MWANA MAMA MWALIMU THEOPHILDA TINKASIMIRE TIKAWA.
Leo hii katika safu yetu ya Mwana mama tunawaletea Mwalimu Theophilda
Tinkasimire Tikawa. Maarufu kama Mwalimu Tinka. Mama mwenye tabasamu na
uchangamfu kila wakati, mwenye kuwapenda watu wote bila ubaguzi, mwenye
kuipenda kazi yake ya ualimu na roho ya kuwasaidia watu wanaomzunguka na hasa
wasiojiweza. Inawezekana sifa hizi zikawa zinapwaya kwa wale wanaomfahamu Mwana
mama huyu kwa karibu, lakini safu hii imejitahidi kiasi cha kuzidi nusu ya sifa
zake. Mwalimu huyu wa miaka mingi
anastaafu kazi ya ualimu mwezi huu baada ya kufikisha miaka 60 ya kuzaliwa. Bila kuona mvi zinazokipamba kichwa chake,
utafikiri ni binti mdogo wa miaka 30, yeye anajivunia mvi zake na hapotezi muda
wake kuweka rangi za kubadilisha rangi ya nywele zake kama wafanyavyo wengine
wanaogopa kuitwa “Bibi” au “Babu” kwa upande wa wanaume.
Mwalimu Tinka, ni mama wa watoto 4, wajukuu 12 na watoto wengine wengi
aliowafundisha sehemu mbali mbali za Tanzania; Tanga, Tabora, Dar-es-Salaam,
Mbeya na Karagwe. Mama huyu ambaye kauli mbiu ya maisha yake imekuwa “ Kukata tama
ni dhambi” ni mfano wa kuigwa. Safu hii ilipoongea na mama huyu kwa nyakati
tofauti, amekuwa akisisitiza kauli mbiu yake: “Unajua nilipofiwa na mme wangu,
mnamo mwaka wa 1990, ningekata tama, nisingekuwa hivi nilivyo. Nisingeweza
kuwasomesha watoto wangu na kuhakikisha wanakua vizuri na kuweza
kujitegemea. Sikukata tama, nilipambana na maisha na kumtegemea Mwenyezi Mungu,
sikufikiria kuolewa tena, bali niliweka nguvu zangu zote kulijenga taifa langu
la Tanzania kwa kufundisha watoto na
kuhakikisha ninawatunza watoto wangu” Alisema Mwalimu Tinka, akiongea na safu
hii.
Wakati anapostaafu na bado ana nguvu, Mwalimu Tinka anatamani “ Kuzunguka
Tanzania yote, nikitoa ushauri kwa wajane. Nimeishi maisha ya ujane, nafahamu
matatizo na uchungu wa kuwa mjane. Kama
kuna kita ambacho siwezi kukisahau hadi naingia kaburini ni tukio na kufiwa na
mme wangu. Hivyo natamani nieleze uzoefu wangu na kuwashauri wajane wenzangu
wazikate tama, maana kukata tama ni dhambi. Tatizo lililo mbele yangu ni
kutokuwa na uwezo wa fedha za kuizunguka Tanzania yote..” Anayasema haya kwa
uchungu mkubwa, maana anaonyesha hamu na nia yake ya kutaka kuizunguka Tanzania
nzima akiwashauri wajane.
Kwa vile ana wasiwasi wa kutoweza kupata fedha za kuizunguka Tanzania,
nzima Mwalimu Tinka, ameaanza kuandika kitabu cha maisha yake. Anaamini, wajane
na watu wengine wakikisoma watapata la kujifunza.
Mwalimu Theophilda TinkasimireTikawa, alizaliwa mnamo mwaka 1952 kijiji cha
Kasheshe – Nyaishozi –Karagwe. Ni mtoto pekee wa Baba Paul Koliko na Mama Agnes
Paul. Kati ya mwaka 1962 na 1968, alipata elimu ya msingi shule za Katoju na
Nyaishozi –Karagwe. Hakuweza kuendelea na elimu ya Sekondari, isipokuwa
alijiunga na Hospitali ya Nyakahanga –Karagwe, ambako alichukua mafunzo ya
kuwasaidia manesi kwa miaka miwili, na baadaye kutoa huduma kama nesi msaidizi.
Wakati akiwa mfanyakazi wa Hospitali ya Nyakahanga, alikutana na mchumba
wake Bwana Joseph Tinkasimile, aliyekuwa akifanya kazi Tanga, kama Afisa
Maliasili wa Mkoa wa Tanga. Walifunga ndoa takatifu kwenye kanisa Katoliki Karagwe
mwaka wa 1970 na kuhamia Tanga. Mungu aliwajalia kumpata Bruno mtoto wao wa
kwanza mnamo mwaka 1971 na mtoto wao pili Felix mwaka 1972. Mnamo mwaka 1974,
walijaliwa kumpata mtoto wao pekee wa kike Leticia Shubira Wamala na mwaka 1979
mtoto wao wa mwisho Victor alizaliwa.
Kati ya mwaka 1976 hadi 1977, Mwalimu Tinka, alijiunga na chuo cha Ualimu
Korogwe na kusoma ualimu daraja la C. Katika hatua hii hawezi kumsahau mshauri
wake Mama Mazoko wa Bukoba, ambaye ndiye aliyemshauri asomee ualimu na
kuendelea kumshauri mambo mengi katika maisha yake. Hadi leo hii Mama Mazoko,
bado ni mshauri wa karibu wa Mwalimu Tinka. “ Mama huyu ndiye alitoa ushauri
nisikatwe mguu nilipopata ajali ya pikipiki kwenye miaka ya tisini. Bila
ushauri wa mama Mazoko, leo hii ningekuwa na mguu mmoja. Hivyo Mama huyu siwezi
kumsahau kwenye maisha yangu, alinishauri nisomee ualimu, na umenisaidia kwenye
maisha yangu na kuwasaidia wengi na bado anaendelea kunishauri” . Alieleza
Mwalimu Tinka, wakati alipoongea na safu hii ya Mwana Mama.
Baada ya kuhitimu. Mwalimu Tinka,
alianza kazi ya kufundisha Shule ya Msingi Kibasila – Dar-es-Salaam mnamo mwaka
1978. Mnamo mwaka wa 1979, alihamia shule ya
msingi Kitete –Tabora. Akiwa Tabora, aliteuliwa kuwa Afisa Utamaduni wa
michezo wa Manispaa(Mji) wa Tabora. Mwaka 1982 - 1983, Mwalimu Tinka alihamia
shule ya msingi Uyole Mbeya. Na mwishoni mwa mwaka wa 1983, alihamia Wilaya ya
Karagwe na kufundisha shule ya msingi Rwambaizi hadi mwaka2002. Kati ya 2002 na
2003, alifundisha kwenye shule mbili za msingi Nyamilima na Kituntu kule
Karagwe.
Mnamo mwaka 2004, Mwalimu Tinka, alihamia tena Dar-es-Salaam na kufundisha
shule ya msingi Kizinga hadi mwaka 2005. Baada ya hapo hadi mwezi huu anapostaafu
alikuwa anafundisha shule ya msingi Toangoma na amejenga makazi yake huko
hukoToangoma.
Kwa vile Mwalimu Tinka, hakusoma masomo ya sekondari, kati ya mwaka 1999 na
2000 alisoma na kushinda mitihani ya sekondari na kujipatia cheti cha kidato
cha nne. Pia mwaka 2011, alipata masomo maalumu ya mwaka mmoja ya ualimu wa
Chekechea. Lakini pia amepata fursa ya kusoma nje ya nchi masomo ya Demokrasia
na Uongozi nchi ya Denmark mwaka 1997.
Mwalimu Tinka, amekuwa mama mshauri kwa watu wengi. Bwana Kaboko wa Dar-es-Salaam
na Profesa Faustine Kamuzola wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, ni miongoni mwa
watu walionufaika na ushauri wa Mwana mama huyu.
Mwana Mama huyu, mbali na ualimu amekuwa kishiriki shughuli mbali mbali
katika jamii kama vile siasa na shughuli za kidini. Amekuwa mwanachama wa UWT
na aligombea nafasi za Ubunge wa viti maalumu, ingawa hakufanikiwa kuchaguliwa.
Hata hivyo aliendelea kujishughulisha na kazi za UWT na CCM.
Kwa upande wa shughuli za kidini, Mwalimu Tinka, alikuwa mwenyekiti wa
WAWATA jimbo katoliki la Rulenge, kwa kipindi cha miaka mitatu. Kazi hii
aliifanya kwa moyo wake wote na kipindi hicho ndipo alipata nafasi ya kusafiri
sana ndani na nje ya nchi.
Ukitoa kichwa chake kuwa na mvi, anaonekana ni kijana! Siri yake ni nini?
Anasema ni matokeo ya kutotunza kinyongo rohoni mwake. Amejaliwa karama ya
kusamehe! Amekumbana na migogoro mingi katika maisha yake na hasa baada ya
kumpoteza mme wake. Waliomsema vibaya, waliomzulia mambo ya uongo, aliwasamehe,
hakuweka kinyongo rohoni mwake. Mfano kuna wakati alisingiziwa kumshitaki
mwalimu mkuu aliyekuwa amevujisha mtihani wa darasa la saba, mgogoro huu
ulikuzwa hadi mtoto wake Victor akapigwa vibaya na kuumizwa na watu
wasiojulikana. Ingawa uchunguzi uliweza kubaini waliotendea kitendo hicho kwa mtoto wake, Mwalimu Tinka, aliwasamehe
watu hao.
Hivyo tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Mwana mama huyu anayestaafu kazi ya ualimu mwezi huu. Amekuwa Mwalimu wa mfano
shule zote alizozifundisha, amekuwa ni Mwalimu anayewapenda watoto, kuwajali na
kuwashauri, amekuwa mama, mzazi wa mfano kwa kuwalea watoto wake kwa maadili
mema, amekuwa ni mjane aliyesimama imara bila kuyumba, kuwakwaza watoto wake na
kuikwaza jamii. Bahati nzuri watoto wake hawakumwangusha, anamshukuru Mungu kwa
Baraka zake.
Safu hii, inamtakia Mwalimu Theophilda Tinkasimire Tikawa, maisha marefu
wakati anapoanza maisha yake ya kustaafu!
Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754 6331 22
0 comments:
Post a Comment