MTOTO WA AFRIKA, NI NANI
ANAJALI?
Kauri mbi ya siku ya
mtoto wa Afrika mwaka huu inasema: “Kuondoa Mila zenye kuleta madhara kwa
watoto: Ni jukumu letu sote”. Tarehe 16.6.2013, kama kawaida ilikuwa ni siku ya Mtoto
wa Afrika .Baadhi ya watu wameikumbuka, lakini inaelekea moto wake unaendelea
kupunguka na kubakia ni siku ya watoto wa shule, kukutana na kuimba nyimbo,
kucheza ngoma na maigizo. Watu wazima wanaanza kuikwepa siku hii. Jana kwenye
taarifa za habari ilionekana asilimia kubwa ya watoto na asilimia ndogo sana ya
watu wazima. Pamoja na jitihada za kuikwepa siku hii ukweli unabaki pale pale
kwamba yaliyotokea Soweto miaka hiyo yanaweza kutokea tena popote kwenye nchi
hizi za Kiafrika na Tanzania ikiwemo. Matendo ya ukiukwaji wa haki za watoto
ikiwemo na uporaji wa ardhi yamekuwa mengi. Binafsi nimejenga utamaduni wa
kuandika makala kila tunapoikumbuka siku hii ya mtoto wa Afrika. Ninaamini
mchago wangu huu unaweza usiwanufaishe watanzania wa leo, lakini kama wasemavyo
kwama “Kilichoandikwa kimeandikwa” ni imani yangu kwamba mchango wangu
utawanufaisha hata watanzania wa kesho. Na ndiyo maana nimeamua kuuliza katika
makala haya: Mtoto wa Afrika, ni nani anajali?
Kauri mbiu ya mwaka huu ni mwiba mkubwa kwetu
sote. Tuna mfumo gani wa kuondoa mila zenye kuleta madhara kwa watoto wetu?
Tuna mfumo gani wa kutokomeza uporaji wa ardhi, tuna mfumo gani wa kuwaambukiza
watoto wetu moyo wa uwajibikaji na uzalendo? Tuna mfumo gani wa kujenga mila
zenye ustaarabu na kuachana na mila za kishenzi kama zile zinazoanza kujitokeza
katika jamii yetu: Watu wanapigwa wanaumizwa na wengine wanauwa, watu wanasingiziwa
na kubambikiziwa kesi; wanaotenda matendo haya ya kinyama bado wanaendelea
kudunda na kupandishwa vyeo. Tuna mfumo gani wa kuwafundisha watoto wetu kusema
ukweli? Kuwa waaminifu, kuacha uchakachuaji, kuacha tabia ya kuuza bidhaa
bandia. Tuna mfumo gani wa kufundisha uadilifu? Elimu mbovu ni kujenga mila
zenye kuleta maafa! Tumeshuhudia watoto wetu wakishindwa vibaya, tumeshuhudia
watoto wetu wakifundishwa kwa kutumia vitabu bandia ambavyo havina viwango:
Alimu mbovu ni maafa matupu!
Mnamo mwaka 1976, Kule Soweto, Afrika ya kusini,
maelfu ya watoto weusi wa shule waliingia mitaani na kufanya maandamano ya
zaidi ya nusu kilomita, wakipinga elimu duni waliyokuwa wakiipata na kudai kufundishwa
kwa lugha yao. Walifanya maandamano ya amani kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa
serikali ya makaburu. Ujumbe huu ulikuwa mchungu kwa wakubwa na hawakuwa tayari
kuusikiliza. Kama kichaa anavyoweza kutumia bunduki kuua mbu, ndivyo makaburu
walivyofanya kwa wanafunzi hao. Mamia ya wasichana na wavulana walipigwa risasi
na kupoteza maisha yao. Kwa vile bunduki
inaua mwili, lakini fikra na roho vinaendelea kuishi, maandamano hayo
hayakuzimwa kwa risasi! Machafuko yaliyofuatia tukio hili yalipoteza maisha ya
mamia ya watu na kuacha majeruhi kadhaa.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoshuhudia
matatizo mengi ya watoto. Tunashuhudia watoto wetu wanavyosukumwa kila siku
kwenye daladala, watoto wanavyosoma kwa shida, shule za msingi wengine wanakaa
chini, sekondari wanasoma bila kuwa na walimu wa kutosha, matokeo yake wanafanya vibaya na kushindwa kuendelea na
masomo ya juu. Lakini pia na wale wanaofanikiwa kuendelea na masomo ya juu,
tunashuhudia wanavyonyanyaswa na Bodi ya mikopo. Tunashuhudia watoto wetu wakikoswa
ajira, tunashuhudia watoto wetu wakibugia dawa ya kulevya, wakilewa pombe,
wavulana wakisuka nywele na kujifananisha na wasichana, wasichana wakitembea
nusu uchi na baadhi ya watoto wetu wakiikimbia nchi kwenda kuishi
ughaibuni. Kwa asilimia kubwa maisha ya
mtoto wa Kitanzania, yanakuwa ni ya shida.
Binafsi, nimeamua mwaka huu niandike juu ya Mtoto wa
Afrika na uporaji wa ardhi na mtoto wa
na elimu mbovu. Kwanini, nimeamua kuandika hivyo: chanzo cha siku ya mtoto wa
Afrika, ni maasi yaliyofanywa na watoto wa Soweto, kwa kukataa kunyanyaswa.
Walikuwa wakipata elimu duni ukilinganisha na ile ya Wazungu. Pia, walitaka
elimu inayotolewa kwa lugha yao. Kule Soweto, watoto walianza kutambua kwamba
wale waliokuwa wakifundishwa katika shule nzuri ndio waliokuwa wakipata kazi nzuri
na vyeo vya juu katika serikali. Hali ya kutamani hali bora ya maisha kwa siku
za mbele, hali ya kutaka kuwa na vyeo na nafasi nzuri za kazi, iliwafanya
wanafunzi kukataa elimu duni waliyokuwa wakiipata. Hawakuogopa nguvu za jeshi
la Makaburu. Walikuwa tayari kupambana bila silaha – na kweli wengi wao
walipoteza maisha. Watoto wa Soweto, walitambua kwamba kujifunza kwa lugha za
kigeni wasingepata maarifa yenyewe. Walitaka wafundishwe kwa lugha ya kwao,
lugha inayofanana mazingira yao, lugha inayogusa maisha halisi, lugha inayoweza
kuharakisha maendeleo. Hoja yangu ni kwamba Bila kuwa waangalifu, inawezekana
na sisi hapa Tanzania, tunaandaa Tanzania ya kesho yenye maasi kama ya Soweto.
Bila kuwa na elimu nzuri na bora, watoto wetu
wakasoma na kupevuka kifikra6/15/2013, tutakuwa tunajiandalia majanga ya Soweto;
bila kuwa na ardhi ya kuwarithisha watoto wetu tunakuwa tunaliandalia taifa
letu migogoro na majanga ya Soweto.
Kumetokea wimbi la uporaji wa ardhi. Watu wenye
fedha wananunua ardhi kubwa kwa kisingizio cha kuwekeza. Matokeo yake vijana
wengi watajikuta hawana ardhi na wataikataa hali hii. Na tunavyosikia kwenye
vyombo vya habari sehemu nyingine hali hii imekataliwa mapema. Tunasikia kule
Manyara jinsi watu wanavyovamia mashamba, kukata mazao na kuwashambulia wanao
miliki mashamba. Tukio la Tegeta, la kukatana mapanga katika harakati za vijana
kufukuzia mbali waporaji wa ardhi, ni la kusikitisha na kutafakarisha; na ni
fundisho pia kwamba vijana wakiamua kudai ardhi yao, patachimbika.
Mgogoro wa ardhi wa Loliondo, tumeshuhudia jinsi
ulivyovuruga amani kwenye maeneo hayo na kupanda mbegu ya maasi na chuki kwa
vizazi vijavyo. Mashirika mbali mbali yasiyokuwa kiserikali yamepiga kelele juu
ya suala hili la uporaji wa ardhi, lakini kelele hizi zimekuwa kama ile sauti
iliayo nyikani. Mashirika haya yamekuwa yakijitahidi kutengeneza majukwaa ya
majadiliano, ili watanzania tukae pamoja na kujadiliana juu ya uhai wa taifa
letu.
Ardhi ni muhimu sana kwa maisha yetu ya leo na
vizazi vijavyo; uchumi wetu unategemea kilimo; bila ardhi hatuwezi kulima,
hatuwezi kupata chakula na mazao ya kuuza na kujipatia fedha za kigeni. Hivyo
ni muhimu sote kusimama pamoja kupinga wimbi hili kubwa la kupora ardhi yetu.
Tuhakikishe kila Mtanzania ana ardhi yake ya kutosha na kupiga vita kwa nguvu
zote ardhi kuwa mikononi mwa watu wachache.
Tunapoikumbuka siku mtoto wa Afrika, ni bora
tukazingatia umuhimu wa ardhi kuwa ustawi wa mtoto wa Afrika. Tukiilinda ardhi
yetu leo, tunaepusha machafuko ya ardhi kesho na keshokutwa. Pia tunapoikumbuka siku ya mtoto wa Afrika ni muhimu sana kutambua elimu bora kwa watoto wetu italiepusha taifa letu
na wimbi kubwa la machafuko. Hivyo basi, Mtoto wa Afrika, ni nani anajali? Ni
mimi? Ni wewe, ni yeye? Ni wao au ni sisi sote! Mungu ibariki Tanzania, Mungu
wabariki watoto wote wa Afrika.
Na,
Padri
Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment