MTWARA KUCHELE 2
Makala iliyopita ya Mtwara Kuchele, ni matokeo ya utafiti uliofanywa na
mwandishi wa safu hii akishirikiana na Mtandao wa Madeni na Maendeleo (TCDD)
kama sehemu ya mafunzo ya ushawishi na utetezi yaliyofanyika tarehe 10-13
Septemba 2013 kwa wanachama wake 30 waliotoka kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa,
Ruvuma, Mtwara, Lindi, Mara, Kigoma, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam na Tabora
ilifanya utafiti kwenye manispaa ya Mtwara Mikindani juu ya ukweli kuhusu
sakata la mradi wa Gesi Mtwara lilitokea kuanzia tarehe 17 Mei 2013. Mafunzo
haya yalifanyika kwenye ukumbi wa Lutheran Centre Mtwara na mwandishi wa makala
hii alishiriki kuendesha mafunzo hayo.
TCDD ilifanya mahojiano na watu 257
kwenye kata 7 kati ya 15 za Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambao kati yao
walikuwa Viongozi wa ngazi ya mkoa 4Viongozi wa ngazi ya wilaya 6 Madiwani 10Viongozi wa serikali za
mitaa 46Wananchi wa kawaida 193.
Wote waliohojiwa, waliomba majina
yao yasitajwe, kwa kuogopa kichapo na mateso ya Gwantanamo. Mzee mmoja
alituelezea kwamba:
“Tambiko maalumu
walilolifanya baadhi ya wazee wa mila, wananchi wa Mtwara kwa kushirikisha
viongozi wa dini na makundi ya jamii mara baada ya madhila ya May 23 mwaka huu
ni kiashiria cha kutokukubaliana na mazingira ya utekelezaji wa mradi wa Gesi
licha ya manufaa kwa taifa yanayoelezwa na viongozi”
Mzee huyu aliyekuwa anazungumza kwa
kujiamini, aliendelea kutuelimisha juu ya vurugu zilizojitokeza Mtwara, kwa kauli
mbiu ya “ Haitoki”, kwamba:
“Kwa namna yoyote ile ridhaa ya
wananchi katika utekelezaji wa miradi inayolenga kutumia raslimali iliyolindwa
kwa miongo kadhaa na vizazi vya jamii ya eneo ambapo mradi unakusudiwa
kutekelezwa ni muhimu na vyema kuheshimiwa ili kuhakikisha kwamba laana za vizazi
hivyo hazijengwi katika kizazi kinachofuata ndivyo imani za asili
zinavyotambuliwa
“Hii inadhihirishwa na hatua
zinazochukuliwa na jamii hizo hasa katika kutekeleza matambiko ambapo heshima
maalumu kwa wafu waliotangulia mbele za haki na kuzikwa kwenye maeneo ambako
miradi inafanyika hupewa nafasi ya kuhamisha makaburi kama sehemu muhimu ya
kutekeleza imani na matambiko.”
Ikumbukwe awali lilishatolewa tamko
kutoka Msimbati kwa bibi Samoe Mtiti (106) kuwa ikiwa serikali itaendelea
kulazimisha mchakato wa gesi bila kusikiliza hoja za wananchi angegeuza gesi
kuwa maji, hatua ambayo ililazimu mbinu mbalimbali za kumshawishi bi Samoe
zifanyike ili hali hiyo isijitokeze. Wakazi wa Mtwara, wanaamini nguvu za Bibi Mtiti, kwamba ana uwezo wa kubadili gesi
kuwa maji, na akitaka gesi isitoke, haiwezi kutoka!
Imani hii kwa Bibi Samoe Mtiti,
inaonyesha wazi jinsi suala zima la Gesi, halijaelezwa vizuri. Watu hawana
elimu juu ya Gesi na matumizi yake. Kama bado wanaamini Gesi inaweza kubadilika
kwa nguvu za miujiza ikawa maji, bado kuna kazi kubwa. Serikali ina wajibu
mkubwa wa kuwaelimisha watu wa Mtwara. Kutumia jeshi kuwapiga na kuwanyamazisha
si njia sahihi ya kuleta mabadiliko na maendeleo. Kinachohitajika ni
kuwasiliza, kujadiliana nao, kuwashirikisha na kuwaelimisha.
Kuna habari za kuaminika kwamba Januari
24, 2013 gari lenye namba za usajili T609 BXG la mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni
ofisa wa idara nyeti liliteketezwa kwa moto na wananchi wa Msimbati kwa kile
kinachoelezwa kuwa lilifika kumteka bi Somoe ambaye kijijini hapo anajulikana
kama mkuu wa kaya. Wako tayari kumlinda bibi huyu kwa gharama yoyote ile, kwa
vile wanaamini ana nguvu za kutenda miujiza.
Mzee, tuliyeongea naye, alikuwa
anajaribu kutufafanulia umuhimu wa ushirikishwaji. Kwamba serikali
haikuzingatia hili, na watu wa Mtwara hawakushirikishwa juu ya uchimbaji wa
gesi, kwani raslimali gesi sasa inazungumzwa kama bidhaa haramu kama ilivyo
bangi kwenye vyombo vya dola! Ukitamka suala la gesi kwa wanamtwara wanakuona
kama vile umetumwa kuwadodosa ili uwachomee utambi kwenye jeshi na hatimaye
wapelekwe Gwantanamo kuteswa; hiki ni kituo cha Jeshi cha Nalyendele, ambacho
kimebatizwa jina la Gwantanamo, kutokana na vitendo vya mateso vinavyoendelea
kwenye kituo hicho.
Wananchi wanaolizungumzia suala la
gesi kwa tahadhari wanatamka bayana kuwa
vyombo vya usalama vinavyoshughulikia ukusanyaji wa taarifa
havikujipa kazi ngumu kujua hasa kwa nini wananchi wanashinikiza gesi
haitoki bila kujali imani, vyama na hali zao. Kiongozi wa serikali za mtaa
tuliyeongea naye wakti wa utafiti huu alituelezea kwamba:
“Hili lilichukuliwa kama ajenda ya
kisiasa na watoa taarifa ngazi za juu na ndiyo sababu katika mazungumzo ya
viongozi wa ngazi ya kitaifa wanaliona kama lilikuwa la kisiasa kumbe hii ni
ajenda ya wana-Mtwara imezingatia zaidi maslahi na ustawi wa wana Mtwara na ni matokeo
ya maumivu ya muda mrefu kucheleweshwa kwenye safari ya kufikia maendeleo ya
kweli”. Na kuongezea kwamba:
“Hivyo maamuzi ya matumizi ya nguvu
ndiyo yakachochea zaidi ufa wa mahusiano baina ya serikali na wananchi
hadi sasa ambapo kama mtu anafanya utafiti atabaini kuwa kati ya watu kumi
unaokutana nao ni nadra kukutana na mtu anayesifia matunda tarajiwa ya miradi
ya gesi kwa Mkoa wa Mtwara huku wengi zaidi wakilaumu mazingira ya utekelezaji
mradi huo”
Serikali
bado inatumia nguvu kubwa kuhakikisha inazima sauti za watu wa Mtwara. Hii
inadhihirishwa na tukio la Septemba 12,2013 katika Kijiji cha Shole –Mtwara.
Wanajeshi walitembeza kipigo kwenye kijiji hicho na baadhi ya watu waliumizwa
vibaya kwa taarifa kwamba kulikuwa na
vipeperushi vya kuwazuia watu kushiriki mapokezi ya Mwenge wa uhuru.
Mapokezi mabaya ya mwenge katika wilaya
ya Mtwara yanadhihirisha kuwepo kinyongo miongoni mwa wananchi ambapo ililazimu
kutumika mbinu za kuwaruhusu wanafunzi kuvaa nguo za nyumbani ili isionekane
kwamba Mwenge unapokelewa na wanafunzi
peke yao, hata hivyo mbinu hii haikusaidia kuficha hasira za wananchi.
Baada ya kichapo cha Kijiji cha Shole,
diwani mmoja wa CCM alitwambia kwamba:
“Matumizi ya nguvu kubwa za dola katika
masuala yanayohitaji utashi wa watu ni kiashiria kuwa kuna pengo la mahusiano
baina ya serikali na wananchi na hivyo kuhitaji chombo kingine kuunganisha
makundi yanayotofautiana ”
Kulingana na maelezo ya wananchi, kwa sasa
chombo kinachopewa nafasi katika kuunganisha mahusiano baina ya wananchi na
mamlaka ya serikali ni mijadala ya pamoja ikihusisha asasi za kiraia ili
kurejesha mawasiliano na kuaminiana ambako kumetoweka.
Wananchi wa Mtwara wanasema ukimya
uliopo sasa si kwamba ni utulivu na amani bali ni utulivu pasipo amani, na
wananchi wanafanya hivi kupisha udhalilishaji na manyanyaso ya matumizi makubwa
ya nguvu za dola.
Kimsingi tangu kutolewa agizo la
kutoitishwa mikutano ya wazi inayojumuisha watu kwenye maeneo ya wazi, Mtwara
imekuwa kisiwa kwa muda sasa kutokana na wananchi kutopata fursa ya kukutanika
kujadili maendeleo ya mkoa wao.
“Hivi sasa msimu wa korosho umeanza lakini hatuwezi
kukubaliwa kuitisha mikutano ya kujadiliana juu ya maslahi ya wakulima wa korosho
kutokana na agizo hilo na kwamba ukifanya mkusanyiko wowote utakuwa umevunja
amri halali ya serikali” . Alituelezea kiongozi mmoja wa serikali za
mitaa.
Utekelezaji wa kamata kamata ya
watuhumiwa wa vurugu za Mei 23 ulioendeshwa kwa usiri mkubwa na nyakati za
usiku kwa kutumia wanajeshi, umetajwa pia kufanywa kwa uonevu mkubwa kwa sababu hata wale ambao hawakuwepo mazingira ya tukio kubebwa
kwa chuki na tofauti zilizokuwepo baina ya baadhi ya viongozi wa mitaa na
wananchi wao.
“ Nilibambikizwa shtaka polisi la
kuchoma nyumba ya waziri wakati hata nyumba yenyewe siifahamu ipo wapi na zaidi
ya yote sehemu ya tukio ni mwendo wa siku nzima sasa nilishirikije na
wakati mimi nilishinda kwenye kibanda
changu sokoni hapa ambapo nilishuhudiwa kikiharibiwa na polisi”. Alituelezea
mama mmoja ambaye ana kesi ya kuichoma moto nyumba ya waziri Fulani wa Mtwara.
Pia tume ya haki za binadamu ambayo
ilifanya ziara wilayani humo kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu
inalaumiwa kwa kuchukua muda mrefu kutoa taarifa ya kasoro zilizojitokeza kwa
upande wa serikali katika udhibiti wa vurugu hizo.
“Vyombo
kama tume ya haki za binadamu ndivyo vinavyojenga imani mbele ya jamii na
kuisaidia serikali kujikosoa lakini kuchelewa kwa taarifa za tathmini yao
kuhusiana na zoezi zima vinafanya tukose imani nacho na kuonekana ni mkono
mwingine wa serikali kukusanya taarifa juu wananchi wanasema nini”. Alilalamika
mama aliyebambikizwa kesi na polisi.
Dhamana zilizotakiwa kutolewa
mahakamani ni kiashiria kingine cha kuwafanya wananchi waliokuwa kwenye tukio
hilo wakose haki mbele ya chombo hicho ambapo kesi mojawapo kila mtu alipaswa
kudhaminiwa kwa Tshs 107 Milioni taslimu! Hiki ni kiasi kikubwa kwa watu ambao
kipato chao ni kidogo.
Viwango hivi ni dhahiri vililenga kuwakatisha
tama wananchi katika mchakato mzima wa kupata haki kwa watuhumiwa wa tukio
hilo.
Mwanaharakati mmoja anaeleza kuwa kwa
ujumla kuna ukandamizaji mkubwa katika suala la tangu ukamataji hadi ufikishaji
wa watuhumiwa mahakamani na hata uendeshaji wa mashauri yao na kuomba msaada wa
kisheria kwa watuhumiwa.
Vyovyote vile suala la Mtwara, linahitaji busara na hasa
kutoa nafasi watu hawa wakasilizwa. Kuendelea kutumia nguvu za dola na kuwanyamazisha
ni kuweka kiporo cha maswali yatakayoulizwa kesho na keshokutwa.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22
0 comments:
Post a Comment