SURA YA URAIS INAFANA VIPI NA UWAZIRI JE?
Kama maneno haya yangetamkwa na mtu ninayemdharau, mtu ambaye si mzalendo
na akili yake ina kasoro kidogo, nisingepoteza muda wangu kuandika. Kwa vile ni
maneno haya yalitamkwa na mtu
ninayemheshimu, tena kijana msomi, ni lazima niandike na kukaripia kwa nguvu
zangu zote. Waswahili wanasema tusipoziba ufa tutajenga ukuta. Na kwamba rafiki
wa kweli ni yule anayekueleza ukweli. Rafiki mbaya ni yule mnafiki anayekusifia
wakati akijua anakudanganya. Labda nianze na swali: Sura ya “Urais” inafanana
vipi na sura ya “Uwaziri” inafanana vipi? Je urais ni mashindano ya urembo?
Tunaongozwa na sura au tunaongozwa na akili, hekima na busara? Rais wa Kenya,
Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, alipoulizwa akienda kwenye mahakama kule Holland,
nchi ataiongozwa vipi, alijibu kwamba kuna twiter. Je tunahitaji sura ipi ya
kutumia twiter? Au tunahitaji sura ipi ya kuweka misingi ya utawala bora,
demokrasia na kufuata katiba ya nchi? Ni sura ya namna gani hiyo?
Mheshimiwa Januari Makamba, amesikika akiwahutubia vijana wa CCM kule Misenyi
Kagera kwamba, CCM, bado ina nafasi kubwa ya kuliongoza taifa letu, maana
akiangaza kwenye vyama vya upinzani haoni mtu yeyote mwenye sura ya Urais na
hakuna mtu mwenye sura ya uwaziri. Kwamba vyama vya upinzani ni wanaharakati
tu! Hakuna historia ya wanaharakati kuongoza nchi?
Ninajua kwamba Januari ni kada wa chama cha Mapinduzi, na yuko kwenye uongozi
wa juu kwenye chama chake hicho, lakini sikutegemea kama angeweza kutoa
matamshi kama haya ambayo yanaturudisha nyuma kabisa wakati wa utawala wa
kifalme. Enzi ambazo uongozi ulitegemea familia na damu ya watu wateule. Hata
kama ungekuwa na akili za kupindukia, bila kuzaliwa kwenye ukoo wa kifalme
usingepata nafasi ya uongozi. Lakini leo hii wakati wa demokrasi, wakati wa
vyama vingi, wakati wa kuwaingiza viongozi madarakani kwa kura, mtu anaweza
kuongea juu ya sura ya Urais na sura ya uwaziri? Huku ni kwenda mbele au ni
kurudi nyuma? Haya ni maneno ya kutamkwa na kijana au mzee ambaye anakaribia
kumaliza maisha yake hapa duniani?
Tunaweza kusema kwamba labda Mheshimiwa Makamba, alikuwa anatoa vijembe vya
kisiasa. Hili linawezekana na wala sina matatizo yoyote , lakini si Makamba,
tunayemfahamu. Tunamfahamu Januari Makamba, mtu mwenye busara na hekima, mtu
anayepima kila neno analotaka kusema. Mtu ambaye zaidi ya miaka minne, alikuwa
msaidizi wa Mheshimiwa Rais Jakaya
Kikwete, akiandaa hotuba zake. Huyu si mtu wa kuropoka tu, ni mtu makini.
Vijembe kama vijembe, sina matatizo navyo. Angesema haoni mtu mwenye uwezo
wa kuongoza nchi kwenye vyama vya upinzani, tungecheka tu na kufurahia
vijembe vyake, maana baada ya hotuba
yake tungempelekea orodha ndefu ya watanzania wenye uwezo mkubwa kuongoza ambao
si wanachama wa CCM, tungempelekea orodha ndefu ya watu wenye busara, hekima na
kipaji cha hali ya juu kuongoza hata kwa viwango vya kimataifa. Tatizo langu
kubwa ni pale anaposema, upande wa wapinzani haoni mtu mwenye “Sura” ya “Urais”
na mwenye “Sura” ya “Uwaziri”. Sura hizi nzuri ziko CCM. Hizi ni sura gani?
Maana kama hizo “sura” zinaendana na uongozi, basi Tanzania tungekuwa mbali;
tusingekuwa na ufisadi wa kutisha; wimbo wa ufisadi hata mtoto aliyezaliwa leo
anaufahamu, hivyo si lazima kutoa mifano
Mtu, tunayemheshimu kama Januari Makamba, akiacha kuona matatizo ya taifa
letu, akaacha kuona changamoto ya Katiba, changamoto ya muungano wetu,
changamoto ya kufuata na kutekeleza mfumo wa demokrasia katika taifa letu,
changamoto ya kuondoa umaskini, changamoto ya kupambana na rushwa na ufisadi,
changamoto ya kupambana na bidhaa bandia, changamoto ya kupambana na madawa ya
kulevya, changamoto ya kuondoa msemo wa “ Tutawasaka popote walipo na
kuwafikisha mbele ya sheria”: Tulisikia hivyo kwa Ulimboka, Kibanda, Mwangosi,
Kamanda Barlow, Mabomu ya Arusha, Mauaji
ya Padri wa Zanzibar na Sasa wasichana Wazungu wamemwagiwa tindikali. Hakuna
anayekamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.. ni misemo ya kutowajibika! “Tutawasaka
popote walipo na kuwafikisha mbele ya sheria”. Badala ya kupambana na kutowajibika na uzembe mwingine
katika taifa letu, Januari Makamba, anatwambia “Sura”. Sura inaweza kupambana
na changamoto zote hizo hapo juu?
Uongozi ni mashindano ya urembo? Kwamba mtu kabla ya kugombea ahakikishe
anajipamba na kujiremba, kujifunza namna ya kutembea na kuongea kwa madaha?
Uongozi unategemea sura ya mtu? Kwamba awe na sura nzuri? Kusema kwamba vyama
vya upinzani havina mtu mwenye sura ya urais, maana yake hakuna mwenye sura
nzuri au sura ya urais inafanana vipi? Uongozi ni sura au ni akili, busara na
hekima? Uongozi ni mtu kuwa na fikra pevu au kuwa na sura ya kuvutia?
Tanzania, sasa hivi iko njia panda na tunapita kwenye kipindi cha mpito. Ni
wakati ambapo tunahitaji kiongozi mwenye upeo mkubwa, kiongozi mwenye akili
nzuri, kiongozi ambaye hafungamani na upande
wowote ule, kiongozi ambaye hafungamani na imani za kidini, kiongozi ambaye
hafungamani na “Upuuzi” wa ushabiki wa vyama vya siasa. Tunahitaji kiongozi
aliyejikomboa kutoka kwenye minyororo ya ukabila na ukanda. Tunahitaji kiongozi
anayeangalia Tanzania kwa umoja wake; kiongozi mzalendo anayeheshimu haki za
binadamu na usawa wa kijinsia. Tunahitaji Kiongozi anayeguswa na matatizo ya
watanzania wote. Nina mashaka makubwa kama sifa hizo hapo juu zinaendana na
sura ya mtu.
Ubaguzi wa hatari kubwa katika dunia yetu hii, ni kuwadhamini watu kwa
kuangalia sura zao, kuangalia rangi ya ngozi, kuangalia pua na nywele, ufupi na
urefu, unene na wembamba. Leo hii utasema hawana sura ya urais, kesho utasema
hawana sura ya “utanzania”, kesho kutwa utasema hawana sura “ukabila” na hasa
kabila lako. Na mwisho utasema hawa si wenzetu! Na matokeo yake ni mapambano ya
kutisha ambayo sina haja ya kutoa mifano, maana sote tunaifahamu. Ubaguzi wa
sura ni hatari na si wa kushabikia. Kama Mheshimiwa Januari Makamba, ni
muungwana na analitakia taifa letu mema, asimame na kuomba msamaha kwamba
maneno yale kule Misenyi, alimponyoka na ulimi uliteleza. Tutaelewa na
kumsamehe, vinginevyo anajiweka kwenye kapu la watu wa kuogopwa katika taifa
letu.
Mategemeo makubwa ya taifa letu ni vijana wetu. Lakini kama vijana wenyewe
wanaanza kuchanganyikiwa kiasi cha kuchanganya uongozi na sura, badala ya
kuuona mnyororo wa uongozi ambao ni akili, hekima, busara na uzalendo, ni hali
ya hatari. Ni lazima sote kwa pamoja kushirikiana kuliokoa taifa letu,
tukiendeleza ushabiki wa “Kipuuzi” na kuendelea kuamini kwamba kuna watu
wateule waliozaliwa kuongoza au kuishi maisha bora zaidi ya wengine,
tutaliangamiza taifa letu badala ya kuliokoa.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment