NDOA YANGU NINGEJUA

UHAKIKI WA KITABU:  NDOA YANGU “NINGEJUA.....!”
 
1.     Rekodi za Kibibliografia.
 
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni NDOA YANGU ‘Ningejua...!’, Kimeandikwa na Charles B Misango. Kitabu hiki kina namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 433 022. Kitabu kina kurasa 109 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
 
II. Utangulizi
 
Kitabu hiki kinaitwa Ndoa Yangu Ningejua...!  Haina maana kwamba mwandishi anaandika juu ya ndoa yake, bali kwa vile ameamua kuandika juu ya ndoa anataka kila mtu aichunguze ndoa yake na yeye akiwemo. Kwa maoni ya mwandishi kama angeandika “Ndoa yako” au “Ndoa zenu” ingekuwa sawa na kuwanyoshea wengine kidole kana kwamba ndoa yake haina changamoto zozote zile. Ni Ndoa yangu... tunaiboresha vipi? Au tuseme: Ndoa yangu, Ningejua....  ningeiboresha au ningefanya chaguo zuri? Au ningezingatia maadili na busara ya kuiongoza ndoa; kuwaunganisha watu wawili ni kazi kubwa ambayo bila uvumilivu na kuchukuliana ni muungano wenye mashaka!
 
Lengo kubwa la mwandishi ni kumwalika kila mwenye ndoa kuichunguza ndoa yake na kutafakari kwa kulinganisha na yale anayoyaandika mwandishi katika kitabu hiki. Msukumo wa kuandika kitabu hiki umetokana na ukweli kwamba siku za hivi karibu na hasa kwenye Jiji la Dar-es-Salaam, ndoa nyingi zinafungwa na sherehe kubwa zinafanyika kwenye kumbi mbali mbali, na jinsi ndoa nyingi zinavyofungwa kwa mbwe mbwe ndivyo ndoa hizo zinavyovunjika na nyingine zinakuwa na changamoto, vurugu na migogoro nyingi baina ya familia za bwana harusi na bibi harusi.
 
Kosa liko wapi? Kwa nini hakuna amani kwenye ndoa?  Tumekosea wapi kama jamii? Haya ndiyo maswali ambayo mwandishi anajaribu kuyajibu baada ya kufanya utafiti wake na kuwahoji watu mbali mbali wenye ndoa.
 
Mwandishi wa kitabu hiki ambaye pia ameoa, maana kwenye shukrani anasema hivi: “ Shukrani za pekee zimwendee MKE WANGU ambaye kwa maisha yake, amenisaidia pasipo yeye mwenyewe kujua, jinsi maisha ya ndoa yanavyoweza kubadilika kutoka namna mmoja hadi nyingine na njia ya kukabiliana nayo”. Kwa wengi mwandishi huyu anajulikana kama MC Kibonge, ingawa ni mwembamba kwa maana ya neno hilo – labda kwa vile mambo yake ni ya “Ubonge bonge” kama alivyoandika kitabu hiki juu ya ndoa. Huyu ni mwandishi aliyebobea na kwa wale wanaosoma gazeti la Tanzania Daima watakuwa wanakutana safu yake ya Nani anajali..., Alifanya kazi kwenye gazeti la Kiongozi na sasa ni mmoja wa wahariri wa gazeti la kila siku  la Tanzania Daima.
 
 
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
 
 
Nitafanya uhakiki wa kitabu hiki, lakini kwanza kwa kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Mwandishi alifanya utafiti juu ya maisha ya ndoa na dodoso lake lilikuwa na maswali kwa wenye ndoa, matokeo yake ndio yalimsukuma kuandika kitabu hiki. Nina imani kama angekutana na majibu chanya, asingeweza kupoteza muda wake kuandika kitabu hiki. Kwa ufupi tu, tutayaangalia baadhi ya maswali:
 
Swali la kwanza kwa wanawake: Kama ungejua Mumeo atakuwa na tabia alizonazo sasa ungekubali akuoe? Jibu lilikuwa ni ama Ningekubali au Nisingekubali.  Wanawake 93 kati ya 100 waliofunga ndoa ya kanisa, walisema kuwa wasingekubali kuolewa. Watano walisema wangekubali, wakati wawili waliobaki walisema kuolewa ama kutoolewa kwao yote sawa. Lakini hata wale watano waliokubali walipotakiwa waseme msingi wa kukubali kwao, baadhi ya majibu yao yalisitisha. Watatu kati yao walisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kuwa waume zao wanawapenda na ni waaminifu na wa kweli kati ndoa zao.
 
Swali hilo hilo waliulizwa wanaume, na majibu hayakuwa tofauti sana, maana wanaume 79 kati ya 100 walihojiwa walisema wasingekubali kuwaoa wanawake hao kama wangefahamu tabia zao, ni 12 tu ndio waliosema wangekubali kuwaoa.
 
Swali la pili kwa wanandoa lilikuwa: Je, Umeoa/kuolewa na Mtu uliyemtaka; Ni chaguo lako halisi. Hapa jibu lilitakiwa Ndiyo au hapana. Ukweli uliojitokeza ni kwamba wengi wamefunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati. Wanaume 49 kati ya 100 yalisema walifunga ndoa na watu ambao hawakuwataka na wanawake 73 walisema waliolewa na wanaume ambao hawakuwa chaguo lao. Kwa lugha nyingine ,ndoa 120 kati ya 200 zilifungwa pasipo hiari wala upendo wa dhati wa wanandoa wenyewe.
 
Utafiti huu umebaini sababu nyingi za kuwalazimisha watu kuolewa bila upendo wa kweli, na sababu hizo ni kama vile Kukosa uaminifu wakati uchumba, Kupata ujauzito bila kutarajia na kulazimika kuolewa na huyo aliyekupatia ujauzito na wakati mwingine kulazimishwa na wazazi.
 
Matatizo katika ndoa yanasababisha ndoa kuvunjika, lakini wakati mwingine ndoa inaendelea hivyo hivyo kwa matatizo. Mtafiti alichunguza na hili pia kutaka kujua:  Sababu gani zinakufanya Uendelee kuishi na Mkeo/Mumeo hadi sasa? Ni watoto? Ni kwa vile ndoa ya kidini? Ni kuogopa laana za wazazi? Ni kuvumilia, Ni upendo? Au ni kuishi kwa mazoea?
 
Wanawake 9 katika ya 100 waliohojiwa walisema wanaishi kwenye ndoa hata kama ina matatizo kwa sababu ya upendo kwa waume zao. Na 4 kati ya hao wanasema pamoja na ukatili wanaoupata katika ndoa zao bado wanaendelea kuwapenda waume zao. Wanawake 86 katika 100 walihojiwa walisema wanaendelea kuishi kwenye ndoa kwa sababu ya watoto wao. Ni wanawake 3 tu kati ya 100 walihojiwa waliosema wanaogopa laana ya wazazi wao.
 
Kwa upande wa wanaume ni kwamba 16 kati ya 100 aliohojiwa walisema pamoja na matatizo kwenye ndoa wanawapenda wake zao na wala hawajuti kuwaoa. Na wanaume 51 walisema ni kwa vile ni ndoa ya kanisa ndio maana wanaendelea kuvumilia matatizo kwenye ndoa zao na wanaume 24 walisema wanavumilia kwa sababu ya watoto. Waliobaki, ingawa majibu hayakufanana sana, lakini maana halisi  ni kwamba kwao kuishi kwenye ndoa au kutokuwa na ndoa ni sawa sawa, wanaishi kwa mazoea tu!
 
Swali jingine la utafiti lilikuwa: Nini chanzo kikubwa cha matatizo katika ndoa?  Je ni kwa kutokuwa  na kipato kizuri pande zote mbili? Au ni wazazi wa pande zote mbili au ni mtu binafsi ndani ya ndoa yake au ni umasikini na kumuasi Mungu?
 
Wanawake 33 kati ya 100 walihojiwa walisema chanzo cha matatizo katika ndoa ni kipato kizuri cha waume zao kinachowafanya wawe na “jeuri” ya kutumia fedha katika starehe na kuiacha familia ikiteseka. Wanawake sita, walisema chanzo ni wazazi wao na 14 walisema chanzo ni wakwe zao. Wanawake saba, walisema marafiki wao wa kike ndio wanasababisha matatizo katika ndoa zao. Kwa bahati mbaya, hakuna mwanandoa aliyekubali kwamba yeye binafsi amechangia kuleta matatizo katika ndoa yake, kila mmoja anajaribu kutafuta mchawi nje ya ndoa.
 
Kwa upande wa wanaume, 13 kati ya 100 aliohojiwa walisema chanzo ni kipato kidogo, hii inasababisha wanawake kuwadharau na vurugu inaanzia hapo. Na wanaume 14 walisema shinikizo la wazazi na hasa mwanamke akichelewa kuzaa ndo chanzo cha vurugu. Katika majibu yote hakuna mwanandoa aliyesema kuwa chanzo cha matatizo ni kuwa mbali na Mungu. Wote wanafikiri wakienda kwenye ibada mara kwa mara wanakuwa karibu na Mungu, hawaangalii ukaribu wa Mungu na maisha yao ya siku kwa siku kwenye ndoa zao.
 
Swali la kizushi, ni kwamba kama talaka ingeruhusiwa mambo yangekuwa vipi? Kusema kweli asilimia 70, wangeomba talaka na kuachana na ndoa zao. Na hili linaonyeshwa na ukweli kwamba wanaume 78 katika ya 100 walihojiwa walikubali kuwa na mahusiano ya kingono nje ya ndoa zao, na wanawake 62 pia walikubali kutembea nje ya ndoa zao.
 
Pia kuna utata wa watoto. Kwa vile siku hizi mtu anaweza kupima DNA, kuna mshangao mkubwa wa kujitokeza; inasemekana kwamba asilimia kubwa ni watoto wa kubambikizwa; wanaume wengi wamekuwa wakiwatunza watoto ambao si wao; ni watoto wa nje. Lakini mtafiti alipoulizia wanaume kuwa na watoto nje ya ndoa asilimia 12, walikubali kuwa na watoto nje ndoa. Na fumbo kubwa linabaki watoto wengi kuwa na baba tofauti na wale wanaojulikana rasmi.
 
Mazingira yanayokizunguka kitabu hiki ni utata katika ndoa, vurugu na magomvi hadi ndoa kuvunjika. Ni kwamba ndoa nyingi hazina amani na hasa ndoa zinazofungwa siku za hivi karibuni hazidumu. Tatizo liko wapi? Tufuatane na mwandishi wa kitabu kuona majibu.
 
IV. Muhtasari wa Kitabu
 
Kitabu hiki kina sura sita, baada ya kutanguliwa na dibaji, shukrani na utangulizi. Dibaji ya kitabu hiki imeandikwa na mheshimiwa Msgr. Padri Deogratias H. Mbiku wa jimbo katoliki la Dar-es-Salaam. Ina maana hiki si kitabu cha mzaha, maana padri huyu ni mgongwe katika Kanisa Katoliki, msomi na mtu anayeheshimika katika jamii. Kukubali kuandika dibaji, ina maana alikisoma kitabu na kuona kinafaa kwenye jamii yetu.
 
Katika dibaji, padri Mbiku, anasema hivi: “ Katika nyanja za dini, jamii, Serikali na siasa, ndoa ni  muhimu sana; kwa sababu bila kuwa na ndoa nzuri na imara, dini, jamii, Serikali na hata siasa zitalegalega na kukosa maadili mema, haki na amani miongoni mwa watu...”. Juu ya mwandishi anasema “ Mwandishi wa kitabu hiki anazungumzia kwa undani na ufasaha sababu za kuvunjika kwa ndoa: sababu za msingi ni ubinafsi, kukosa maandalizi ya kina; binadamu wenzetu; na ibilisi... Lakini mwandishi haachii uchambuzi wake kwenye sababu tu, bali pia anatoa ushauri na rai kuhusu nini kifanyike ili kuboresha ndoa. Hatimaye, anaongelea wajibu wa Kanisa katika kuzishughulikia ndoa ili ziwe msingi imara kwa jamii, dini, Serikali na hata siasa”
 
Utangulizi, umeandikwa na mwandishi mwenyewe. Hapa anajaribu kuelezea kwa undani juu ya kichwa cha kitabu kuitwa “Ndoa yangu”. Hakutaka kusema ndoa yako au ndoa yenu, kwa maana kwamba anapozungumzia maisha ya ndoa kwa vilele na yeye anayaishi maisha hao, hawezi kujiweka kando. Lakini pia anaposema ndoa yangu haina maana kwamba anaongelea ndoa yake mwenyewe. Anataka kila mtu atakapokuwa anakisoma kitabu hicho, aseme “Ndoa yangu, ningejua...”
 
Sura ya kwanza ya kitabu hiki ni Ningejua. Kwa kiasi kikubwa sura hii mwandishi anatoa mrejesho wa utafiti alioufanya juu ya ndoa. Mrejesho wa jumla ni kwamba kati ya watu 200, waliohojiwa, 170 wanajuta kufunga ndoa na wenzio, kama wangejua tabia zao mapema, wangefanya uamuzi mwingine. Kadhalika 122 kati ya 200 waliohojiwa wanakiri kufunga ndoa na watu ambao hawakuwapenda kwa dhati na hawakuwa changuo lao.
 
Katika sura hii ya kwanza, kutokana na maswali ya dodoso: Kama ungejua mumeo atakuwa na tabia alizonazo sasa ungekubali akuoe, Kama ungejua mkeo atakuwa na tabia alizo nazo sasa, ungekubali kumuoa? Mmeo/Mkeo ni chaguo lako halisi? Tunaona kwamba asilimia kubwa katika ndoa wanaangukia mikononi mwa watu ambao hawakuwatarajia. Mwandishi anatoa  asilimia kuonyesha jambo hili. Na sababu kubwa zikiwa ni kulazimishwa na wazazi, kukosa uaminifu wakati wa uchumba, kupata ujauzito kabla ya ndoa na mambo mengine kama kufuata mali na cheo cha mtu.
 
Pamoja na ndoa kuwa na matatizo bado watu wanaendelea kuishi kwenye ndoa hizo. Asilimia kubwa ya wanawake walihojiwa walisema wanavumilia magumu ya ndoa kwa sababu ya watoto. Si upendo na wala si shinikizo la dini, bali nia watoto. Na asilimia kubwa ya wanaume wanavumilia machungu ya ndoa kwa shinikizo la dini.
 
Pia kwenye utafiti huu, mwandishi naweka wazi kwamba wanandoa wengi wanatembea nje ya ndoa na kuzaa watoto nje ya ndoa zao. Asilimia kubwa wanalifanya suala la watoto wa nje ya ndoa kuwa ni la siri na wengine wanalifichua kwa wenzao wa ndoa. Wanaume wanaongoza kuwa na namba kubwa ya watoto wa nje ya ndoa.
 
Sura ya pili ni swali: Nilikosea wapi?
Katika sura hii mwandishi anajaribu  kuangalia sababu zinazopelekea watu kuangukia kwenye chaguo baya na kujiingiza kwenye matatizo ya ndoa.
Kosa la kwanza ni: Hatukujijua! Ni muhimu mtu kujijua yeye ni nani na aliumbwa kwa ajili gani. Ili mtu afanye uchaguzi mzuri na kumpata mwenzi wa maisha ni vyema, ajijue kwanza. Kwa kujiua, anaweza akawajua na wengine na hatima kumjua ni mtu gani anaweza kuwa mwenzi wa maisha.
 
Kosa la pili ni  kwamba:  Hatukujua wito wetu: “ Kila mtu ameletwa duniani kwa sababu maalumu. Hivyo, si kila mwanaume ama mwanamke alipangiwa maisha ya ndoa kama ambavyo wengi wetu tunadhani..” (uk wa 19). Ka kutetea hoja hii mwandishi naonyesha historia ya watu ambao waliishi maisha yao yote bila kuingia kwenye ndoa na wengine walizaliwa wakiwa matowashi. Ili ndoa iwe ya furaha na amani ni muhimu wanandoa wakatambua wito wao.
 
Kosa la tatu: Tulikurupuka! Kwamba watu wanapotafuta wachumba hawatulii na kuchunguza na kutafakari juu ya wachumba wao: “ Ni kama tulirukia gari lililokuwa katika mwendo bila ujuzi..” (Uk wa 22). Mtu anapomtafuta mchumba kwa lengo la kufunga ndo ni lazima ajipatie muda wa kutosha. Uchumba wa siku moja na ya pili kufunga ndoa ni hatari kubwa.
 
Kosa la nne: Hatukuzijua familia za wenzetu: “ Tulitakiwa kujua historia ya maisha ya familia ya wenzetu kikamilifu. Kujua kama wana maisha ya ajabu kama vile uchawi ama  wapenda ushirikina. Maana kama huyu alizaliwa, akalelelewa katika maisha ya aina hii, uwezekano wa yeye kushiriki matendo hayo ni mkubwa...” ( Uk wa 26).
 
Kosa la tano ni: Hatukuwajua wenzetu:
Ni muhimu kumfahamu mwenzako vizuri kabla ya ndoa. Ni muhimu pa kuwafahamu marafiki zake, kufahamu kama huyu ni msiri au ni muwazi? Na je mlikutana katika mazingira gani? Ni mazingira ya kuruhusu mtu kuwa wazi au ni mazingira ambayo yanaweza kuwa ni shinikizo? Je tulikutana kazini? Tulikutana kanisani au kwenye baa? Kama tulikutana kwenye baa, kesho na keshokutwa tabia kama hiyo inaweza kujirudia.
 
Kosa la sita na saba, ni kutojua uzito wa agano. Maana ndoa ni  agano linalowaunga watu wawili, kwa imani nyingine, hawa wanakuwa kitu kimoja. Si wawili tena bali ni kitu kimoja. Je wanandoa tunajua uzito huu kabla ya kufunga ndoa? Tunatafakari juu ya uzito huu kabla ya kufanya uamuzi?
 
 
Sura ya tatu ni swali pia: Ndoa yangu ni mpango wa Mungu?
Mwandishi, anataka tutafakari juu ya ndoa kama mpango wa Mungu. Tunafunga ndoa kujifurahisha au tunafunga ndoa kuendeleza Mango wa Mwenyezi Mungu wa kupendana na kuzaa kwa lengo la kuujaza ulimwengu?
 
Sura ya nne ni swali jingine: Nani maadui wa ndoa yangu? Katika utafiti uliofanywa, ambao unajadiliwa kwenye sura ya kwanza. Wanandoa walipoulizwa swali hili, wote waliwanyoshea wengine kidole, kwamba maadui wa ndoa zao ni ndugu, wazazi na marafiki. Walishindwa kutaja kwamba adui mkubwa wa ndoa ni wanandoa wenyewe. Kuna suala la kuendeleza utoto katika ndoa. Mtu anafunga ndoa lakini anashindwa kuachana na tabia zake za kitoto; hiki ni chanzo cha matatizo katika ndoa nyingi. Pili kuna suala la kuendeleza ukahaba kwenye ndoa na hiki ni chanzo cha matatizo mengi kwenye ndoa. Kuna tatizo la kunyimana tendo la ndoa; likisababishwa na kutembea nje ya ndoa na wakati mwingine unywaji wa pombe kupindukia. Kuna kauli mbovu kwenye ndoa, ujeuri, majivuno na kudharauliana.
 
Ni wazi hatuwezi kukwepa kabisa ushawishi wa wazazi katika ndoa zetu. Bila uangalifu, uhusiano wa wazazi unaweza kujenga matatizo makubwa katika ndoa zetu. Ndugu, jamaa na marafiki nao wanaweza kuleta matatizo makubwa kwenye ndoa. Na la mwisho ambalo watu wengi wanasahau ni kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.  Ndoa, ambayo haina msingi wa dini ni vigumu kusimama na kustawi. Hayo ndo maoni ya mwandishi juu ya matatizo yanayozikumbwa ndoa nyingi.
 
Sura ya tano ni swali pia: Tufanye nini sasa?
Mwandishi anasema: “ Kwa sisi tulioingia  katika ndoa, sasa si wakati wa kujihukumu wala kuhukumu wengine. Si wakati wa kujua kama tulikuwa na wito wa ndoa ama hapana. Si wakati wa  kuwashambulia wenzetu kwa mabaya yanayotendeka ama yaliyotendeka siku za nyuma ndani ya ndoa zetu. Si wakati wa kujua iwapo tulifunga ndoana watu wasio wetu wala chaguo la Mungu..”. Kwa maoni ya mwandishi, kila wakati ni wakuanza maisha upya. La msingi ni kumrudia Mwenyezi mungu na kuishi kwa kutekeleza mpango wake. Na la msingi ni kujuta na kuomba msamaha, kuwaomba wenzetu wa ndoa msamaha, kuwaomba watoto msamaha na kuiomba jamii nzima msamaha.
 
Sura ya sita: Wajibu wa kanisa.
Katika sura ya mwisho, mwandishi analigeukia kanisa na kulibebesha mzingo mkubwa wa kulinda na kutunza ndoa. Kwa maoni yake ni kwamba Familia ndiyo msingi wa kila kitu. Msingi wa kanisa, msingi ya jamii. Bila kuwa na ndoa nzuri ni vigumu kuwa na jamii nzuri. Hivyo kanisa lina wajibu mkubwa kuhakikisha ndoa zinakuwa imara na zinadumu.
 
V. TATHIMINI YA KITABU.
 
Nianze kwa kumpongeza Charles B. Misango, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli kazi hii inaburudisha, inasikitisha na kufikirisha. Utafiti wake juu ya ndoa, umeweka ukweli wazi. Na kila atakayekisoma kitabu hiki atakuwa makini kumchangua mwenzi wa maisha.
 
Pili, ni maoni ya baadhi ya watu waliokisoma kitabu hiki:
Fred Jackosn wa  Keko Dar-es-Salaam, anasema “ Kama nisingesoma kitabu hiki na kuamua kufuatilia kwa ukaribu historia ya familia na ukoo wa mchumba wangu, ningejikuta naishi na mtu aliyebobea uchawi. Kitabu hiki kimeokoa maisha yangu” (uk wa 109)
 
Naye Betty wa NMB Makao Makuu Dar-es-Salaam, anasema: “ Huu ni funuo wa ajabu sana katika maisha yangu ya ndoa. Kitabu kimenisaidia sana kujua namna gani kudumisha upendo na amani kati yangu na mume wangu, upi wajibu wangu katika ndoa yangu” (uk 109).
 
Na Peter Mizambwa wa Kisarawe, anasema hivi : “ Kama kuna wachumba watakaokisoma kitabu hiki na kuamua kufuata kile kilichoanikwa, hakika wataamua kuanza upya, maana wengi tumechumbiana kienyeji kabisa...”(Uk 109)
 
Kyaruzi-Rc wa Magomeni, anasema “ Hiki ni kitabu kilichoanika ukweli mtupu wa maisha ya wanandoa wengi. Kitasaidia sana kuamsha akili za wanandoa na kurejesha amani katika ndoa nyingi zilizosambaratika na hata zisizo na amani. Kimetoa pia ukweli juu ya wajibu wa Kanisa kuhusiana na malezi ya wanandoa na kitaokoa wengi”
 
Zainabu Rahab wa Mikocheni, naye anasema “ Kitabu hiki ni kioo halisi cha kila mwanandoa. Ingefaa kila aliye katika uchumba akisome kwa makini ili kupata msaada wa Mungu katika safari  ya uchumba...” (Uk wa 109).
 
Tatu, mwandishi wa kitabu hiki ametuingiza ndani ya tafakuri. Utafiti wake unaonyesha wazi jinsi ndoa nyingi zilivyokuwa na matatizo. Swali la kujiuliza sote ni je, ndoa ni Mpango wa Mungu? Je, Mungu alitaka tuishi kwenye kifungo hiki cha ndoa, au mpango wake ulikuwa ni sisi pia kuishi kama wanyama wengine? Ukiangalia asilimia ya wanandoa wanao kwenda nje ya ndoa zao, unakuwa na mashaka. Na je mbona Mwenyezi Mungu, anaendelea kuumba watu wazuri bila kukoma? Mbona hawezi kuviwekea kizingiti vishawishi ndani ya miili yetu? Yeye si ni Muumba wa vyote? Vinavyoonekana na visivyoonekana? Je ndoa ni tendo la ndoa au ni zaidi ya hapo? Mvuto unaokuwepo kati ya Me na Ke, unaweza kufungiwa tu kwenye ndoa? Mbona hata baada ya mtu kufunga ndoa, bado macho yanaendelea kuona na mvuto unabaki? Mvuto ni dhambi au kuutukuza uumbaji wa Mwenyezi Mungu? Kusifia uumbaji wa Mwenyezi Mungu ni dhambi? Na kusifia mipaka yake ni wapi? Kuona na kuacha? Kuona na kugusa? Au Kuiingia kwenye ndoa? Na tuiingie na wangapi kwenye ndoa? Ndoa ya mke mmoja na mwaume mmoja? Mwanaume mmoja wanawake wengi? Au wanawake wengi mme mmoja? Au maisha ya uhuru bila ndoa, lakini tunatenda tendo la ndoa? Ni upi ni mpango wa Mungu? Ni changamoto!
 
Nne, mwandishi ameonyesha wazi kwamba mara nyingi tunachezea kifungo hiki cha ndoa. Hakuna mafunzo kwa vijana. Tumepuuzia mafundisho yetu ya jando na unyago kiasi kwamba vijana wetu wanatenda na kufuata uzoefu wa kila siku bila kuwa na mafunzo ya maisha.
 
Tano, mwandishi anaonyesha wazi kwamba ndoa nyingi zina siri kubwa; watoto wa nje na nyumba ndogo. Hata wale ambao ni watu wa “Mungu” nao wana nyumba ndogo na watoto wa nje. Mungu, apishe mbali maana kufuatana na utafiti wa kitabu hiki, watu wakiamua kupima DNA, ndoa nyingi zitasambaratika maana watoto wengi watagundulika ni wa kubambikizwa.
 
Sita, kitabu hiki kianzishe mjadala kwenye jamii yetu, ili tutafute mamoja na ushauri wa mwandishi, jibu  la tufanye nini ili ndoa zetu ziwe imara. Tufanye nini ili tufanye uchaguzi mzuri wakati wa kuwatafuta wenzi wa maisha.
 
 
VI. HITIMISHO.
 
Kama kawaida yangu, ningependa kuwashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Ni imani yangu kwamba watajifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki na hasa utafiti uliofanywa na mwandishi.
 
Lakini, pia ningependa kuwashauri wale wote watakaokisoma kitabu hiki watafute pia na vita bu vya Dr. Binagwa, juu ya ndoa. Utafiti wa mwandishi wa kitabu hiki unamwandaa msomaji kuvisoma vitabu vya Dr. Binagwa, ambaye anaandika kwa undani juu ya mahusiano kwenye ndoa. Maana, haitoshi kutaja kwamba kuna suala la kunyimana tendo la ndoa, lakini pia kuna maelezo juu ya tendo lenyewe na sababu za kufikia hatua ya kunyimana.
 
Dr.Binagwa, anafafanua vizuri hata juu ya tendo lenyewe. Haitoshi tendo tu, bali kuna namna ya kutenda  tendo hilo. Hivyo kuna mengi juu ya ndoa, na kwa kusoma vitabu hivi, mtu atagundua kwamba ndoa ni kitu kipana ambacho bila mafunzo ni vigumu kukiishi. Ndoa zinavunjika kwa vile sote tumepuuzia suala la kufundisha juu ya ndoa. Ni muhimu kurudisha mafundisho ya Jando na Unyago. Pia ni muhimu kusoma na vitabu vya Jando na Unyago, ambavyo zamani tulivisoma tukiwa sekondari.
 
Mwisho ni ushauri kwa mwandishi, kwamba sasa ana kazi ya kufanya.  Yeye pia ni lazima atafute vita bu vya Dr. Binagwa na kuvisoma na kuona jinsi vinavyomsaidia kuandika kita bu kingine juu ya ndoa. Hiki sasa ni utafiti. Tunataka kitabu cha ndoa kutoka kwa mtu wa ndoa kama yeye na ikiwezekana atoe mifano ya ndoa yake mwenyewe. Kama tunataka kulisaidia taifa letu, na kama tunakubaliana kwamba taifa imara linajengwa na familia imara ni lazima mwandishi aonyeshe hili kwa mifano zaidi.
 
Je watu wawili wanaweza kuishi ndoa yao na ikawa imara? Au wanaihitaji msaada wa ndugu jamaa na marafiki? Tendo la ndoa, ni la wawili, lakini maisha mengine yanayoizunguka ndoa, kama uwazi, kujifunua na kutafuta msaada kwa wengine, kutafuta  ushauri, ndoa na ndoa kusaidiana; kufundishana uvumilivu na kuchukuliana ni jambo la muhimu sana. Hatimaye ndoa si ya watu wawili, bali ni suala la jamii nzima. Ndoa ikibaki kwenye kuta za watu wawili, ni vigumu sana ndoa hiyo kusimama na kudumu.
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
 
 

0 comments:

Post a Comment