MWANA MAMA MCHUNGAJI SAFINA MARIA MAGDALENA JESUS.
Leo katika safu yetu ya Mwana Mama, tunawaletea Mchungaji Safina Jesus. Yeye
mwenyewe, anapenda ajulikane kwa jina lake kamili ambalo ni: Mchungaji Safina
Maria Magdalena Victoria Jesus. Waliomfahamu siku za nyuma na hata alipokuwa
akiishi na kufanya kazi nchini Uingereza, walimfahamu kwa jina la Safina
Yussaph Haruna. Ni mwana mama aliyekulia kwenye imani ya Ukatoliki, akaingia
kwenye imani ya Uislamu na hatimaye
kupokea wito wa kuwa mchungaji na kupokea kipaji cha uponyaji mwaka 2011, akiwa
nchini Uingereza. Kwa ufupi ni kwamba ni mama aliyeonja imani zote, Ukristu wa
dhehebu mbali mbali na Uislamu.
Hapana shaka kwamba uzoefu wake wa imani hizi zote ndo unamsukuma kuwa na
hamu na shauku la kuanzisha nyumba ya ibada, kanisa la watu wote; wenye imani
tofauti, maoni tofauti lakini wenye nia na lengo la kujenga jumuiya yenye
mshikamano na upendo. Jumuiya yenye maendeleo na heshima kwa binadamu wote bila
ubaguzi wa aina yoyote ile.
Mbali na mvuto wa mama huyu kwenye huduma ya uchungaji na uponyaji, ni
mapenzi yake kwa watoto yatima. Amejipanga kufungua kituo cha watoto yatima
kule Kigamboni, ili watoto hawa wapate elimu ya kuwasaidia kuacha kuzurura
mitaani na kuomba omba. Yeye ana imani kwamba haitoshi kumsaidia mtoto Yatima
chakula na nguo, maana mahitaji ya kila siku ni lazima yaendelee maisha yake
yote; hivyo ni lazima kumsaidia mtoto yatima ili aweze kujisaidia mwenyewe.
KITUO cha watoto yatima kinatarajiwa kujengwa jijini Dar es Salaam
ambacho kitachukua watoto zaidi ya 1000 na kwamba watoto hao watapewa elimu ya
ufundi kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya kujitegemea na kuachana na
kuombaomba
“Watoto
watajifunza kupitia walimu waliobobea ili kuweza kuwa chachu ya kujiajiri
baada ya umri wa kujitegemea na kuongeza nguvu kazi ya taifa. Hatuwezi
kuendelea kuhubiri injili wakati watoto wako mitaani, hivyo lazima tuwe na njia
mbadala za kuweza kusaidia taifa hili ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya
watoto yatima ambao watapata elimu ya kiroho na elimu ya kujitegemea kwa kuwa
na ujuzi,” alisema Safina .
Pia anasema alipokuwa nchini Uingereza kiu yake ilikuwa inamtuma
kufanya jambo linalohusiana na watoto akiwa nchini Tanzania kwa kujenga kituo
ambacho kitakuwa sehemu ya chuo kwa ajili ya watoto yatima na mitaani kupata
elimu ya ujuzi mbalimbali.
Mwana mama huyu alizaliwa Iringa mnamo
mwaka 1979, Baba yake anatokea Iringa, wakati mama yake anatokea Bukoba. Baada
ya masomo yake, alifanya kazi kwenye jiji la Dar-es-Salaam na hasa kwenye sekta
ya mahoteli. Baadaye alihamia nchini Uingereza na kuishi kwenye bonde la Bevois
na kufanya kazi Bexhill,East Sussex kwenye kanisa la Mtakatifu Barnabas. Ni
wakati huo alipoitwa kumtumika Bwana Yesu.
Mama huyu, alipata daraja la uchungaji
kutoka kwa Mheshimiwa sana Askofu Mkuu Richard Palmer, wa Episcopal Free Church
ya Southampton. Na baada ya kumpatia daraja hilo Askofu Mkuu huyo alisema hivi
juu ya Mama huyu: “ Nafurahi sana kuwa na mchungaji huyu kama mtumishi,
nafikiri atakuwa mzuri sana, ni mtu aliyejitoa kwa moyo wake wote kwa huduma
hii”.
Lengo la mama huyu hapa Tanzania, ni
kujenga uhusiano kati ya Kanisa la Mtakatifu Barnabas na Tanzania; kuamusha
imani ya kumpenda na kumtumikia bwana Yesu Kristu kwa matendo. Pia ana ndoto za
kupanua huduma hii kwenye nchi mbali mbali za Afrika na popote pale ambapo roho
mtakatifu atamwelekeza.
Wakati anajiandaa kupata sehemu ya
kujenga nyumba ya Ibada, anaendelea kusali na kuhubiri kwenye nyumba yake
maeneo ya Kimara. Anawakaribisha watu wa imani zote, maana lengo lake kubwa ni
kuijenga jumuiya ya watoto wa Mungu, wanaokutana kusali pamoja na kushirikiana
kujenga jumuiya yenye amani na maendeleo.
Mama huyu anapinga mwenendo wa Mashoga
na wasagaji; anapinga kwa nguvu zote watu wanaokubali na kukumbatia utamaduni
huu, pia anapinga kwa nguvu zote wanaowalaani na kuwatenga mashoga na
wasagaji. Msimamo wake ni kwamba watu
hawa pia wanahitaji huruma ya mwenyezi Mungu. Kazi ya jamii si kuwatenga watu
hawa na kuwalaani, bali ni kwasikiliza, kusali nao na kutafuta njia ya kuwasaidia
na kuwabadilisha. Anatoa ushuhuda wa kuwasaidia baadhi ya watu hawa na sasa
wameachana na tabia hiyo. Hivyo nyumba yake ya ibada inawakaribisha wa watu wa
aina zote.
Pia Mama huyu ni miongoni mwa
wanaoamini kwamba Bwana Yesu, aliliacha kanisa lake mikononi mwa Mwanamke,
yaani Maria Magdalena. Biblia inaeleza vizuri kwamba Maria Magdalena, ndiye
aliyesifiwa na Bwana Yesu, kuyafahamu mafundisho yake na kuyashika. Ingawa
baadaye mfumo dume, uliingia kanisani mnamo mwaka 321 ukiongozwa na Mfalme
Constatine wa himaya ya Warumi, na kubadilisha ukweli wote wa kanisa kuachwa
mikononi mwa mwanamke. Hivyo anawahimiza wanawake popote walipo kujitokeza
kuliongoza kanisa. Wanawake kujitokeza kupokea huduma ya uchungaji na utumishi.
Mambo manne yanamtofautisha mama huyu
na wachungaji wengi tuliowazoea: Kwanza ni mtizamo wake juu ya watoto Yatima;
lengo lake la kuwasaidia watoto yatima ili baadaye wajisaidie wenyewe ni
tofauti na nyumba za watoto yatima tulizozizoea za kuwapatia chakula, malazi,
matibabu na wakati mwingine masomo, bila mpango mzima wa kuwaandalia maisha ya
baadaye.
Pili, msimamo wake juu ya mashoga na
wasagaji ni tofauti kabisa na kauli nyingine ambazo tumezizoea na kuzisikia.
Hili la kuwapokea, kuwasikiliza na kuwasaidia kubadilika ni jipya kabisa na ni
jambo zuri na la kuungwa mkono na wanaharakati wote wa kutetea haki za
binadamu.
Tatu; mpango wake wa kuwashirikisha
watu wote wa imani mbali mbali, kusali pamoja na kufanya kazi pamoja, ni muhimu
sana hasa wakati huu ambapo dalili za kutoelewana miongoni mwa imani mbali
mbali hapa chini linaanza kujitokeza.
Nne, imani yake kwamba Kanisa liliachwa
kwenye Uongozi wa mwanamke, ni jambo linalomtofautisha Mwana mama huyu na
wachungaji wengine tuliowazoea. Hivyo huyu ni Mwana mama wa mfano kwetu sote.
Huyo ndiye Mchungaji Safina Maria Magdalena Victoria Jesus.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment