BURIANI TA MWALIMU ELIAS BILAULI LWAKATARE
Tunamlilia na kumsindikiza kwa pambio Baba yetu, Babu yetu, Mwalimu wetu,
Ndugu yetu, Rafiki yetu, Jirani yetu, muumini mwenzetu na Mtanzania mwenzetu. Wimbo wa “Engozi za
Omukama..” (Upendo wa Mungu) umsindikize kwenye nyumba yake ya milele. Kwa umri
wa miaka 95 na miezi 9, tuna haki ya kuimba “Engozi za Omukama”. Tulipenda
kuendelea kuishi naye na kufurahia “Ubaba” na “Ualimu wake”, lakini yametimia,
na jina la aliye juu lihimidiwe!
Ta Mwalimu Elias Bilauli Lwakatare, aliaga dunia tarehe 8.11.2013 jijini Dar-es-Salaam,
na kusafirishwa hadi kijijini kwake Ibwera Bukoba na kuzikwa kwa heshima kubwa.
Umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuaga mwili wake kwenye Ibada katika kanisa
la Lutheran Msasani, na umati mkubwa uliojitokeza kwenye mazishi yake kule
Bukoba ni ishara kwamba mzee huyu alikuwa miongoni mwa watu waliotoa mchango
mkubwa wa kulijenga Taifa letu la
Tanzania.
Pamoja na ukweli kwamba Mwalimu Elias, alikuwa na watoto wenye majina
makubwa kama vile Bwana Samwel Lwakatare,
mtoto wake wa kwanza, ambaye kumbukumbu zinavyoonyesha ndiye Mwafrika wa kwanza
kuwa General Manager wa mgodi wa Almasi wa Mwadui na badaye alishika nyadhifa kubwa serikalini, Dkt Johnson Lwakatare,
bingwa wa magonjwa ya moyo, Bwana Muganyizi Lwakatare, mwanasiasa machachari na
wengine waliobaki; Mwalimu Elias Lwakatare alilijenga jina lake yeye mwenyewe
na hakuruhusu umaarufu wa watoto wake uyumbishe msimamo wake ndani ya jamii.
Aliishi maisha ya kawaida ya kijijini, akishirikiana na kila mwana kijiji.
Kabla magari hayajawa mengi na usafiri ukiwa wa shida, Mwalimu Elias,
alilitumia gari lake kuwasafirisha watu kutoka Ibwera hadi Bukoba mjini.
Alikuwa dreva mzuri sana, na aliendesha gari hadi kwenye uzee wake wa
miaka themanini.
Wale wote aliowafundisha na wale waliozaliwa wamkuta amestaafu ualimu
waliendelea kumtambua na kumheshimu kama Ta Mwalimu Elias. Ualimu, ulikuwa
ndani ya damu yake, aliendelea kufundisha hata baada ya kustaafu na alitamani
watoto wote, wa ndugu, jamaa na majirani zake wasome na kufanikiwa kama watoto
wake mwenyewe. Hivyo kijijini Ibwera, alikuwa ni mtu wa kutafuta shule na
kuwaelekeza wazazi kuwapeleka watoto wao kwenye shule mbali mbali. Wakati
ambapo shule za sekondari zilikuwa chache, Ta Mwalimu Elias, alikuwa kama
mitandao ya kisasa ambayo ukibofya unapata habari yoyote unayoitafuta. Watu
wengi walikimbilia kwake kupata habari za shule na elimu kwa ujumla. Aliwapenda
vijana na alifurahia mafanikio ya vijana wote wa Ibwera na eneo lote la Ikimba.
Ta Mwalimu Elias, aliupenda sana mchezo wa mpira wa miguu, aliucheza na
kuufundisha kwa vijana. Alipenda kuimba na alishiriki kwenye kwaya na
kuiongoza, pia alikuwa kiongozi msaidizi wa kikundi cha tarumbeta. Pia alikuwa
skauti na kuwaongoza vijana kwenye uskauti.
Mbali na mambo ya Elimu, Ta Mwalimu Elias, alikuwa mtu mcha Mungu. Alikuwa
muumini mwaminifu wa kanisa lake la KKT usharika wa Katwe. Alilihudumia kanisa
lake na kulipenda, lakini pia aliheshimu imani za watu wengine. Alikuwa karibu
sana na Wakatoliki waagilikana na Waislamu. Hakuwa na ubaguzi wa kidini, na
jambo hili limejionyesha wazi wakati wa mazishi yake; watu wa dini mbali mbali
walishirikiana kumsindikiza kwenda kwenye nyumba yake ya milele.
Ta Mwalimu Elias, alizaliwa katika kijiji cha Kibeta jirani kabisa na mji
wa Bukoba, tarehe 12/01/1918, akiwa mtoto wa kwanza wa Mama Mkalinda na Baba
Ntangeki. Alikuwa na wadogo zake Paulo Kyebereka, Ephraim Mutagurwa, Josephata
Katente, Geraldina na Evelina.
Msingi wa Imani na Elimu aliupata kutoka kwa Mzee Isaya Mukoyogo, ambaye
alikuwa karibu na familia yao. Mafunzo ya Imani aliyoyapata kutoka kwa Mzee
Isaya, yalipelekea Ta Mwalimu Elias, kuingizwa kwenye Imani ya Kikristu na
kubaziwa na Mchungaji W. Hopser wa kanisa la Kashura, mchungani huyo ndiye
alimchagulia jina la Elias, na kuzaliwa upya katika imani ya Kikristu, wazazi
wake wa ubatizo walikuwa Mzee Isaya Mukoyogo na mke wake.
Ta Mwalimu Elias, alisoma shule ya msingi Kibeta hadi
darasa lanne na kuhamia Ditrict school ya Kigarama. Enzi hizo hapo hapo
Kigarama kulikuwa na Chuo cha Ualimu, hivyo alijiunga na chuo cha Ualimu na
kuhitimu vizuri. Baada ya kuhitimu alifanya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo
hapo hapo Kigarama. Alipoonyesha kufuzu, aliajiriwa kama Mwalimu wa Kanisa la
Kilutheri shule ya Kibeta, akilipwa mshahara wa shilingi 18, wakati huo zikiwa ni fedha
nyingi. Baada ya kufundisha kwa muda hapo Kibeta, alipandishwa cheo na kuwa
mkuu wa shule hiyo. Kwa vile Ta Mwalimu Elias, alikuwa mwalimu mzuri na
alifanya kazi yake kwa moyo wake wote, alipandishwa cheo tena kuwa Mkaguzi wa
shule, kazi aliyoifanya kwa miaka mingi hadi kustaafu.
Ta Mwalimu Elias, mbali na kazi za Ualimu na ukaguzi wa mashule, alifanya
kazi nyingine nyingi za kanisa. Alishiriki katika kutafsiri Biblia katika Lugha
ya Kihaya ambayo inatumika hadi leo hii. Kazi za kanisa zilimpatia nafasi ya
kusafiri sana ndani na nje ya nchi. Alitembelea nchi za Denmark, Sweden, Norway
na Uingereza.
Ta Mwalimu Elias, alifunga ndoa takatifu na Mama ma Ephrazia Mitanda,
katika Kanisa la KKT Kashura mnamo mwaka wa 1939. Katika ndoa yao hiyo
wamejaliwa kuwapata watoto 12, wajukuu 46 na vitukuu 40. Watoto wao ni: Samuel
Lweyemamu, Elisa Kaijage,Lena Hulda,Kokushubila;Emiliana Kokubelwa;Johnson,Muhumuliza;Dina
Kokuganyilla; Godwin Mushobozi,Gracewell Mwesiga, Lilian Murungi;Stella
Abela;Wilfred,Muganyizi na Victor Bainomugisha. Kati yao, wawili Godwin
Mushobozi na Gracewell Mwesiga, wametangulia mbele ya haki, Mungu awalaze
mahali pema peponi.
Ta Mwalimu Elias na mke wake Ma Ephrazia Mitanda, waliendelea kuishi
Kibeta-Buguruka hadi mnamo mwaka 1952, walipohamia Ibwera, Bukoba vijijini. Na
wote sasa wamezikwa huko huko Ibwera, ingawa bado wana shamba lao la Kibeta
ndani ya Manispaa ya Bukoba.
Pamoja na kumlilia Ta Mwalimu Elias, awe kwetu mfano wa kuigwa. Mzee wetu
alifanya kazi za serikali, kazi za dini na kazi za kijamii bila kuwa na
mgongano wa maslahi. Amekuwa muumini wa Kanisa la KKT, lakini aliwafundisha
watoto wa dini zote na kuwapenda, ameshirikiana na watu wote kwenye jamii bila
kuangalia imani za dini zao, hakutumia umaarufu wa watoto wake kama kinga ya
aina yoyote ile au ukuta wa kumtenganisha na jamii iliyomzunguka, alikuwa
mzalendo na mwaminifu wa Taifa lake na alilolitumikia kwa nguvu zote hadi siku
yake ya mwisho. Apumzike kwa amani Ta Mwalimu Elias Bilauli Lwakatare. Amina.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22.
0 comments:
Post a Comment