HISTORIA FUPI YA
BABY WO!
MTOTO WETU MWOLEKA CHRISTOPHER KARUGENDO
Mtoto wetu Mwoleka Christopher Karugendo, alizaliwa tarehe 10.3.2012 majira
ya saa mbili na nusu za usiku kwenye Hospitali ya Kairuki Dar-es-Salaam. Muda
mfupi baada ya kuzaliwa ilibainika
kwamba mtoto alikuwa na tatizo la kutokuwa na uwezo wa kunyonya. Tatizo hili
liliendelea kuwa kubwa hadi akawa analishwa kwa mpira kupitia puani. Hali hii
ilipelekea Mama na mtoto kuendelea kukaa hospitali kwa Kairuki zaidi ya mwezi
mmoja.
Katika jitihada za kutaka kuyaokoa maisha ya Mtoto Mwoleka, ulifanyika
uamuzi wa kumhamishia Muhimbili. Huko nako Madaktari na manesi walijitahidi
kumsaidia mtoto ili aweze kunyonya bila ya mafanikio. Siku zilivyokuwa
zikisogea ndivyo matatizo mengine yalianza kujitokeza; shingo la mtoto
halikuweza kukaza na mwili nzima ulikuwa hauna nguvu.
Mwezi wa sita 2012, kwa msaada wa ndugu na marafiki, ulifanyika uamuzi wa
kumpeleka mtoto Mwoleka India kwa matibabu zaidi. Madaktari na manesi wa
Hospitali ya Appolo – Chinai India,
walijitahidi kufanya vipimo vya kila aina na hatimaye kugundua kwamba kulikuwa
na tone la damu kwenye ubongo wa mtoto. Walituelezea kwamba hilo ndilo tatizo
kubwa na ndicho chanzo cha mtoto kushindwa kunyonya na viungo vyake kulegea, na
kwamba tatizo hilo litakwisha lenyewe kadri mtoto atakavyoendelea kukua.
Madaktari wa India, walishindwa kutamka jina la Mwoleka, wao walimbatiza
mtoto wetu jina la Woleka. Na dada zake wakalifupisha zaidi hadi kuwa Baby Wo.
Hivyo mtoto wetu alijulikana kwa wengi kama Baby Wo.
Baada ya kutoka India, tulishuhudia jinsi Mtoto Mwoleka, alivyokuwa akipiga
hatua hadi kuacha kulishwa kwa mpira. Tulikuwa tumejipanga kumhudumia mtoto
wetu kwa nguvu zetu na upendo wetu wote.
Ni bahati mbaya kwamba, lilijitokeza tatizo jingine la kubanwa kifua, na
tatizo hili lilimsumbua sana mtoto hadi kufikia kulazwa mara kwa mara
Muhimbili. Hata hivyo, madaktari waliweza kumshughulikia vizuri. Kusema kweli
tulianza kuwa na matumaini makubwa na kuanza kujipanga kusherehekea siku yake
ya kuzaliwa tarehe 10.3.2013.
Bila kutarajia, ukajitokeza ugonjwa mwingine wa kuharisha na mtoto kulazwa
Muhimbili. Mtoto wetu aliharisha siku saba bila kukoma na huu ndio ugonjwa
ulioyachukua maisha yake tarehe 20.2.2013 majira ya jioni.
Tunawashukuru nyote mliojitahidi kwa njia moja ama nyingine kuyaokoa maisha
ya Mtoto wetu. Kwa namna ya pekee tunawashukuru madaktari na manesi wa
Hospitali ya Kairuki na Muhimbili, pia madaktari na manesi wa Hospitali ya
Appolo –Chenai India bila ya kuwasahau madaktari, manesi na wafanyakazi wa
Hospitali ya Temeke ambao kwa muda wote huo walikuwa bega kwa bega na mfanyakazi
mwenzao Dr.Rose Birusya, ambaye ndiye mama wa mtoto Mwoleka.
Tumesikitika, tumeumia na kuteswa sana kwa kifo cha mtoto wetu Baby Wo. Tunaomba Mungu amlaze mahali pema peponi.
Amina.