GESI HAITOKI! IKITOKA ITABADILIKA KUWA
MAJI: KINJEKITILE NAMBA 2
Ikumbukwe awali lilishatolewa tamko
kutoka Msimbati kwa bibi Samoe Mtiti (106) kuwa ikiwa serikali itaendelea
kulazimisha mchakato wa gesi bila kusikiliza hoja za wananchi angegeuza gesi
kuwa maji, hatua ambayo ililazimu mbinu mbalimbali za kumshawishi bi Samoe
zifanyike ili hali hiyo isijitokeze. Wakazi wa Mtwara, wanaamini nguvu za Bibi Mtiti, kwamba ana uwezo wa kubadili gesi
kuwa maji, na akitaka gesi isitoke, haiwezi kutoka!
Ni yale yale ya Kinjekitile, ya
kubadilisha risasi kuwa maji. Kwa haraka na kwa tabia ya kuangalia mambo juu
juu unaweza kusema kwamba huu ni upuuzi. Lakini hapa kuna kitu cha kujifunza.
Ule muujiza wa Kinjekitile, wa kugeuza risasi kuwa maji uliwapatia wapiganaji
hamasa na nguvu za kupambana na wavamizi. Hata kama walishindwa, walikufa kwa
heshima kubwa wa kipambana na silaha za kisasa kutetea nchi yao. Historia inawatambua
na kuwaheshimu. Hivyo si lazima miujiza hii iwe upuuzi wakati wote.
Kuna habari za kuaminika kwamba Januari
24, 2013 gari lenye namba za usajili T609 BXG la mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni
ofisa wa idara nyeti liliteketezwa kwa moto na wananchi wa Msimbati kwa kile
kinachoelezwa kuwa lilifika kumteka bi Somoe ambaye kijijini hapo anajulikana
kama mkuu wa kaya. Wako tayari kumlinda bibi huyu kwa gharama yoyote ile, kwa
vile wanaamini ana nguvu za kutenda miujiza.
Imani hii kwa Bibi Samoe Mtiti,
inaonyesha wazi jinsi suala zima la Gesi, halijaelezwa vizuri. Watu hawana
elimu juu ya Gesi na matumizi yake. Kama bado wanaamini Gesi inaweza kubadilika
kwa nguvu za miujiza ikawa maji, bado kuna kazi kubwa. Serikali ina wajibu
mkubwa wa kuwaelimisha watu wa Mtwara. Kutumia jeshi kuwapiga na kuwanyamazisha
si njia sahihi ya kuleta mabadiliko na maendeleo. Kinachohitajika ni kuwasikiliza,
kujadiliana nao, kuwashirikisha na kuwaelimisha.
Vinginevyo watasimama kidete na miujiza
ya Bibi Samoe Mtiti, itawatia hamasa kupigania haki yao na kukubali kufa, ili
historia isiwacheke baadaye. Kama nilivyosema hapo juu si lazima miujiza iwe
upuuzi wakati wote. Ni wazi hakuna muujiza wa kuibadilisha gesi kuwa maji na
wala risasi kugeuka na kuwa maji. Lakini muujiza wa kubadilisha akili za mtu,
akaacha kufikiri na kutenda kama wanyama wengine upo; tunashuhudia vitendo vya
kujitoa muhanga kwa matumaini kwamba kule “Mbinguni” watakuta maisha mazuri na
dhawabu kubwa.
Hivyo kiongozi yeyote mwenye busara,
anaposhughulika na watu wenye Imani aina ya Bibi Samoe Mtiti, ni lazima awe
makini kutotumia nguvu. Maana imani ikikolea, mtu anaacha kufikiri na kuyaweka
maamuzi yake mikononi mwa watu wengine. Wanachosema anafuata kwa kuogopa
kuambiwa hana imani! Au kuambiwa yeye ni msaliti! Ni vigumu kupambana na mtu wa
namna hii, hata kama serikali ina nguvu za kutisha.
Mzee, aliyetuelezea habari hizi za Bibi
Samoe Mtiti, wakati tukifanya utafiti juu ya vurugu za Mtwara, alikuwa akijaribu kutufafanulia umuhimu wa
ushirikishwaji. Kwamba serikali haikuzingatia hili, na watu wa Mtwara
hawakushirikishwa juu ya uchimbaji wa gesi, kwani raslimali gesi sasa
inazungumzwa kama bidhaa haramu kama ilivyo bangi kwenye vyombo vya dola!
Ukitamka suala la gesi kwa wanamtwara wanakuona kama vile umetumwa kuwadodosa
ili uwachomee utambi kwenye jeshi na hatimaye wapelekwe Gwantanamo kuteswa;
hiki ni kituo cha Jeshi cha Nalyendele, ambacho kimebatizwa jina la Gwantanamo,
kutokana na vitendo vya mateso vinavyoendelea kwenye kituo hicho.
Kwa maoni ya mzee huyo ni kwamba kwa
namna yoyote ile ridhaa ya wananchi katika utekelezaji wa miradi inayolenga
kutumia raslimali iliyolindwa kwa miongo kadhaa na vizazi vya jamii ya eneo
ambapo mradi unakusudiwa kutekelezwa ni muhimu na vyema kuheshimiwa ili
kuhakikisha kwamba laana za vizazi hivyo hazijengwi katika kizazi kinachofuata
ndivyo imani za asili zinavyotambuliwa.
Wananchi wanaolizungumzia suala la
gesi kwa tahadhari wanatamka bayana kuwa
vyombo vya usalama vinavyoshughulikia ukusanyaji wa taarifa
havikujipa kazi ngumu kujua hasa kwa nini wananchi wanashinikiza gesi
haitoki bila kujali imani, vyama na hali zao. Hili lilichukuliwa kama ajenda ya
kisiasa na watoa taarifa ngazi za juu na ndiyo sababu katika mazungumzo ya
viongozi wa ngazi ya kitaifa wanaliona kama lilikuwa la kisiasa kumbe hii ni
ajenda ya wana-Mtwara imezingatia zaidi maslahi na ustawi wa wana Mtwara na ni matokeo
ya maumivu ya muda mrefu kucheleweshwa kwenye safari ya kufikia maendeleo ya
kweli.
Hivyo maamuzi ya matumizi ya nguvu
ndiyo yakachochea zaidi ufa wa mahusiano baina ya serikali na wananchi
hadi sasa ambapo kama mtu anafanya utafiti atabaini kuwa kati ya watu kumi
unaokutana nao ni nadra kukutana na mtu anayesifia matunda tarajiwa ya miradi
ya gesi kwa Mkoa wa Mtwara huku wengi zaidi wakilaumu mazingira ya utekelezaji
mradi huo.
Matumizi ya nguvu kubwa za dola katika
masuala yanayohitaji utashi wa watu ni kiashiria kuwa kuna pengo la mahusiano
baina ya serikali na wananchi na hivyo kuhitaji chombo kingine kuunganisha
makundi yanayotofautiana.
Wananchi wa Mtwara wanasema ukimya
uliopo sasa si kwamba ni utulivu na amani bali ni utulivu pasipo amani, na
wananchi wanafanya hivi kupisha udhalilishaji na manyanyaso ya matumizi makubwa
ya nguvu za dola.
Kimsingi tangu kutolewa agizo la
kutoitishwa mikutano ya wazi inayojumuisha watu kwenye maeneo ya wazi, Mtwara
imekuwa kisiwa kwa muda sasa kutokana na wananchi kutopata fursa ya kukutanika
kujadili maendeleo ya mkoa wao.
Hivi sasa msimu wa korosho umeanza lakini hawawezi
kukubaliwa kuitisha mikutano ya kujadiliana juu ya maslahi ya wakulima wa korosho
kutokana na agizo hilo na kwamba ukifanya mkusanyiko wowote utakuwa umevunja
amri halali ya serikali.
Utekelezaji wa kamata kamata ya
watuhumiwa wa vurugu za Mei 23 ulioendeshwa kwa usiri mkubwa na nyakati za
usiku kwa kutumia wanajeshi, umetajwa pia kufanywa kwa uonevu mkubwa kwa sababu hata wale ambao hawakuwepo mazingira ya tukio kubebwa
kwa chuki na tofauti zilizokuwepo baina ya baadhi ya viongozi wa mitaa na
wananchi wao.
Kwa ujumla kuna ukandamizaji mkubwa katika
suala la tangu ukamataji hadi ufikishaji wa watuhumiwa mahakamani na hata
uendeshaji wa mashauri yao na kuomba msaada wa kisheria kwa watuhumiwa. Dhamana
zilizotakiwa kutolewa mahakamani ni kiashiria kingine cha kuwafanya wananchi
waliokuwa kwenye tukio hilo wakose haki mbele ya chombo hicho ambapo kesi
mojawapo kila mtu alipaswa kudhaminiwa kwa Tshs 107 Milioni taslimu! Hiki ni
kiasi kikubwa kwa watu ambao kipato chao ni kidogo.
Viwango hivi ni dhahiri vililenga kuwakatisha
tama wananchi katika mchakato mzima wa kupata haki kwa watuhumiwa wa tukio
hilo.
Kulingana na maelezo ya wananchi, kwa sasa
chombo kinachopewa nafasi katika kuunganisha mahusiano baina ya wananchi na
mamlaka ya serikali ni mijadala ya pamoja ikihusisha asasi za kiraia ili
kurejesha mawasiliano na kuaminiana ambako kumetoweka.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment