KODI YA LINE ZA SIMU NI
MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA?
Wakati bei ya muda wa
maongezi iko juu na yenye utata; na hili
si kwa Vodacom peke yake bali ni kwa mitandao yote ya simu; wakati tunashangaa na
kulalamika ni kwa nini wawakilishi wetu Bungeni, wasilione hili na kuhakikisha
bei ya muda wa maongezi inakuwa na unafuu ili tuweze kufikia kile kinachoitwa
maisha bora kwa kila Mtanzania tunaongezewa na hii kodi ya line za simu. Pamoja
na faida kubwa itakayotokana na kodi hii (kama tulivyoelezwa, ambavyo si
tofauti sana na yale tunayoelezwa kila mwaka bila kuona utekelezaji) bado huu
ni mzigo mkubwa kwa mtu anayeitumia simu yake kwa matumizi ya lazima na muhimu.
Binafsi nina mashaka na uwiano wa fedha na
muda. Kwamba ninapolipa shilingi elfu moja ni mfumo gani unatumika kuhakikisha
kwamba muda nilioutumia thamani yake ni shilingi elfu moja. Kuna mfumo gani wa
wazi wa kuhakikisha fedha tunazolipa kwa kununua vocha za muda wa maongezi
zinawiana na muda; mfano kama ni elfu moja kwa daika tatu ikajulikana, ikiwa
kinyume mtu akalalamika Pia na uwiano wa
kodi na matumizi ya line ya simu; kwamba anayetumia simu kuzalisha milioni moja
kwa mwezi, alipe kodi ya shilingi elfu moja na yule anayezalisha elfu kumi kwa
mwezi alipe kodi ya line ya simu shilingi elfu moja na anayebeep akapigiwa
alipe kodi ya elfu moja kwa mwezi! Tumelishwa kasumba na makampuni haya ya simu
(Sawa na madawa ya kulevya) kwamba fedha zikiisha kwenye simu ni lazima
utakwenda mwenyewe kununua. Hatulalamiki ili kutaka kujua uwiano wa fedha na
muda. Kama mtandao una wateja milioni mmoja, hata ukigonga shilingi miambili
kwa kila mteja, unakuwa una fedha nyingi. Inajionyesha wazi kwamba Vodacom, na
mitandao mingine ya simu wanatengeneza faida kuliko kutoa huduma. Hii ni sawa
kwa vile wao wanafanya biashara. Basi, biashara yao iwe nzuri kwa kutoa huduma
iliyo juu ya kiwango na si chini ya
kiwango. Na biashara yao iwe na uwiano wa fedha na muda. Lakini pia kwa vile
kodi ya line za simu imeanza, kuwepo uwiano kati ya matumizi ya simu na ulipaji kodi.
Kwa mitambo ya kisasa,
makampuni ya simu yanaweza kujua ni watu gani wanatumia huduma yao kutengeneza
faida kubwa na ni watu gani wanatumia mitandao yao kwa huduma ya lazima kama
kutoa taarifa za misiba, kutuma karo na matumizi mengine madogo madogo. Mfano,
wale wanaotumia huduma ya Mpesa, wale wanaopitishia zaidi ya milioni kumi
kwenye mtandao kwa mwezi, watalipa je kodi ya elfu moja sawa sawa na
anayepitisha elfu hamsini kwa mwezi?
Wakati baadhi yetu tunajiuliza
mantiki ya serikali inayoamini kwenye kauli mbiu ya Maisha bora kwa kila
Mtanzania, kukubali viwango vya muda wa maongezi kuwa sawa kwa watanzania wote;
maskini wa vijijini, wafanyakazi na wafanyabiashara wakubwa, bado tunaletewa na kodi hii ya line za simu iliyo sawa kwa
watanzania wote. Katika hali ya kawaida na kwa nchi ambayo bado katiba yake
inatambua na kufuata Ujamaa, mkulima wa kijijini anayetumia simu yake kuita
gari la wagonjwa kumbemba mama mjamzito,
atalipa muda wa maongezi sawa na mfanyabiashara anayetumia simu yake kufanya
“Dili” la bilioni tano? Au mkulima wa vijijini anayetumia simu kusambaza ujumbe
wa msiba kwa ndugu na jamaa, atalipa muda wa maongezi sawa sawa na
mfanyabiashara anayetumia simu yake kusambaza ujumbe wa kudai madeni yake kwa
wateja wake zaidi ya bilioni kumi?
Kwa wengine mawasiliano
ya simu ni anasa, wengine ni biashara na walio wengine ni huduma ya muhimu.
Kuna wanaotumia simu kutongoza wanawake na kuzungumza mambo ya mapenzi siku
nzima, hawa wakilipishwa kodi ya line za simu ni sawa, kuna wanaotumia simu
kufanya biashara na kuwasiliana na wateja, hawa nao wakilipishwa kodi ya line
za simu ni sawa, lakini wale wanaotumia
simu kama huduma muhimu kwenye jamii kuwatoza kodi ya line za simu si sawa
sawa. Mfano mtu anayenunua simu ya kiganjani kwa bei ya shilingi milioni moja,
na wakati mwingine anazo zaidi ya tano za bei hiyo hiyo, maana kila mtandao una
simu yake, atalipaje kodi ya line za simu na muda wa maongezi sawa sawa na mtu
anayenunua simu ya kiganjani kwa bei ya shilingi hamsini?
Kiasi kikubwa cha watu
wa vijijini wenye watoto wao wanaoishi na kufanya kazi mijini, wanakuwa na simu
ambazo mara nyingi hawana uwezo wa kununua muda wa maongezi, wanachofanya ni
“Kubeep”, wasipotumiwa muda wa maongezi basi wanapigiwa simu na watoto wao. Leo
hii hawa kuwatoza kodi ya line za simu ni kuwalazimisha kuachana na huduma hii
muhimu.
Wakati tunategemea
serikali iwe upande wa wananchi na kuwalinda dhidi ya makampuni makubwa ya
uwekezaji, tunashuhudia kinyume chake. Makampuni ya simu kama yalivyo makampuni
mengine yapo hapa kufanya biashara na kuendelea kuwapumbaza wananchi:
Tarehe 27 Januari
Alhamisi mwaka 2005 vyombo vya habari vilitoa habari inayosema: " Vodacom
yawaangukia wateja wake - KAMPUNI ya simu za
mkononi Vodacom imetoa maelezo yaliyosababisha hitilafu na kukatika kwa
mawasiliano katika mtandao wake uliosambaa nchini kote Ijumaa iliyopita.....
Tunawaomba radhi wateja wetu wapendwa kwa usumbufu uliotokea na hasa katika
kipindi cha sikukuu na tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kuwa tatizo
limerekebishwa na huduma za Vodacom zitaendelea kama kawaida....Taarifa
ilimkariri Jose dos Santos, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, akisema kama ishara
ya kuonyesha masikitiko na nia njema, wateja wote wa Vodacom watapewa SMS 10 za
bure kwa mkupuo kuanzia Januari 27,2005".
Wateja wa Vodacom,
walifurahia meseji za bure. Kama kawaida yetu watanzania hatupendi kutafakari
na kuyaangalia mambo kwa undani. Ofa hii inaweza kumfumba mtu macho akaacha
kuona mambo mengine muhimu. Na kwa vile Vodacom, hawana mfumo wa kutoa maoni na
kujadiliana na wateja wao, furaha hii ya meseji ilibaki kuwa furaha ya mtu
mmoja mmoja au vikundi. Ukweli ni kwamba jambo hili linaigusa jamii nzima maana
mtadao wa Vodacom umeenea nchi nzima. Na jambo la mawasiliano linamgusa kila
mwananchi. Mtwara hadi Karagwe, Kigoma hadi Arusha, wanaguswa na mafanikio au
matatizo ya Vodacom. Mawasiliano si anasa, ni kitu muhimu na cha lazima katika
jamii yoyote ile.
Mbali na na sms za bure,
makampuni haya ya simu yamekuwa yakitoa misaada ya madawati na vitu vingine
vidogo vidogo vya kuwapumbaza watanzania na kuwafumba macho, lakini ukweli ni
kwamba makampuni haya yanapata faidi kubwa. Kufuatana ukweli huo, serikali
iliyo makini ingetengeneza mfumo wa viwango tofauti vya bei ya muda wa
maongezi; watu wanaozitumia simu kwa anasa, wawe na viwango vyao, watu
wanaozitumia simu zao kwa biashara wawe na viwango vyao na watu wanaotumia simu
kwa matumizi ya lazima na muhimu wa wawe na viwango vyao. Na kwa mantiki hiyo
hiyo basi hizi kodi za line za simu zitolewe na makampuni yenyewe, hata hivyo
yanakuwa yamevuna vyakutosha. Kwa mfumo huu, tunaweza kuimba wimbo wetu wa
maisha bora kwa kila Mtanzania, vinginevyo ni kuendelea kuwahadaa wananchi na
kuwalazimisha kuendelea kuishi kwenye umaskini mkubwa.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment