MWANA MAMA, MA CLEMENTINA RUTABANZIBWA.
Leo katika safu yetu ya Mwana Mama, nawaletea Marehemu
mama yetu Mpendwa Ma Clementina Rutabanzibwa na kuwatangazia wasomaji wangu
maslahi binafsi kwamba huyu ni Mama yangu Mkubwa. Si kwa upendeleo bali mama
huyu ni miongoni mwa mama wengi wanaolitumikia taifa letu, kwa uadilifu,
uzalendo na uaminifu mkubwa lakini hawasikiki! Hatujajenga utamaduni wa kuandika
historia ya watu wanaotoa mchango mkubwa wa maendeleo katika taifa letu na hasa
wanawake. Makala hizi za Mwana Mama zinalenga kuujenga utamaduni huu. Hivyo
hata kama Mama huyu asingekuwa jamaa yangu, ningeshika kalamu na kuandika juu
yake.
Ua letu
limepukutika! Mama yetu Mkubwa Omugonzibwa Ma Clementina Rutabanzibwa, aliaga
dunia tarehe 23.3.2013 na tulimzika kwa heshima zote za kidini, kiserikali,
kiutamaduni, kijamii na mshikamano siku Jumamosi tarehe 30.3.2013 kijiji cha
Ibura Bukoba. Ni machozi ya furaha
kwamba mama yetu amepumzika akiwa na umri wa miaka 85, baada ya kuugua kwa
kipindi cha miaka 7, lakini pia ni machozi ya uchungu maana
hatuwezi kuzungumza naye, hatuwezi kucheka naye na hatuwezi kucheza naye tena
hasa zile ngoma za Waganda, ambazo alipokuwa akifurahi alizicheza kwa ustadi
mkubwa. Ni mama ambaye hakuwa na makubwa na aliwapenda watu wote bila kutegemea
chochote kutoka kwao, alikuwa mvumilivu na mcha Mungu! Mama yetu ni ua ambalo
tulipenda liendelee kuchanua na kuzipamba familia zetu na jamii nzima. Lakini
sasa ua letu la upendo, amani na mshikamano, limepukutika! Ni wajibu wetu sisi
tuliobaki nyuma kuchanua na kupendeza! Huo ndio ujumbe wa maisha ya Marehemu
Mama yetu Ma Clementina. Upumzike kwa
Amani mama yetu mpendwa.
Wakati wa ibada ya mazishi ya Mama Clementinaya, Askofu Msaidizi
Methodius Kilaini, alizitaja sifa nyingi za mama yetu; kwamba mama huyu mbali
ya kuwa mchamungu na kuwalea watoto wake kwa msingi wa imani na maadili bora,
alikuwa mama mwenye upendo kwa watu wote na ni miongoni mwa watu ambao walikuwa
wakijitolea kutoa chakula bure kwa mapadre wa Jimbo katoliki la Bukoba. Alikuwa
ni mama mwenye moyo wa kusaidia watu anaowafahamu na asiowafahamu. Ushuhuda huu
wa Askofu Kilaini, uliungwa mkono na watu wote waliotoa salaam za rambirambi
kutoka viongozi wa serikali na vyama vya siasa. Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Makazi Profesa Anna Tibaijuka, naye alitaja maslahi binafsi kwamba huyu alikuwa
kama mama yake mzazi pia aliziunga mkono sifa alizozitoa Askofu Kilaini, alimtaja Mama
Clementina, kama mfano wa kuigwa, kwamba ni mmoja kati ya wanawake wachache
wa taifa letu waliotoa mchango mkubwa
lakini hawasikiki.
Marehemu Ma Clementina Tunu Mundigo ( au, kwa waliokuwa
karibu naye alijulikana kama Ma Keleme) alizaliwa akiwa mtoto wa kwanza wa Mzee
Clemence Mundigo na Ma Shelestina Mpabuka, tarehe 15 Desemba 1927 , huko
Kagondo – Karugulu, Bukoba Vijijini. Alisoma shule ya msingi Bukoba na baadaye
baba yake, ambaye alipenda na kuithamini elimu, alimpeleka mama yetu shule za
Bwanda na baadaye Nabingo zote za huko Uganda. Ni wakati ambapo watoto wa kike
walikuwa wanaachwa nyuma kielimu na kutoa upendeleo kwa wavulana, lakini baba
yake na Ma Clementina, alikuwa wa pekee, alimsomesha binti yake hadi elimu ya
juu. Kwa maneno mengine, Mama yetu alikuwa msomi ambaye hakujitukuza kama
ilivyo jadi ya ndugu zake akina “Nshomile”. Alipoongea kingereza, ndipo mtu
angeanza kuhisi kiwango chake cha elimu, vinginevyo baada ya mme wake kustaafu
na kuishi kijijini hakuwa na tofauti na
wanawake wote wa vijijini.
Mnamo tarehe 21 Aprili 1948 Ma Keleme, alifunga ndoa
takatifu na Omulangira Gosbert Marcel Rutabanzibwa ( sasa naye ni hayati)
katika parokia ya Rubya, Bukoba. Katika
ndoa yao ya miaka 49 waliyoishi pamoja, walibarikiwa kupata watoto tisa, wa
kike watano: Sr.Clementia, Hilda, Jean, Lucy na Adeline, na walipata watoto wa kiume
wanne: Patrick, John-Bosco,Anthony na Victor. John-Bosco na Victor walikwishatangulia
mbele ya haki. Ma Clementina, amejaliwa kuwa na wakwe, wajukuu na kitukuu.
Mme wa mama yetu,
Omulangira Gosbert Rutabanzibwa, ni miongoni mwa wasomi wa kwanza wa taifa
hili. Ukienda Uhamiaji faili la kwanza na Pasi ya kusafiria nje ni la Mwalimu
Nyerere, la pili ni la Mzee Kawawa na la tatu ni la Mzee Gosbert Rutabanzibwa.
Alisoma na Marehemu baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kule
Makerere Uganda. Baada ya Uhuru, Omulangira Gosbert Rutabanzibwa, alilitumikia
taifa letu kwa Nyanja mbali mbali. Alikuwa balozi wetu New Dehli (India),
Ottawa (Canada) na Washington,DC (Marekani). Huko kote aliambatana na Mama yetu
Ma Clementina. Kuna ushuhuda kwamba Mama yetu, aliwajali na kuwahudumia vizuri
watanzania waliokuwa kwenye nchi hizi ambazo mme wake alikuwa balozi.
Pia kuna ushuhuda mwingine kwamba Ma Clementina, alijenga
uhusiano katika nchi hizo za kigeni na kuendeleza utamaduni wa ukarimu wa Mtanzania.
Kuna mwandishi wa vitabu wa Amerika, anayemtaja Ma Clementina kwenye kitabu
chake kwa kushangazwa na kitendo cha mama huyu kumsindikiza kutoka kwenye
nyumba ya Balozi wa Tanzania, hadi kwenye gari wakati wa kipindi kikali cha
baridi. Ma Clementina, alimshangaza mzungu huyo kwa jibu lake: “ Utamaduni wetu
sisi tunamsindikiza mtu akija kututembelea, kwa vile wewe una gari, ni lazima
nikusindikize hadi kwenye gari lako..!”
Hizi ni baadhi ya sifa za Mama yetu, lakini kuna sifa
nyingine nyingi. Mme wake alikuwa Balozi na kuiwakilisha serikali ya Tanzania,
nchi za nje; sifa alizozipata Balozi Rutabanzibwa, zilikuwa na msingi mkubwa –
nyuma ya sifa hizo ni Ma Clementina. Mama huyu aliwajibika katika kujenga na
kulea familia yake katika misingi ya Kikristo na kizalendo miaka yote ya uhai
wake. Kwa wengi waliomfahamu, alikuwa mama aliyejinyima mengi maishani ili
familia yake, mme wake na watoto wafike
mbali kiroho na kimaisha. Kutokana na jitihada hizo, Balozi Rutabanzibwa,
anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliolitumikia taifa letu kwa uadilifu mkubwa.
Watoto wa Ma Clementina wanaofanya kazi hapa Tanzania, wanatajwa kuwa ni
miongoni mwa watanzania wachache wenye kulitumikia taifa hili kwa uzalendo
uliotukuka. Hivyo mama huyu alikuwa na sifa ya kuitunza familia yake vizuri kwa
kuiandaa kulitumikia taifa letu la Tanzania. Kifo chake si pigo tu kwa familia,
ndugu na jamaa, bali ni kwa watanzania wote.
Mama yetu ni mfano bora wa msemo wa “ Mama ni moyo wa
familia na mama ni mzazi wa taifa”. Mama yetu ametoa mchango mkubwa kwa taifa letu kwa kuilea kwa maadili bora
familia yake kiasi cha kutoa watu bora wa kulitumikia taifa letu kwa uzalendo
mkubwa.
Tunamlilia mama yetu, tunamkumbuka na kumwombea ili
Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www. Karugendo.net
0 comments:
Post a Comment