UHAKIKI WA KITABU:  MERCHANT POLITICS AND THE MOCKERY OF MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA

1.     Rekodi za Kibibliografia.

Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni  MERCHANT POLITICS AND THE MOCKERY OF MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA, Kimeandikwa na Lawrence I.M Kilimwiko. Mchapishaji wa kitabu hiki ni  Konrad Adenauer Stiftung na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978- 9987- 716-01-2. Kitabu kina kurasa 116 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi

Kitabu hiki kilizinduliwa mwezi wa pili Jijini Dar-es-Salaam na bahati nzuri mchambuzi wa kitabu hiki alikuwa miongoni mwa watu waliopata mwaliko wa kuhudhuria sherehe za uzinduzi huo. Majadiliano yaliyofuata baada ya uzinduzi wa kitabu hiki yamechangia kwa kiasi kikubwa uchambuzi huu ninaoufanya. Hapa na pale nimezingatia maoni na michango ya washiriki mbali mbali. Pia  baadhi ya majibu ya maswali kutoka kwa mwandishi wa kitabu hiki yaliyoulizwa wakati wa uzinduzi yameingizwa kwenye uchambuzi  huu kwa namna moja ama nyingine.

Kitabu hiki kinakuja wakati wake. Tunapoandika Katiba mpya na tunaelekea uchaguzi wa 2015, ni muhimu kuanza kutafakari juu ya siasa yetu na mfumo tunaoutumia katika siasa za Tanzania.  Bwana Lawrence Kilimwiko, ametuchokoza na kutuelekeza katika mjadala huu. Ni imani yangu kwamba kitabu hiki kitaleta mchango mkubwa na hasa kama jitihada itafanyika kukitafsiri kitabu hiki kutoka lugha ya kigeni.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa kimombo, na labda ndiyo hiyo dhihaka yenyewe inayoongelewa katika kitabu hiki? Mtu ambaye analenga kusahihisha mwenendo wa siasa ndani ya nchi ambayo lugha yake kuu ni Kiswahili na kuamua kuandika kwa lugha ya kigeni, si tu kwamba inashangaza, bali ni dhihaka. Mwandishi anasisitiza kwamba tunafanya mambo kwa kushinikizwa na wafadhili, na yeye anaandika kwa lugha ya kigeni dalili ya wazi kwamba naye anashinikizwa na wafadhili kwa kuandika lugha wanayoifahamu wao? Ukombozi kamili na kufanya mambo sahihi ni pamoja na kuitumia lugha ya taifa. Mtu anayetumia lugha za wengine kujieleza na “kusambaza” ujumbe kwenye jamii, si mtu huru! Kwa Kiswahili cha kawaida, kitabu hiki kinaitwa Biashara ya Siasa na Dhihaka ya  Vyama vingi Tanzania. Hoja ya mwandishi ni kwamba badala ya Tanzania kuwa na mfumo wa siasa wa vyama vingi kutokana na uhitaji wake kama ilivyo katika nchi zilizoendelea, mfumo uliopo kwa sasa hivi ni wa kisheria zaidi. Na kwamba kutokana na kushinikizwa na wafadhili kuachana na mfumo wa chama kimoja, kulibuniwa vyama bandia huku vile vilivyoanzishwa kwa nia njema vikisongwa na vizingiti vingi katika kuviendesha. Hivyo badala ya kuwa na vyama vilivyoanzishwa kutokana na uhitaji iwake katika jamii, kumekuwepo na vyama bandia vilivyougeuza mfuo wa vyama vingi badala ya kuwa huria kuwa holela na dhihaka mbele ya  dunia yetu ya leo.

Mwandishi anakumbusha historia ya Tanzania na vyama vingi. Kwamba CCM, ilikuwa imegoma kukumbatia mfumo wa vyama vingi. Lakini baada ya shinikizo la wafadhili, ilibadilisha msimamo wake na kuelekeza nguvu zote kwa mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo hili lilifanyika shingo upande na Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali  kilibuni mbinu ambazo kutokana na historia ya nyuma, vyama vipya visingeweza kufua dafu mbele yake; Sheria ilitungwa ya kuvitaka vyama visajiliwe lakini siyo CCM ambacho kilisajiliwa pasipo kufuata masharti kwa vyama vingine. CCM pia ilijinyakulia rasilimali zote zilizokuwa zimekusanywa na watanzania wote ikiwemo vitega uchumi, majengo na hata viwanja vya michezo mikoani kote.

Kwa kuogopa wafanyabiashara wakubwa kujiunga na vyama vingine vya siasa, CCM ililegeza masharti yake ya chama cha wakulima na wafanyakazi na kufungua milango yake kwa kila mtu hata mijizi, matapeli, mawakala wa ubepari, ukabaila na hata wale wasiokuwa na maadili wala uzalendo.

Matokeo yake ikawa ni kwa chama hicho maarufu barani Afrika kutekwa nyara na genge la mijizi,  na kwa mkakati kasi ya ajabu uongozi wa CCM ukawa mikononi mwa watu wasiokuwa wajamaa, wazalendo na wala waadilifu. Siasa ya ujamaa na kujitegemea ikageuzwa kibao na kuwa siasa ya kujimegea, kubinafsisha mali za vijiji na kupora ardhi, wanyama pori na rasilmali nyingine.

Mwandishi anasisitiza hoja yake kwa kutoa mfano kwamba kuibuka kwa CHADEMA kama chama kimbilio la wanyonge ni ishara tosha ya pale CCM ya vibopa ilipojifikisha na kuifanya siasa ya vyama vingi kugeuka dhihaka tupu. Mfumo huria wa kisiasa nchini umegeuka kuwa mfumo holela.

Kitabu hiki kimeandikwa ili kuibua fikra mpya kuhusu mfumo mzuri wa kuendesha siasa za vyama vingi vinavyotokana na makundi ya wanachama wenye msimamo, itikadi na falsafa moja ya wanaokusanyika kwa hiari  yao na siyo sheria  kama ilivyo sasa.

Lawrence Musanguka Kilimwiko, ni mwandishi mkongwe ambaye amefanya kazi ya uandishi wa habari zaidi ya miaka 30 akiandika juu ya masuala ya siasa. Ameandika vitabu vingi vikiwemo: Media Power and Politics in Tanzania (2009), The Fourth Estate in Tanzania (2002), The Spokesperson: A Media User Friendly Guide (2004) na Biashara ya Dini, Siasa na Ufisadi.

Lawrence Kilimwiko, alisomea uandishi wa habari kule India, pia alisomea mahusiano ya kimataifa kwenye chuo kikuu cha Jahawaharlal India na amesoma Sayansi ya siasa na uongozi Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam.


III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha Biashara ya Siasa na Dhihaka ya  Vyama vingi Tanzania , ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Kwanza nikubali kwamba jambo hili la kuandika kitabu juu ya mwenendo wa siasa, si la kawaida hapa Tanzania. Tumekuwa tukisoma vitabu vinavyojadili mwenendo wa siasa katika mataifa mengine na hasa yale yaliyoendelea. Hivyo kazi hii si ya kawaida.

Lakini pia kuna ukweli kwamba leo hii taifa letu linapitia katika wakati mgumu kwa vile tulifanya kosa kubwa la kuifanya siasa kuwa biashara. Tatizo la biashara ni kwamba bidhaa ikikaa sokoni, ni lazima wanunuzi waje na daima mwenye  dau kubwa ndo anafanikiwa kuondoka na bidhaa sokoni.

Na tabia ya biashara ni ushindani, ni mbinu na ujanja. Ikibidi kwenye biashara ni lazima kuhakikisha anayekuzibia njia unamwondosha. Haya ndiyo tunayoyashuhudia sasa hivi katika taifa letu. Haya matukio ya kuwateka watu, kuwapiga na kuwaumiza, ni dalili kwamba kuna watu wanaoziba njia za wafanyabiashara wa siasa.

Siasa ikifanywa biashara, inapoteza maana yake. Ndani ya siasa tunapata wawakilishi wa wananchi. Kwa maana kwamba wananchi wanamchagua mmoja wao kuwawakilisha katika vyombo vya kutunga sheria na kuitawala nchi. Kwa maana nyingine ni kwamba kama ingebidi, wananchi wangelazimika kutumia njia zozote zile kumshawishi mtu wanayempenda ili akubali kuwawakilisha. La kushangaza ni kwamba katika biashara ya siasa, mwakilishi ndiye anafanya mbinu za ushawishi hata kutumia fedha ili wananchi wamchague na kumtuma kuwawakilishia. Hii ni kinyume kabisa na kwa vyovyote ni dhihaka!

Kitabu hiki kinaandikwa wakati tunatengeneza katiba mpya na tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Ni wakati ambapo Chama tawala tayari kinaona nguvu mpya ya vyama vya upinzani na nguvu mpya ya vijana ambao kwa kiasi kikubwa hawaeleweki vizuri, lakini upepo wa kutumia fedha kwa kila hatua, ni dalili tosha kwamba chama ambacho kitakuwa kimefanikiwa vizuri kufanya biashara ya siasa kinaweza kuibuka mshindi, maana fedha ni sabuni ya roho kama wasemavyo Waswahili.

Vyovyote vile, uwe upinzani au chama  tawala, bila fedha ni vigumu kuupata uongozi ndani ya vyama au ndani ya serikali. Maana yake ni nini? Kwa upande mkubwa wenye fedha ni wazee na wazee hawa ndo wanataka wabaki madarakani kwa njia zozote zile.

Mazingira mengine yanayokizunguka kitabu hiki ni  kwamba sasa hivi kila kitu kimekuwa biashara; siasa ni biashara, elimu ni biashara hata na afya ni biashara. Kwa vile siasa ni biashara kuna uwezekano mkubwa kumpata kiongozi asiyekuwa na uwezo, wa kuongoza na kufikiri, lakini ana uwezo wa fedha. Badala ya kutawaliwa na fikira, tunatawaliwa na fedha. Na kwa vile elimu imekuwa ni biashara, tumeanza kupata matokeo yanayofanana na biashara, badala ya kupata elimu bora na nzuri kwa ukombozi wa watanzania tunapata elimu mchoko na watoto wetu wanaendelea kuwa wajinga. Matokeo ya mtihani wa mwaka huu yameonyesha kabisa ninachokielezea. Na kwa vile afya imegeuzwa kuwa biashara, watu wanaweza kuingiza hadi dawa bandia au zile zilizokwisha muda wake.

Kwa kifupi ni kwamba Biashara ya siasa, imebadilisha kabisa mwelekeo wa  taifa letu. Haya ndiyo mambo yanayokizunguka kitabu hiki na kwa njia moja ama nyingine haya ndiyo yaliyomsukuma mwandishi kuandika kitabu hiki.


IV. Muhtasari wa Kitabu

Mwandishi amekigawa kitabu katika sura saba ambazo zinaongelea; sheria zinazoongoza uanzishwaji wa vyama vingi vya siasa, matumizi na ushawishi wa fedha katika siasa za Tanzania, mabadiliko yaliyoingiza siasa katika biashara, biashara ya siasa kutawala siasa za Tanzania, na pia anaangalia njia mbali mbali ambazo zinaweza kuuinua upinzani hadi kufikia kuishika dola.

Mwandishi anakwenda mbali na kuangalia biashara ya siasa kuanzia miaka ya 80, akiunganisha siasa hizi na ujio wa soko huria na kile kilichokuja kujulikana kama Azimio la Zanzibar. Siasa hizi zilizoingia Tanzania, kwenye miaka ya 80, silifutilia mbali uwezekano wa mtu maskini, hata kama ana akili nzuri kushiriki kwenye uongozi wa taifa letu la Tanzania.

Mwandishi, katika kitabu chake anakwenda zaidi kuandika na kusema kwamba, inakuwa shida kwa mwananchi wa kawaida kuchaguliwa kuongoza, maana hawezi kuwa na fedha za kununua uongozi.

Kilimwiko, anajadili hoja ya Uzawa, iliyoibuliwa na Mchungaji Chritopher Mtikila ya Uzawa na : “Walalahoi” , (Gabacholi) Wahindi, na kuonyesha kwamba mali nyingi ya Tanzania iko mikononi mwa Wahindi. Ukweli kwamba Mtikila, alisikilizwa na kuzoa washabiki wengi ilikuwa ni dalili ya wazi kabisa kwamba ufa kati ya walionacho wasiokuwanacho ulikuwa unapanuka sana.

Mwandishi anaifananisha CCM na mnyama mkubwa aina ya mjusi “Dinosaur”. Mnyama huyu alikuwa mkubwa kuliko wanyama wote hapa duniani, lakini sasa ametoweka kabisa. Na la kushangaza ni kwamba mnyama huyu alikuwa anaishi hapa Tanzania. Kwa vile CCM imejiingiza katika biashara ya siasa na kukubali kutawaliwa na kuongozwa na fedha badala ya itikadi, fikra, sera na kuijenga nchi, mwisho wake unaweza kuwa kama wa mnyama mkubwa “Dinosaur” aliyepotea kwenye uso wa dunia.

Kilimwiko anamalizia kitabu chake kwa kugusia vyama vya upinzani na hasa Chadema na CUF. Anaonyesha jinsi vyama hivi vilivyopitia vipindi vigumu, pamoja na jitihada za kuonyesha kwamba vyama hivi ni vibaya, lakini bado hadi leo hii vyama hivi vinaendelea kuishi na kusonga mbele. CUF, kilibatizwa kwamba ni chama cha Wapemba na kilikuwa kikiendeshwa na fedha za Waislamu wenye itikadi kali. Sifa hizi zililenga kukimaliza chama hiki, lakini ilishindikana. Nacho Chadema, kilibatizwa jina la kuwa ni chama cha matajiri, wakristu na wachaga. Hata hivyo chama hiki kinaendelea kupanuka na kukubalika kwenye jamii ya watanzania.

V. TATHIMINI YA KITABU.

Nianze kwa kumpongeza ndugu yetu Lawrence Kilimwiko, kwa kuandika kitabu hiki cha aina yake juu ya siasa za Tanzania. Kitabu hiki ni cha kwanza kuandikwa juu ya siasa kiasi kinaweza kumsaidia mtu yeyote yule awe mgeni au mwenyeji, kuona Tanzania tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi kama mambo yataachwa kwenda kama yanavyokwenda hivi sasa.

Pili, Kilimwiko, ametoa changamoto kwa watanzania wote na hasa waandishi wa habari kuyachambua maisha yetu ya kila siku ili yatusaidie kujipima, kujisahihisha na kusonga mbele. Kitabu ni kati ya njia zinazosaidia jamii kujiona.

Tatu, mwandishi amefanikiwa kufunua ubovu ulio katika mifumo yetu ya utawala na jinsi fedha inavyoongoza na kuweka mbali fikra na maadili bora, bila yeye kuonyesha ushabiki wa aina yoyote ile.

Nne, mwandishi amefanikiwa kuionyesha dhihaka ya vyama vya siasa katika Taifa letu la Tanzania; na ukweli kwamba kama vyama vyote vinaweza kuwa na uwanja wa ushindani ulio sawa, hakuna chama ambacho kingekuwa kinajizolea ushindi wote. Pamoja na matumizi ya fedha, bado chama cha CCM kinabebwa na dola.


VI. HITIMISHO.

Kama kawaida yangu ya uchambuzi wa vitabu, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki ambacho kwa kiasi kikubwa kimechambua siasa za Tanzania na vyama vya siasa.

Kwa upande wa mwandishi ni kumuomba kufanya jitihadi kubwa kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya taifa. Kama nilivyosema hapo mwanzoni, ni kwamba inashangaza mtu ambaye anatoa changamoto ya siasa za Tanzania, yeye mwenyewe anaandika kwa lugha ya kigeni. Hoja yake kubwa ni kwamba kosa kubwa la taifa letu ni kufanya na kutenda kwa maelekezo ya wafadhili wa nchi za nje. Kosa hili ambalo analielezea kwa ufasaha mkubwa ndani ya kitabu chake analifanya yeye mwenyewe! Tunaweza kusema Kilimwiko, aliandika kwa lugha ya Kizungu kwa vile kazi yake ya kuandika imechangiwa fedha na shirika la nje? Kama jibu ni kweli basi naye anasukumwa na wa nje kuandika juu ya siasa za Tanzania.

Inawezekana kabisa tukatoweka kama taifa na kutokomea kusikojulikana kama alivyotokomea mnyama mkubwa aina  “Dinosaur” kama hatufanyi jitihada za kutosha kuitumia lugha yetu. Rais wa China, aliyeitembelea Tanzania juzi, alitumia lugha yake kulihutubia Taifa la Tanzania, na watafsiri wakafanya kazi yao. Haina maana kwamba Rais huyu hafahamu Kizungu, ila ni ile hali ya kujivunia lugha yake. Lakini Rais wetu Mheshimiwa Dkt Jakaya Kikwete, alitumia Kizungu kujibu hotuba ya Rais wa China. Hii inaonyesha wazi kwamba hata kama tunapinga kutawaliwa na Wazungu, ukweli ni kwamba wanaendelea kututawala na watatutawala milele yote kama hatufanyi jitihada za kujinasua kuanzia kutumia lugha zetu badala kuzishabikia lugha zao.

Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754 633122



0 comments:

Post a Comment