Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Esther Bulaya



MWANA MAMA MHESHIMIWA ESTER AMOS BULAYA.

Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea Mheshimiwa Ester Bulaya mbunge wa viti maalumu kundi la vijana wa chama cha mapinduzi mkoa wa Mara. Kama kawaida yetu hatuandiki juu ya maisha binafsi juu ya Ester Bulaya, hayo tunawaachia watu wengine. Sisi tunamwangalia Mwana Mama Ester Bulaya na mchango wake katika taifa letu la Tanzania. Pia tunajua wazi kwamba mengi yameandikwa juu ya Mheshimiwa Ester Bulaya: hata hivyo  tumeamua kuandika juu yake kwa kuamini yanayoandikwa juu yake ni ya kisiasa na mara nyingi yenye ushabiki wa chama chake cha CCM. Sisi tunamwandika mama huyu kwa jicho tofauti na ndiyo maana tunaamini ana sifa za kuingia kwenye safu iliyoanzishwa kwa lengo la kuandika habari za mama wanaotoa mchango mkubwa katika taifa letu, lakini habari zao haziandikwi na wala hazijulikani.
Sifa kuu aliyonayo Mheshimiwa Ester Bulaya, ni kupigania haki za vijana bila kuangalia itikadi zao za vyama, dini wala kabila zao. Yeye amejipanga kupigania haki za vijana wa Tanzania; Mwana mama  huyu ni miongoni mwa vijana wachache wanaoona ukweli kwamba hatima ya uhai wa Tanzania, iko mikononi mwa vijana.  Huyu ni miongoni mwa vijana wachache wanaoona ukweli kwamba vijana wa Tanzania wakiuungana na kufanya kazi kwa pamoja, hata kama watakuwa na itikadi tofauti za vyama, wataweza kulijenga taifa lenye maendeleo na lenye kujiamini . Hivyo amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na vijana wote, na hasa wanasiasa wenzake, wabunge wenzake bila kujali wanatoka chama gani cha siasa.
Msimamo wake huo wa kushirikiana na vijana wa vyama vya upinzani, umemwingiza matatani ndani ya chama chake. Chama chake cha CCM, kinamwangalia kwa jicho la tahadhari na baadhi wakifikiri ni Mwana mama huyu ni msaliti. Yeye mwenyewe anasema kwa kujiamini: “Nipo bungeni kuwawakilisha vijana na niko tayari kupoteza hata uhai wangu kwa kulitetea taifa langu hata kama nitaonekana msaliti katika chama changu kwa kukemea maovu,”
Wakati CCM, wakimtilia shaka Ester Bulaya na kumkosoa kushirikiana na wapinzani, kuna wanaomchukulia Mheshimiwa Bulaya, kuwa ni mwoga: Anaona nusu tu ya ukweli, haitoshi kushirikiana na vyama upinzani. Muhimu ni kutambua kuwa CCM si baba wala mama, na wala CCM si Tanzania! Kwa maana kwamba CCM, itapita kama vitakavyopita vyama vyote  vya siasa. Tanzania itabaki! Hivyo kitu muhimu ni Tanzania. Ukweli huu Mheshimiwa Ester Bulaya anauona nusu nusu! Maana kuna wakati naye anakumbwa na wimbi kubwa la kukitukuza na kukishangilia chama chake hata bila kutafakari na kuchucha uzito wa hoja inayokuwa jukwaani. Siku atakapobahatika kuuona ukweli huu mzima, huyu atakuwa miongoni mwa vijana wa kulivusha Taifa letu kuelekea maendeleo na utulivu wa kisiasa.
Mheshimiwa Ester Bulaya, alizaliwa Ilala Dar-es-Salaam, tarehe 3 Machi 1980. akiwa darasa la sita, baba yake mzazi Amos Bulaya aliyekuwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa cheo cha meja katika kambi ya Pangawe, Morogoro alifariki dunia na akiwa kidato cha pili, mama yake Hadija Ismail alifariki dunia pia.  Hivyo alilelewa na baba yake mdogo Paul Bulaya (Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye alimsomesha hadi alipomaliza elimu yake ya sekondari na chuo. Yawezekana hali ya kujiamini na kujisimamia, hali ya kuwapenda vijana na watoto na kupenda kuwasaidia, imejengwa na hali ya kuwapoteza wazazi wake akiwa binti mdogo? Hili ni swali la kumuuliza wakati wa kufanya naye mahojiano.
Mheshimiwa Ester Bulaya, alisoma shule ya msingi ya Kurasini Dar-es-Salaam na Sekondari ya Makongo. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na chuo cha Uandishi wa habari cha Morogoro na kujipatia Diploma  ya Uandishi wa habari. Alifanya kazi kwenye gazeti la Uhuru mwaka 2002 mpaka 2008, alipopata nafasi ya kwenda Amerika kusoma masomo ya Uongozi.
Alipoingia Bungeni, amekuwa sauti ya vijana na watoto. Tumemsikia mara nyingi akitetea haki za vijana na watoto. Pia anapigania haki ya mtoto wa kike na kuamini njia ya kumkomboa mtoto wa kike ni kumpatia elimu. Tulisikia kwenye vyombo vya habari jinsi alivyojitolea kumsomesha mtoto Penina Wayoga, hadi kidato cha sita, baada ya binti huyu kuuonyesha kufanya vizuri kidato cha nne.
Tunasikia jinsi Mheshimiwa Ester Bulaya, anavyowahamasisha vijana wa Mkoa wa Mara, kushirikiana kupitia mchezo wa mpira wa miguu. Mbinu hii, wameitumia wanasiasa wengi wenye kuona mbali. Kwa kucheza pamoja vijana wanashirikiana na kutoa tofauti miongoni mwao. Mashindano ya mpira anayoyaendesha Mheshimiwa Ester Bulaya, hayana itikadi ya kisiasa na wala hayaangalii imani ya vijana hawa. Ni michezo ya vijana, ambao kwa kucheza pamoja, kwa kushindana, wanajenga mahusiano na uelewa mpana wa kutofautiana kwa mawazo, kutofautiana kwa misimamo, lakini kushirikiana kuijenga Tanzania moja.
Kama anavyosema yeye mwenyewe: “Maendeleo hayaji kama hushirikiani na vijana katika uamuzi na utekelezaji, vijana wote bila kujali itikadi za vyama wanapaswa kuungana kukemea maovu na kupandikiza mbegu mpya ya ushindi na maendeleo ya nchi yetu,”
Tumesikia jinsi Mheshimiwa Ester, anavyotoa misaada kwa vijana na hasa katika jimbo lake la Bunda. Misaada hii imekuwa tishio kwa wale wanaotaka kugombea ubunge katika jimbo hilo. Bila kuingia kwa ndani nia na lengo lake la kutoa misaada, ni wazi kwamba umoja anaoujenga kupitia misaada yake hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inawaunganisha vijana, ni mchango mkubwa utakaobaki na kudumu hata kama yeye hatafanikiwa kugombea na kupita kama mbunge wa jimbo hilo. Kwa vile anaamini kuwekeza kwa vijana, ni mtu muhimu ambaye hata bila kuchaguliwa kuwa mbunge anaweza kuendelea kuchangia kulijenga taifa letu. Si lazima mtu awe mbunge ndo achangie maendeleo. Lakini ikitokea akafanikiwa kurudi bungeni kwa kupigania na kuchaguliwa kama mbunge wa jimbo, wananchi wa Bunda watakuwa wamempata mwakilishi mzuri.
 Kipaji cha uongozi cha Mheshimiwa Ester Bulaya kilijionyesha wakati akiwa darasa la kwanza alipoteuliwa kuwa kiongozi wa darasa hali ambayo iliendelea hadi akiwa darasa la saba katika shule ya msingi Kurasini, jijini Dar es Salaam. Pia akiwa shule ya sekondari Makongo aliteuliwa  kuwa kiranja jambo ambalo liliwafurahisha hata ndugu zake hasa baba yake mdogo ambaye ndiye alikuwa akiishi naye kwa wakati huo. Mnamo mwaka 2000 alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Morogoro, (MSJ) kuchukua Diploma ya uandishi wa habari ambako pia alikuwa Waziri wa Maendeleo ya jamii na Michezo.
Jina la Esther lilianza kuonekana kwenye vyombo vya habari mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipokuwa mwandishi katika kampuni ya Uhuru Publications Ltd inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Esther aliyeingia bungeni baada ya kushinda nafasi za uwakilishi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utekelezaji katika jumuiya hiyo anasema kazi kubwa anayofanya ni kushirikisha vijana katika kujiletea maendeleo yao.
Huyo ndiye Mwana Mama Ester Bulaya, Mheshimiwa Mbunge, mwandishi wa habari, mpambanaji na mwanaharakati.
Na,
Padri Privatus  Karugendo,
+255 754 633122.
























https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjVSV1caXKW6EdPOn47eLUoj-1ng9yUB3SeRerLVlpgYQuj_MydJbrffH_FLd_82YCFTF4j8VEpUZnbkC7ope94mBFPglk0V9sDPNdaMPwHf-8eq_hyphenhyphenNdM8niFuTxKa9SHtsHdtOpfFupdH/s1600/1597.jpg


MWANA MAMA CHRISTOWAJA GERSON MTINDA
Leo katika safu yetu ya Mwana mama tunawaletea Mheshimiwa Christowaja Mtinda, msomi ambaye ameamua kuingia kwenye siasa. Kuna kelele nyingi kwamba wasomi wanatelekeza taaluma zao na kutimkia kwenye siasa; na mara nyingi wamelaumiwa wanaume! Kumbe kuna na wanawake wasomi waliotimkia kwenye siasa. Mama huyu ambaye alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, sasa ni mbunge wa viti maalum kupitia chama cha CHADEMA.
Pia kumekuwa na tuhuma kwamba CHADEMA, wanachagua wabunge wa viti maalum kwa upendeleo na wakati mwingine bila kuangalia uwezo na elimu ya mhusika. Mama huyu ni mfano mzuri wa Mbunge wa viti maalum, ambaye ana uwezo mkubwa hata wa kupigania Jimbo lake akalipata. Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2010, alikuwa mstari wa mbele kwenye kampeni za chama chake ili kuhakikisha kinapata wabunge wengi wa kuchaguliwa na Mgombea  urais kupitia chama chake anafanikiwa kuingia Ikulu. Ingawa hilo halikuwezekana, lakini kura nyingi alizozipata Dr.Slaa kwenye uchaguzi mkuu huo na mchango wa Mheshimiwa Christowaja, ulikuwepo.
Si lengo la safu hii kugeuka uwanja wa wanasiasa! Tukifanya hivyo tutajiingiza kwenye matatizo makubwa ya kufuatwa na waheshimiwa ili tuandike habari zao. Tunaandika bila kuombwa; tunaandika kwa kumfuatilia Mwana mama kwa muda na kubaini mchango wake katika taifa letu. Na tunafanya hivyo baada ya kutafiti kwenye magazeti na mitandao ya kijamii na kuona kwamba Mwana Mama huyu hajaandikwa sana, hasa juu ya mchango wake. Na kusema kweli mama wengi wanafanya mambo mengi mazuri, lakini hawaandikwi wala kutajwa popote! Tunalenga kutoa nafasi ya wanawake wanaotoa mchango mkubwa katika jamii, lakini hawajulikani na habari zao haziandikwi, wajulikane na kusikika. Ni imani yangu kwamba kwa nafasi ya Ubunge, Christowaja, anaandikwa sana, maana ni miongoni mwa wabunge wanawake wanaochangia hoja Bungeni. Hata hivyo mwana mama huyu hakuanzia Bungeni na wala hakuwa kwenye siasa muda mrefu.  Kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwanafunzi wa digrii ya uzamivu chuo kikuu cha Sussex Uingereza. Hivyo mama huyu ni msomi. Yangejulikana haya, uzushi kwamba Chadema, wanachaguana tu bila vigezo yasingesikika.
Sina lengo langu kuandika maisha binafsi ya Mheshimiwa Christowaja, ninamlenga mwana mama Mwalimu, ambaye amechangia kufundisha watoto wetu, watoto wa taifa hili la Tanzania. Ninaandika juu ya Christowaja, mama mwenye bidii na kiu ya elimu. Mama huyu amepanda hatua kwa hatua. Alianza na diploma, akapanda hadi kupata digrii ya kwanza, digrii ya uzamili hadi kuelekea uzamifu. Ni mfano mzuri kwa wanawake wengine ambao kwa namna moja ama nyingine wamepumbazwa kiasi cha kuambiwa “ Mwanamke anaweza akiwezeshwa”; wakati ukweli wenyewe ni kwamba Mwanamke anaweza siku zote.
Sababu nyingine kubwa ya kuamua kuandika juu ya Mheshimiwa Christowaja, ni msimamo wake wa kuunga mkono hoja zote za kizalendo bila kutanguliza chama chake. Pamoja na mapenzi makubwa anayoyaonyesha kwa chama chake cha Chadema, lakini mama huyu amekuwa miongoni mwa wabunge wachache sana wanaoangalia matatizo ya taifa letu bila ushabiki wa vyama vya siasa. Pamoja na ukali wa kawaida wa vyama vya upinzani, maana wao wanafanya kazi ya kuisahihisha na kuisimamia serikali, mama huyu amekuwa akiwasilisha hoja zake kwa busara na hekima. Ni mpole kwa kuongea, lakini mkali kwa kupenyeza hoja bila kuipindisha. Huyu ni mpambanaji kama walivyo wabunge wengine wa vyama vya upinzani, na kwa sababu anazungumza na kuchangia; hatuna budi kuhakikisha anajulikana na habari zake kuandikwa.
Mama huyu ni miongoni mwa wabunge walio upande wa wanyonge; watetezi wa watoto, anatetea elimu bora kwa watoto wetu, wanawake na watu walio pembezoni. Ni mwana mama anayelilia uongozi bora katika taifa letu, anapiga vita rushwa na ufisadi. Ni mwanaharakati ambaye anapigania rasilimali za Tanzania kuwanufaisha watanzania wote. Pia ni miongoni mwa wabunge waaminifu wa kukalia viti vyao. Bunge letu lina sifu ya kuwa na viti wazi. Wakati wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, tulimsikia Mbunge, akilalamika Bunge kujadili wizara nyeti kama ya kilimo wakati Bungeni kulikuwa na Mawaziri watano na manaibu mawaziri watano. Pia kwa kuangalia kupitia luninga mtu aliweza kuona viti vingi vikiwa vitupu. Na wakati mwingine hata vile ambavyo vina watu, wabunge wanakuwa kwenye michapo wakati Bunge likiendelea. Kinara wa zoezi hili ni Waziri Mkuu, ambaye mara nyingi anaonekana akijadiliana na watu kwenye kiti chake wakati Bunge likiendelea. Pamoja na utetezi kwamba anakuwa kazini, ukweli una baki kwamba anakuwa hafuatilii yanayojadiliwa Bungeni. Kama ni kazi, si ni bora abaki kwenye ofisi yake, kuliko kuwadanganya watu yuko Bungeni wakati anaendesha mikutano ndani ya mkutano!
Hata yeye Mheshimiwa Christowaja, atashangaa, kusoma habari hizi, maana tunaandika bila kuhojiana naye. Tunaandika yale tunayoyaona juu yake. Tunaandika ili wengine wakamtafute na kufanya naye mahojiano. Hivyo katika makala zitakazofuata, tutasikia juu ya familia yake na mengine mengi juu yake. Tunaandika ili wengine wajiulize huyu ni nani? Ni mbinu mpya ya kuwachokoza waandishi kuanza kuwafuatilia watu mbali mbali na kuwahoji na hasa wanawake ambao kwa miaka mingi wamewekwa pembeni.
Christowaja Mtinda, alizaliwa tarehe 13.5. 1968. Alisoma shule ya msingi Kititimo kati ya mwaka 1976 hadi 1982. Alijiunga na shule ya sekondari ya Msalato mnamo mwaka 1983- 1986 na kidato cha tano na sita shule ya sekondari ya Kilakala Morogoro mwaka wa 1987-1989. Alipomaliza masomo ya sekondari alijiunga na chuo cha DSA kusomea Diploma ya Material Management. Baada ya kupata Diploma hiyo, mwana mama huyu hakutulia, aliendelea kuisaka elimu na mwaka 1996 hadi 1998, alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Morogoro kusomea diploma ya Ualimu. Alipomaliza Diploma yake ya Ualimu, alifundisha shule ya Sekondari ya St Mary’s 1998- 1999 na shule ya sekondari ya Airwing ya Dar-es-Salaam, mwaka 1999-2000. Kiu yake ya elimu haikukoma na mwaka  2000 hadi 2004 alijiunga na Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam kuchukua shahada yake ya kwanza ya Ualimu. Bidii aliyokuwa nayo kwenye masomo, aliendelea na shahada ya uzamili hapo hapo chuo kikuu cha Dar-es-Salaam mwaka wa 2004-2006.
Mbali na kuwa mwalimu kwenye shule za sekondari na Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mkwawa, mama huyu alifanya pia kazi kwenye Baraza la mitihani Tanzania. Ni mama mwenye uzoefu katika Nyanja mbali mbali. Hata na michango yake kwenye Bunge, inaonyesha kwamba si mtu aliyeingia kwenye siasa kutafuta kazi, bali ni mtu alikuwa na kazi yake; msomi, mtaalamu wa elimu na mambo mengine mbali mbali kama kufanya kazi kwenye duka la dawa la Twiga.
Huyo ndiye Mheshimiwa Christowaja Gerson Mtinda, msomi aliyetimkia kwenye siasa!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

MWANA MAMA, MA CLEMENTINA RUTABANZIBWA.

Leo katika safu yetu ya Mwana Mama, nawaletea Marehemu mama yetu Mpendwa Ma Clementina Rutabanzibwa na kuwatangazia wasomaji wangu maslahi binafsi kwamba huyu ni Mama yangu Mkubwa. Si kwa upendeleo bali mama huyu ni miongoni mwa mama wengi wanaolitumikia taifa letu, kwa uadilifu, uzalendo na uaminifu mkubwa lakini hawasikiki! Hatujajenga utamaduni wa kuandika historia ya watu wanaotoa mchango mkubwa wa maendeleo katika taifa letu na hasa wanawake. Makala hizi za Mwana Mama zinalenga kuujenga utamaduni huu. Hivyo hata kama Mama huyu asingekuwa jamaa yangu, ningeshika kalamu na kuandika juu yake.
 Ua letu limepukutika! Mama yetu Mkubwa Omugonzibwa Ma Clementina Rutabanzibwa, aliaga dunia tarehe 23.3.2013 na tulimzika kwa heshima zote za kidini, kiserikali, kiutamaduni, kijamii na mshikamano siku Jumamosi tarehe 30.3.2013 kijiji cha Ibura Bukoba. Ni machozi  ya furaha kwamba mama yetu amepumzika akiwa na umri wa miaka 85, baada ya kuugua kwa kipindi cha miaka 7, lakini pia ni machozi ya uchungu maana hatuwezi kuzungumza naye, hatuwezi kucheka naye na hatuwezi kucheza naye tena hasa zile ngoma za Waganda, ambazo alipokuwa akifurahi alizicheza kwa ustadi mkubwa. Ni mama ambaye hakuwa na makubwa na aliwapenda watu wote bila kutegemea chochote kutoka kwao, alikuwa mvumilivu na mcha Mungu! Mama yetu ni ua ambalo tulipenda liendelee kuchanua na kuzipamba familia zetu na jamii nzima. Lakini sasa ua letu la upendo, amani na mshikamano, limepukutika! Ni wajibu wetu sisi tuliobaki nyuma kuchanua na kupendeza! Huo ndio ujumbe wa maisha ya Marehemu Mama yetu  Ma Clementina. Upumzike kwa Amani mama yetu mpendwa.
Wakati wa ibada ya mazishi  ya Mama Clementinaya, Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, alizitaja sifa nyingi za mama yetu; kwamba mama huyu mbali ya kuwa mchamungu na kuwalea watoto wake kwa msingi wa imani na maadili bora, alikuwa mama mwenye upendo kwa watu wote na ni miongoni mwa watu ambao walikuwa wakijitolea kutoa chakula bure kwa mapadre wa Jimbo katoliki la Bukoba. Alikuwa ni mama mwenye moyo wa kusaidia watu anaowafahamu na asiowafahamu. Ushuhuda huu wa Askofu Kilaini, uliungwa mkono na watu wote waliotoa salaam za rambirambi kutoka viongozi wa serikali na vyama vya siasa. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Profesa Anna Tibaijuka, naye alitaja maslahi binafsi kwamba huyu alikuwa kama mama yake mzazi pia aliziunga mkono  sifa alizozitoa Askofu Kilaini, alimtaja Mama Clementina, kama mfano wa kuigwa, kwamba ni mmoja kati ya wanawake wachache wa  taifa letu waliotoa mchango mkubwa lakini hawasikiki.
Marehemu Ma Clementina Tunu Mundigo ( au, kwa waliokuwa karibu naye alijulikana kama Ma Keleme) alizaliwa akiwa mtoto wa kwanza wa Mzee Clemence Mundigo na Ma Shelestina Mpabuka, tarehe 15 Desemba 1927 , huko Kagondo – Karugulu, Bukoba Vijijini. Alisoma shule ya msingi Bukoba na baadaye baba yake, ambaye alipenda na kuithamini elimu, alimpeleka mama yetu shule za Bwanda na baadaye Nabingo zote za huko Uganda. Ni wakati ambapo watoto wa kike walikuwa wanaachwa nyuma kielimu na kutoa upendeleo kwa wavulana, lakini baba yake na Ma Clementina, alikuwa wa pekee, alimsomesha binti yake hadi elimu ya juu. Kwa maneno mengine, Mama yetu alikuwa msomi ambaye hakujitukuza kama ilivyo jadi ya ndugu zake akina “Nshomile”. Alipoongea kingereza, ndipo mtu angeanza kuhisi kiwango chake cha elimu, vinginevyo baada ya mme wake kustaafu na kuishi kijijini hakuwa na tofauti  na wanawake wote wa vijijini.
Mnamo tarehe 21 Aprili 1948 Ma Keleme, alifunga ndoa takatifu na Omulangira Gosbert Marcel Rutabanzibwa ( sasa naye ni hayati) katika parokia  ya Rubya, Bukoba. Katika ndoa yao ya miaka 49 waliyoishi pamoja, walibarikiwa kupata watoto tisa, wa kike watano: Sr.Clementia, Hilda, Jean, Lucy na Adeline, na walipata watoto wa kiume wanne: Patrick, John-Bosco,Anthony na Victor. John-Bosco na Victor walikwishatangulia mbele ya haki. Ma Clementina, amejaliwa kuwa na wakwe, wajukuu na kitukuu.
Mme wa  mama yetu, Omulangira Gosbert Rutabanzibwa, ni miongoni mwa wasomi wa kwanza wa taifa hili. Ukienda Uhamiaji faili la kwanza na Pasi ya kusafiria nje ni la Mwalimu Nyerere, la pili ni la Mzee Kawawa na la tatu ni la Mzee Gosbert Rutabanzibwa. Alisoma na Marehemu baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kule Makerere Uganda. Baada ya Uhuru, Omulangira Gosbert Rutabanzibwa, alilitumikia taifa letu kwa Nyanja mbali mbali. Alikuwa balozi wetu New Dehli (India), Ottawa (Canada) na Washington,DC (Marekani). Huko kote aliambatana na Mama yetu Ma Clementina. Kuna ushuhuda kwamba Mama yetu, aliwajali na kuwahudumia vizuri watanzania waliokuwa kwenye nchi hizi ambazo mme wake alikuwa balozi.
Pia kuna ushuhuda mwingine kwamba Ma Clementina, alijenga uhusiano katika nchi hizo za kigeni na kuendeleza utamaduni wa ukarimu wa Mtanzania. Kuna mwandishi wa vitabu wa Amerika, anayemtaja Ma Clementina kwenye kitabu chake kwa kushangazwa na kitendo cha mama huyu kumsindikiza kutoka kwenye nyumba ya Balozi wa Tanzania, hadi kwenye gari wakati wa kipindi kikali cha baridi. Ma Clementina, alimshangaza mzungu huyo kwa jibu lake: “ Utamaduni wetu sisi tunamsindikiza mtu akija kututembelea, kwa vile wewe una gari, ni lazima nikusindikize hadi kwenye gari lako..!”
Hizi ni baadhi ya sifa za Mama yetu, lakini kuna sifa nyingine nyingi. Mme wake alikuwa Balozi na kuiwakilisha serikali ya Tanzania, nchi za nje; sifa alizozipata Balozi Rutabanzibwa, zilikuwa na msingi mkubwa – nyuma ya sifa hizo ni Ma Clementina. Mama huyu aliwajibika katika kujenga na kulea familia yake katika misingi ya Kikristo na kizalendo miaka yote ya uhai wake. Kwa wengi waliomfahamu, alikuwa mama aliyejinyima mengi maishani ili familia yake, mme wake na  watoto wafike mbali kiroho na kimaisha. Kutokana na jitihada hizo, Balozi Rutabanzibwa, anatajwa kuwa miongoni mwa watu waliolitumikia taifa letu kwa uadilifu mkubwa. Watoto wa Ma Clementina wanaofanya kazi hapa Tanzania, wanatajwa kuwa ni miongoni mwa watanzania wachache wenye kulitumikia taifa hili kwa uzalendo uliotukuka. Hivyo mama huyu alikuwa na sifa ya kuitunza familia yake vizuri kwa kuiandaa kulitumikia taifa letu la Tanzania. Kifo chake si pigo tu kwa familia, ndugu na jamaa, bali ni kwa watanzania wote.
Mama yetu ni mfano bora wa msemo wa “ Mama ni moyo wa familia na mama ni mzazi wa taifa”. Mama yetu ametoa mchango mkubwa kwa  taifa letu kwa kuilea kwa maadili bora familia yake kiasi cha kutoa watu bora wa kulitumikia taifa letu kwa uzalendo mkubwa.
Tunamlilia mama yetu, tunamkumbuka na kumwombea ili Mwenyezi Mungu ampumzishe mahali pema peponi.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www. Karugendo.net



UHAKIKI WA KITABU:  MERCHANT POLITICS AND THE MOCKERY OF MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA

1.     Rekodi za Kibibliografia.

Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni  MERCHANT POLITICS AND THE MOCKERY OF MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA, Kimeandikwa na Lawrence I.M Kilimwiko. Mchapishaji wa kitabu hiki ni  Konrad Adenauer Stiftung na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978- 9987- 716-01-2. Kitabu kina kurasa 116 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi

Kitabu hiki kilizinduliwa mwezi wa pili Jijini Dar-es-Salaam na bahati nzuri mchambuzi wa kitabu hiki alikuwa miongoni mwa watu waliopata mwaliko wa kuhudhuria sherehe za uzinduzi huo. Majadiliano yaliyofuata baada ya uzinduzi wa kitabu hiki yamechangia kwa kiasi kikubwa uchambuzi huu ninaoufanya. Hapa na pale nimezingatia maoni na michango ya washiriki mbali mbali. Pia  baadhi ya majibu ya maswali kutoka kwa mwandishi wa kitabu hiki yaliyoulizwa wakati wa uzinduzi yameingizwa kwenye uchambuzi  huu kwa namna moja ama nyingine.

Kitabu hiki kinakuja wakati wake. Tunapoandika Katiba mpya na tunaelekea uchaguzi wa 2015, ni muhimu kuanza kutafakari juu ya siasa yetu na mfumo tunaoutumia katika siasa za Tanzania.  Bwana Lawrence Kilimwiko, ametuchokoza na kutuelekeza katika mjadala huu. Ni imani yangu kwamba kitabu hiki kitaleta mchango mkubwa na hasa kama jitihada itafanyika kukitafsiri kitabu hiki kutoka lugha ya kigeni.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa kimombo, na labda ndiyo hiyo dhihaka yenyewe inayoongelewa katika kitabu hiki? Mtu ambaye analenga kusahihisha mwenendo wa siasa ndani ya nchi ambayo lugha yake kuu ni Kiswahili na kuamua kuandika kwa lugha ya kigeni, si tu kwamba inashangaza, bali ni dhihaka. Mwandishi anasisitiza kwamba tunafanya mambo kwa kushinikizwa na wafadhili, na yeye anaandika kwa lugha ya kigeni dalili ya wazi kwamba naye anashinikizwa na wafadhili kwa kuandika lugha wanayoifahamu wao? Ukombozi kamili na kufanya mambo sahihi ni pamoja na kuitumia lugha ya taifa. Mtu anayetumia lugha za wengine kujieleza na “kusambaza” ujumbe kwenye jamii, si mtu huru! Kwa Kiswahili cha kawaida, kitabu hiki kinaitwa Biashara ya Siasa na Dhihaka ya  Vyama vingi Tanzania. Hoja ya mwandishi ni kwamba badala ya Tanzania kuwa na mfumo wa siasa wa vyama vingi kutokana na uhitaji wake kama ilivyo katika nchi zilizoendelea, mfumo uliopo kwa sasa hivi ni wa kisheria zaidi. Na kwamba kutokana na kushinikizwa na wafadhili kuachana na mfumo wa chama kimoja, kulibuniwa vyama bandia huku vile vilivyoanzishwa kwa nia njema vikisongwa na vizingiti vingi katika kuviendesha. Hivyo badala ya kuwa na vyama vilivyoanzishwa kutokana na uhitaji iwake katika jamii, kumekuwepo na vyama bandia vilivyougeuza mfuo wa vyama vingi badala ya kuwa huria kuwa holela na dhihaka mbele ya  dunia yetu ya leo.

Mwandishi anakumbusha historia ya Tanzania na vyama vingi. Kwamba CCM, ilikuwa imegoma kukumbatia mfumo wa vyama vingi. Lakini baada ya shinikizo la wafadhili, ilibadilisha msimamo wake na kuelekeza nguvu zote kwa mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo hili lilifanyika shingo upande na Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali  kilibuni mbinu ambazo kutokana na historia ya nyuma, vyama vipya visingeweza kufua dafu mbele yake; Sheria ilitungwa ya kuvitaka vyama visajiliwe lakini siyo CCM ambacho kilisajiliwa pasipo kufuata masharti kwa vyama vingine. CCM pia ilijinyakulia rasilimali zote zilizokuwa zimekusanywa na watanzania wote ikiwemo vitega uchumi, majengo na hata viwanja vya michezo mikoani kote.

Kwa kuogopa wafanyabiashara wakubwa kujiunga na vyama vingine vya siasa, CCM ililegeza masharti yake ya chama cha wakulima na wafanyakazi na kufungua milango yake kwa kila mtu hata mijizi, matapeli, mawakala wa ubepari, ukabaila na hata wale wasiokuwa na maadili wala uzalendo.

Matokeo yake ikawa ni kwa chama hicho maarufu barani Afrika kutekwa nyara na genge la mijizi,  na kwa mkakati kasi ya ajabu uongozi wa CCM ukawa mikononi mwa watu wasiokuwa wajamaa, wazalendo na wala waadilifu. Siasa ya ujamaa na kujitegemea ikageuzwa kibao na kuwa siasa ya kujimegea, kubinafsisha mali za vijiji na kupora ardhi, wanyama pori na rasilmali nyingine.

Mwandishi anasisitiza hoja yake kwa kutoa mfano kwamba kuibuka kwa CHADEMA kama chama kimbilio la wanyonge ni ishara tosha ya pale CCM ya vibopa ilipojifikisha na kuifanya siasa ya vyama vingi kugeuka dhihaka tupu. Mfumo huria wa kisiasa nchini umegeuka kuwa mfumo holela.

Kitabu hiki kimeandikwa ili kuibua fikra mpya kuhusu mfumo mzuri wa kuendesha siasa za vyama vingi vinavyotokana na makundi ya wanachama wenye msimamo, itikadi na falsafa moja ya wanaokusanyika kwa hiari  yao na siyo sheria  kama ilivyo sasa.

Lawrence Musanguka Kilimwiko, ni mwandishi mkongwe ambaye amefanya kazi ya uandishi wa habari zaidi ya miaka 30 akiandika juu ya masuala ya siasa. Ameandika vitabu vingi vikiwemo: Media Power and Politics in Tanzania (2009), The Fourth Estate in Tanzania (2002), The Spokesperson: A Media User Friendly Guide (2004) na Biashara ya Dini, Siasa na Ufisadi.

Lawrence Kilimwiko, alisomea uandishi wa habari kule India, pia alisomea mahusiano ya kimataifa kwenye chuo kikuu cha Jahawaharlal India na amesoma Sayansi ya siasa na uongozi Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam.


III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha Biashara ya Siasa na Dhihaka ya  Vyama vingi Tanzania , ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Kwanza nikubali kwamba jambo hili la kuandika kitabu juu ya mwenendo wa siasa, si la kawaida hapa Tanzania. Tumekuwa tukisoma vitabu vinavyojadili mwenendo wa siasa katika mataifa mengine na hasa yale yaliyoendelea. Hivyo kazi hii si ya kawaida.

Lakini pia kuna ukweli kwamba leo hii taifa letu linapitia katika wakati mgumu kwa vile tulifanya kosa kubwa la kuifanya siasa kuwa biashara. Tatizo la biashara ni kwamba bidhaa ikikaa sokoni, ni lazima wanunuzi waje na daima mwenye  dau kubwa ndo anafanikiwa kuondoka na bidhaa sokoni.

Na tabia ya biashara ni ushindani, ni mbinu na ujanja. Ikibidi kwenye biashara ni lazima kuhakikisha anayekuzibia njia unamwondosha. Haya ndiyo tunayoyashuhudia sasa hivi katika taifa letu. Haya matukio ya kuwateka watu, kuwapiga na kuwaumiza, ni dalili kwamba kuna watu wanaoziba njia za wafanyabiashara wa siasa.

Siasa ikifanywa biashara, inapoteza maana yake. Ndani ya siasa tunapata wawakilishi wa wananchi. Kwa maana kwamba wananchi wanamchagua mmoja wao kuwawakilisha katika vyombo vya kutunga sheria na kuitawala nchi. Kwa maana nyingine ni kwamba kama ingebidi, wananchi wangelazimika kutumia njia zozote zile kumshawishi mtu wanayempenda ili akubali kuwawakilisha. La kushangaza ni kwamba katika biashara ya siasa, mwakilishi ndiye anafanya mbinu za ushawishi hata kutumia fedha ili wananchi wamchague na kumtuma kuwawakilishia. Hii ni kinyume kabisa na kwa vyovyote ni dhihaka!

Kitabu hiki kinaandikwa wakati tunatengeneza katiba mpya na tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Ni wakati ambapo Chama tawala tayari kinaona nguvu mpya ya vyama vya upinzani na nguvu mpya ya vijana ambao kwa kiasi kikubwa hawaeleweki vizuri, lakini upepo wa kutumia fedha kwa kila hatua, ni dalili tosha kwamba chama ambacho kitakuwa kimefanikiwa vizuri kufanya biashara ya siasa kinaweza kuibuka mshindi, maana fedha ni sabuni ya roho kama wasemavyo Waswahili.

Vyovyote vile, uwe upinzani au chama  tawala, bila fedha ni vigumu kuupata uongozi ndani ya vyama au ndani ya serikali. Maana yake ni nini? Kwa upande mkubwa wenye fedha ni wazee na wazee hawa ndo wanataka wabaki madarakani kwa njia zozote zile.

Mazingira mengine yanayokizunguka kitabu hiki ni  kwamba sasa hivi kila kitu kimekuwa biashara; siasa ni biashara, elimu ni biashara hata na afya ni biashara. Kwa vile siasa ni biashara kuna uwezekano mkubwa kumpata kiongozi asiyekuwa na uwezo, wa kuongoza na kufikiri, lakini ana uwezo wa fedha. Badala ya kutawaliwa na fikira, tunatawaliwa na fedha. Na kwa vile elimu imekuwa ni biashara, tumeanza kupata matokeo yanayofanana na biashara, badala ya kupata elimu bora na nzuri kwa ukombozi wa watanzania tunapata elimu mchoko na watoto wetu wanaendelea kuwa wajinga. Matokeo ya mtihani wa mwaka huu yameonyesha kabisa ninachokielezea. Na kwa vile afya imegeuzwa kuwa biashara, watu wanaweza kuingiza hadi dawa bandia au zile zilizokwisha muda wake.

Kwa kifupi ni kwamba Biashara ya siasa, imebadilisha kabisa mwelekeo wa  taifa letu. Haya ndiyo mambo yanayokizunguka kitabu hiki na kwa njia moja ama nyingine haya ndiyo yaliyomsukuma mwandishi kuandika kitabu hiki.


IV. Muhtasari wa Kitabu

Mwandishi amekigawa kitabu katika sura saba ambazo zinaongelea; sheria zinazoongoza uanzishwaji wa vyama vingi vya siasa, matumizi na ushawishi wa fedha katika siasa za Tanzania, mabadiliko yaliyoingiza siasa katika biashara, biashara ya siasa kutawala siasa za Tanzania, na pia anaangalia njia mbali mbali ambazo zinaweza kuuinua upinzani hadi kufikia kuishika dola.

Mwandishi anakwenda mbali na kuangalia biashara ya siasa kuanzia miaka ya 80, akiunganisha siasa hizi na ujio wa soko huria na kile kilichokuja kujulikana kama Azimio la Zanzibar. Siasa hizi zilizoingia Tanzania, kwenye miaka ya 80, silifutilia mbali uwezekano wa mtu maskini, hata kama ana akili nzuri kushiriki kwenye uongozi wa taifa letu la Tanzania.

Mwandishi, katika kitabu chake anakwenda zaidi kuandika na kusema kwamba, inakuwa shida kwa mwananchi wa kawaida kuchaguliwa kuongoza, maana hawezi kuwa na fedha za kununua uongozi.

Kilimwiko, anajadili hoja ya Uzawa, iliyoibuliwa na Mchungaji Chritopher Mtikila ya Uzawa na : “Walalahoi” , (Gabacholi) Wahindi, na kuonyesha kwamba mali nyingi ya Tanzania iko mikononi mwa Wahindi. Ukweli kwamba Mtikila, alisikilizwa na kuzoa washabiki wengi ilikuwa ni dalili ya wazi kabisa kwamba ufa kati ya walionacho wasiokuwanacho ulikuwa unapanuka sana.

Mwandishi anaifananisha CCM na mnyama mkubwa aina ya mjusi “Dinosaur”. Mnyama huyu alikuwa mkubwa kuliko wanyama wote hapa duniani, lakini sasa ametoweka kabisa. Na la kushangaza ni kwamba mnyama huyu alikuwa anaishi hapa Tanzania. Kwa vile CCM imejiingiza katika biashara ya siasa na kukubali kutawaliwa na kuongozwa na fedha badala ya itikadi, fikra, sera na kuijenga nchi, mwisho wake unaweza kuwa kama wa mnyama mkubwa “Dinosaur” aliyepotea kwenye uso wa dunia.

Kilimwiko anamalizia kitabu chake kwa kugusia vyama vya upinzani na hasa Chadema na CUF. Anaonyesha jinsi vyama hivi vilivyopitia vipindi vigumu, pamoja na jitihada za kuonyesha kwamba vyama hivi ni vibaya, lakini bado hadi leo hii vyama hivi vinaendelea kuishi na kusonga mbele. CUF, kilibatizwa kwamba ni chama cha Wapemba na kilikuwa kikiendeshwa na fedha za Waislamu wenye itikadi kali. Sifa hizi zililenga kukimaliza chama hiki, lakini ilishindikana. Nacho Chadema, kilibatizwa jina la kuwa ni chama cha matajiri, wakristu na wachaga. Hata hivyo chama hiki kinaendelea kupanuka na kukubalika kwenye jamii ya watanzania.

V. TATHIMINI YA KITABU.

Nianze kwa kumpongeza ndugu yetu Lawrence Kilimwiko, kwa kuandika kitabu hiki cha aina yake juu ya siasa za Tanzania. Kitabu hiki ni cha kwanza kuandikwa juu ya siasa kiasi kinaweza kumsaidia mtu yeyote yule awe mgeni au mwenyeji, kuona Tanzania tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi kama mambo yataachwa kwenda kama yanavyokwenda hivi sasa.

Pili, Kilimwiko, ametoa changamoto kwa watanzania wote na hasa waandishi wa habari kuyachambua maisha yetu ya kila siku ili yatusaidie kujipima, kujisahihisha na kusonga mbele. Kitabu ni kati ya njia zinazosaidia jamii kujiona.

Tatu, mwandishi amefanikiwa kufunua ubovu ulio katika mifumo yetu ya utawala na jinsi fedha inavyoongoza na kuweka mbali fikra na maadili bora, bila yeye kuonyesha ushabiki wa aina yoyote ile.

Nne, mwandishi amefanikiwa kuionyesha dhihaka ya vyama vya siasa katika Taifa letu la Tanzania; na ukweli kwamba kama vyama vyote vinaweza kuwa na uwanja wa ushindani ulio sawa, hakuna chama ambacho kingekuwa kinajizolea ushindi wote. Pamoja na matumizi ya fedha, bado chama cha CCM kinabebwa na dola.


VI. HITIMISHO.

Kama kawaida yangu ya uchambuzi wa vitabu, ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki ambacho kwa kiasi kikubwa kimechambua siasa za Tanzania na vyama vya siasa.

Kwa upande wa mwandishi ni kumuomba kufanya jitihadi kubwa kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya taifa. Kama nilivyosema hapo mwanzoni, ni kwamba inashangaza mtu ambaye anatoa changamoto ya siasa za Tanzania, yeye mwenyewe anaandika kwa lugha ya kigeni. Hoja yake kubwa ni kwamba kosa kubwa la taifa letu ni kufanya na kutenda kwa maelekezo ya wafadhili wa nchi za nje. Kosa hili ambalo analielezea kwa ufasaha mkubwa ndani ya kitabu chake analifanya yeye mwenyewe! Tunaweza kusema Kilimwiko, aliandika kwa lugha ya Kizungu kwa vile kazi yake ya kuandika imechangiwa fedha na shirika la nje? Kama jibu ni kweli basi naye anasukumwa na wa nje kuandika juu ya siasa za Tanzania.

Inawezekana kabisa tukatoweka kama taifa na kutokomea kusikojulikana kama alivyotokomea mnyama mkubwa aina  “Dinosaur” kama hatufanyi jitihada za kutosha kuitumia lugha yetu. Rais wa China, aliyeitembelea Tanzania juzi, alitumia lugha yake kulihutubia Taifa la Tanzania, na watafsiri wakafanya kazi yao. Haina maana kwamba Rais huyu hafahamu Kizungu, ila ni ile hali ya kujivunia lugha yake. Lakini Rais wetu Mheshimiwa Dkt Jakaya Kikwete, alitumia Kizungu kujibu hotuba ya Rais wa China. Hii inaonyesha wazi kwamba hata kama tunapinga kutawaliwa na Wazungu, ukweli ni kwamba wanaendelea kututawala na watatutawala milele yote kama hatufanyi jitihada za kujinasua kuanzia kutumia lugha zetu badala kuzishabikia lugha zao.

Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754 633122