MWANA MAMA
MAREHEMU GRACE AIKAELI MBOWE
Mungu ailaze
mahali pema peponi roho ya Marehemu Grace Aikaeli Mbowe! Pia Mungu awafute
machozi watoto wake, mme wake na ndugu na jamaa wote! Siandiki tanzia hii kwa
vile Grace, alikuwa dada wa rafiki yangu Mheshimiwa Freeman, wala siandiki
tanzia hii kwa vile marehemu alikuwa ni dada wa Mwenyekiti wa Chadema, na wala
siadiki tanzia hii kwa vile Grace, alizikwa na Askofu na viongozi wa Serikali
na vyama siasa.
Na wala
siandiki tanzia kumsifia dada Grace, kuwa ni mtu mwema, mwenye huruma, mwenye
upendo, mvumilivu na mnyenyekevu, maana kila mtu akifikia hatua hiyo ya kulala
milele, hizo ndizo sifa zinazomsindikiza. Labda mchawi! Lakini katika hali ya
kawaida; unyenyekevu, upendo, uvumilivu na huruma, ni sifa za kila binadamu
anapoiacha dunia yetu na kujiunga na muumba wake.
Na wala sina
lengo la kumpamba Grace kwa sifa nyingi, maana mimi ni nani? Mwenye uwezo wa
kumsifu ni Muumba wake aliye Mbinguni. Hata hivyo ni imani yangu kwamba sifa
zake zimeimbwa na wanasiasa ambao wameteka nyara wasifu wa marehemu na kuugeuza
kuwa mtaji wa siasa zao.
Hata hivyo
siwezi kuukataa ukweli kwamba ninalia na wanaolia na kusikitika na
wanaosikitika. Msiba wa ndugu yako ni msiba wako pia, msiba wa rafiki yako ni
msiba wako pia. Pamoja na kwamba natafuta maneno ya kuwatuliza wafiwa na
kuonyesha kushiriki msiba huu, halikuwa lengo langu kubwa:
Naandika
tanzia hii kuendeleza kusudio la kuanzisha safu hii ya Mwana Mama. Hii ni
nafasi ya kuandika Mwana mama ambaye ametoa mchango mkubwa katika taifa letu,
lakini hasikiki na wala hakuna kilichoandikwa juu yake. Na marehemu Grace, ni miongoni mwa akina mama
hao.
Ni bahati
mbaya kwamba dada yetu Grace, amesindikizwa na malumbano ya kisiasa! Vyombo
vyote vya habari, mitandao ya kijamii, imeamua kuweka pembeni mchango wake
katika taifa letu na kuelekekeza nguvu zote kwenye siasa. Ni jambo la
kusikitisha sana kwamba Tanzania tunapoteza mwelekeo na uandishi wetu umekuwa
ni wa kuongozwa na kuelekezwa na
wanasiasa.
Chadema na
CCM, ni vyama vya siasa ambavyo vimetekea nyara wasifu wa dada yetu Grace.
Badala ya kutuelezea mchango wake katika maisha yake ya miaka hamsini kasoro,
tunaletewa siasa na mambo mengi ya kuzusha kwa faida ya siasa na wanasiasa.
Grace
alifariki katika ajali ya gari katika
eneo la Kabuku, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wakati akielekea jijini Dar es
Salaam. Watu wengine walipoteza uhai katika ajali hiyo. Hivyo ni kifo kama vifo vingine.
Bahati mbaya
hadi sasa hivi hakuna anayetwambia kwamba dada yetu Grace alikuwa mwanamke wa pili
kusajiliwa na bodi ya wahandisi nchini akiwa kama Ofisa mpimaji (Quantity
Surveyer) baada ya kuhitimu elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitengo
ardhi (ARU).
Hii ni sifa
kubwa kwa marehemu. Ni wazi kwa ujuzi huo na kisomo chake ametoa mchango mkubwa
katika taifa letu. Hapana shaka kwamba kwa kifo chake, pengo kubwa limetokea
katika fani yake ya uhandisi. Haya ndiyo tunataka tuyasikie, na haya ndiyo
yanatusukuma kuandika tanzia hii, ili kumlilia huyu dada yetu ambaye kifo
kimemchukua mapema.
Kuiacha sifa
hii kubwa na kuendeleza nyimbo za siasa, ni kumkosea haki marehemu. Kila
binadamu ana uhuru wa kufanya mambo yake binafsi. Suala la mapenzi ya siasa ni
suala la mtu binafsi, lakini huduma kwa jamii, kama hii ya(Quantity Surveyer)
ambayo dada yetu alikuwa amesomea, si suala binafsi. Hili ni suala la kijamii
na ni suala la kitaifa. Kwa kujenga sifa ya mtu ndani ya jamii, masuala ya
kijamii yanashika nafasi ya kwanza mbele ya masuala ya binafsi. Hata kama
Grace, alihama chama cha Chadema, chama ambacho kaka yake ni Mwenyekiti, hili
ni suala binafsi ambalo si muhimu sana ukilinganisha na mchango wa dada Grace
katika jamii kubwa ya watanzania.
Kama Grace,
alifika chuo kikuu na kusoma masomo hayo ya sayansi, ni wazi huko nyuma
alifanya vizuri. Tunataka tusikie wasifu wake katika shule za sekondari.
Tungependa kusikia na kufahamu alikuwa ni mtoto wa namna gani wakati akisoma.
Huo ndio wasifu wa Grace na wala si huu wa Chadema na CCM.
Nina imani kuna mambo mengine mengi aliyoyatenda dada Grace, zaidi ya haya ya Chadema na CCM. Hivyo
ninategemea, baada ya wasifu huu wa uchokozi, wengine watajitokeza na kutuimbia
wasifu chanya wa dada yetu.
Mpaka mazishi yake yakaongozwa na Askofu, ina maana
huyu alikuwa mtu wa sala, alikuwa mtu wa kanisa. Tusikie wasifu wake wa
kumpenda Mungu wake na watu wake. Huu ndiyo wasifu wa dada yetu Grace na wala si huu wasifu wa CCM na Chadema.
Dada Grace alikuwa na watoto. Huyu alikuwa mama wa namna gani? Tunataka
kusikia watoto wake wakiimba wasifu wake. Lakini vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii, imewanyamazisha watoto wa marehemu na kuteka nyara wasifu wa mama yao
mpenzi.
Grace, ni mtu aliyesimama kama mtu, kama mama wa familia. Kuunganisha
wasifu wake na wa ndugu zake, ni kumkosea haki kama binadamu. Hata hivyo kama
nilivyodokeza hapo juu, huyu ni mama mhandisi, kuna mengi ya kuandika juu yake
na kumbukuka zaidi ya kumeza wasifu wake makusudi mazima.
Pia, watanzania tujifunze kuandika na kuheshimu wasifu wa watu. Tusichanganye
wasifu na vitu vingine ambavyo vinakuja na kupita. Daima wasifu wa mtu ni vitu
vile visivyopita! Ni mchango wa marehemu
katika jamii husika; na mara nyingi tunafikiria mchango chanya!
Mungu amlaze mahali pema dada yetu mpendwa Grace Aikaeli Mbowe.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment