NI YESU WA WAPI?

JE,NI  YESU WA NAZARETI , WA ULAYA AU WA NAGERIA?

Jana usiku (31.8.2013) nilikuwa uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nilikuwa napokea mgeni kutoka Ujerumani. Wakati tukisubiri ndege kuwasili, niliona kundi la watu wamevaa T-shirt zenye maneno  “Karibu Mchungaji  Ma, uione Tanzania”. Walikuwa wakimsubiri mgeni wao kwa hamu. Nilitaka kufahamu huyo mchungani anayesubiriwa hivyo ni nani? Nikaambiwa ni mchungaji wa Kanisa... nimesahau jina la kanisa, ametumwa kutoka Nigeria, kuja hapa Tanzania kuhubiri neno la Mungu na kuimarisha “Ukristu”. Alikuwa anahamia hapa na familia yake. Sina uhakika ni makanisa mangapi hapa Tanzania yanaendeshwa na wachungaji kutoka Nigeria; mengine makubwa, na wana makanisa makubwa pia,  mengine madogo, wanasalia kwenye kumbi za starehe, mfano hawa niliokutana nao uwanja wa ndege wanasalia kwenye kumbi za Sunset Mbezi Makonde. Ni wazi hizi zote ni harakati za kupambana na matatizo yanayotuzunguka.
Nilichojiuliza usiku ule, baada ya kuona wamisionari hawa wa Nigeria, ni je hawa wanakuja kuleta Neno la Mungu, au ni wawekezaji kama wengine wanaokuja kuwekeza na kuchota kila kitu? Wanigeria wanaogopwa dunia nzima kwa tabia zao za ujanja na udanganyifu. Labda hawa wachungaji  “wameokoka”? Fedha zinazokusanywa kwenye makanisa haya zinajenga Ufalme wa Mungu, au zinachangia kuongeza matatizo yanayotuzunguka?
Mbele yetu kuna hitaji muhimu na la haraka. Ni hitaji la kutafuta mfumo wa kupambana na matatizo yanayomzunguka mwanadamu wa leo. Mamilioni ya watu wanaishi kwenye mateso kila siku ya Mungu. Kuna njaa, vita, umasikini, upweke, magonjwa, uonevu, ubaguzi nk. Hapa Tanzania, watu wanakufa kwa UKIMWI, malaria na magonjwa mengine yanayotibika. Ujambazi, ufisadi, rushwa na kutowajibika vinasambaratisha uchumi wetu. Namba ya wajane na wagane inaongeza kwa kasi, watoto yatima, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi inaongezeka kwa kasi ya kutisha. Tufanye nini kuondokana na mateso na mambo mengine yanayotishia uhai wa mwanadamu na hasa Mtanzania. Je, huyu Yesu wa Nazareti, Ulaya na Nigeria, anaweza kuwa jibu? Anaweza kutusaidia kutengeneza mfumo wa kupambana na matatizo yetu? Tunaweza kumgeukia? Tunaweza kumkimbilia? Anaweza kutulinda? Anaweza kutusaidia? Anaweza kutuwezesha? Anaweza kututoa usingizini? Anaweza kutupatia mwanga wa Hekima na Busara, ili tuyatawale mazingira yetu na kuyalazimisha yatutumikie? Je wote wanaomfuata Yesu wa Nazareti, wa Ulaya na Nigeria, wamekuwa wakivutiwa na mfumo wake wa kupambana na matatizo ya dunia yetu? Au wanavutiwa na mambo mengine ambayo si muhimu sana katika kusaidia maisha ya binadamu? Je, wanapambana na matatizo au wanayakimbia na kujifanya hawayaoni?
Wanaojiunga na  makanisa haya ya Kinigeria, wanavutiwa na neno la Mungu au miujiza ya uponyaji na utajiri usiokuwa na maelezo? Taarifa za kuaminika ni kwamba kila anayejiunga na makanisa haya ni lazima awe tajiri. Atamiliki magari, manyumba na utajiri mwingine mkubwa. Waumini wanavutiwa na mali au Neno la Mungu?

Mamilioni ya watu kwa miaka mingi wamekuwa wakilitaja jina la Yesu na kumwabudu, lakini wachache kati ya mamilioni ndiyo waliomwelewa Kristu na namba chache kabisa ndiyo waliofuasa kile alichokitaka kitendeke. Maneno ya Yesu Kristu, yamebadilishwa na kupindishwa ili yatekeleze kile watu wanachokitaka, na wakati mwingine maneno yake yamebadilishwa na kupindishwa yasimaanishe kitu chochote! Jina la Yesu, limetumiwa kubariki maovu ya kila aina, kama wale waliokuwa wakiongoza vita na kuuwa watu huku wakitanguliza msalaba na Biblia. Latin Amerika, mamilioni ya watu walipoteza maisha yao na sehemu nyingine kizazi kilifutika kabisa katika harakati za kueneza neno na mafundisho ya Yesu Kristu. Lakini pia jina la Yesu, limetumiwa kuwashawishi na kuwaletea imani kubwa wanaume na wanawake wengi hata kufikia hatua ya kupumbazika na kufanya matendo ya kijinga, kama kujinyima chakula na kuitesa miili yao kufikia kiwango cha uwendawazimu. Yesu amekuwa akitukuzwa na kuabudiwa kwa yale ambayo hakuyalenga, yale aliyo yapinga na kuyakemea kuliko yale aliyoyalenga, aliyoyahubiri, aliyoyatetea na kuyafia. Jambo la kushangaza ni kwamba mambo ambayo Yesu, aliyapinga wakati wa uhai wake, yalifufuliwa, yalihubiriwa na kusambazwa dunia nzima kwa jina lake.

Hatuwezi kumuunganisha moja kwa moja Yesu wa Nazareti na hii dini kubwa ya Kizungu, inayojulikana kama Ukristu. Yeye alikuwa mwanzilishi wa dini kubwa zaidi ya hii tunayoifahamu. Yeye  anasimama juu ya Ukristu na kutoa hukumu juu yale yote dini hii imeyafanya kwa jina lake. Hata hivyo Ukristu, hauwezi kudai mumiliki Yesu Kristu, maana mtu huyu alikuwa ni wa binadamu wote.

Je, hii ina maana kwamba kila binadamu (Mkristu na asiyekuwa Mkristu) ana uhuru wa kumtafsiri Kristu katika maisha yake jinsi anavyotaka? Inawezekana kabisa kila mtu akamtumia Kristu anavyotaka kwa mabaya na mazuri? Lakini yeye alikuwa ni mtu aliyekuwa na imani nzito ambayo alikuwa tayari kuifia. Je, hakuna namna ya watu, wenye imani na wasiokuwa na imani kumpatia nafasi takika maisha yao Yesu huyu wa Nazareti, akazungumza yeye mwenyewe kwenye mioyo yao? Je, hakuna namna ya watu kulinganisha matatizo yao, nyakati zao na zile za Yesu wa Nazareti?
Tishio lililopo leo si la mtu binafsi, kabila, taifa au bara. Tishio ni la dunia nzima, ni tishio la ubinadamu. Tumefika mahali tunachanganyikiwa na kufikiri kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuzuia tishio la kuumaliza ulimwengu na binadamu. Wapo vichaa kama Kibwetere na wajinga wengine wanaofikiri kwamba mwisho wa dunia na ubinadamu vinashuka kwa miujiza, kwamba tunaweza kulala na kuamka tunakuta dunia imekwisha. Huu ni ujinga mtupu! Mwisho wa dunia, unaletwa na matendo ya binadamu ya muda mrefu. Matendo ya ubinafsi yasiyozingatia umuhimu wa binadamu na viumbe vingine, yanaweza kupelekea mwisho wa dunia. Hili si jambo la kutokea leo ama kesho, lakini mtu anayejali ni lazima kuhakikisha anarithisha dunia hii kwa vizazi vijavyo. Tunakata tamaa kwamba hakuna tena mfumo mzuri wa maisha unaowafaa binadamu wote. Mfumo wa kuweza kuangalia na kutengeneza maisha bora ya mwanadamu wa leo na kesho.

Siku za nyuma kidogo tulifikiri labda silaha za nyukilia zingeweza kutumika kuteketeza ulimwengu. Tumeanza kupunguza woga huu, lakini mambo mengine mengi kama vile uharibifu mazingira, uchimbaji ovyo wa madini, upungufu wa chakula na ardhi nzuri ya kustawishia chakula, hatari ya kupungua kwa maji na ongezeko la binadamu, ni vitisho vipya kwa uhai wetu na ulimwengu tunamoishi. Ukweli kwamba binadamu wanaongezeka kwa kiasi cha milioni 80 kwa mwaka, ni tishio  kwamba kwa miaka michache ijayo, matumizi ya maji na chakula yatakuwa katika hali mbaya duniani kote. Ukweli kwamba magazeti, vitabu na utengenezaji wa karatasi za kuandikia unaitafuna misitu ni tishio la uharibifu wa mazingira katika enzi hizi tulizomo.
Kuna uharibifu mkubwa katika kila biashara zinazofanywa kwa lengo la kupata faida. Kila mtu analenga kupata faida bila kuangalia matokeo ya vitendo vyake. Viwanda vingi vimekuwa vikiharibu mazingira kwa moshi unaotoka viwandani, lakini pia uchafu unaotiririshwa kutoka viwandani kwenda mitoni na kwenye maziwa na bahari umechangia uharibifu mkubwa wa viumbe katika maji. Ni wazi ili tupone, panahitajika mabadiliko makubwa. Swali ni je ni nani atakubali  hasara ya kusimamisha viwanda vyake?
Inakuwa ngumu kuwashawishi watu kubadili mtido wa maisha, ili kurefusha maisha yao wenyewe, inakuwa ngumu zaidi kuwashawishi kufanya hivyo ili kuyarefusha maisha ya watu wengine. Inakuwa ngumu zaidi na zaidi kuwaambia kufanya hivyo kwa lengo la kunusuru maisha ya mabilioni ambao bado hawajazaliwa; kuicha dunia yetu ikiwa salama kwa vizazi na vizazi. Sisi tuliikuta salama, ni jukumu letu kuiacha ikiwa salama.
Kuna ukweli kwamba dunia hii ina  baadhi ya watu, wake kwa waume wenye nia njema, na wanayaona matatizo yote hayo na wangependa kufanya chochote kuleta mabadiliko. Daima wanaonyesha nia yao njema na wengine wako tayari hata kuyapoteza maisha yao ili kufanikisha kuleta mabadiliko. Lakini wanaweza  kufanya nini? Mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache kinaweza kufanya nini kwenye matatizo haya ya Ulimwengu wa kisasa? Kilicho mbele yetu ni kitu kikubwa, ni mifumo ya dunia hii iliyojikita na kustawi! Ni mifumo ya ubepari, soko huria na utandawazi. Mara ngapi tunasikia kilio cha watu kwamba mtu hawezi kupambana na  mifumo?
Nani wa kutuokoa? Yesu wa Nazareti, Yesu wa Ulaya au Yesu wa Nigeria? Tutaokolewa na Uislamu au Ukristu? Tutaokolewa na dini nyingine au dini za jadi? Au tukimbilie ukombozi wa fikra na kutawaliwa fikra pevu?
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122.

0 comments:

Post a Comment