MWALIMU
NA WATOTO WAKE
Nilikuwa sikupanga kuandika makala hii. Nimekuwa
nikijizuia kuandika juu ya Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ninaogopa
kuwekwa kwenye kundi la wanafiki, wanaoandika kumlilia na kumkumbuka Mwalimu,
lakini matendo yao ni tofauti kabisa na ya Mwalimu. Wanamlilia Mwalimu wakati
wanakataa Shirikisho la Afrika ya Mashariki. Wanamlilia Mwalimu wakati
wanawafukuza wakimbizi na wahamiaji haramu. Wanamlilia Mwalimu wakati wanawagawa watanzania katika makundi
ya vyama, makabila na dini. Wanamlilia Mwalimu wakati wanayashibisha matumbo
yao na kulitelekeza taifa. Wanamlilia mwalimu wakati wana ukumbatia ubepari na
kuabudu fedha. Wanamlilia mwalimu wakati wanashindwa kuitetea na kuilinda
Katiba ya Taifa letu. Wanamlilia Mwalimu wakati wanaitelekeza lugha yetu ya
Kiswahili na kutupilia mbali utamaduni wa taifa letu. Mwalimu, alikuwa Mjamaa,
alikuwa mtetezi wa haki za binadamu, alikuwa msomi na mchambuzi, alikuwa
mwandishi, alikuwa na hekima na busara. Alikuwa na upendo na huruma, zaidi ya
yote alikuwa na “vision”. Mwalimu hakutawaliwa na ushabiki wa kisiasa.
Alikwenda kwa hoja, ukimshinda kwa hoja anakuunga mkono. Hakuna anayeyafuata ya
Mwalimu. Wengi wanaojifanya kumkumbuka ni wanafiki wakubwa. Mifano mingi ya
wanafiki. Sikupenda nichanganywe na wanafiki hao, hivyo niliamua kukaa kimya
kuandika juu ya mwalimu.
Leo nimeamua kuandika kwa vile mhariri wa Raia
mwema, amenitumia ujumbe na kuniomba kuandika kitu juu ya mwalimu, maana Jumatatu
ni Nyerere Day. Na kwamba siku hiyo litakuwepo toleo maalumu la Mwalimu, hivyo
nina uhuru kuandika maneno mengi kiasi nitakacho. Juu ya mwalimu ni vigumu
kuandika maneno yaliyo chini ya elfu moja! Kwa wale wasiomfahamu Mwalimu,
vizuri watashindwa kuandika hata maneno mawili. Lakini wale wanaomfahamu, wale
wanaofahamu uwazi wake, wema wake, uzalendo wake, umaskini wake, ni lazima
washawishike kama mimi kuandika mengi. Kwa vile Nyerere Day, ni mara mmoja kwa
mwaka hakuna hatari ya watu kuzichoka makala ndefu.
Lakini la msingi lililonisukuma kuandika makala
hii ni kitendo cha kukutana na Mtoto wa Mwalimu kwenye Daladala. Nilipanda daladala
ya Posta-Mwenge. Tulipofika kituo cha Palm Beach, mtoto wa Mwalimu Nyerere,
ambaye nilitokea kufahamiana naye siku za nyumba, alipanda kwenye Daladala. Sikushangaa,
ila kusema kweli si jambo la kawaida na hasa kwenye nchi za Afrika; mtoto wa aliyekuwa
Rais wa nchi, tena rais wa kwanza na Baba wa taifa kupanda daladala si jambo la
kawaida. Huyu angekuwa na gari lake, na dreva wa kumwendesha. Huyu angekuwa na
ulinzi mkali nk. Lakini Mtoto wa Mwalimu, aliingia kwenye daladala kama msafiri yeyote yule. Nina imani
ndani ya daladala ile ni wachache au labda hakuna mwingine zaidi yangu mimi
aliyetambua kwamba huyo alikuwa mtoto wa Baba wa Taifa.
Siku nzima nilitafakari juu ya Mwalimu.
Nilitafakari juu ya upekee wake. Nilitafakari juu ya uongozi wake, juu ya
uzalendo wake, juu ya mapenzi yake kwa taifa la Tanzania na watu wake. Lakini
zaidi nilitafakari juu malezi ya watoto wake: Mwalimu aliwapatia watoto wake
malezi ambayo watoto wote watanzania waliyapata.
Watoto wake walisomea shule zile walikosomea watoto wote wa Tanzania. Mwalimu
aliamua kutoa elimu ya bure si kwa watoto wake, bali kwa watoto wote wa
Tanzania. Kama si mpango wa Mwalimu, wa kutoa Elimu ya bure watu wengi leo hii
wasingekuwa na elimu waliyonayo.
Makongoro Nyerere, alipokuwa anasoma Tabora Boys,
nilikuwa Seminari Kuu ya Kipalapala Tabora. Nilitokea kumfahamu kwa karibu.
Alikuwa anakuja kutembea Kipalapala na kula mapera kama watoto wengine. Alikuwa anapenda muziki na
kuimba – pale Kipalapala tulikuwa na bendi ya muziki, hivyo alikuwa akijichanganya
kwenye bendi hiyo na kupiga gita na kuimba. Alikuwa akitembea kutoka Tabora
Boys hadi Kipalapala kwa miguu kama
watoto wengine. Bila kuambiwa kwamba ni mtoto wa Rais, ilikuwa vigumu
kutambua. Alikuwa hana majivuno, kwa sababu alikuwa amelelewa katika mazingira
ya kujitambua kwamba yeye hana tofauti na watoto wengine.
Mwalimu hakumpatia mtoto wake yeyote yule cheo cha
upendeleo ndani ya serikali yake na wala hakuwashawishi watoto wake kuingia
kwenye siasa. Sote tulishuhudia Makongoro, alivyojiingiza kwenye siasa – badala
ya kuiingia kwenye chama cha Baba yake, akajiunga na upinzani.
Rose Nyerere, aliingia Bungeni, baada ya kifo cha Baba
yake. Historia haituonyeshi mtoto wa Mwalimu, aliyependelewa kwa aina yoyote
ile. Kila mmoja mahali alipo, amepambana kama watoto wengine wote
wanavyopambana na maisha na kufanikiwa.
Mwalimu , hakuwapendelea watoto wake. Aliwapenda
watoto wote wa Tanzania. Alijenga shule za watoto wote wa Tanzania, alijenga vyuo vya watoto wote wa
Tanzania. Lengo lake kubwa lilikuwa kuiandaa Tanzania yenye neema kwa vizazi vijavyo . Mwalimu, hakuwapeleka watoto
wake kusoma nje ya Tanzania. Kama kuna mtoto wake aliyefanikiwa kusoma nje,
atakuwa alisaidiwa na Wamisionari. Ninakumbuka Mwalimu mwenyewe akiwa hai,
alisema kwamba mmoja wa watoto wake alipata msaada kusoma Canada, na kwamba
msaada huo ulitolewa na wamisionari.
Nina imani kama Mwalimu angekuwa hai bado, wajukuu
zake wangesoma kwenye sekondari za kata! Mwalimu, hakupenda kuwatenga watoto
wake na jamii. Watoto wake walijiunga na
Jeshi la Kujenga taifa kama watoto wengine. Na kule waliishi na kufanya kila
kitu kama watoto wengine wote walivyokuwa wakifanya.
Leo hii wale wote wanaojifanya wanamlilia Mwalimu,
ni nani anafuata mifano yake? Ni mtoto gani wa kiongozi anapamba daladala? Ni
mtoto gani wa kiongozi anasoma kwenye sekondari za kata? Ni mtoto gani wa
kiongozi asiyesoma nje ya nchi? Tumesikia habari za baadhi ya watoto wa viongozi kuwashikia watu
bastola, lakini hawafikishwi mbele ya sheria. Tumeshuhudia watoto wa viongozi
wakiingizwa kwenye siasa na kupata nafasi za juu. Tumeshuhudia watoto wa
viongozi wakifanya biashara na kupata upendeleo.
Wapo baadhi ya watu wanaomlaumu sana mwalimu kwa
siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Wengine wanamlaumu Mwalimu kwa kile
wanachokiita “Kuitelekeza” familia yake, kwamba hakuwatafutia watoto wake
nafasi nzuri katika mfumo wa serikali. Wanasema mwalimu alikosea, wanasema
mwalimu alidumaza uchumi wetu. Ukweli ni kwamba Mwalimu, aliona mbali zaidi yetu. Siasa ya Ujamaa na Kujigemea, ilikuwa
silaha kubwa ya kupambana na Ukoloni mambo leo. Mwalimu, alijua wazi kabisa,
kwamba utafika wakati tuzidiwe nguvu na Ukoloni Mambo leo, alijua wazi kwamba
tutafikia mahali tuvamiwe na wawekezaji kwa mgongo wa Utandawazi. Hivyo alitaka
kulijengea Taifa misingi ya kujilinda. Kama tungefanikiwa kujenga Taifa la Ujamaa na Kujitegemea,
kamwe tusingemezwa na Utandawazi, bali tungeshiriki kwenye utandawazi. Sasa,
hakuna cha kushiriki ni kumezwa kabisa. Hakuna cha kushiriki bali ni utajiri
wetu kuporwa na wageni. Badala ya kujenga uchumi wa taifa letu, tunajenga na
kukuza uchumi wa mataifa mengine. Badala ya kuulinda Uhuru wetu, tunakubali
kuwa “watumwa”!
Kwa mtazamo wangu, ni kwamba Mwalimu alifanya
makosa mawili katika maisha yake: Kosa la kwanza, ambalo limemgharimu sana, ni
kuwaamini sana watu. Mwalimu, aliwaamini watu. Watu hawa aliowaamini mwalimu,
ndio wale wale walioangusha na kuzika Vision yake. Wale aliowaamini ndio
waliolizika Azimio la Arusha kule Zanzibar. Ni
watu wachache wa aina ya Mzee Kawawa, walibaki waaminifu kwa Mwalimu.
Wengine walikuwa wanafiki, walitaka vyeo na utajiri wa haraka. Walionyesha
unyenyekevu kwa Mwalimu, walizungumza kama Mwalimu na kuvaa nguo kama za
Mwalimu. Baada ya Mwalimu, kutoka madarakani, watu hawa walibadilika haraka,
walianza kuongea lugha nyingine na kuvaa nguo za Kizungu. Kosa la pili la Mwalimu, ni kwenda Haraka. Mfano,
hakujipatia nafasi kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi wa
Azimio la Arusha. Hakuwaandaa watu kupokea Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Alifanya haraka ya kutaifisha, viwanda, mashule na mahospitali. Uharaka huu,
ambao haushangazi kwa Mwanamapinduzi, kama alivyokuwa Mwalimu, ndiyo sababu
kubwa ya kuanguka kwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Mimi ni kati ya watu wanaomlaumu Mwalimu kwa
uharaka wake. Mimi ni kati ya watu wanaoamini kwamba labda kama Mwalimu,
angefanya maandalizi ya zaidi ya miaka 20 – watu wakajadili, wakatafakari na
kutafuta uzoefu wa ujamaa katika nchi za ujamaa za wakati ule, labda Ujamaa
wetu usingekufa. Lakini pia mimi ni miongoni mwa watu wanaotetea Uharaka wa
Mwalimu. Ni kweli kwamba aliona mbali. Alifikiri kwamba bila kujenga Ujamaa kwa
haraka, tungemezwa bila maandalizi.
Baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui
wa Taifa letu kwamba ni Maradhi, Ujinga na Umaskini. Na kwamba silaha pekee ya
kupamba na maadui hawa ni: Ardhi, Siasa safi, Uongozi bora na watu. Aliamini pia kwamba ili haya yote yafanyike
ni lazima tuwe na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa hii, ililinda utajiri
wa Taifa letu. Hatukusikia malalamiko ya madini kusombwa na kupelekwa nje,
hatukusikia wizi wa magogo, hatukuzikia vitalu vya wawindaji. Tulisikia Kisomo cha
watu wazima, tulisikia Siasa ni Kilimo, tulisikia mvua za kwanza ni za kupandia
n.k
Kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Mwalimu
hakuwapendelea watoto wake, bali aliwapenda watoto wote wa Tanzania. Wimbo wetu
wa Taifa, unaonyesha wazi jinsi Mwalimu alivyokuwa na upendo kwa watoto kama
taifa la Kesho. Watoto wanatajwa na kuombewa baraka nyingi katika wimbo huu wa
Taifa. Lakini upendo wake kwa watoto haukuishia hapo, ulivuka mipaka ya
Tanzania, na kuenea kwenye bara lote la Afrika. Vituo kama kile cha Mazimbu,
kule Morogoro, vilianzishwa ili kuwapatia Elimu ya ukombozi watoto wa wakimbizi
kutoka Msumbiji. Lakini pia nchi nyingine nyingi za Afrika kama Angola, Botswana,
Zimbabwe, Namibia n.k. zilipata Kivuli kizuri sana kutoka kwa
Mwalimu.
Tunaposherehekea Nyerere Day, ni watanzania
wangapi, ni viongozi wangapi wanawapenda watoto wa Tanzania, kama alivyowapenda
Mwalimu Nyerere? Ni nani anahakikisha watoto wetu wanapata malezi bora, elimu
bora na afya njema? Ni nani anawaandalia watoto wetu Tanzania ya kesho yenye
neema? Hadi leo hii Taifa letu limeshindwa kusimamia usafiri salama wa watoto
wetu kwenda shule. Watoto wanasukumwa na kunyimwa nafasi kwenye daladala.
Wasomi wa vyuo vikuu wanasumbuka kupata mikopo. Maadili ya watoto wetu
yanakwenda ovyo, watoto wameachwa bila mtu wa kuwaelekeza. Tunachimba madini na
kuwaachia watoto wetu mashimo, tunakata miti kwa fujo na kuuza magogo nchi za
nje na kutunza pesa hizo kwenye uchumi wa nchi za nje. Viongozi wanawapendelea
watoto wao, wanawasomesha nchi za nje kwenye vyuo vizuri. Watoto wengi
wanaobaki wanajengewa Sekondari za kata!
Tumkumbuke Mwalimu Nyerere, kwa kujiwekea mkakati
wa kuongeza mapenzi kwa watoto wetu. Tuwapatie watoto wetu elimu bora, mazingira
bora na yenye kuvutia, afya njema na kuwajengea Tanzania ya kesho yenye Neema.
Mwenye Mungu, amlaze mahali pema peponi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba
yetu wa Taifa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment