AGPAHI - GEITA

KIKUNDI CHA KINAMAMA TUSHIKAMANE MASUMBWE – GEITA.
 
Kama kawaida ya safu hii, ni kukuletea habari za Mwana mama. Tunajitahidi kukuletea habari za akina mama ambao wako penzoni na habari zao hazisikiki wala kuandikwa. Na kawaida tumekuwa tukiwaletea habari za mama mmoja mmoja na tutatendelea kufanya hivyo.
Leo imejitokeza tofauti kidogo tu, na tunakuletea Kikundi cha Kinamama Tushikamane kutoka Wilaya mpya ya Mbogwe mkoa wa Geita. Kikundi hiki kilianzishwa na wanawake wanaoishi na virusi vya UKIMWI, kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu maambukizi yaVVU na UKIMWI, kuelimisha jamii juu ya unyanyapaa na kunyanyapaliwa, kuikumbusha jamii kwamba mtu mwenye virusi vya ukimwi ana haki ya kuoa na kuolewa na kupata mtoto asiye na maambukizi, kuelimisha jamii juu ya kuzuia maambukizi mapya wa VVU na la msingi kwao ni kuelimisha juu ya kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuhamasisha watu kupima afya zao; maana bila kupima ni vigumu kujua mgonjwa na mzima na vigumu kuwaanzishia dawa wangojwa na hasa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Tumeamua tuandike juu ya wanawake hawa kwa pamoja, maana wote wanafanya kitu kinachofanana. Wote hawa wana sifa ya Mwana Mama, ambaye tunamwandika kwenye safu hii. Pamoja na mambo mazuri ya kutetea na kuulinda uhai, wanayoyafanya wanawake hawa, wana sifa moja kubwa ya kushinda vita kubwa ya kujinyanyapaa wao wenyewe. Hatua hii ni kubwa na ni muhimu sana katika zoezi zima la kupambana na UKIMWI. Mtu akijinyanyapaa mwenyewe, anapoteza maisha haraka sana. Mtu akijinyanyapaa mwenyewe, anaufanya ugonjwa huu kuwa wa siri na matokeo yake hawezi kupata msaada kwa wakati. Wanawake hawa wa Masumbwe, wameshinda mtihani huu na kuna haja ya kuwapongeza na kuwatolea mfano, ili watu wengine wajifunze na kuiga mfano wa wanawake hawa wa Masumbwe.
Septemba 26 2013, wakati wa kufungua Jengo la Kliniki ya huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi, kituo cha afya cha Masumbwe, wilaya ya Mbogwe, wanawake hawa walisimama mbele ya umati mkubwa uliokuwa umekusanyika siku hiyo na kutangaza mafanikio yao; kwamba miongoni mwao zaidi ya wanawake  6, ambao wana virusi wamefanikiwa kujifungua watoto wasiokuwa na virusi; kwamba wanafuata masharti ya kumeza dawa za kupunguza makali ya virusi; kwamba wanachangiana fedha za kusaidiana katika kikundi chao.
Wanawake hawa, walisimama na kujitangaza, bila aibu yoyote ile, kwamba wao walipimwa na kukutwa na virusi, na walifuatilia dawa bila kuchoka na matokeo yake wameweza kujifungua watoto wasiokuwa na virusi na wenyewe wanaendelea vizuri na wanaweza kushiriki shughuli zote za kuzalisha mali. Watoto hao waliozaliwa bila virusi walionyeshwa pia kwenye mkutano huo.  Wanawake hawa waliendelea kuwahimiza watu wengine kujitokeza kupima, ili watakao kutwa na virusi, wapate dawa za kurefusha maisha na kumkinga mtoto asipate maambukizi.
Kwenye picha hapo chini, wanaonekana wanawake hao wa Masumbwe, wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi. Ni moyo wa ushujaa na kujikubali katika jamii ambayo bado ina unyanyapaa, maana wakati wanawake hao wakisoma risala yao, kuna maneno yaliyokuwa yakipita miongoni mwa wasikilizaji kwamba hao ni “Wauaji”. Wanajijua kwamba wao ni wagonjwa, lakini wanaendelea kusambaza. Kuna sauti za chini chini zilizokuwa zikisikika kwamba “ Hawa ni watu wa kuawa, ili wasiendelee kusambaza ugonjwa”. Kila mtu alikuwa na la kwake kusema, lakini sauti ya pamoja, ikiungwa mkono  na mgeni rasmi, shirika la AGPAHI, waandishi wa habari, wageni waalikwa na watu wengine wenye mapenzi mema, ilikuwa ikiiunga mkono juhudi za wanawake hawa wa Masumbwe.
Watu wote wanaopambana na UKIMWI, wamekuwa wakihimiza watu kujitolea kupima afya zao, ili watakaokutwa na virusi, waanzishiwe dawa za kupunguza makali, lakini jambo ambalo limesisitizwa kwa nguvu zote ni kukinga maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Shirika  la AGPAHI ambalo kwa msaada wa watu wa Amerika, limeweza kujenga jengo la Kliniki ya huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kituo cha Masumbwe, wamekuwa mstari wa mbele kuhimiza kuzuia virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.Tunaweza kusema kwamba huo ndiyo utume wa AGPAHI, kupunguza au kufuta kabisa uwezekano wa virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Hivyo mafanikio ya akinamama wa Masumbwe ni mafanikio ya AGPHAHI pia. Ni mafanikio wa watu wa Amerika wanaotoa fedha zao ili zisaidie katika zoezi hili la kupunguza makali ya virusi vya UKIWMI na kuzuia virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Na pia ni mafanikio yetu sote maana tunaimba wimbo wa Tanzania  bila UKIMWI inawezekana; iwezekane kwa vitendo na kupiga hatua!
Pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto katika zoezi zima. Akinamama hawa wa Masumbwe, pamoja na kufurahia kujifungua watoto wasiokuwa na virusi, bado walielezea changamoto zinazowakabili katika jamii; Changamoto kubwa ni ya unyanyapaa, ingawa wao wanajitahidi sana kutojinyanyapaa, bado huko mtaani wananyoshewa kidole kwamba wanazaa watoto wakati wao ni wagonjwa, wengine wanawalaumu kuendelea kufanya tendo la ngono wakati wakijua kwamba wao ni wagonjwa; hivyo kuna ambao wanawapachika majina ya “Wauaji”; na kwamba watoto wao wanapocheza na watoto wengine, wanabaguliwa na kunyoshewa kidole kwamba wao ni waathirika wa UKIMWI na kwamba uchumi ni kikwazo kikubwa, maana wakati mwingine hawapati matunzo kulingana na afya za zilivyo.
Ili kupambana na tatizo la ukata, wanawake hao wameamua kufungua akaunti benki na kujiwekea sheria ya kuchanga shilingi 500, kila mwezi. Wakati wa kufungua kituo chao hapo Masumbwe, walikuwa na shilingi 30,000 kwenye akaunti yao. Kwa kuguswa na moyo wa wanawake hao, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe akishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Geita, walianzisha harambee ya kuchangia mfuko huo wa akina mama wa tushikamane na kuweza kuutunisha.
Vyo vyote vile hawa ni wanawake wenye sifa zote  za kuandikwa kwenye safu hii ya Mwana Mama.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment