha
wazi kwamba mpango huu bado haujafahamika vizuri na wengi wanaonyesha
hawakufahamu kabisa kwamba kuna mpango kama huu napa kwetu Tanzania. Ni wazi
TEITI wana kazi ya ziada ya kuhakikisha taarifa zao zinasambazwa na
kufafanuliwa kwa wananchi. Ni jambo la
kujipongeza kwamba sasa kupitia mpango huu, kwa yeyote anayejali na kufuatilia
masuala ya mapato katika taifa letu,
anaweza kupata takwimu za uhakika juu ya mapato yanayotokana na madini, mafuta
na gesi asilia.
Ni wazi si kazi ya TEITI kufuatilia
fedha hizi zinazolipwa na makampuni ya uziduaji wa madini, mafuta na gesi
asilia zinatumika vipi? Zinanunua mashangingi na kulipia safari za viongozi nje
ya nchi? Zinatumika kulipia matibabu ya viongozi na vigogo wengine nje ya nchi?
Zinatumika kulipa posho za wabunge na viongozi wengine serikalini au zinatumika
kwa lengo la “Maisha bora kwa kila Mtanzania” na “Big results now”? Hii ni kazi
ya wabunge wetu, kufuatilia na kupiga kelele juu ya matumizi ya fedha hizi.
Hata na wananchi wenyewe baada ya kusoma na kuelewa taarifa hizi za TEITI wanaweza kuhoji na kuwashinikiza
wawakilishi wao, madiwani na wabunge kufuatilia kwa karibu matumizi ya mapato
haya yanayotokana na madini, mafuta na gesi asilia. Fedha hizi zitakuwa ninaingizwa kwenye mfuko
wa maendeleo kwa malengo ya kujenga barabara, kununua dawa, kulipia elimu ya
juu ya vijana wetu na kazi nyingine nyingi za kijamii. Je fedha hizi zinafika
kweli na kufanya kazi hizi? Pamoja na ukweli kwamba makampuni haya ya uziduaji yanatuibia
bado kuna ulazima wa kuhakikisha ukweli huu
na kuuelezea bila kuacha utata wa aina yoyote nyuma yake.
Ingawa bado kuna utata kwenye takwimu hizi ambazo TEITI wanatoa; makampuni yakionyesha kulipa zaidi, na
serikali ikionyesha kupokea pungufu, ni
masuala ambayo kwa ufuatiliaji wa karibu yanaweza kupata maelezo. Pia
utata mwingine, kwamba asilimia 99 ya mapato yote yatokanayo na madini, mafuta
na gesi asilia yanalipwa na makampuni 23, ni jambo ambalo bado linahitaji
maelezo ya kina. Ni kitu gani kinatokea kwa makampuni mengine zaidi ya 400
yaliyosajiliwa na yanafanya kazi ? Ni
kwamba hayapati faidia kabisa kiasi cha kushindwa kulipa kodi, au hayazalishi chochote?
Na kama hayazalishi chochote ni kwa nini yaendelee kuwepo?
Pamoja na mwanga unaotolewa na mpango huu wa TEITI ,bado kuna hoja kwamba
mpango huu ungeweza kwenda mbali zaidi. Hoja yenyewe ni kwamba, kwa nini
usifanywe ulinganifu wa faida wanayoipata
makampuni na kodi wanazozilipa? Madini,
mafuta na gesi asilia vinauzwa kwenye soko la dunia. Hivyo si kazi ngumu
kufahamu makampuni haya yanapata faida kiasi gani. Mfano ukiangalia bei ya
dhahabu kwenye soko la dunia, na ukaangalia kiasi cha dhahabu ambacho makampuni
haya yanaripoti kuchimba na kuuza nje ya nchi utapata takwimu kubwa ambayo bila
maelezo ya kina ni kana kwamba taifa letu linayapatia makampuni haya zawadi! Ukifanya
ulinganifu wa faida wanayoipata, baada ya kuondoa fedha za uendeshaji, ni kweli
inawiana na kile wanachokilipa?
Mfano sasa hivi ulinganifu uliofanyika kwenye taarifa tatu za TEITI,
unaonyesha wazi kabisa kiasi ambacho makampuni yanalipa. Na hii imewezekana kwa
makampuni na serikali kuonyesha risiti za malipo na vielelezo vingine. Hivyo
mawazo yaliyokuwepo kwamba makampuni haya hayalipi kabisa sasa haipo.
Kinachotakiwa sasa ni makampuni kuonyesha risiti za mauzo, risiti za uendeshaji
ili kubaini faida wanayoipata mwishoni ili kufanya ulinganifu wa kodi
zinazotolewa na faida inayopatikana. Ulinganifu huu ndio wenye tija kwa taifa
letu. Yawezekana pamoja na makampuni haya kulipa kodi, wanapata faida kubwa na
kutuachia mashimo na uharibifu wa mazingira.
Mpango huu wa kuhamasisha uwazi una uwajibikaji, unaweza kwenda mbali kiasi
cha kuwezesha mikataba ya uchimbaji
madini na uzinduaji wa mafuta na gesi asilia kuwekwa wazi? Maana swali la
kujiuliza ni lini makampuni haya yanapoanza kulipa kodi hizi serikalini? Kuna
taarifa kwamba kuna Resolute kule Nzega, ambao umekuwa ukichimba dhahabu kwa
kipindi cha miaka 16, ulianza kulipa
kodi miaka miwili ya mwisho. Pia kuna taarifa za kuaminika kwamba kuna migodi
ya kuchimba dhahabu ambayo itafikia mwisho wa kuchimba dhahabu bila kulipa
kodi, kwa kisingizio kwamba kwa miaka yote hiyo wamekuwa wakifanya hasara? Inashangaza
kuona kampuni inapata hasara na inaendelea kuwepo na kuchimba madini zaidi ya
miaka 16?
Kama hili ni kweli, kwa nini basi mango huu wa TEITI, usifanye utafiti ili
kubaini ukweli huu? Maana kama mtu anapata hasara kila mwaka, kwa nini aendelee
kuchimba au kutafuta mafuta na gesi
asilia kwa kipindi cha miaka kumi? Haya ni maswali ambayo watu wanajiuliza
kama ambavyo huko nyuma walikuwa wakilalamika kwamba tunaachiwa mashimo, wakati
makampuni yanalipa kodi. Ukweli huu umewekwa wazi na mpango wa TEITI. Hata kama
taarifa hii ya TEITI haijasambazwa kiasi cha kutosha, ukweli umejulikana na
hasa kwa wale walio kwenye ngazi ya kutoa maamuzi. Ndio maana ni muhimu pia kwa TEITI kutuweka
wazi juu ya hoja hii ya watu kuendelea kuchimba na kuendeleza shughuli za
uziduaji wakati wanafanyia hasara. Tunaposema TEITI waende mbele zaidi ya hapa
walipo tuna maana ya kufanya ulinganifu wa faida ya makampuni na kodi
wanazozilipa. Na pia kuhakikisha taarifa zao zinasambazwa kwa njia mbali mbali;
kwa radio, luninga, magazeti, semina na hata mashuleni.
Uelewa mpana, uwazi na uwajibikaji katika miradi ya madini, mafuta na gesi asilia utaliepushia taifa letu na balaa
itokanayo na miradi hii kama tunavyosikia kwenye nchi nyingine za Afrika.
Vurugu za gesi kule Mtwara ni dalili za balaa kubwa linaloweza kulikumba taifa
letu. Dawa pekee ni uwazi na uwajibikaji; hivyo mpango huu wa TEITI uwezeshwe
ili uweze kwenda mbali zaidi.
Na
Padri Privatus Karugendo
255 754 633122
0 comments:
Post a Comment