MWANA MAMA CHRISTOWAJA GERSON MTINDA
Leo katika safu yetu ya Mwana mama tunawaletea Mheshimiwa Christowaja
Mtinda, msomi ambaye ameamua kuingia kwenye siasa. Kuna kelele nyingi kwamba
wasomi wanatelekeza taaluma zao na kutimkia kwenye siasa; na mara nyingi
wamelaumiwa wanaume! Kumbe kuna na wanawake wasomi waliotimkia kwenye siasa.
Mama huyu ambaye alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, sasa ni mbunge wa viti
maalum kupitia chama cha CHADEMA.
Pia kumekuwa na tuhuma kwamba CHADEMA, wanachagua wabunge wa viti maalum
kwa upendeleo na wakati mwingine bila kuangalia uwezo na elimu ya mhusika. Mama
huyu ni mfano mzuri wa Mbunge wa viti maalum, ambaye ana uwezo mkubwa hata wa
kupigania Jimbo lake akalipata. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010,
alikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za chama chake ili kuhakikisha kinapata
wabunge wengi wa kuchaguliwa na Mgombea
urais kupitia chama chake anafanikiwa kuingia Ikulu. Ingawa hilo
halikuwezekana, lakini kura nyingi alizozipata Dr.Slaa kwenye uchaguzi mkuu huo
na mchango wa Mheshimiwa Christowaja, ulikuwepo.
Si lengo la safu hii kugeuka uwanja wa wanasiasa! Tukifanya hivyo
tutajiingiza kwenye matatizo makubwa ya kufuatwa na waheshimiwa ili tuandike
habari zao. Tunaandika bila kuombwa; tunaandika kwa kumfuatilia Mwana mama kwa
muda na kubaini mchango wake katika taifa letu. Na tunafanya hivyo baada ya
kutafiti kwenye magazeti na mitandao ya kijamii na kuona kwamba Mwana Mama huyu
hajaandikwa sana, hasa juu ya mchango wake. Na kusema kweli mama wengi
wanafanya mambo mengi mazuri, lakini hawaandikwi wala kutajwa popote! Tunalenga
kutoa nafasi ya wanawake wanaotoa mchango mkubwa katika jamii, lakini hawajulikani
na habari zao haziandikwi, wajulikane na kusikika. Ni imani yangu kwamba kwa
nafasi ya Ubunge, Christowaja, anaandikwa sana, maana ni miongoni mwa wabunge
wanawake wanaochangia hoja Bungeni. Hata hivyo mwana mama huyu hakuanzia
Bungeni na wala hakuwa kwenye siasa muda mrefu.
Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwanafunzi wa digrii ya uzamivu chuo
kikuu cha Sussex Uingereza. Hivyo mama huyu ni msomi. Yangejulikana
haya, uzushi kwamba Chadema, wanachaguana tu bila vigezo yasingesikika.
Sina lengo langu kuandika maisha
binafsi ya Mheshimiwa Christowaja, ninamlenga mwana mama Mwalimu, ambaye
amechangia kufundisha watoto wetu, watoto wa taifa hili la Tanzania. Ninaandika
juu ya Christowaja, mama mwenye bidii na kiu ya elimu. Mama huyu amepanda hatua
kwa hatua. Alianza na diploma, akapanda hadi kupata digrii ya kwanza, digrii ya
uzamili hadi kuelekea uzamifu. Ni mfano mzuri kwa wanawake wengine ambao kwa
namna moja ama nyingine wamepumbazwa kiasi cha kuambiwa “ Mwanamke anaweza
akiwezeshwa”; wakati ukweli wenyewe ni kwamba Mwanamke anaweza siku zote.
Sababu nyingine kubwa ya kuamua
kuandika juu ya Mheshimiwa Christowaja, ni msimamo wake wa kuunga mkono hoja
zote za kizalendo bila kutanguliza chama chake. Pamoja na mapenzi makubwa
anayoyaonyesha kwa chama chake cha Chadema, lakini mama huyu amekuwa miongoni
mwa wabunge wachache sana wanaoangalia matatizo ya taifa letu bila ushabiki wa
vyama vya siasa. Pamoja na ukali wa kawaida wa vyama vya upinzani, maana wao
wanafanya kazi ya kuisahihisha na kuisimamia serikali, mama huyu amekuwa
akiwasilisha hoja zake kwa busara na hekima. Ni mpole kwa kuongea, lakini mkali
kwa kupenyeza hoja bila kuipindisha. Huyu ni mpambanaji kama walivyo wabunge
wengine wa vyama vya upinzani, na kwa sababu anazungumza na kuchangia; hatuna
budi kuhakikisha anajulikana na habari zake kuandikwa.
Mama huyu ni miongoni mwa wabunge walio
upande wa wanyonge; watetezi wa watoto, anatetea elimu bora kwa watoto wetu,
wanawake na watu walio pembezoni. Ni mwana mama anayelilia uongozi bora katika
taifa letu, anapiga vita rushwa na ufisadi. Ni mwanaharakati ambaye anapigania
rasilimali za Tanzania kuwanufaisha watanzania wote. Pia ni miongoni mwa
wabunge waaminifu wa kukalia viti vyao. Bunge letu lina sifu ya kuwa na viti
wazi. Wakati wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, tulimsikia Mbunge, akilalamika
Bunge kujadili wizara nyeti kama ya kilimo wakati Bungeni kulikuwa na Mawaziri
watano na manaibu mawaziri watano. Pia kwa kuangalia kupitia luninga mtu
aliweza kuona viti vingi vikiwa vitupu. Na wakati mwingine hata vile ambavyo
vina watu, wabunge wanakuwa kwenye michapo wakati Bunge likiendelea. Kinara wa
zoezi hili ni Waziri Mkuu, ambaye mara nyingi anaonekana akijadiliana na watu
kwenye kiti chake wakati Bunge likiendelea. Pamoja na utetezi kwamba anakuwa
kazini, ukweli una baki kwamba anakuwa hafuatilii yanayojadiliwa Bungeni. Kama
ni kazi, si ni bora abaki kwenye ofisi yake, kuliko kuwadanganya watu yuko
Bungeni wakati anaendesha mikutano ndani ya mkutano!
Hata yeye Mheshimiwa Christowaja,
atashangaa, kusoma habari hizi, maana tunaandika bila kuhojiana naye.
Tunaandika yale tunayoyaona juu yake. Tunaandika ili wengine wakamtafute na
kufanya naye mahojiano. Hivyo katika makala zitakazofuata, tutasikia juu ya
familia yake na mengine mengi juu yake. Tunaandika ili wengine wajiulize huyu
ni nani? Ni mbinu mpya ya kuwachokoza waandishi kuanza kuwafuatilia watu mbali
mbali na kuwahoji na hasa wanawake ambao kwa miaka mingi wamewekwa pembeni.
Christowaja Mtinda, alizaliwa tarehe
13.5. 1968. Alisoma shule ya msingi Kititimo kati ya mwaka 1976 hadi 1982.
Alijiunga na shule ya sekondari ya Msalato mnamo mwaka 1983- 1986 na kidato cha
tano na sita shule ya sekondari ya Kilakala Morogoro mwaka wa 1987-1989.
Alipomaliza masomo ya sekondari alijiunga na chuo cha DSA kusomea Diploma ya
Material Management. Baada ya kupata Diploma hiyo, mwana mama huyu hakutulia,
aliendelea kuisaka elimu na mwaka 1996 hadi 1998, alijiunga na Chuo cha Ualimu
cha Morogoro kusomea diploma ya Ualimu. Alipomaliza Diploma yake ya Ualimu,
alifundisha shule ya Sekondari ya St Mary’s 1998- 1999 na shule ya sekondari ya
Airwing ya Dar-es-Salaam, mwaka 1999-2000. Kiu yake ya elimu haikukoma na
mwaka 2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo
kikuu cha Dar-es-Salaam kuchukua shahada yake ya kwanza ya Ualimu. Bidii
aliyokuwa nayo kwenye masomo, aliendelea na shahada ya uzamili hapo hapo chuo
kikuu cha Dar-es-Salaam mwaka wa 2004-2006.
Mbali na kuwa mwalimu kwenye shule za
sekondari na Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mkwawa, mama huyu alifanya pia kazi
kwenye Baraza la mitihani Tanzania. Ni mama mwenye uzoefu katika Nyanja mbali
mbali. Hata na michango yake kwenye Bunge, inaonyesha kwamba si mtu aliyeingia
kwenye siasa kutafuta kazi, bali ni mtu alikuwa na kazi yake; msomi, mtaalamu
wa elimu na mambo mengine mbali mbali kama kufanya kazi kwenye duka la dawa la
Twiga.
Huyo ndiye Mheshimiwa Christowaja
Gerson Mtinda, msomi aliyetimkia kwenye siasa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
No comments:
Post a Comment