TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA: USHUHUDA KUTOKA GEITA NA SHINYANGA.
Tarehe 26 Septemba,2013 Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mheshimiwa Magalula S.
Magalula, alifungua jengo la kliniki ya huduma na matunzo kwa watu wanaoishi na
virusi vya Ukimwi (VVU), katika kituo cha Afya Masumbwe wilaya mpya ya Mbogwe –
Mkoa wa Geita. Na tarehe 27 Septemba 2013 Mheshimiwa AnnaRose Nyamubi, Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga, akafungua jengo jingine la Kliniki ya tiba na matunzo kwa
watu wenye VVU, katika kituo cha Afya Kambarage – Shinyanga mjini.
Majengo haya mawili, la Masumbwe na la Shinyanga, yamejengwa na Shirika la Kitanzania
AGPAHI(Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative) kwa msaada wa watu wa
Amerika, kupitia shirika la CDC (Centre for Disease Control).
Shirika la AGPAHI lilianza kazi nchini Tanzania, mwaka wa 2011, (Kwa
kuzaliwa na Shirika la Kimataifa la EGPAF ‘Elizabeth Glaser Pediatric AIDS
Foundation’ na kuendeshwa na watanzania) linafanya kazi zake katika Mikoa ya
Geita, Shinyanga na Simiyu katika jitihada za kupambana na Virusi vya Ukimwi
katika Mikoa hii mitatu kwa msaada wa watu wa Marekani na kwa kusaidiana na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala
za Mikoa na Serikali za mitaa yaani TAMISEMI ili kuwezesha upatikanaji wa tiba
na matunzo kwa watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini pia
upatikanaji wa huduma ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto.
Kwa kipekee shirika hili la AGPAHI, linakazania huduma hii ya kuzuia virusi
kutoka kwa mama mwenda kwa mtoto. Kwa maoni ya shirika hili jambo hili
linawezekana kabisa, kila mtu akitimiza wajibu wake; wananchi wakapima afya zao
kwa hiari, serikali na wadau wengine wakatoa huduma za uhakika, tunaweza kwa
asilimia 100 kuzuia virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na hatimaye
kutokomeza virusi kwa watoto.
Majengo haya mawili yaliyofunguliwa Masumbwe na Shinyanga, ni mazuri na
yamejengwa kisasa. Yana idadi ya vyumba 5 ambavyo ni chumba cha usajili wa
wagonjwa, chumba cha ushauri nasaha, vyumba viwili vya waganga na chumba cha
kutunzia dawa. Pia majengo haya yana
vyoo vizuri na vya kisasa. Ni majengo yanayolenga kupunguza unyanyapaa na watu
wenye virusi kujiona wametelekezwa. Huko nyuma kwenye vituo vya afya huduma hii
ilitolewa kwenye chumba kimoja na msongamano ulikuwa mkubwa kiasi cha
kuwakatisha tama wagonjwa na wengine kuamua kuikimbia huduma hii.
Pamoja na majengo mawili yaliyofunguliwa, AGPAHI, inafanya kazi pamoja na
watendaji wa Mkoa na Halmashauri katika kuboresha huduma kwenye vituo 68
vinayotoa huduma za matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI na
vituo 284 vinavyotoa huduma za kukinga maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto(PMTCT) katika mikoa hiyo mitatu.
Kliniki ya Masumbwe ilianza kutoa huduma ya matunzo na matibabu mwaka 2006
kwa kupata msaada kutoka shirika la CDC chini ya uratibu wa Elizabeth Glaser
Pediatric Aids Foundation na baadaye AGPAHI (Tunaweza kusema kwamba AGPAHI ni
mtoto wa Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation). Hadi kufikia Juni 2013,
kliniki ya Masumbwe imeweza kuhudumia jumla ya wateja 1,437, wanaume wakiwa 538
na wanawake 899. Kati yao ni watoto 106 walio chini ya miaka 15. Katika
kliniki hii, wateja 1,030 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU na UKIMWI
na kati yao ni watoto 79 walio chini ya umri wa miaka 15. Kufikia Juni 2003
jumla ya wateja 714 walikuwa hai na kati yao watoto 50.
Kliniki ya Kambarage- Shinyanga nayo ilianza kutoa huduma mwaka 2006. Nayo
kufikia Juni 2013, imeweza kuhudumia jumla ya wateja 1,713 wanaume wakiwa 488
na wanawake 1,225.Kati yao ni watoto 113 walio chini ya umri wa miaka 15.
Katika kliniki hii wateja 854 wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU na
UKIMWI. Kati yao ni watoto 66 walio chini ya umri wa miaka 15. Hadi Juni mwaka
huu jumla ya wateja 553 walikuwa hai na wanaendelea kutumia dawa za kupunguza
makali ya VVU na UKIMWI, na kati yao watoto 9 chini ya miaka 15 wako hai.
Takwimu hizi zinaonyesha umuhimu wa kliniki za tiba na matunzo kwa watu
wanaoishi na VVU na UKIMWI, maana idadi ya vifo inapungua sana na hasa
uwezekano wa Mama wenye virusi kuzaa watoto wasiokuwa na virusi. Ushuhuda
uliotolewa na wanawake 16 wa Kliniki ya Masumbwe, ni kwamba jambo hili
linawezekana. Wanawake hawa wanaishi na virusi, lakini kwa vile wanatumia dawa
za kufubaza virusi, wamezaa watoto wasiokuwa na virusi. Tatizo linalojitokeza
ni mwitikio mdogo wa wanawake wajawazito kupima ili kujua hali zao. Mkurugenzi
mtendaji wa shirika la AGPAHI Bwana Laurean Rugambwa, kwenye risala yake kwa
Mgeni Rasmi, wakati wa kufungua jengo la kutoa huduma ya tiba na matunzo kituo
cha Masumbwe, wilaya na Mbogwe, alieleza
tatizo hili: “ Ndugu mgeni rasmi, hatua ya kwanza kabisa katika jitihada
za kuzuia maambukizi ya virusi toka kwa mama kwenda kwa mtoto ni kupima kwa hiari
wajawazito wote. Taarifa zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi
Juni mwaka huu, kinamama 2,649 tu kati ya 6,796 (39%) waliopimwa hali zao
katika wilaya ya Bukombe na Mbogwe ikiwamo. Kiwango hiki ni kidogo sana hivyo
ndoto ya kutokomeza maambukizi kwa watoto haitaweza kutimia. Hivyo ni wajibu
wetu sote kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kuwafikia akinamama wengi
zaidi”
Na kwa upande wa Shinyanga, Bwana Laurean Rugambwa, alieleza: “.. Taarifa
zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha Mwezi Aprili hadi Juni ni kinamama 1857 tu
kati ya 2968(63%) ndio waliopimwa hali zao katika manispaa ya Shinyanga. Vile
vile, katika halmashauri ya wilaya Shinyanga vijijini, kipindi cha Aprili hadi Juni,
akinamama 2,434 tu ndio waliopima hali zao kati ya 4,150 (59%) ya akinamama
ambao waliotakiwa kupima hali zao. Kiwango hiki bado kiko chini hivyo ndoto ya
kutokomeza maambukiki kwa watoto haitaweza kutimia.”
Ushuhuda huu wa Bwana Laurean Rugambwa, mkurugenzi mtendaji wa AGPAHI,
unaonyesha kwamba “TANZANIA BILA UKIMWI INAWEZEKANA” kila mwananchi akitimiza
wajibu wake. Jambo hili haliwezi kutimia kwa hotuba tu za majukwaani bila kuhimizana,
kushauriana, kuelekezana na kuwa na mifumo ya utekelezaji. Panahitajika
jitihada za pekee kuhakikisha wanawake wajawazito wote wanapima hali zao ili
kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Ni lazima sote kushiriki kama alivyobainisha Bwana Laurean Rugambwa
kwenye risala yake:
“ ...Zaidi ya hayo, wanaume lazima tubadili tabia, na pia tuwe tayari
kupimwa afya zetu tukiwa pamoja na wenzi wetu. Tukifikia hatua hii, tutaweza
kuzuia maambukizi ya VVU kwa watoto wanaozaliwa kwani baba na mama watakuwa
wanajua afya zao kabla ya kuamua kupata mtoto, na mama akipata ujauzito afahamu
kwamba anaweza kupata dawa za kuzuia maambukizi kutoka kwake kwenda kwa mtoto.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumezuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda
kwa mtoto”
Mbali na changamoto hii ya idadi ndogo ya wajawazito kupima hali zao, Bwana
Laurean Rugambwa, alielezea changamoto nyingine: “ Ndugu mgeni rasmi,
changamoto kubwa tunazozipata katika manispaa hii ya Shinyanga ni kupotea kwa
wateja walioanza kupata huduma katika kliniki zetu, unyanyapaa wa watu wanaoishi
na virusi vya ukimwi katika jamii na ushiriki mdogo wa wanaume katika huduma za
uzuiaji wa maambukimi ya VVU toka kwa mama kwenda kwa mtoto”.
Changamoto hii ya kupotea kwa wateja, pamoja na jitihada zinazofanywa na
AGPAHI na wadau wengine kuwarudisha, ziko kwenye maeneo yote ambayo AGPHAI, inatoa
huduma hizi; Mkoa wa Shinyanga, Geita na Simiyu. Chanzo cha kupotea kwa wateja
hawa, ni waganga wa jadi na imani za kidini. Kuna waganga wa jadi
wanaowaaminisha watu kwamba wana uwezo wa kutibu UKIMWI, lakini ni ujanja wa
kujipatia fedha. Pia kuna viongozi wa kiroho wanaoamini kwamba UKIMWI utapona
kwa miujiza ya Mungu, matokeo yake ni watu wanaotumia dawa za kufubaza virusi,
kupoteza maisha wanapoacha kutumia dawa na kukimbilia kwa waganga wa jadi na
imani za kidini.
Changamoto nyingine iliyotajwa na Bwana Laurean Rugambwa, katika jitihada
za shirika lake kuhudumia watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ni “ Mheshimiwa
mgeni rasmi, pamoja na juhudi zetu za kutoa huduma, tunakwamishwa na uhaba wa
watoa huduma katika vituo vilivyo vingi, na wengine kuacha kazi. Hapa inabidi
tuangalie kwa jinsi gani tunaweza kuboresha huduma hizi kwa kutumia rasilimali
watu zilizopo”
Akijibu risala ya Mkurugenzi mtendaji wa AGPAHI, Mkuu wa Mkoa wa Geita,
alisema: “ Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo AGPHAI
katika kuendelea kutatua changamoto hizi. Naomba nitumie nafasi hii kuwataka
viongozi wote hasa timu za uendeshaji wa afya na Halmashauri zote kuhakikisha
kuwa wanatengeneza mpango wakuwezesha vituo vingi vya afya kuwa na uwezo wa
kutoa huduma za tiba na matunzo na hivyo kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma
hizo kwa urahisi. Halikadhalika,
halmashauri kupitia idara zake mbalimbali zitengeneze utaratibu unaozihusisha
idara mbalimbali nje ya idara ya afya kuhakikisha kuwa wale wote waliokwisha
andikishwa kwenye huduma za tiba na matunzo wanaendelea kubaki kwenye huduma.
Na ni muhimu zaidi kutengeneza utaratibu utakaowezesha kuwafuatilia na
kuwarudisha kwenye huduma wale wote walioacha kuhudhuria kwenye kliniki zao”.
Msimamo huu wa Mkuu wa Mkoa wa Geita, ndio uliokuwa Msimamo wa Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga, hivyo msimamo wa Serikali. Tuna imani kwamba Serikali
ikitekeleza msimamo huu na kuhakikisha kuna mifumo ya kuwadhibiti waganga wa jadi
wenye ujanja wa kutaka kujipatia fedha kwa ulaghai, imani za kidini ambazo
zinawapumbaza watu wenye virusi kuamini kupona kwa miujiza, kuzuia watu
kutoroka huduma na tiba kwenye kliniki hizi za watu wanaoishi na Virusi, mifumo
ya kuhakikisha wajawazito wote wanapima hali zao, wanaume nao wanashiriki
kwenye zoezi la upimaji, wahudumu wa afya wanapatikana, unyanyapaa unapungua na
kila mwananchi anatimiza wajibu wake katika zoezi zima la kutokomeza UKIMWI,
hapana shaka kwamba Tanzania bila UKIMWI inawezekena.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22
0 comments:
Post a Comment