SWALI LANGU KWA RAIS OBAMA: GAIDI NI NANI?
Juzi nilikutana na mtu wa kawaida kwenye mitaa, akaniambia yeye
hafurahishwi na ujio wa Baraka Obama, maana rais huyu anakuja Tanzania
kufuatilia maslahi ya Amerika. Na mwingine akaniambia Raisi Obama, anafuatilia
nyendo za China, na kasi kubwa ya China kushirikiana na nchi zinazoendelea. Kuna
wengine walioniambia kwamba Obama, ataleta neema kubwa Tanzania. Kila mtu ana
mawazo yake juu ya ujio wa Obama Tanzania. Kule Afrika ya kusini, tumeshuhudia
wanafunzi wakiandamana kwa mabango kupinga ujio wa Rais Baraka Obama, kwenye
nchi yao. Tunaweza kusema ujio wa Obama katika nchi za Afrika, utapokelewa kwa
hisia tofauti. Pamoja na ukweli kwamba Obama ni mwana wa Afrika, bado kuna
ukweli kwamba yeye kama Rais Amerika, ujio wake ni nguvu za Amerika na sera za
Amerika. Na tujuavyo Amerika iko mstari wa mbele kupambana na ugaidi
unaofafanuliwa kwa misamiati ya kimarekani.
Ningepata bahati ya kukutana Rais Obama, bahati ambayo ni ndoto za mchana, ningemuuliza
swali langu moja: Gaidi ni nani? Sina lengo la kuutetea ugaidi kwenye makala
hii, ninajua ugaidi ni mbaya, unawagusa waliomo na wasiokuwemo; usumbufu wa
kusafiri nchi za nje unatugusa sote, mtu ukipanda ndege unakuwa na wasi wasi,
ukiwa kwenye majengo makubwa na kwenye mkusanyiko wa watu roho haitulii! –
hakuna aliye salama mbele ya ugaidi na hasa ugaidi huu wa kulipua ndege na
majengo. Ninachofanya kwenye makala hii ni kuwataka wasomaji wangu
tutafakari juu ya Ugaidi. Ukienda Afghanistan na Iraq, watu watakwambia gaidi
ni Osama au ni Wamarekani? Wakati Afrika ya Kusini ikipigania uhuru wake,
Mandela, alikuwa ni gaidi namba moja. Hata kule Kenya wakati wa huru,
wapiganaji wa Mau Mau, walijulikana kama Magaidi. Hivyo kila mtu anaweza kuwa
gaidi kutegemeana na nyakati na mapambano yaliyopo. Ndo maana ningetamani sana
kusikia Mheshimiwa rais Obama, ana jibu gani kuhusu gaidi! Yeye kwa maoni yake
gaidi ni nani?
Kuiingilia nchi huru kijeshi kama Amerika ilivyofanya kule Pakistan katika
harakati za kumwangamiza Osama, ni ugaidi au ni kitendo chenye baraka zote kwa
vile ninalenga kuyalinda maisha ya watu wenye thamani kubwa hapa duniani?
Kitendo hicho kingefanywa na nchi nyingine kingelaaniwa kwa nguvu zote. Kwa
vile kimefanywa na kiranja wa dunia, sote tunafyata mkia na kushangilia.
Je ugaidi ni njia mojawapo wa wanyonge kutetea haki zao? Ugaidi ni njia
mojawapo ya kupigania uhuru na haki ya kujitawala? Mwenye nguvu kubwa kama
ilivyo Amerika njia pekee ya kupambana naye ni ugaidi? Inawezekana Osama,
alikuwa akiwatetea wanyonge? Bila kutaka kuingia sana kwenye mjadala wa ugaidi
na ugaidi ni nini, niendeleze swali langu kwa Raisi Obama. Gaidi ni nani?: Je
kifo cha Osama kitamaliza ugaidi duniani? Kwamba baada ya yeye kufa hatusikii
tenda vitendo vya kigaidi? Bila kuwa na dunia yenye haki na usawa; dunia ambayo
kila mtu anaruhusiwa kuishi na kuheshimiwa; dunia ambayo binadamu wote
tunatumia rasilimali kwa usawa; dunia ambayo haina ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa
dini ugaidi utakwisha?
Kwa Amerika Osama, alikuwa gaidi na kwa watetezi wa haki za Waislamu, Osama
alikuwa shujaa na mtetezi wa wanyonge. Wakati Wamarekani wanashangilia kifo cha
Osama; kinyume kabisa na utaratibu wa maisha ya mwanadamu, maana tumefundishwa
kupenda adui na kutoushangilia msiba wa mwenzio, Pakistan maandamano
yanaendelea kupinga mauaji wa Osama. Maana yake ni kwamba uelewa wa Ugaidi kwa Wamarekani,
ni tofauti kabisa na uelewa wa ugaidi kwa watu wa Pakistan na nchi nyingine
ambazo bado ziko kwenye harakati ya kujikomboa kiuchumi na kupiga hatua ya
maendeleo.
Dunia nzima inapigana na ugaidi. Inataka kutokomeza
ugaidi. Kusema kweli hata na mimi ugaidi siupendi kabisa. Ugaidi unawaingiza
waliomo na wasiokuwemo, unapoteza maisha ya watoto wadogo na watu wema na
wapenda amani. Hatuwezi kufanikiwa
kupambana na ugaidi kama hatukubali kufutilia mbali mawazo potofu kwamba kuna
binadamu bora kuliko wengine. Kama hatukubali kufuta mawazo kama ya le ya
Hitler, kwamba kuna kitu kama “Royal Blood”. Watoto wa Gaza, wanaoshuhudia
unyama wa leo unaofanywa na Waisraeli, hawezi kulifuta hili akilini mwao mpaka
pale watakapokuwa na kushika bunduki au kuvaa mabomu na kwenda kulipiza kisasi
kwa kujilipua.
Obam, alipoitembelea Israeli, alisema hata yeye
hawezi kumvumilia mtu anayerusha makombora kuelekea walikolala mabinti zake
wawili. Hivyo hivyo hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kuvumilia kuona maisha
ya watoto wake yakiteketea. Hata Wapalestina hawawezi kuvumilia hilo. Hakuna
mtu anayeweza kuvumilia hilo; kama hana nguvu za kutosho atajaribu kutumia
mbinu zozote zile kuyalinda maisha ya watoto wake, maisha yake binafsi na
maisha ya watu wengine wanaomzunguka. Inawezekana mbinu hizi zikawa na sura ya
ugaidi, lakini kwa vyovyote haziwezi kuwa na tofauti kubwa na yule anayetumia nguvu
za kijeshi kuyalinda maisha ya mtoto wake au watu wake.
Waisraeli, wanasema wanawalinda
watu wao. Kama wao wana haki ya kufanya hivyo, kwa nini na Wapalestina wasiwe
na haki ya kuwalinda watu wao. Rais wa Amerika, Mheshimiwa Barack Obama,
anasema Amerika, itashirikiana na kila mpenda Amani. Ni imani yangu kwamba
dunia nzima inapenda Amani. La msingi ni kuhakikisha kwamba tunayatumia yote
tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa usawa. Tunaitutumia ardhi kwa usawa na
kuyalinda mazingira kwa pamoja, tunatumia chakula kwa usawa na kuhakikisha
kwamba hakuna anayekufa kwa njaa, vinginevyo njaa inaweza kuvunja amani,
wanaokufa kwa njaa wanaweza kushawishika kuchukua silaha ili kupambana na wenye
chakula kingi. Tutumie maji kwa usawa, vinginevyo vita mbaya inayoweza kutokea
huko mbele ni kugombania maji. Hadi leo hii kuna sehemu hapa duniani ambako
maji yanavunja amani. Kwa ufupi ni kwamba tutumie rasilmali za dunia hii kwa
usawa. Maana yake ni kwamba, Obama, asishughulike tu na usalama wa Amerika,
bali atafute chanzo cha yale yanayoweza
kuvunja usalama si wa Amerika peke yake bali wa dunia nzima. Dunia ikiendelea
kugawanyika kwenye makundi ya walionacho na wasiokuwa nacho, wenye madaraka
makubwa na wanyonge, wenye damu safi na wenye damu chafu, wenye dini bora na
wenye dini duni, wenye rangi bora ya ngozi na wenye rangi duni, wenye haki na
wasiokuwa na haki, itakuwa ni ndoto kujenga Dunia yenye amani. Kama Obama,
anasimamia mabadiliko, kama kauli mbiu yake katika kampeni na katika utawala
wake – ni lazima ahakikishe mabadiliko ya kweli yanakuja si Amerika peke yake,
bali dunia nzima. Mwenyezi Mungu, alituumba tufaidi kila kilicho hapa duniani
kwa usawa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment