MWANA MAMA PENINA MHANDO.
Leo katika safu ya Mwana mama, tunawaletea Penina Mhando ambaye anajulikana
pia kama Penina Mlama. Huyu ni mwandishi wa NGUZO MAMA na nguli wa sanaa za
maonyesho ambaye pia ni mwandishi mahiri wa tamthiliya za Kiswahili. Huyu ndiye
mtunzi wa Hatia, Tambueni Haki Zetu, Heshima Yangu, Pambo na Lina Ubani! Wakati Waswahili wanasema
kwamba la kuvunda halina ubani, mama huyu anasema la kuvunda lina ubani!
Mwenyewe aliigiza mchezo alioutunga mwenyewe wa Lina ubani na kuwasisimua watu
wengi.
Huyu ni mama mpole na mnyenyekevu, hana mbwembwe za kisomi, maandishi yake
yanachoma na kufikirisha zaidi ya anavyoonekana yeye mwenyewe. Ni
mwanamapinduzi na mwanaharakati wa haki za binadamu kupindukia. Siku za hivi
karibuni ameipumzisha kalamu yake lakini, kilichoandikwa kimeandikwa. Maigizo
aliyoyatunga, yakitinga jukwaani ni lazima kila mtu aguswe na utunzi huo na
kutambua msimamo wa mwandishi huyu mkimya anayependa kuzunguza kwa kalamu na
maigizo.
Akiigiza sehemu ya Mama Liundi, kwenye kesi iliyovuma hapa Tanzania, ya
mama aliyewanywesha watoto wake sumu kwa kisa cha kufuzwa na bwana wake, ndipo
unapotambua uwezo mkubwa wa profesa Penina Mhando. Akiigiza unaona picha nzima
kana kwamba tukio hilo ndo linatokea. Ni mama mwenye kipaji kikubwa na msomi
ambaye anajishusha ili kutoa mchango wake katika jamii.
Huyu si mtu wa maneno, bali matendo. Inawezekana anatoa ujumbe kwa wasome
wenzake kwa ujumbe wa maagizo: “ Mimi ni msomi kama nyinyi, fuateni mfano,
jishushe tulijenge taifa letu, maana la Kuvunda lina Ubani”. Nimemlisha maneno
hayo, lakini mwenye macho si lazima kumwambia tazama!
Mama Penina Mhando alikuwa mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam kwa
miaka mingi kabla ya kwenda Nairobi Kenya kufanya kazi na Baraza la Wanawake Waelimishaji wa Afrika (Forum for
African Women Educationalists –
FAWE) , kwenye ofisi ya makao makuu, jijini Nairobi.
Mama huyu ambaye ni profesa, alizaliwa
mnamo mwaka 1948, katika Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Alifanikiwa
kumaliza masomo ya juu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo alipata: B.A
(Hons) – Elimu, Lugha na Sanaa za Maigizo, M.A. – Sanaa za Maigizo, Ph.D –
Sanaa za Maigizo.
Penina alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sanaa za
Maigizo kwa kupanda ngazi kuanzia
Msaidizi wa Mkufunzi, Mkufunzi, Mkufunzi Mkuu hadi Mhadhiri Mshiriki.
Pia mama huyu alishiriki uongozi kwenye Idara hiyo ya Sanaa na Maigizo kama
Mwongozi, Idara ya Sanaa ya Muziki na Maigizo, akiwa na majukumu ya
kupanga na kuendesha mipango ya ukufunzi, utafiti na huduma kwa jamii,
ushiriki wa kina katika mipango ya Maendeleo ya Maigizo ambapo
maigizo yalitumika kama njia ya kuhamasisha jamii katika kiwango cha
shina, kwenye maeneo ya vijijini:
Pia Mwongozi Mshiriki wa Kitivo –
Utafiti na Uchapishaji, Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii akiwa na
majukumu ya kupanga, kusimamia na kukagua utafiti na sera ya uchapishaji
na mipango katika idara kumi na mbili (12) za Kitivo. Majukumu
haya yalikuwa pamoja na kuhamasisha upatikanaji wa fedha kwa utafiti wa
Kitivo na uchapishaji,
ikiwa pamoja na majarida ya wakufunzi:
Pia Kaimu Mwongozi wa Kitivo, Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii
Akiwa na majukumu ya kupanga, kuratibu na kukagua utafiti wa ukufunzi na huduma
Ushiriki katika uwekaji wa sera zinazohusiana na mipango ya mafunzo. Uongozi wa
idara kumi na mbili (12) na idara moja ya utafiti, zote zikiwa chini ya Kitivo:
Pia,Ofisa Mkuu wa Ukufunzi (Deputy Chancellor) Akiwa na majukumu ya
kusimamia, kuratibu na kukagua shughuli za utafiti na ushauri katika Vitivo vya
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo viwili vishiriki. Chuo Kikuu cha Dar-es
Salaam kina Vitivo 10 na Taasisi za Utafiti 10.Majukumu yalikuwa uwekaji wa
sera uhamasishaji wa fedha kutoka serikalini na kwa wafadhili kwa kuendesha
mipango ya utafiti sehemu/vifaa vya ukufunzi, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi
na walimu, Uratibu wa shughuli za kawaida za utawala za Chuo Kikuu zinazohusiana
na uingiaji (Admissions) wa Wanafunzi, Utafiti na Uchapishaji, Maendeleo ya
/Walimu na Wafanyakazi, Stashahada za Juu, Uhusiano wa Nje na Miradi, Ukufunzi
katika Chuo Kikuu, Ualimu na Uajiri.
Pia alishirikia shughuli za kijinsia kwenye chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
kama Mratibu wa Kitengo cha Uendeshaji
wa Shughuli za Kijinsia cha
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akishughulikia upungufu wa uwiano wa kijinsia katika uingizaji wa wanafunzi, uajiri na wakufunzi na
wafanyakazi, masomo pamoja na
maslahi yote kwa ujumla Mratibu
wa Mradi wa TUSEME ambao unatumia sanaa
katika kumwezesha msichana kufanya vizuri zaidi katika masomo Mratibu wa Mpango wa Sanaa ya Maigizo kwa Maendeleo ambao unatumia Sanaa ya Maigizo
kuwawezesha wanawake katika
vijiji kupata mafanikio katika maendeleo.
Pia mama huyu ameshiriki mambo mengi ya kijamii kama, Mratibu wa mpango wa
kumwendeleza mtoto kupitia sanaa katika
shule za msingi jijini Dar es Salaam.
ufundishaji wa waalimu na kuendesha Tamasha la Watoto la Maigizo Na mambo
mengine kama vile; Mwanachama - Chama cha Sanaa cha Paukwa, Mratibu - Kikundi
cha Maigizo cha Watoto cha Chuo Kikuu wakati ule akiwa Mratibu - TUSEME: Elimu
ya Demokrasia kwa wanafunzi wasichana na shule za sekondari nchini Tanzania, Mwanachama
- Kamati ya Uendeshaji wa Semina za Lugha katika mabadiliko yanayotarajiwa katika
muundo wa ukufunzi, Mwanachama - Chama cha Wanawake wa Afrika katika Utafiti na
Maendeleo (African Associationfor Women for Research and Development– AWARD).
Tunzo ambazo Prof. Penina Mlama amewahi kupata ni kama ifuatavyo: Tunzo ya
Nane ya Utafiti wa Sayansi ya Jamii katika Afrika ya Mashariki na Kusini, Tunzo
ya Utafiti wa Masomo ya Marekani – New York University ,Tunzo ya Mfuko wa
Rockerfeller katika Sayansi ya Jamii kwenye Upembuzi wa Maendeleo, Shindano
Maalum la Jinsia na Maendeleo – Shirika la Utafiti wa Sayansi ya Jamii katika
Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora wa Kike katika filamu ya “Mama Tumaini”
TFC/NORAD, Tamasha la Filamu la SADDC, Harare, Tunzo ya Shaaban Robert kwa
Uhamasishaji wa Kiswahili nchini Tanzania, 1999, iliyotolewa na Baraza la
Kiswahili la Taifa
Mwanamke wa Mwaka – Taasisi ya Marekani ya Maisha ya Watu, USA.
Katika maisha yake ya kazi yake, Prof. Penina Mlama amejishughulisha
na kazi nyingi za utafiti wa kina, na kuweza kuchapisha idadi kadhaa ya
vitabu na makala, pamoja na utengenezaji wa filamu na maigizo mengi.
Huyo ndo Mama Penina Mhando, ambaye amefanya mambo mengi, ingawa hasikiki
sana siku hizi, lakini mchanga wake katika taifa letu ni mkubwa.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net.
No comments:
Post a Comment