MTWARA “KUCHELE”, VURUGU ZA MTWARA JIBU ANALO RAIS KIKWETE.
Moja ya ziara zake katika mkoa wa Mtwara, Rais Jakaya Mrisho Kiwete,
aliwaambia watu wa Mtwara: “Mtwara Kuchele”, maana yake “ Mtwara kumekucha”.
Ziara hii ilifanyika kabla ya vurugu za Mtwara. Mheshimiwa Rais aliwaambia watu
wa Mtwara, kwamba gesi iliyovumbuliwa kwenye mkoa wao itaharakisha maendeleo na
yeye atahakikisha viwanda vingi vinajengwa, vijana wanapata kazi , uchumi wa
mkoa huo unapanda na mji wa Mtwara unabadilika na kufanana Dubai. Na kwa matani,
akawaambia , “ Ningekuwa na uwezo, ningehamisha gesi yote hii na kuipeleka
Bagamoyo”. Maneno haya yako midomoni na moyoni mwa kila mtu wa Mtwara,
aliyesikiliza hotuba hiyo ya Mheshimiwa Rais.
Tarehe 11.9.2013 mpaka tarehe 15.9.2013, nilifunga safari kwenda Mtwara,
kuchunguza chanzo cha vurugu ya “Haitoki”. Hatukuzoea kusikia vurugu hizi mkoa
wa Mtwara. Mwaka 2005, nilikuwa mwangalizi wa uchaguzi mkuu kupitia TEMCO;
nilishuhudia upole wa watu Mtwara. Kampeni za wagombea mwaka huo wa uchaguzi
zilitawaliwa na wali na vinywaji. Wakipikiwa wali na kunywa pombe za kienyeji,
wanaimba na kucheza na kusahau matatizo mengine ya mkoa wao. Hivyo vurugu za
gesi zilipotokea, watu wakafa na mali zikaharibiwa, kila mtu aliyeufahamu mkoa
huu wa Mtwara, alishangaa na kujiuliza kulikoni.
Mtu wa kwanza niliyeongea naye, ni kijana wa Bajaji, ambaye kwa maoni yake
kasheshe zote za vurugu za gesi zilianzishwa
na Hotuba ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, ya kuibadilisha Mtwara
kufanana na Dubai, ahadi ya kujenga viwanda na kuhakikisha vijana wanapata
ajira.
“Huwezi kuamini, hotuba hiyo ya Mheshimiwa Rais, ilianza kuleta matunda,
maana tulianza kuona watu wengi wanakuja kununua viwanja hapa Mtwara. Kuna mzee
ninayemfahamu, aliuuza kiwanja chake ufukweni, kwa bei ya milioni mia mbili
hamsini” alinieleza huyu kijana wa
Bajaji.
“La kushangaza, hata kabla ya kuliona jiwe la msingi la kuijenga Dubai ya
Mtwara, tulisikia kwamba gesi inasafirishwa kwenda Bagamoyo”. Hayo ni maneno ya kijana aliyenibeba kwenye
Bajaji, kutoka maeneo ya Bima- Mtwara kuelekea Makao makuu ya kanisa la KKKT
mjini Mtwara. Hakukubali kunitajia jina lake. “Tunaogopa sana siku hizi, jina
langu likitokea gazetini, nitakamatwa na kupelekwa Gwantanamo, huko nitapigwa
na kuteswa, kama ambavyo watu wengine wamepigwa na kuteswa, wengine hadi leo
hii hawajarudi” alinieleza huyo kijana wa Bajaji. Gwantanamo ni kituo cha Jeshi
cha Nalyendele. Kilikuwa ni kituo cha ukombozi wa nchi ya Msumbiji, lakini leo
hii kimegeuka kuwa ni kituo cha mateso makubwa ya kunyamazisha sauti za “Gesi
haitoki”
“Utani ukawa ukweli, gesi inakwenda Bagamoyo. Rais wetu alitwambia angekuwa
na uwezo, angesomba gesi yote na kuipeleka Bagamoyo. Wakati huo tulijua ni
utani. Tunamjua Rais ana utani mwingi. Lakini baada ya kuambiwa kwamba mabomba
yatasafirisha gesi yetu ya Mtwara kwenda Bagamoyo, tukajua sasa si utani bali
ni kweli. Na tulijua, maana Rais wa nchi ana uwezo wote...” Aliendelea
kunieleza kijana wa Bajaji.
Kwa maelezo ya kijana huyu ni kwamba wazee walipoona Dubai ya Mtwara
inayeyuka, walitaka kuwa na maongezi na Mkuu wa Mkoa, ili kujua kulikoni.
Lakini kwa kiburi, Mkuu wa Mkoa, alikataa kukutana nao. “ Hivyo wazee walipanga
kuitisha maandamano, lakini Mkuu wa Mkoa aliyapiga marufuku maandamano hayo”
Aliendelea kunieleza huyu kijana wa Bajaji.
Kwa maoni ya kijana huyu wa Bajaji, kama Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
angelikubali kuwasikiliza wazee au kuwakubalia maandamano yao, vurugu, vifo na
uharibifu wa mali uliojitokeza Mtwara usingekuwepo. Alihitimisha maongezi yetu
kwa kusema “ Vurugu za Mtwara chanzo chake ni ahadi za Mheshimiwa Rais Kikwete
na kiburi cha Mkuu wetu wa mkoa...”
Ingawa sababu za vurugu zinatajwa mbili ambazo ndizo kubwa, bado kuna mambo
mengine mengi, kama mpasuko ndani ya chama cha CCM mkoani Mtwara, elimu
ndogo watu waliyonayo juu ya masuala ya gesi na suala zima la ushirikishwaji.
Kila mtu unayezungumza naye kwenye mji wa Mtwara, atakwambia kwamba suala zima
la gesi limezungukwa na usiri mkubwa na wananchi hawakushirikishwa. Hata na
viongozi wa serikali za mitaa, madiwani na wenyeviti wa mitaa, wanalalamika
kutoshirikishwa.
Inashangaza kusikia watu wakisema kwamba gesi inakwenda Bagamoyo, hakuna
anayesema inakwenda Dar-es-Salaam. Pia uelewa wa gesi, kuhusu uchimbaji wake hadi hatua ya
kuisafirisha ni mdogo, maana nilielezwa juu ya mzee mmoja ambaye ni mvuvi wa
miaka mingi, siku moja aliona meli kubwa baharini, akarudi na kutangaza kwamba
meli zimeanza kuinyonya gesi na
kuisafirisha bila hata serikali kujua. Kumbe hizo ni meli zinazofanya maandalizi
ya kuanza kuchimba gesi baharini.
Pamoja na uelewa mdogo wa masuala ya gesi, wana hoja nzito: Kama mchakato
wa gesi unachua miaka mingi kumi na tano
hadi ishirini kama wataalam wanavyoeleza, kwa nini wanaona magari yamebeba
mabomba na vituo vya mabomba haya vimewekwa sehemu mbali mbali kutoka Mtwara
hadi Dar-es-Salaam? Maandalizi yanaoyesha gesi inaondoka kesho ama keshokutwa!
Siku tano nilizokaa Mtwara, nikijaribu kutafiti na kuchunguza chanzo cha
vurugu za “Gesi haitoki”, uharibifu wa mali na vifo vilivyotokea, nilipata
majibu yanayofanana kwa karibu sana na maoni ya kijana wa Bajaji. Niliongea na
viongozi wa serikali, vijana wa vijiweni, wazee, wanawake, viongozi wa dini, wafanyabiashara,
vyama vya siasa, na wote majibu yalifanana! Ukimtoa diwani mmoja wa CCM,
aliyekubali jina lake kutajwa wengine wote hawakutaka kwa kuogopa kupelekwa
Gwantanamo. Hivyo si busara hata kulitaja jina la Diwani huyo wa CCM.
Mbali na sababu mbili kubwa za kuanzisha vurugu za gesi nilizozitaja hapo
juu, watu wa Mtwara, wazee kwa vijana
wanaimba historia ya machungu ya mkoa wao. Kwamba: Kulikuwa na reli inatoka
Nachingwea hadi Mtwara, lakini iling’olewa; Kwamba kulikuwa na mtambo wa
kusukuma maji, lakini uliondolewa na kupelekwa sehemu nyingine; Kwamba kulikuwa
na mpango wa Mtwara corridor lakini
ulipotelea kusikojulikana; Kwamba Bandari ya Mtwara ndiyo yenye kina kirefu na
uwezo wa kupokea meli nyingi kwa wakati mmoja, lakini ilitelekezwa na vifaa
vingine kuondolewa na kupelekwa Dar-es-Salaam, Kwamba uwanja wao ndege ni
miongoni mwa viwanja vikubwa vya mwanzo kabisa baada ya uhuru, lakini kiwanja
chao cha ndege kilitelekezwa, wakasikia vikiendelezwa viwanja vingine kama vile
cha Kilimanjaro na cha Dar-es-Salaam; Kwamba kulikuwa na kiwanda cha kubangua
korosho, lakini hakipo tena; kwamba kwa vile Mtwara ulikuwa ni uwanja wa
mapambano ya kuikomboa Msumbiji, hakuna aliyependa kuwekeza au kufanya kazi
Mtwara; Kwamba kulikuwa na kilimo cha pamba lakini kimekufa jumla; kwamba
barabara ilikuwa mbaya hadi siku za hivi karibuni walipojengewa daraja la Mkapa
na Barabara ya lami ambayo hata hivyo bado zaidi ya kilomita thelathini hazijakamilika; Kwamba bei ya korosho
imeendelea kuwa chini na umasikini umeongezeka na kubwa zaidi kwamba ahadi za
Songosongo kuleta maendeleo mkoa wa Lindi mbona hazijatekelezwa?
“Uamuzi wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Bagamoyo, umeamsha
mshikamano miongoni mwa wananchi, kusema kweli imetonesha vidonda vya historia
ya machungu ya Mkoa wetu. Na kusema ukweli hakuna aliye nyuma ya vurugu hizi;
ni mshikamano wa wananchi wa Mtwara” alinieleza diwani wa CCM, ambaye jina lake
nalitunza kwa sasa.
Kufuatana na maelezo ya diwani huyu ni kwamba vuguvugu za “Gesi haitoki” zilikuwa
na hatua kuu nne:
Baada ya kusikia matangazo ya kuisafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda
Bagamoyo, na baada jitihada za kukutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa
kushindikana, wanamtwara waliibuka na kauli mbiu ya: “ Gesi kwanza, vyama
baadaye”. “Vyama vyote vya siasa viliungana na kuwa na sauti moja juu ya gesi”
alinieleza diwani huyu wa CCM.
Hatua ya pili, ilikuja na kauli mbiu ya “ Gesi kwanza, uhai baadaye”. Hapa
ndipo mapambano yalianza baina ya polisi na wananchi. Kijana wangu wa Bajaji
aliniambia kwamba mapambano hayo yalikuwa makubwa na yakutisha! “Kama wananchi
tungelikuwa na silaha, mapambano haya yangekuwa mabaya sana” Alinieleza kijana
huyu.
Hatua ya tatu ya vuguvugu na vurugu za Gesi katika Mkoa wa Mtwara, ilikuja
na kuli mbiu ya “Gesi haitoki” .Hapa ndipo serikali ilipoamua kutumia nguvu
kubwa, mali ziliharibiwa na watu walikufa. Hadi sasa serikali inasema walikufa
watu watatu. Lakini kuna habari za pembeni zinazosema watu waliokufa kwenye
machafuko haya ni zaidi ya 18, na
wengine wanasema ni kama 100! Hata hivyo hadi leo hii bado watu wanakamatwa,
wanapelekwa Gwantanamo, wanateswa na wengine hadi leo hii hawajarudi kwenye
majumba yao.
Hatua ya nne ya vuguvugu na vurugu za Gesi ni “Gesi itoke tu lakini...”.
Sasa hivi kila mtu unayekutana naye Mtwara, anasema “Gesi itoke”. “Wameamua
kutuletea jeshi letu la Wananchi, kutupiga na kutufanya vibaya, Gesi itoke,
lakini tutasusia shughuli zote za serikali na tunawasubiri kwenye uchaguzi wa
2015” Alinieleza mfanyabiashara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Tarehe 14.9.2013, tulishuhudia Mwenge wa Uhuru ukiingia Mtwara kimya kimya
kwa ulinzi wa kutisha. Siku tatu kabla ya ujio wa Mwenge, vipepererushi na
ujumbe mfupi kwenye simu za viganjani ulianza kupita kuwahamasisha watu kususia
sherehe za Mwenge. Ni kwamba Mtwara, wanaheshimu sana ujumbe mfupi wa simu,
hata bila kujua unatoka wapi; ujumbe ukisema maduka yasifunguliwe, agizo
linatekelezwa; ujumbe ukisema hakuna kutoka nje, mitaa inashinda bila watu.
Hivyo na ujumbe wa kususia sherehe za Mwenge, ulitekelezwa kiasi kikubwa;
Wanafunzi na wafanyakazi wa serikali ndio waliojitokeza kuupokea Mwenge wa
Uhuru.
Kwa kuangalia kwa nje, ni kwamba sasa hivi Mtwara kuna utulivu, lakini
hakuna amani. Kuna utulivu kwa vile jeshi linatumia nguvu na watu hawana tena
jukwaa la kutoa maoni yao, wanaishi kwa woga. Jeshi linaweza kutesa miili yao
na kuweka utulivu wa nje tu, lakini ndani ya mioyo yao wana makovu makubwa na
hasira. Mtu mwenye hekima, angeshughulikia kuponya makovu na wala si kuendelea
kutumia nguvu kubwa kuwalazimisha watu kukubali yale wasiyoyaelewa vizuri na
wala kufahamu jinsi watakavyofaidika nayo.
Baadhi ya watu wameamua kuishi porini kwa kuogopa nguvu za Jeshi. “Kuna mtu
aliyekaa porini siku saba kwa kuwaogopa wanajeshi. Mtu huyu alikuwa ni dreva
kwenye kampuni Fulani ya mhindi, baada ya siku saba aliporudi kazini,
alifukuzwa kwa utoro. Kitendo cha kumfukuza kilimshutua sana, na baada ya siku
chache alikufa kwa shinikizo la moyo. Mifano kama hii tunayo mingi, lakini
tumeamua kukaa kimya” Alinieleza mwenye kiti wa mtaa ambaye hakutaka jina lake
litajwe.
Ubakaji, kuwangilia watu kinyume na maumbile, udhalilishaji na mateso
mengine ni baadhi ya vitu vinavyotajwa kutokea na kuendelea kutokea Mtwara. “Vurugu
zote hizi Mbunge wetu wa Mtwara mjini alisimama upande wa wananchi na kutetea
haki za Mkoa wetu bila woga. Hata Mkuu wa wilaya ya Mtwara, alikuwa upande
wetu. Hawa wawili wanakubalika na wakisema jambo tunasikia, ingawa tumemgomea
Mkuu wetu wa Wilaya kushiriki sherehe za Mwenge”. Alinielezea mama mmoja ambaye
alionekana kama mwanasiasa, lakini hakutaka kusema ni wa chama gani
“Si kweli kwamba hatutaki Gesi itoke na kuwanufaisha watanzania wengine.
Hoja yetu ni je Gesi ikitoka, sisi tunabaki na hali gani? Umasikini? Dubai yetu
iko wapi? Kama ni kuisafirisha Gesi kwenda kuiuza nchi za nje kwa nini isisafirishwe
kwa kupitia bandari ya Mtwara? Kama ni kuzalisha umeme, kwa nini mitambo ya
kuzalisha umeme isijengwe Mtwara, na umeme ukasafirishwa kwa nguzo?”
Alilalamika kiongozi mmoja wa dini niliyeongea naye.
Katika harakati za kurudisha imani ya wananchi, serikali imewapeleka baadhi
ya watu wa Mtwara , nchini Thailand kujifunza mafanikio ya miradi ya Gesi.
Lakini kuna manung’uniko kwamba safari hiyo haikuwa ya lazima, ni matumizi
mabaya ya fedha, wakati kuna kipindi cha Baragumu la Msimbati, kinachorushwa
kwenye luninga na kuelezea mafanikio ya Gesi ya Songosongo. Kwa nini watu hawa
wasingepelekwa Songosongo kujifunza mafanikio ya huko kuliko kutumia fedha
nyingi kuwasafirisha watu kwenda nchini Thailand? Hata hivyo na uchaguzi wa
nani aende Thailand, haukuwa wa wazi. Tulipoongea na mmoja kati ya wale waliokwenda Thailand, alisema “ Mimi nafikiri nilichanguliwa kwa vile niko
karibu na Waziri Fulani”
Mtu wa kumaliza vurugu za Mtwara, ni Rais mwenyewe. Kila mtu tuliyeongea
naye, alitoa jibu hili. “Tunamtaka Rais wetu aje hapa abadilishe usemi wake,
aje atwambie kwamba sasa Dubai ni ndoto, mbali na hapo hatumtaki mtu yeyote
hapa...” Alinieleza mzee ambaye ilionyesha ana ushawishi mkubwa kwenye jamii
inayomzunguka..
Kwa kifupi ni kwamba watu wa Mtwara wamepoteza imani na Mkuu wao wa Mkoa,
hawataki kumsikia waziri wa Elimu, ambaye wanasema alikwenda Mtwara kuwatukana:
“Mtwara mnafanya kazi ya kutiana mimba
mambo ya Gesi mtayafahamu?” Hawataki kumsikia Shehe Mkuu wa Mkoa. Pia hawataki
kumsikia waziri wa nishati na madini,
ambaye naye wanasema aliwatukana. Wanamtaka Rais wao ambaye wakati wa kuomba
kura, alienda kuongea nao, na sasa wanataka aende aongee nao.
Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment