UHAKIKI WA KITABU: SUGU, MUZIKI
NA MAISHA: From The Streets To Parliament.
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni SUGU,
MUZIKI NA MAISHA:From The Streets To Parliament, Kimeandikwa na kuchapishwa na
Sugu na amekipatia kitabu chake namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu
duniani (ISBN): 978 9987 9491 1 3
.Kitabu kina kurasa 147 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni
mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Hiki ni kitabu kinachoyaelezea maisha ya
Mheshimiwa Sugu: Joseph Osmund Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya mjini kupitia chama
cha CHADEMA. Ndani ya kitabu hiki anaelezea vizuri jinsi Muziki ulivyoyajenga
maisha yake na jinsi alivyoibuka kutoka mitaani kuelekea kwenye Bunge.
Sugu mwenyewe anasema: “ Nilipokuwa mdogo
sikutarajia kabisa kama siku moja ningekuja kujulikana na kuwa maarufu kiasi
hiki na kwa jina la Sugu... Jina hili hapo nimelipata kuitpita muziki wa Rap au
Bongo Flava, lakini historia halisi inaonesha wazi kuwa ninastahili na kwa
kweli nimelipenda sana kwa maana naamini linaendana na mimi hasa...Nahani
kwamba nililipenda jina la Sugu kuliko haa niavyoyapenda majina yangu mengine
ya mwanzo niliyowahi kuyatumia... Naamini kuwa nimeweza kufika hapa nilipo
kisanii, hata kimaisha kiujumla kwa sababu ya kuwa Sugu, maisha yangu yote
nimejitahidi kuwa Sugu, Nimekuwa Sugu kwa vikwazo mbali mbali maishani.”
Ingawa kitabu hiki kimeandikwa na Mheshimiwa
Mbunge, tena kutoka chama cha upinzani,
si kitabu cha siasa. Mwandishi anaelezea jinsi alivyopambana na maisha na jinsi
anavyoendelea kupambana na maisha. Ni mbunge aliyotoka kwenye mazingira ya watu
wa kawaida; hakutoka kwenye familia ya Kisiasa na wala hakubebwa kwenye nafasi
yake kama tulivyozoea kuwaona viana wengi wakibebwa na baba zao, jamaa zao au
rafiki zao kuingia katika siasa na wakati mwigine kupata nafasi za juu
serikalini.
Kitabu kina sura 11 na zote zinaelezea mapambano
ya maisha. Pia kitabu kina picha nyingi zinazoonyesha maisha ya Sugu, kuanzia
shuleni, harakati zake za Muziki na hatimaye kuingia Bungeni. Kwa kurasa
zinazofuata nitakifanyia uhakiki kitabu hiki, baada ya kuelezea kidogo
mazingira yanayokizunguka kitabu chenyewe.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Hiki ni kitabu cha
kizazi kipya. Hata lugha iliyotumika ni ya kizazi kipya! Bila kuwa makini mtu
atafikiri ni kitabu cha kiuni. Ukweli ni kwamba lugha iliyotumika kwenye kitabu
hiki ndiyo lugha ya vijana wengi. Ni lugha ya wakati uliopo, itakuja na kupita
na hakuna haja kugombana nayo maana wakati ukuta.
Misemo kama vile: ‘Mbongo’
‘siriaz’ ‘wangenimaindi’’stori’ ‘mademu’ na mingine mingi imejaa kwenye kitabu
hiki. Twaweza kusema kwamba si kiswaili sanifu, lakini ndo lugha ya vijana.
Kama tunataka kuwasiliana na vijana, hatuwezi kukwepa Lughaya vijana. Misemo
hii inaleta mvuto wa kipekee kwenye kitabu hiki ambacho mwisho wake ni kutoa
ujumbe mzito kwa vijana wa Tanzania na kwa wananchi wote wa Tanzania.
Kitabu hiki ambacho
kinayaelezea maisha ya Sugu kinakuja na falsafa mpya: Maisha ni ubishi!:
“Maisha nivile unavyoishi, inakubidi uwe mbishi...”. Na huu ni msemo wa kizazi
kipya. Maana yake ni kutokukata tamaa na kuendelea kupambana hadi kinaeleweka.
Sugu, anaelezea mapambano yake na walimu, mapambano yake na maisha hadi
kusafiri hadi kusini mwa Afrika akitafuta maisha. Katika safari ya maisha yake,
anatuonyesha falsafa hii ya “Maisha ni ubishi”. Ameteleza mara nyingi na
kuanguka, lakini daima alisimama na kusonga mbele.
Kitabu hiki kinakuja
wakati watanzania wengi hawajajenga tabia ya kusoma vitabu na kuandika vitabu.
Wengine wanasema ukitaka kuificha siri kwa mtanzania, iandike siri hiyo kwenye
vitabu. Hakuna atayeiona maana wengi hawasomi. Tuna wabunge wengi, na wengi wao
ni wasomi, ni wangapi wameandika vitabu? Ni wangapi wameandika juu ya maisha
yao? Kwa kiuandika juu yamisha yake, inaonyesha jinsi Sugu, alivyomsomaji wa
vitabu
IV. Muhtasari wa Kitabu
Kwa kifupi kitabu hiki
cha Mheshimiwa Sugu, kinaelezea maisha yake kuanzia utotoni, maisha ya shule,
harakati ya kutafuta maisha, maisha ya kufanya kazi, maisha ya muziki, wivu
kwenye fani ya muziki, manyanyaso ya mapromota, wizi wa kazi za wasanii na
hatimaye maisha ya kisiasa. Yeye mwenyewe amefanya muhtasari wa kitabu chake
kwa maneno : Muziki na Maisha: From The
Streets to Parliament.
“Jina langu halisi ni
Joseph Osmund Mbilinyi. Nilizaliwa 01.05.1972 katika Hospitali ya Serikali ya
Mkoa ya Ligula mjini Mtwara... Mimi ni mtoto wa kwanza kwa mama yangu nikiwa na
wadogo zangu wanne..” (Uk 1)
“ Kuna wakati niliishi maisha
mazuri ya ‘kiushuani’, yaani ‘dingi’ mambo safi ambapo nyumbani kila kitu cha
muhimu kilikuwa kinapatikana kwa familia, wengine wanaita familia yenye neema
au familia bora au hata familia ya mboga tatu!... Kuna wakati niliishi maisha
halisi ya uswahilini. Haya ni masiha ya shida ambapo mimi na wadogo zangu watatu
wakati huo tulilala chumba kimoja...” (uk 1&2).
“Maisha yangu ya utotoni yalikuwa
ni ya kuhamahama kutokana na kazi ya baba yetu ambaye alikuwa mwajiriwa, hali
hii imesababisha niwe na marafiki wengi wa utototni ambao nilisoma nao shule za
msingi na sekondari katika mikoa ya Arusha, Mtwara, Da-es-salaam na Mbeya” (Uk
2).
“Hapa tulifanya utundu wote mpaka
kuvuta “ganja”! Sishauri vijana na hasa wanafunzi wajihusishe na mam bo haya
leo na nakemea kwa nguvu zote, lakini nakiri tulipitia ile kiti aisee” (Uk 7).
Inashangaza sana kuona unyoofu wa
Sugu. Kutaja hata mabaya aliyoyafanya utotoni. Anayaandika maisha yake kwa
uwazi wa kupitiliza. Ni watu wachache
wenye ushupavu huu wa kukubali kujivua nguo mwenyewe.
Baada ya kuelezea maisha yake ya
utotoni, Sugu, anaelezea “Ubishi wake
wakati wa kusoma shule” Na kuonyesha
kwamba daima alipigania haki na hakuwa na woga wa kusema ukweli na kuusimamia.
“Nikaondoka kuelekea bwenini
ambapo nilitoa mizigo yangu na kusaidiwa na wanafunzi wa vidato vya chini,
walikuwa ananipenda kwa kuwa niliongoza kampeni ya kuzuia wanafunzi wa vidato vya hcini kuonewa hasa wale wa form
one, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku wao kutumwa kufua nguo za wanafunzi wa
vitadto vya juu, kampeni hii tuliiendesha na Gibbo pamoja na Bonny” (Uk 11).
Anaelezea alivyotetea haki wakati
akiwa shuleni, hakukubali kuonewa wala mtu mwingine kuonewa. Baada ya kumaliza
kidato cha nne, alijaribu kwenda Bondeni, bila mafanikio. Anaelezea safari yake
ya kwenda Bondeni, ambayo linafanana zile nyingi tunazozikia, jinsi vijana
wanavyojaribu kutoroka kwenda Bondeni kutafuta maisha. Yote hayo yako kwenye
falsafa ya Sugu, kwamba “Maisha ni ubishi”. Maana yake ni lazima kupambana bila
kurudi nyuma.
Sehemu inayovutia sana katika
kitabu chake ni maisha yake ya Muziki. Hapa kuna vituko vya mafanikio,
kushindwa, kudhurumiwa, kunyanyaswa, kuoneana wivu na vituko vya “Wadosi”
(wahindi) jinsi wanavyowanyanyasa wasanii wa muziki.
Sugu, amefichua malalamiko ya
wasanii ya siku nyingi kwamba kazi zao zinaibiwa na wala serikali haifanyi
mpango wowote ule kutunza haki za wasanii. Wadosi, wanavyatua kanda na DVD za
wasanii na kuziuza, bila wasanii kupata faida yoyote ile.
Safari za Sungu nje na ndani ya
nchi zina mvuto wa kipekee katika kitabu hiki. Anaonyesha wazi jinsi Muziki ulivyomsaidia
kusafiri sana nje ya nchi na kumsaidia kupanuka kifikira. Pamoja na kwamba yeye
aliishia kidato cha nne, lakini kuzunguka sehemu mbali mbali duniani kulimfanya
aonekane msomi wa kutupwa.
“Mwezi Oktoba mwaka huo, nikiwa
tayari nimekaa Uingereza kwa miezi takriban miwili nilipata taarifa toka ‘Bongo’ kwamba nilitumiwa
mualiko kwenda Sweden kushiriki tamasha la muziki la WOMEX lililotarajiwa
kufanyika Stockholm mwaka 1998” (Uk 73).
Pamoja na kupata nafasi nyingi za
kwenda nje, Sugu, hakupenda kukaa nje ya nchi. Alirudi nyumbani kuendelea
muziki wake na hatimaye kufanikiwa kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chama cha
CHADEMA.
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Sugu, kwa kazi
aliyoifanya ya kuandika kitabu juu ya maisha yake. Ni watu wachache ambao
wanafanikiwa kuandika maisha yao. Hata wasomi, wanashindwa kuandika maisha yao.
Mara nyingi maisha ya watu wengi yanaandikwa na wengine baada ya wao kutoweka
hapa duniani. Ukweli ni kwamba kazi hii
ni nzuri sana . Kitabu hiki kinaburudisha,
kinasikitisha na kufikirisha.
Pili, nimpongeze kuyaandika maisha yake kwa uwazi
bila kificho. Penye sifa ametaja bila kuongeza chumvi, penye lawama amesema
bila kificho. Ameelezea tabia zake mbaya na nzuri. Kawaida ni kazi ngumu mtu
kujichambua mwenyewe. Mara nyingi kazi hii inafanywa na watu wengine, si mtu
mwenyewe. Maana kuna hatari mtu kujipendelea na kuficha mengine ambayo ni
mabaya. Lakini Mhesimiwa Sungu, amefanya kazi hii kwa kunyoofu mkubwa.
Ukizingatia hatua aliyopo hivi sasa, angeweza kuficha tabia nyingine kama
kuvuta ganja na kuwapenda mademu kupindukia.
Tatu, ni pongezi kwa kazi ya kufichua manyanyaso
ya wasanii wa Muziki. Kumekuwepo malalamiko ya wizi wa kazi za wasanii, lakini
Mheshimiwa Sugu, amefichua wizi huu kwa kuuelezea vizuri.
“Nilipopata taarifa za kuenea kwa kanda feki za
album yangu niliamua kuanza uchunguzi na hatimaye nikapata habari kwam ba dula
la Congo Corridor lililoko Kariakoo walikuwa wakitengeneza na kuuza kazi zangu
bila ya makubaliano yoyote na mimi...Siku moja niliamua kujitutumua na kwenda
dukani kwao, nilipania kupambana kulinda haki yangu, nilipofika niliingia
dukani ambapo nilimkuta ‘mdosi’ mwenyewe na wafanyakazi wake, niliulizia ile
kanda lyangu nikapewa, baada ya kuhakikisha kwamba ilikuwa feki nilijitam bulisha mimi ni nani
na nikawauliza kwanini walikuwa wanauza album yangu bila kuwaruhusu... yule
mdose alinifokea kwa dharau na kunitishia kuita polisi ...” ( Uk 57)
“Wadosi, wamelidhibiti game, wanafanya wanavyotaka
wao kwa msaada wa wadau wachache wazalendo wasio na uchungu wa wasanii wa
naoteseka akiwemo Ruge. Wakati sisi walikuwa wakitufuata Sinza, leo hii kila
siku wasanii wanajazana kwenye mabenchi nje ya ofisi zao utadhani wagonjwa
wakiwa kwenye foleni hopspitali. Kutokana na hali hiyo, hata kama msanii mmoja
au kume watajaribu ‘kuwakomalia’ wapate haki zao, kuna wenzao zaidi ya mia
watawapelekea kazo zao tena huku wakilia na kubembeleza hivyo kukwamisha juhudi
za mtu mmoja mmoja katika kujikwamua” (Uk 84)
“Kwanini tunasema ‘wadosi’ ni wezi? Tunawaita wezi
kwa kuwa tunaamini wanafaidika na mfumo
mbovu wa biashara ya muziki na pengine hata wanautetea na kuulinda mfumo huu
uendelee kuwepo kwa kuwa una faida kwao....” (Uk 84}
Wasanii wa muziki wanapata shida sana kuuza kazi
zao. Mawakala, ambao wengi wao ni “wadosi” wanawanyanyasa na kuwaibia kazi zao.
Wakati mwingine msanii wa muziki analazimika kuuza kazi yake yote kwa fedha
kidogo, wakati aliyenunua anatengeneza fedha nyingi na wakati mwingine kwa
kufyatua kanda na CD feki.
Nne, Mheshimiwa Sugu, ameelezea vizuri manyanyaso
wanayoyapata wasanii wa muziki kutoka kwa mapromota. Amewataja mapromota hao
kwa majina yao na jinsi wanavyowanyanyasa wasanii wa muziki. Na hapa
anaunganisha na vyombo vya habari kama vile Radio na TV. Vyombo hivi vinafanya
kazi ya kuzitangaza kazi za wasanii kwa kuzirusha kwenye Radio na TV. Lakini
kufuatana na maeleoz ya Mheshimiwa Sugu, kwenye kitabu chake ni kwamba bila
kutoa rushwa kazi yako haiwezi kuingizwa kwenye kwenye Radio au TV.
“Nakumbuka rushwa hii ilianzia kwenye redio na
wasanii wakaona mkombozi wao alikuwa ni TV, hasa Channel 5, lakini mdudu wa
rushwa alipoingia na huko ikawa balaa zaidi, mimi mwenyewe ni muathirika wa
tatizo hili nakumbuka niliporudi kwenye game kwama 2004 nilipeleka vido yangu
kwa ‘Moto chini’ pale, dada mmoja aliyekuwa anahusika akaipokea vizuri kabisa
na kuisifu baada ya kuiangalia. Video ile ikapigwa silku chache na mara
ikaingia kwenye top ten, ikaendelea kupanda kidogo naghafla itatolewa kwenye
ite top ten na hata ikawa haipigwi kwenye vipindi vingine, nilishangaa
mazingira iliyotolewa... Sikuamini alichosema! Aliniambia live kwenye simu kuwa
nyimbo yangu ilitolewa kwenye chati na hata kuacha kupigwa kwa kuwa mimi sikuwa
natoa ushirikiano na sikwenda ‘kuwaona’, yaani maana yake slikwenda kuwapelekea
pesa” (Uk114).
Tano, mwandishi amefanikiwa kutumia lugha ya
vijiweni ili kufikisha ujumbe wake. Anasema ametokea mitaani kuingia mjengoni,
ametumia lugha hiyo ya mitaani kuyaelezea maisha yake. Hata hivyo na kwa umri
wake, yeye ni kizazi kipya. Kizazi hiki kina mambo yake, kina lugha yake. Kama
niivyosema mwanzoni, wengine watafikiri ni kuivuruga lugha na si kiswaili
sanifu. Lakini ndo hivyo jamii inapiga hatua na kupitia hatua mbali mbali. Kuna
kazi wasomi kuhakikisha kiswahili sanifu, kinabaki na kutunzwa; lakini pia kuna
haja ya kukubali lugha ya vijana.
Na hatimaye ni pongezi kwa maelezo yake juu ya
Ubunge wa Mbeya. Haikuwa kazi raihisi. Yalikuwa mapambano na kufuatana na
falsafa yake ulikuwa ni “Ubishi”. Akafanikiwa kuingia Mjengoni, lakini kwa kuwa
yeye anakumbuka alikotokea: kutoka mitaani hadi kuingia mjengoni, anaukumbuka
Muziki na anaendelea kutumbuiza hadi leo hii
VI. HITIMISHO.
Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu
kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Kwa vijana ambao wanakata tamaa na maisha,
wajifunze kutoka kwa Sugu, kwamba maisha ni ubishi. Kwa kusoma kitabu cha Sugu,
kuona jinsi alivyopambana na maisha na hatimaye kufanikiwa kuingia mjengoni,
nao wafuate nyayo.
Namshauri mheshimiwa Sugu, pindi akitaka kutoa
toleo la pili la kitabu chake, atafute wahariri wazuri, warekebishe makosa ya
hapa na pale, ili kitabu kiwe kizuri zaidi. Hata sasa kitabu chake si kibaya,
ingawa kuna makosa madogo ya hapa na pale. Si makosa ya kukichafua kitabu, bali
yakiondoka itakuwa vizuri zaidi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment