WANYARWANDA WANAMKUBUKA
MWALIMU.
Mwalimu Nyerere alikuwa
Baba wa taifa la Tanzania, Baba wa Afrika na Baba wa watetea haki za binadamu
duniani kote. Jambo hili inajidhihirisha wazi kila mwaka watu wanapokusanyika
kumkumbuka na kumwombea. Sala kubwa ni ile ya kumtaka Mwenyezi Mungu, kumweka
kwenye kundi la watakatifu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Hapa Tanzania, kila
mwaka tarehe 14.10.2011 ni Nyerere Day na ni siku ya mapumziko. Afrika kusini
nao siku hii ni ya kumkumbuka Mwalimu
kwa majadiliano na tafakuri juu ya mawazo yake na mawazo mengi yanayofanana na
ya Mwalimu ya Haki za binadamu na maswala ya uchumi wa dunia hii ya Utandawazi.
Kule Amerika, wapenda amani na watetezi wa haki za binadamu wanakusanyika
kusali na kuomba siku ya kukumbuka kifo cha mwalimu Nyerere. Serikali ya
Rwanda, imetangaza rasmi tarehe 14. 10. 2011 kuwa ni Nyerere Day. Wanyarwanda
wanasema kwamba kumbukumbu ya mwalimu ni Sherehe, maana Mwalimu aliacha mambo
mengi mazuri nyuma yake.
Sherehe hizi za
kumkumbuka Mwalimu nchini Rwanda zinaratibiwa na Jumuiya ya Urafiki baina ya
Wanyarwanda na Watanzania – RWATAFA (Rwanda Tanzania Friendship Association).
Kwa faida ya msomaji wa makala hii ni bora kutambua kwamba RWATAFA ina ndugu
yake Tanzania, Jumuiya ya Urafiki baina
ya Watanzania na Wanyarwanda –TARAFA (Tanzania Rwanda Friendship Association).
Kwa pande zote mbili Jumuiya hizi za urafiki zimesajiliwa na kutambuliwa
kisheria.
Mwaka huu sherehe za
kumbuka Mwalimu Nyerere zimefanyika kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia cha Kigali-KIST kwa ibada nzuri ya misa iliyoongozwa na mapadri
watatu walioishi Tanzania na baadaye ngoma, nyimbo, mashairi na hotuba za
kumbukuka Mwalimu Nyerere.
RWATAFA, chini ya mwenyekiti
wake Mzee Isidore Gahamanyi katika jitihada zake za kutaka kudumisha undugu na
urafiki na TARAFA, iliamua mwaka huu kuwaalika Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Wakuu wa
wilaya zote za Mkoa wa Kagera, Wabunge wa mkoa wa Kagera, Madiwani wa Mkoa wa Kagera, Walimu wakuu wa shule ambazo
wakimbizi wa Rwanda walisomea nchini Tanzania, na wawakilishi wa TARAFA, ili
kushiriki nao kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere. Ujumbe wa TARAFA kutoka
Dar-es-Salaam uliongozwa na Mwakilishi wa mwenyekiti na Mama Eva Chiwele
aliyemwakilisha katibu wa Tarafa. Kwa bahati mbaya wabunge wote hawakuweza
kufika Kigali kwenye sherehe hizi, kwa sababu wako kwenye vikao vya kamati za
Bunge, lakini Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Kanali mstaafu Fabian Massawe,
akiongozana na Mkuu wa wilaya ya Ngara Kanali mstaafu Salum Nyakonji, Mkuu wa
wilaya ya Missenyi/Karagwe Kanali mstaafu Issa Njiku, mkuu wa wilaya ya Muleba
Bibi Angelina Mabula, Mkuuwa Wilaya ya Biharamulo Bwana Kahindi, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Karagwe Bwana S.R.Kashunju, Mwenyekiti wa Halimashauri ya wilaya ya Ngara Bwana John
Shimimana, Kaimu Katibu Tawala wa wilaya ya Karagwe bwana Alex Bantu, Kaimu
Mkurugenzi wa wilaya ya Karagwe bwana
Ernest Kahabi, madiwani wa Ngara, Biharamulo na Karagwe, Mwalimu Mkuu wa Shule
ya Msingi ya Muyenzi, Ngara Mama Consolata Ndayagowe na wajumbe wa TARAFA, Mama
Eva Chiwele na mwakilishi wa Mwenyekiti wa TARAFA walifika Kigali kwenye
sherehe hizi za Kumbukumbu ya Kifo cha Mwalimu Nyerere.
Makala hii ina malengo
makuu matano: Kwanza ni kuwa habarisha watanzania kwamba Wanyarwanda
wanamkumbuka na kumuenzi Mwalimu kwa heshima kubwa. Mwandishi wa makala hii
ameshuhudia mwenyewe jambo hili. Wanyarwanda wanasema wana sababu nyingi za
kumkumbuka mwalimu: Wanasema, baada ya
vita ya 1959, Umoja wa Mataifa uliamua wakimbizi wa Rwanda wapelekwe Canada,
lakini mwalimu alikataa na kuwapatia hifadhi Tanzania, na kwamba wakimbizi wa
Rwanda waliokwenda Burundi, DRC na Uganda, hawakupata uraia wa nchi hizo,
lakini wale waliokimbilia Tanzania walipatiwa uraia, walisoma kwenye shule za
serikali, walitibiwa kwenye hospitali za serikali na walipata huduma zote kama
watanzania wengine, na kwamba mauaji ya kimbali yalipotokea, Mwaimu Nyerere,
alikuwa kiongozi wa kwanza duniani kukemea na kuyalaani mauaji hayo.
Lengo la pili la makala
hii ni kuwashukuru wanajumuiya ya RWATAFA, kuwakaribisha watanzania na
kuwatunza nchini Rwanda, kuanzia tarehe 14.10.2011 hadi tarehe 18.10.2011.
Ukarimu wao ulikuwa mkubwa mno, Mungu peke yake ndo anaweza kuulipa wema huo.
Tatu ni kuishukuru
Nyerere Foundation, kwa kukubali kulipa tiketi za ndege za Kwenda Kigali na
Kurudi Dar-es-Salaam za Mwakilishi wa Mwenyekiti wa TARAFA na mama Eva Chiwele,
aliyemwakilisha katibu wa TARAFA kwenye sherehe hizo. Ni jambo la kujivunia kuona
Nyerere Foundation, inazilea na kuziwezesha jumuiya zinazojitokeza kumuenzi
Mwalimu Nyerere. Ni imani yetu kwamba Nyerere Foundation, itaendelea na kazi
hii nzuri ya kuilea TARAFA, ili Jumuiya
hizi mbili TARAFA na RWATAFA ziwe daraja imara la kuunganisha Tanzania na
Rwanda.
Nnne ni kuwajulisha
watanzania kwamba Rwanda kuna utulivu na amani. Nchi hii ya jirani ni fursa
nzuri kwa watanzania kwenda na kuwekeza. Kuna watanzania ambao wameanza
kuwekeza Rwanda na wataalamu wengi wanaofundisha kwenye vyuo vya Rwanda
wanatoka Tanzania. Hata hivyo bado kuna nafasi kubwa ya kuwekeza nchini Rwanda.
Nchi hii sasa hivi inapiga hatua kubwa ya maendeleo. Mji wa Kigali ni msafi
kuzidi miji mingi hata na ya Ulaya ambao nimewahi kuitembelea. Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe, alisema ni lazima ajifunze siri ya usafi
huo ili naye afanye hivyo mkoani Kagera. Mkuu wa Wilaya ya Muleba Bi Angelina
Mabula, alituchekesha aliposema “ Usafi wa Kigali unatisha, kiasi hata miti
inaogopa kupukutisha majani”. Ukweli si kwamba miti inaogopa kupukutisha
majani, bali kuna watu wanafanya usafi kila wakati. Mkuu wa wilaya ya
Biharamulo, Bwana Kahindi, alilalamika kwamba watu wake wa Biharamulo wanahama
hama, hivyo ni vigumu kufikia hatua ya usafi wa Rwanda, lakini alisema kwa
vyovyote vile ni lazima afanye jitihadi kuuweka mji wa Biharamulo katika
hali ya usafi kama alivyoona kule
Rwanda.
Tano, ni kuishukuru
serikali ya Rwanda, Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania na Ubalozi wa Tanzania
nchini Rwanda. Mwaliko wetu ulikuwana ni wa wananchi, maana TARAFA na RWATAFA
wanalenga kujenga mahusiano ya wananchi kwa wananchi. Hata hivyo serikali ya
Rwanda ilikuwa tayari kukutana na sisi na kutuelezea maendeleo, matumaini na
changamoto nchini Rwanda. Tuliweza kukutana na Mawaziri, Maseneta, Wabunge,
wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Jambo la kufurahisha na kujifunza ni kwamba
viongozi hawa wote umri wao ni kati ya miaka 30 hadi 45. Vijana ndo wanaiongoza
nchi, wazee wamebaki kama washauri. Ubalozi wa Rwanda nchini Tanzania, ulitusaidia
ushauri wakati wa kuandaa safari yetu ni mlezi wa karibu wa TARAFA. Balozi wa
Tanzania nchi Rwanda, Dk. Marwa Mwita Matiko alishiriki na sisi sherehe za
kumbukumbu ya Mwalimu na kutukaribisha Ubalozini.
Kusema kweli Kumbukumbu
ya Mwalimu Nyerere, hapa Kigali, lilikuwa ni tukio la kujenga undugu kati ya
Tanzania na Rwanda. Na jambo la kufurahisha ni kwamba undugu huu unajengwa
katika ngazi ya wananchi kwa wananchi. Ni imani ya RWATAFA na TARAFA kwamba
undugu ukijengeka baina ya wananchi wa nchi hizi mbili, serikali zitatekeleza
zinataka zisitake.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment