MWANA MAMA MAREHEMU DAKTARI YVONA SWAI
Leo katika safu yetu ya Mwana mama, nawaletea Marehemu Daktari Yvona TwagilaYesu Swai, Mtanzania
mwenye asili ya Rwanda ambaye alilitumikia taifa la Tanzania kwa uaminifu na
uzalendo uliotukuka. Labda mambo haya ya kufanya kazi kwa uamini na uzalendo
yanazaliwa kwenye damu? Baba wa Daktari Yvona, ambaye naye ni Daktari, ndiye
daktari wa kwanza kugundua mgonjwa mwenye virusi vya Ukimwi mwaka 1983 katika
hospitali ya Ndolage. Ni daktari ambaye pamoja na uzee wake wa miaka 82, bado
anaendelea kuwahudumia watanzania. Jina la Daktari TwagilaYesu, linasikika mkoa
mzima wa Kagera, Tanzania na hata kwenye mataifa mbali mbali maana mzee huyu
amezunguka dunia nzima akielezea na kufundisha juu ya ugonjwa hatari wa Ukimwi.
Amefanya kazi kwa uzalendo na anaendelea kuchapa kazi kwa uaminifu mkubwa.
Katika mpangilio wangu wa kuwaletea
wasifu wa mwana mama mmoja kila siku ya Jumamosi, nilikuwa na mpango wa
kuwaletea Mwana mama Daktari Yvona Swai, lakini kwa vile alikuwa anaumwa kwa
muda mrefu, sikutaka kuandika juu yake bila kumjulia ali . Nilifunga safari
hadi Bukoba na kwenda kijijini kwao Kamachumu-Bukoba, huko nilikutana na Baba
yake Mzazi ambaye naye ni Daktari TwagilaYesu. Bahati mbaya siku hiyo
niliyofika nyumbani kwao, ndiyo siku Mungu alimuita kwake mpendwa wetu Daktari
Yvona Swai. Hivyo sikuweza kuongea naye! Atazikwa Moshi siku ya Jumamosi tarehe
30.3.2013. Mungu amlaze mahali pema peponi!
Daktari Yvona Swai, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa mgongo. Alifanyiwa
upasuaji na kupona, lakini baadaye ulijitokeza ugonjwa wa kansa ambao
umemsumbua zaidi ya miaka miwili hivi. Alijitahidi kupambana na ugonjwa huo
bila ya kukata tamaa. Mama huyu alikuwa mchapakazi na wakati mwingine
hakujihurumia. Nakumbuka kumgombeza, nilipoikutana naye akiendesha gari kubwa
baada ya kufanyiwa upasuaji wa mgongo. Jibu lake, wakati ule nikilikumbuka leo
hii tunapouaga mwili wake, machozi yanatoka. Alinijibu hivi: “ Kaka, sipendi
kuendesha gari, lakini nikilala nani atawatunza watoto wangu?...”. Muda wote
walihangaikia watoto wake. Sasa amelala milele, je nani atawatunza watoto wake?
Je Mungu anakisikia kilio hiki? Na kama anasikia, amekubali kumtenga Yvona na
watoto wake? Amekubali watoto hawa wabaki yatima? Mipango yake ni mkubwa,
tubaki kusema tu Jina lake lihimidiwe!
Watu wa Karagwe, Bukoba na Tanzania nzima wamepata pigo la kuondokewa na
Daktari huyu ambaye kama walivyo madaktari wanaofanya kazi vijijini alikuwa
mchapakazi. Kwa miaka yote aliyoifanya ameokoa maisha ya watu wengi hasa wanawake
na watoto. Alifanya kazi bila kujihurumia na bila kusubiri mshahara; madaktari
wanaofanya kazi vijijini, pamoja na kuunga mkono mgomo wa madaktari wenzao,
pamoja nao kutaka kufanya kazi katika mazingira mazuri hawakuacha kuwahudumia
watu. Kama serikali ingekuwa sikivu na yenye shukrani madaktari wanaofanya kazi
vijijini na hasa Madaktari wasaidizi popote walipo wangeshukuriwa kwa namna ya
pekee. Daktari Yvona, aliendelea kuchapa kazi kwa moyo wote. Siku za mwisho wa
maisha yake alikuwa Katibu mtendaji wa
Shirika la Msalaba mwekundu mkoa wa Kagera. Alikuwa mstari wa mbele
kushughulikia majanga ya kila aina yaliyokuwa yakijitokeza mkoa wa Kagera na
kwingineko. Aliendesha kwa ufanisi mradi wa kukusanya damu salama na kuiweka
kwenye benki ya damu kwa matumizi ya baadaye.
Daktari Yvona, alizaliwa tarehe 23.8.1960, alisoma shule ya msingi Kashasha
na sekondari ya Kilosa. Alipomaliza kidato cha sita alisomea Diploma ya uganga
katika Chuo cha Bugando na baadaye alijiendeleza hadi kuwa Daktari Msaidizi.
Pia alijiendeleza kwa kozi mbali mbali katika nyanja ya Afya.
Daktari Yvona, aliolewa na Daktari Swai, ambaye walikutana Karagwe, wote
wakiwa watumishi wa serikali. Mungu aliwajalia watoto wanne, Lilian, Sylivia,
Rogers na Frank. Kwa mapenzi ya Mungu, kama
tunavyosema na kuamini siku zote, Daktari Swai, alipoteza maisha yake
kwenye ajali ya MV Bukoba mnamo mwaka wa 1996. Bahati mbaya mwili wa Dakta Swai
hakupatikana, hivyo kuongeza majonzi kwa Daktari Yvona, ndugu
na jamaa wote.
Wakati ule watoto wote walikuwa bado wadogo. Daktari Yvona, alijifunga kibwebwe
kuwalea watoto wake na kuendelea kuchapa kazi za kulijenga taifa letu. Huyu ni
mama wa mfano ambaye ameweza kwa kiasi kikubwa kuwatunza watoto akiwa amesimama
peke yake bila mme wake. Leo hii Lilian ni mwalimu, Sylivia amemaliza shahada
ya kwanza ya Ufamasia, Rogers na Frank
wameanza mwaka wa kwanza shahada ya udaktari. Ili kukamilisha usemi wa Daktari
TwagilaYesu, baba wa Daktari Yvona, kwamba udaktari uko kwenye damu!
Tuna utamaduni wa kumsifia mtu akiwa amekufa. Ndo maana nilitaka kuandika
wasifu huu wa Daktari Yvona akiwa hai, ila imeshindikana. Binafsi nimepata
bahati ya kufanya kazi na mama huyu ambaye leo hii tunamlilia. Huyu alikuwa ni
mama wa aina yake! Aliwapenda watu wote, hakuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile,
alishirikiana na wasomi, walishirikiana na watu wa kawaida kabisa hadi wale wa
vijiweni! Hakujiona wala kujikweza. Bila kuambiwa au kumkuta kazini kwake,
ilikuwa vigumu kutambua kwamba huyu alikuwa ni daktari. Ni mama ambaye huruma
ilikuwa kubwa kuliko uwezo wake! Pamoja na kwamba baada ya kuondokewa na mume
wake, alikuwa akifanya kila kitu kuwasomesha na kuwatunza watoto wake, hakuacha
kutoa misaada kwa wengine.
Kuna mambo mengi niliyojifunza kwa mama huyu na la kwanza ni hili la “kaka”
na “dada”. Watu wote walikuwa “Kaka” na “Dada”. Kusema kweli alijitahidi kiasi
chake kuishi maisha ya hayo. Binadamu ni binadamu, inaezekana aliteleza hapa na
pale, lakini kwa asilimia kubwa “Udada” na “Ukaka” alikutimiza. Hili limejionesha
wazi wakati wa msiba wake jinsi watu wa kila aina, watu wa kutoka sehemu mbali
mbali walivyofika kumlilia na kumuaga.
Jambo jingine jingine nililojifunza kwa mama huyu ni Kumtegemea Mwenyezi
Mungu, na siku zote kuomba na kushukuru. Magumu mengi aliyoyapata katika maisha
yake, kama lile la kuondokewa na mme wake, silaha yake kubwa ilikuwa ni kuomba
na kushukuru. Niseme tu kwamba mama huyu alikuwa mcha Mungu!
Na jambo jingine ni kusamehe na kusahau. mama huyu hakutunza kinyongo. Alijaliwa
kusahau haraka wale waliomtenda vibaya. Kwa kuiga tabia tunaweza kujenga jamii
isiyokuwa na visasi.
Mama huyu alinifundisha kufanya kazi kwa bidii, kufanya kazi kwa uzalendo
na hasa kuwatumikia watu maana hiyo ndiyo faraja ya kuendelea kuishi hapa
duniani. Daima alisema “ Kaka sisi si bora zaidi ya wale waliotutangulia, kama
Mungu ametupendelea kuendelea kuishi, basi tutumie nguvu zetu na uwezo wetu
kuwatumikia watu. Ipo siku nasi tutaitwa na kuiacha dunia hii…”. Siku yake ya
kuitwa imefika, ametuacha nyuma ingawa hatuko bora kuliko yeye aliyetutangulia.
Na sisi siku yetu yaja, hivyo faraja yetu iwe kuwatumika watu!
Tumesikitika kumpoteza dada yetu mcheshi, mwenye utundu, mbunifu na shupavu
wa kupambana na changamoto za maisha. Mungu amlaze mahali pema peponi Daktari
YvonaSwai.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net
0 comments:
Post a Comment