TEITI 1

MPANGO WA TEITI UTALETA UWAZI KWENYE MADINI, MAFUTA
NA GESI ASILIA AU NI MSAMIATI KAMA MINGINE?

Tanzania ni mabingwa wa misamiati na kauli mbiu, kama kigezo cha maendeleo kingekuwa ni hesabu ya misamiati na kauli mbiu, basi tungekuwa mstari wa mbele katika maendeleo. “Kilimo kwanza”, sasa imemezwa na “Big results now”. MKUKUTA, MKURABITA, Kasi Mpya, na maisha bora kwa kila Mtanzania ni nyimbo za kumbukizi!
Yawezekana mpango wa TEITI, utajiunga kwenye mlolongo huu wa nyimbo za kusadikika au ndo tunapiga hatua na kuanza utamaduni mpya? Utamaduni wa uwazi katika mipango ya matumizi ya rasilimali na kuhakikisha utajiri huu wa rasilimali unawanufaisha watanzania wote? Wakati watanzania wanalilia usiri kwenye mikataba ya madini na kilio cha Gesi asilia kule Mtwara, Tanzania imejiunga na Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya Madini, Gesi asilia na Mafuta (EITI) (Extractive Industries Transparency Initiative). Hivyo kwa Tanzania, mpango huu unajulikana kama TEITI( Tanzania Extractive Industries Transparency Initiative).
Mpango wa Uhamasishaji wa uwazi na Uwajibikaji Katika Tasnia ya Uziduaji (Asasi ya EITI) ulitangazwa mara ya kwanza kwenye Mkutano wa Dunia juu ya Maendeleo Endelevu uliofanyika Johannesburg, Afrika ya Kusini mnamo Mwaka 2002 na kuzinduliwa rasmi London Uingereza 2003. Nchi wanachama wa asasi hii ya kimataifa ya EITI hutakiwa kuweka wazi malipo ya kodi kutoka kampuni za uchimbaji wa madini, gesi asilia na mafuta; na mapato yanayopokelewa Serikalini. Kupitia taarifa hizi za malipo ya kodi  na mapato wananchi hushirikishwa katika usimamizi wa rasilimali hizi kwa kujadili na kutoa michango yao ili kuboresha sera na sheria kwa ajili ya kuongeza mapato.
Asasi hii ya EITI ilianzishwa kwa kutambua kwamba madini, mafuta na Gesi asilia vinaweza kuinua kipato na kuleta maendeleo duniani, lakini sehemu ambazo serikali ni dhaifu utajiri huu unaweza kuleta rushwa, ufisadi machafuko na kuleta ufukara kwa watu wengi. Hivyo kuwa na mpango wa uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika tasnia hii ya uziduaji wa madini, mafuta na gesi asilia ni muhimu sana.
Mnamo tarehe 18 Novemba, 2008, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa tamko kwa umma juu ya nia yake ya kujiunga na asasi ya EITI ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa sekta za madini, gesi asilia na mafuta. Katika mkutano wa nne wa EITI wa dunia uliofanyika tarehe 16 Februari, 2009 Doha, Qatar, Bodi ya EITI iliipatia Tanzania uanachama wa awali baada ya kukamilisha taratibu za kujiandikisha.
Utekelezaji wa EITI hapa nchini unasimamiwa na Kamati Tekelezi ambayo imeundwa na wajumbe 16 kutoka asasi za kiraia, kampuni na Serikali. Wajumbe watano kwa kila kikundi. Kamati hiyo huongozwa na mwenyekiti ambaye hatoki katika kundi lolote. Katika utendaji wa shughuli za kila siku, Kamati inasaidiwa na Sekretarieti.
Kama mpango huu utatekelezwa vizuri na kukwepa nyimbo za kusadikika, misamiati na Kauli mbiu nyingine nyingi tulizozizoea, utatusaidia kupiga hatua kubwa katika kusimamia utajiri wetu rasilimali zetu . Kulingana na kigezo cha IMF, nchi ambazo mchango wa sekta za madini, mafuta na gesi asilia katika pato la mwaka au mauzo ya nje hufikia asilimia 25, hutambulika kuwa ni nchi zenye utajiri wa mali asili. Hapa Tanzania mchango wa sekta ya madini pekee katika mauzo ya nje ni zaidi ya asilimia 25 ya mapato ya fedha za kigeni. Takwimu za miaka mitatu iliyopita zinaonesha mapato ya fedha za kigeni kutoka sekta ya madini ni asilimia 38.2 kwa mwaka 2007,  asilimia 34 kwa mwaka 2008 na asilimia 35 kwa mwaka 2009. Hivyo na sisi ni miongoni mwa nchi zenye utajiri wa mali asili;
Hivyo basi mpango huu wa TEITI unahitajika ili kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia kwa kuweka wazi malipo ya kodi kutoka kwenye makampuni ya uziduaji na mapato yaliyopokelewa serikalini. Kuongeza ufahamu kwa umma kwa kuchapisha malipo na mapato yatokanayo na madini, mafuta na gesi asilia, hivyo kuongeza ushiriki wao katika usimamizi wa sekta za madini, mafuta na gesi asilia.
Mpango huu pia utaisaidia serikali na wadau kupata taarifa sahihi na kwa wakati za malipo na mapato yanayotokana na shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asilia. Uwazi katika taarifa za malipo na mapato ni msingi mzuri wa kuboresha usimamizi na utawala bora katika tasnia ya uziduaji.
Sasa hivi, watanzania wanalalamika kwamba makampuni ya madini, mafuta na gesi asilia wanawaibia. Mtwara, kila mwananchi anasema “gesi” haitoki! Wanalalamika kwamba utajiri wao utaibiwa na kupelekwa sehemu nyingine. Lakini hakuna anayeweza kusema kwa uhakika ni kiasi gani cha fedha tunaibiwa. Mpango huu wa TEITI, unawataka makampuni na serikali kuweka malipo wazi; Makampuni yaonyeshe yamelipa kodi kiasi gani na serikali ionyeshe imepokea kiasi gani. Kwa kufanya ulinganifu wa mapato na kodi, tunaweza kupata msingi mzuri wa kujenga hoja ya kuibiwa na wawekezaji au kuibiwa na serikali. Tunaweza kuwa na msingi wa kuiwajibisha serikali na kuuliza maswali yenye kuhitaji majibu ya uhakika.
Hadi leo hii ninapoandika makala hii, TEITI, imetoa taarifa tatu za malipo ya kodi, mrabaha na tozo kutoka kampuni za uchimbaji madini na gesi asilia. Katika makala hii nitajadili taarifa ya pili ya mwaka wa fedha 2009/10
Pamoja na mambo mengine mengi, taarifa ya ulinganisho ya TEITI, inaonyesha kwa mwaka wa fedha wa 2009/10 kampuni zililipa kiasi cha shilingi 424 bilioni ikilinganishwa na mapato ya shilingi 419 bilioni yaliyopokelewa serikalini. Matokeo hayo yanaonyesha tofauti ya malipo na mapato kwa kiasi cha shilingi bilioni 5. Hii ni sawa na asilimia 1 ya jumla ya mapato yaliyopokekewa na serikali katika kipindi hicho.
La kuzingatia hapa ni kwamba makampuni yaliyofanyiwa ulinganifu, ni yale yenye uwezo wa kulipa kodi zaidi ya shilingi milioni 200, kwa mwaka wa fedha wa serikali, makampuni 23, kati ya makampuni zaidi ya 400, ndo yalitimiza kigezo hicho.
Kwa taarifa hizi za TEITI, tunaweza kufahamu ni makampuni gani yanalipa kodi na yanalipa kiasi gani. Tunaweza kufahamu serikali inapata kiasi gani. Mfano taarifa ya pili ya TEITI, inaonyesha makampuni yalilipa kiasi kikubwa, lakini serikali inaoyesha imepokea pungufu. Nani anasema uongo? Serikali au makampuni? Tunaweza kujadili kwa uhakika, bila kulalamika tunaibiwa, wakati hatuna takwimu.
Pamoja na changamoto nyingine ambazo TEITI, inakumbana nazo ni kwamba kwa sasa Tanzania haina sheria ya TEITI. Ni vigumu kuwafanya wadau washiriki katika zoezi la ulinganisho kwa hiari bila kuhimizwa. Kwa Ulinganisho wa taarifa ya pili kwa mfano,  baadhi ya kampuni hazikuweza kuwasilisha fomu za takwimu walipoombwa kufanya hivyo, na wengine walioweza kuwasilisha fomu za takwimu walishindwa kukidhi masharti yote. Bila kuwepo sheria inakuwa vigumu kuwahimiza.
Changamoto nyingine kubwa ni mpango huu kufahamika kwa wananchi. Hadi leo hii ni watanzania wangapi wanafahamu kwamba kuna mpango wa TEITI? Ni watanzania wangapi wamesikia au kuona taarifa za TEITI juu ya ulinganisho wa kodi na mapato kutoka kampuni za uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia? Kulingana na umuhimu wa TEITI ni muhimu, wananchi kushiriki kwa kiasi kikubwa. Kamati tekelezi ambayo ina wajumbe 5 kutoka kwenye asasi za kirai, ni muhimu kuundwa kwa kufuata ushirikishwaji. Wachaguliwe kidemokrasia na si kuingia kwenye kamati kwa vile mtu ana asasi. Mara nyingi Asasi za kiraia zinaanzishwa na baadhi ya watu, bila kuwa na ushirikishwaji mkubwa kwenye jamii. Si mara zote Asasi kuwakilisha matakwa ya jamii nzima. Suala la utajiri wa madini, mafuta na gesi asilia ni la jamii nzima, hivyo linahitaji uwakilishi mpana. Ni muhimu kwenye kamati hii  waingie watu wanaoguswa na maendeleo ya taifa letu. Bila kuwa na Kamati tekelezi yenye upeo na msimamo imara, mpango wa TEITI, utakuwa ni miongoni mwa nyimbo za kusadikika tulizozizoea.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22.
pkarugendo@yahoo.com

0 comments:

Post a Comment