UHAKIKI WA KITABU: IS IT THE
FUNDAMENTAL CHANGE?
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni IS IT THE
FUNDAMENTAL CHANGE?, Kimeandikwa na Bagaya Ibrahim Kisubi na Nyanjura Doreen
Mchapishaji wa kitabu hiki ni waandishi wenyewe na wamekipatia kitabu chao namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu
duniani (ISBN): 9970-9069-0-1. Na anwani yao ya parua pepe ni thefundamentalchange@gmail.com
Kitabu kina
kurasa 137 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus
Karugendo. Ukitaka kukipata kitabu hiki piga simu au tuma sms kwenye namba +255
754 6331 22. Bei ya kitabu hiki ni shilingi elfu 15 za kitanzania.
II. Utangulizi
Kitabu hiki IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE?,
kimeandikwa na vijana wawili wa Uganda. Vijana hawa ni Bagaya Ibrahim Kisubi na Nyanjura Doreen na
wote wawili wanasoma chuo kikuu cha Makerere. Wamezaliwa, wakamkuta Rais
Museveni akiitawala Uganda; wakasoma shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu
bado Rais Museveni anaendelea kuitawala Uganda.
Historia inawambia vijana hawa wawili kwamba Rais
Museveni, aliingia madarakani akiwa na ahadi ya kuleta Fundamental Change:
Madiliko ya msingi au mabadiliko muhimu katika utawala wa nchi ya Uganda
iliyokuwa imeparanganyika wakati wa utawala Idi Amin, ukombozi baada ya Idi
Amin, na utawala wa pili wa Obote.
Swali la vijana hawa, ni je Museveni kuendelea
kukaa madarakani na kuikandamiza demomrasia ndiyo Mabadiliko ya muhimu
aliyowahaidi waganda?
Vijana hawa ambao wanatamani mabadiliko ya kweli
ndani ya nchi yao ya Uganda, wanatumia misemo ya watu watatu wa zamani ili
kuelezea vizuri kilicho moyoni mwao. Wanawanukuu Mchungaji Martin Niemoller wa
Ujerumani, Martin Luther King na Napoleon. Nafsiri ni yangu:
“ Walipowashambulia Wajamaa, nilikaa kimya kwa
vile mimi sikuwa mjamaa. Wakawashambulia wa vyama vya ushirika na wafanyakazi
pia nikaa kimya maana sikuwa kwenye vyama hivyo. Wakawashambuliwa wayahudi
nikakaa kimya, sikuwa myahudi mimi. Wakashambuliwa wakatoliki, kwa vile
nilikuwa protestant, nikajikalia kimya. Waliponigeukia mimi na kunishambulia
hakukuwa tena na wa kusimama kunitetea” Mchungaji Martin Niemoller.
“Maisha yetu yanafikia mwisho siku tunapokaa kimya
kwa mambo ya msingi” Martin Luther King.
“Dunia inateseka sana, si kwa sababu ya watu
wakatili na wabaya, bali kwasababu ya ukimya wa watu wazuri” Napoleon.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha IS IT THE FUNDAMENTAL CHANGE?, ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Tarehe 11 mwezi wa nne ni siku yenye kumbukumbu nzito kwa nchi za Uganda na Tanzania. Tarehe kama hiyo mnamo mwaka 1979, majeshi ya ukombozi ya Tanzania na Uganda (Wapiganaji wa msituni) yalifanikiwa kumtimua Iddi Amin kutoka Kampala, na kuandikwa historia ya kumaliza utawala wa kimabavu uliodumu Uganda zaidi ya miaka tisa. Wakati ule ilionekana Iddi Amin, alikuwa amekaa miaka mingi madarakani. Leo hii Rais Yoweri Kaguta Museveni, anakaribia kufikisha miaka 20 akiwa madarakani. Wameziba midomo ya watu wengine kusema na kuhoji na hili halikuwa ni lengo Rais Museveni, alipokuwa akiingia madarakani.
Ingawa
ushindi huo wa 1979 ulipokelewa kwa
furaha na wanganda pamoja na ndugu zao Watanzania, bado kuna ukweli ambao hadi
leo hii bado unaishia ndani ya mioyo ya wanganda. Pamoja na mabaya yote
yaliyoandikwa na kutangazwa juu ya Iddi Amin, ukweli unabaki kwamba huyu ni
rais pekee wa Uganda ambaye hakuwa na mali binafsi, hakuwekeza fedha nje ya
nchi; alitumia fedha ya Uganda kwa maendeleo ya Uganda.Hakuwa na fedha nje ya
nchi, aliamini fedha zote ni zake na kama zake yeye Rais, bali fedha ni za
waganda. Alipokuwa akiikimbia Uganda, alikuwa na uwezo wa kubeba vitu vingi,
lakini hata ndege ya Rais ambayo eti alienda kuinunua akiwa na fedha kwenye
mkoba na kuwa mtu wa kwanza kununua ndege kwa mtindo huo, hakuondoka nayo,
aliicha maana aliamini si mali yake bali ni mali ya Waganda. Inasemekana kwamba
nyumba za Ubalozi wa Uganda katika nchi
nyingi zenye uhusiano na Uganda zilijengwa na Iddi Amin. Hata nyumba nzuri za
Mapolisi zilijengwa na Iddi Amin. Ingawa Iddi Amin, alikuwa mtu ambaye hakuwa
na elimu ya juu, lakini alipenda elimu. Vijana wote waliomaliza kidato cha sita
wakati wa utawala wake na kushinda kwa daraja la kwanza, aliwapeleka wote kwa
nguvu kujifunza ualimu, ili warudi na kuwafundisha watoto wengine. Walimu wengi
walipoikimbia Uganda kwa kuogopa usalama wa maisha yao, Iddi Amin, eti alitumia
ndege yake ya Urais, kwenda Ghana, kusomba walimu na kuwaleta Uganda ili
wawafundishe watoto wa Uganda. Yapo mengi mazuri aliyoyafanya Iddi Amin, lakini
yalifunikwa kwa propaganda za kisiasa. Si lengo la uchambuzi huu kumtetea Iddi Amin, bali ni kutolea mfano wa
tarehe 11 mwezi wa nne.
Kumbu
kumbu nyingine mbaya ya terehe hiyo ya 11 mwezi wa nne ni mwaka huu
alipokamatwa na kuwekwa ndani binti mdogo wa miaka 22, Nyanjura Doreen, na
kuwekwa ndani kwa kuandika kitabu kinachomkosoa Rais Yoweri Museveni. Furaha ya
kumfukuza Iddi Amin, imeanza kuleta machungu
na masikitiko katika nchi ya Uganda zaidi ya miaka 31 Iddi Amin kutoka
madarakani. Kwa vile Tanzania, ilishiriki kikamilifu kumfukuza Iddi Amin,
haiwezi kukaa kimya, historia inapojirudia. Ni lazima watanzania kushirikiana
na waganda kulaani kitendo cha serikali ya Uganda kumkamata Binti Mdogo na
kumfunga gerezani kwa kitendo cha kuandika kitabu.
Nyanjura
Doreen na mwenzake Bagaya Ibrahim Kisubi, wameandika kitabu : “Is It The
Fundamental Change?” wakilenga kufichua ukweli uliojificha juu ya maisha na
utawala wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda. Wanasema Rais Yoweri,
alipoingia madarakani, alitoa ahadi ya kuleta mabadiliko ya msingi.
Kinachoonekana leo ni tofauti kabisa. Vijana hawa wawili na wengine wengi
nchini Uganda, wamezaliwa wakati Rais Yoweri akiitawala Uganda, wamekuwa
wamesoma hadi chuo kikuu, bado Rais ni
Yule Yule. Na hili ndilo swali lao kubwa, kwamba mabadiliko ya msingi yanaweza
kuwa na maana yoyote ile kwa kumtengeneza Rais wa maisha? Kwa kuizika demokrasia
na kunyamazisha vyama vya siasa vya upinzani?
Walichofanya
vijana hawa ni kukusanya maneno ya Rais Museveni mwenyewe, na kuhoji ukweli wa
yale yote aliyoyatamka siku akiingia madarakani hadi leo hii. Na jibu ni kwamba
wakati umefika wa “Mzee” kupisha kizazi kipya. Kitu ambacho Rais Museveni na
serikali yake hawako tayari kukisikia, na ndicho kisa cha Kumkamata na kumuweka
Doreen na mwezake ndani.
Unapofika
wakati vijana wakawa tayari kwa lolote, ni hali ya kuogopesha. Kwanza vijana ndiyo asilimia kubwa ya watu duniani.
Siku vijana wakikubaliana kuungana na kuwa na sauti moja na kuamua kuingia mitaani; viongozi wanaotaka kuzeekea madarani
watapata taabu kubwa sana. Watajikuta nje ya Bunge na ni jambo la kusikitisha
kwamba huko vijijni hawatapokelewa
Nilikutana
na Nyanjura Doreen,mwaka huu jijini Mwanza siku ya Pasaka, akiwa na nakala
chache za kitabu chake cha “Is it The Fundamental Change?” Ni vigumu kuamini
kwamba msichana mdogo kama Doreen, anaweza kuwa na maneno ya kuongea; maneno ya
kuwaomba viongozi waliokaa muda mrefu madarakani, waachie ngazi vijana
chipukizi. Doreen Nyanjura,aliniomba
nikifanyie uhakiki kitabu chake na kukiweka kwenye magazeti ya Tanzania. Lengo
lake kubwa lilikuwa ni kukisambaza kitabu hicho kabla ya kukizundua Jijini
Kampala tarehe 11.4.2012. Nafikiri alijua wazi kwamba uwezekano wa serikali ya
Uganda kukizuia kitabu hicho kisizinduliwe na kusambazwa ni mkubwa, hivyo aliamua kusambaza nakala chache nchi jirani.
Na
huo ulikuwa ujumbe tosha kwa Serikali ya Uganda kwamba mbinu za kizamani za
kuzuia vitabu kusomwa, kuzuia vitabu kuzinduliwa, zimepitwa na wakati. Sasa
kitabu kimefika Tanzania, kutoka hapa kitasambaa Kenya, Rwanda , Burundi na
nchi nyingi za kiafrika hata na Ulaya na Amerika. Na kitendo cha kuwakamata
waandishi wa kitabu hiki na kuwaweka
ndani ni mtindo wa kizamani usiokuwa na tija. Hata mtu ambaye alikuwa hana
habari juu ya Nyanjara Doreen, sasa amemfahamu na atataka amfahamu
vizuri kwa kutaka kufahamu ni kwanini binti mdogo kama huyo akamatwe na kuwekwa
ndani, kutafanya kitabu hicho kitafutwe kwa udi na uvumba.
Wakati
akinipatia nakala ya kitabu chake alisema “ Karugendo, nisaidie kukitangaza
kitabu hiki, maana najua yaliyo mbele yangu. Museveni, atanikamata na kuniweka
ndani. Pia anaweza kuamua kuvichoma vitabu vyote”. Nilimsihi kwa vile alikuwa
Tanzania, na ana hofu ya kukamtwa, basi
abaki Tanzania kama mkimbizi wa kisiasa. Jibu laki lilikuwa “ Siwezi kuikimbia
nchi yangu, ninajua nina haki zote za kutoa maoni yangu, ni haki yangu kutetea
haki na kuhakikisha demokrasia na mabadiliko ya msingi yanatendeka nchini
Uganda. Ni bora nikamatwe, nifungwe na hata ikibidi niifie nchi yangu”.
Nilishangaa kuona binti mdogo wa miaka 22, akiwa na ushupavu wa kutisha. Na
kweli siku mbili baada ya kukutana naye Jijini Mwanza, alikamatwa siku ya
kukizindua kitabu chake na kutupwa gerezani.
Uzinduzi
wa kitabu chao ulikuwa ni waina yake. Waandishi walivalia nguo za wasomba taka
taka na kushikilia mifagio na vyombo vya kukusanyia takataka na kuelekea kwenye
uwanja wa Katiba wa jijini Kampala ili kuusafisha waweze kuzindua kitabu chao
kwenye uwanja ulio safi. Polisi waliwakamata wakiwa njiani kuelekea kwenye
uwanja wa Katiba.
Nyanjura
Doreen na Bagaya Ibrahim Kisubi, hawakupenda kuwa kimya; walitaka
kuyashughulikia mambo ya msingi: Kutetea demokrasia, kutetea haki za binadamu,
kutetea uhuru wa kujieleza na kumweleza wazi wazi rais Museveni kwamba amekaa
sana madarakani wakati umefika wa kuwaachia wengine nafasi ya kuliongoza taifa
la Uganda.
Pamoja
na ukweli wa kujua kitakachotokea;
kukamatwa, kupigwa, kuwekwa ndani na wakati mwingine kupoteza maisha yao, bado
waliendelea na mipango yao ya kukizindua kitabu chao kwenye uwanja wa katiba.
Hili linashangaza ni ujumbe si kwa Rais Museveni peke yake, bali kwa marais ya
Afrika ya mashariki na Afrika nzima: Kwamba mabadiliko ya msingi yataletwa na
Kizazi kipya. Matumizi ya silaha yanapitwa na wakati. Mbele yetu ni nguvu ya
kizazi kipya mbayo kuizuia ni lazima mtu awe tayari kuwekwa kwenye rekodi ya mauaji ya kimbali.
Nilipomshawishi
Nyanjura Doreen, kubaki Tanzania kama mkimbizi wa siasa, alikataa kabisa. Kwa
maneno yake mwenyewe alisema: “ acha niende kufungwa, acha nife kama ni kufa
kwani mimi ni bora zaidi ya nani? Septemba I 2009 zaidi ya vijana 40 waliuawa, hawa ni
pamoja Kauma Joseph, Nakazi Deborah,
Nahumma Brenda, Katum Richard, Kalamba Ronald, Kamoga Sula, Aliwo Abed,
Nabakoza Christine, Bisso Steven,Ssango Kyobe, Ikongo Samuel, Mayanja Bruno, Bukenya
Faisal, Mukwanga Kaziru, Benjamin Parnot
Ateere, Batiibwe Badru, Muganga Huzair,Busulwa Hassan, Bwesigwa, Grace
Sserunjogi, Joseph,Muganga Hakim, Kafuma Frank, Nampijja Jackie, Magembe Ali,
Lukwago Sulaiti, Karungi Annet, Erimweya Mawanda, Nsereko Robert, Batibwe
Abdullah, Nampijja Beatrice, Nahumma Brenda, Ngaba Moses. Vijana wote hawa
isipokuwa Batiibwe Badru aliyekuwa na umri wa miaka 39, walikua kati ya miaka 2-25. Na wengine walikufa
kwenye Makaburi ya Kasubi, Masaka, Kampala, Gulu, Jinja, Mbale na sehemu
nyinginezo”.
Alinielezea
haya kwa uchungu mkubwa. Akilalamika kwamba vijana ambao wangepaswa kuwa
shuleni wakisoma, wanakamatwa na kuwekwa
gerazani. Yeye Doreen na Mwenzake, wako mwaka wa mwisho kwenye chuo
kikuu cha Makerere.
Waswahili
wana msemo wa “Mwenzako akinyolewa wewe
tia maji” Sisi watanzania tunajifunza nini kutokana na tukio la Serikali ya Uganda kuwakamata na
kuwashitaki waandishi?
Baada
ya kuona mazingira yanayokizunguka kitabu hiki kilichoandikwa na vijana hawa wa
Uganda, sasa kwa kufupi tuone muhtasari wa kitabu chenyewe.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Kitabu hiki kina sura
sita. Katika sura ya kwanza tunaelezewa historia ya Uganda, kuanzia Ukoloni,
utawala wa kwanza wa Obote, utawala wa Iddi Amin, utawala baada ya kumfukuza
Iddi Amin na hatimaye Museveni kuingia madarakani.
“ Mwaka 1966...
ilishangaza sana Iddi Amin, alipotoka DRC na dhahabu kubwa na kuiuza kwenye
Benki ya Uganda na kujipatia fedha ipatayo paundi 17 elfu...” tafsiri yangu.Uk 20
Obote, alimtumia Iddi
Amin, kuvuruga utawala wa Kabaka na hatimaye Iddi Amin, akumwondoa Obote
madarakani. Uk 22- 23.Inaonyesha wazi kwamba kama Obote, angelikuwa mwangalifu
angemshutukia mapema Iddi Amin.
Hatimaye Iddi Amin,
akawafukuza wahindi kutoka Uganda, kwa kisingizio cha kuinyonya Uganda, huku
wakipeleka fedha nje ya nchi. Uk 24.
Sura yote ya kwanza
inaelezea matatizo ya uongozi yaliyoikumba Uganda hadi kufikia hatua ya Iddi
Amin Kuivamia Tanzania, na kosa hilo likasababisha Iddi Amin kufukuzwa Uganda.
Sura ya pili inaelezea
jinsi Museveni alivyoingia madarakani tarehe kama ile ya Iddi Amin kuingia
madarakani. Vijana hawa wanaonyesha tarehe hiyo inavyokuwa na aina fulani ya
kuwafananisha Museveni na Iddi Amin.
Katika sura hii ya pili
ndo tunavyosikia Museveni,aliyeingia madarakani akiwaahidi waganda Mabadiliko
ya muhimu, alivyoanza kufanya mbinu za kubaki madarakani kwa kuongeza mihula ya
utawala wake. Hadi leo hii baada ya zaidi ya miaka 20 madarakani, Museveni hana
mpango wa kuondoka madarakani.
Sura ya tatu inaelezea
mambo ya ukweli na muhimu juu ya Museveni: Katika kitabu hiki vijana hawa wanasisitiza
kwamba kuna mambo mengi muhimu yasiyojulijana juu ya Museveni:
Umri wa Rais Museveni ni
utata mtupu, hadi yeye hafahamu alizaliwa lini(Uk 54). Kwa maoni ya vijana hawa
ni kwamba hata Museveni akitaka kugombea urais 2016, hakuna wa kuhoji juu ya
umri wake, maana hata yeye mwenyewe hafahamu umri wake.
Wazazi wake nao wana
utata. Kwa uhakika mama yake ni Esteeri Kokundeka. Lakini mtu anayejulikana kama
baba yake Amos Kaguta, kuna mashaka kama
huyu ni baba yake (Uk 54). Ni kwamba familia ya Museveni, haikuwa na uwezo wa
kumsomesha, hadi familia ya Byanyima, ikajitosa kumsaidia kusoma.
Maelezo ya vijana hawa
kwenye kitabu chao ni kwamba Museveni hakuwa na akili za kipekee darasani, ndo
maana alipomaliza sekondari hakuweza kupata nafasi ya kusoma Makerere.
Alitafutiwa nafasi Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.
Maisha ya kisiasa ya
Museveni, yalianzia Dar-es-salaam. Na baada ya kumaliza masomo, Museveni, alipata
kazi kwenye serikali ya Obote, sehemu ya usalama wa taifa – kitengo kilichokuwa
kinamsaidia Obote, kuendelea kubaki madarakani kwa mabavu. Iddi Amin
alipopindua Uganda, Museveni , hakuwa na njia nyingine zaidi ya kukimbia.
Hakukimbia kwa moyo wa kizalendo bali alikimbia kuiokoa roho yake ( Uk 55).
Tunaelezwa kwamba, kwa
kazi yake ya usalama wa Taifa, wakati wa Obote, Museveni, ambaye kwa wakati ule
alikuwa kijana alikuwa na fedha nyingi, kiasi kwamba baada ya kukimbilia
Tanzania alikuwa na fedha za kutosha kiasi cha kuponda maisha. Aliponda maisha
na msichana ambaye baadaye ndiye alifunga naye ndoa, Janet Kataha.
Maisha ya starehe ya ya Museveni hayakuchukua muda, kwa vile hakuwa
na kazi. Alihangaika kutafuta kazi Tanzania nzima bila mafanikio, hadi
akalazimika kufundisha Chuo cha Ushirika Moshi.Mshahara kiduchu alioupata kwa
kufundisha Chuo cha ushirika Moshi, ndo ulimsaidia kufunga ndoa na Janet mnamo
mwaka 1973. (Uk 57).
Baada ya kujiingiza
kwenye ukombozi wa Uganda Museveni, alijawa na uchu wa madaraka.Aliamini
matumizi ya nguvu kuingia madarakani. Hadi leo hii lugha yake ni “Mauaji” ili
kulinda utawala wake. Kwa kulinda utawala kwake, Museveni anaua hata watu
waliokaribu yake. Hii ina ushahidi wa miaka mingi. Rafiki zake wa karibu
kama Mwesiga Black, Raiti Omongin na V.
Rwaheru, walikufa kwenye mazingira ya kutatanisaha ( Uk 60).
Ilishangaza kwamba Iddi
Amin, alinunua ndege ya rais kwa dola
alizokuwa amebeba mfukoni mwake, ukweli ni kwamba hata Museveni anaposafiri nje
ya nchi anabeba dola mfukoni kana kwamba hatarudi tena Uganda. Jamaa wa
Museveni wanaishi kwenye nyumba za serikali na kupata mshahara (Uk 72).
Sura ya nne, inaelezea
juu ya siasa za Uongo za Museveni. Tunaelezwa mambo yote kumi ambayo Museveni,
aliorodhesha kuyatekeleza alipoingia madarakani mwaka 1986. Mambo haya mengi ni
kinyume na jinsi alivyoahidi mbele ya waganda. Mabadiliko ya msingi, yamekwama!
Museveni, aliwashambulia viongozi wa Afrika waliokuwa wakienda kwenye mikutano
ya kimataifa na ndege zao za kifahari wakati watu wao wakifa kwa njaa, ni
viongozi wa ovyo! Leo hii yeye ana ndege ya kifahari ambayo inatumika
kuihudumia familia yake. Waganda walishuhudia ndege hii ikimbeba mtoto wa
Museveni kwenda Ujerumani kujifungua.
Sura ya tano inajadili
mzimu wa Luwero. Ukweli ni kwamba watu wengi walikufa Lowero ukilinganisha na
wale waliochinjwa na Iddi Amin. Museveni, amekuwa kilaumu uongozi wa Obote,
kuendesha mauaji ya Lowero, lakini ukwei ni kwamba Museveni, ndiye chanzo cha
mauaji haya!
Sura ya sita inajadili
vuguvugu la mabadiliko na jitihada za Museveni kunyamazisha nguvu hizi za
vijana. Kitabu hiki ni sehemu ya
vuguvugu hizi.
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kuwapongeza vijana hawa wawili kwa
kujitosa kuandika kitabu hiki huku wakijua hatari kubwa iliyo mbele yao. Ukweli
ni kwamba kazi hii ni nzuri sana . Kitabu hiki kinaburudisha, kinasikitisha na kufikirisha.
Pili niwapongeze vijana hawa wawili kwa
kuthubutu kuandika mambo haya ambayo wengi wangeogopa kuyaandika. Inahitaji moyo wa ushupavu kuandika kitabu kinayofichua
ukweli uliofichika, juu ya kiongozi aliyemadarakani mwenye vyombo vyote vya
usalama na madaraka makubwa juu ya uhai wa kila raia ndani ya taifa lake.
Tatu, ni
ule uzalendo wa kuwa tayari kufa kwa kulitetea taifa. Wakati watu wazima
wanaogopa kujitokeza kupinga utawala wa mabavu, vijana wadogo wenye umri wa
miaka 23, wanajitokeza kuwa msatari wa mbele kuongoza mapambano.
VI. HITIMISHO.
Ni wazi ningependa kuwashauri wasomaji wangu
kukinunua kitabu hiki na kukisoma. Nimeelekeza namba za simu ambazo ni +255 754
6331 22 ili kukipata kitabu hiki. Pamoja na ukweli kwamba bei ya kitabu hiki ni
kubwa, ni muhimu kukinunua na kujisomea yale tunayoyajua na tusiyoyajua.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment