WABUNGE WETU WATENGENEZE
MAJUKWAA YA MAJADILIANO MAJIMBONI KWAO.
Ukisikiliza jinsi
mjadala unavyokwenda kwenye Bunge la Bajeti linaloendelea Dodoma, utagundua
kwamba wabunge wetu hawana mawasiliano na wananchi waliowatuma bungeni. Wabunge
wanawasilisha maoni yao binafsi badala ya kuwasilisha maoni ya wananchi;
wanaunga mkono hoja zote, kana kwamba hoja hizo zimetengenezwa na malaika; kama
huo ndio ukweli, ya nini basi hoja hizo kuletwa Bungeni? Kwanini wabunge
wapoteze miezi miwili wakijadili kitu ambacho wanafahamu fika kwamba mwisho
wake ni ndiyo asilimia mia moja? Kama mchango wa maoni ya wabunge hauwezi
kusaidia kubadilisha chochote ndani ya bajeti inayowasilishwa na serikali, ina
maana gani basi bajeti hiyo kupelekwa Bungeni? Huku si kufuja fedha za
walipakodi wa Tanzania? Kama wabunge hawana mchango wowote kwa bajeti, kwa nini
kuijadili? Ni busara na ni kubana matumizi kama serikali ingeandaa Bajeti na
kutusomea na maisha yakaendelea kama kawaida kuliko kupoteza muda na fedha
nyingi tukijadili kitu ambacho kimefanyiwa maamuzi tayari! Wabunge wanaviogopa
vyama vyao vya siasa kuliko wanavyowaogopa wananchi waliowatuma Bungeni; Mbunge
anapotangazwa na Tume ya uchaguzi, anakuwa si mbunge wa chama bali ni mbunge wa
wananchi wa jimbo zima; hivyo kukiogopa chama chake wakati wa kujadili maswala
ha kitaifa ni kuwasaliti na kuyazika maendeleo ya wananchi waliomtuma Bungeni.
Jinsi Bunge letu lilivyo hivi sasa lenye wabunge wengi wa chama kimoja chenye
kujali maslahi yake na kuziba masikio kwa kilio cha wananchi walio weni, hata
mswada wa kutunga sheria ya kuruhusu madawa ya kulevya ukiwasilishwa Bungeni
utapitishwa, maana ni utamaduni wa “ndiyo” na “kuunga mkono asilimia mia moja”
bila kutafakari na kuzingatia maoni ya wananchi.
Mfano mzuri ni Mpango wa
Maendeleo wa miaka mitano uliopitishwa juzi Bungeni. Uliletwa Bungeni
ujadiliwe; lakini jinsi mjadala
ulivyokwenda ilijionyesha wazi kwamba mpango huo ulishapitishwa tayari na
yeyote aliyekuwa na maoni tofauti alionekana kama msaliti. Swali la kujiuliza
ni kama Mpango huo ulishapitishwa
tayari, kwa nini ulipelekwa Bungeni? Ili wa wabunge wetu wapate posho? Ili
tutambue kwamba CCM ndicho chama tawala? Hoja hapa si kuupinga mpango huo, na
ni imani yangu kwamba hata wabunge waliokuwa na maoni tofauti si kwamba
walilenga kuupinga mpango wenyewe. Ukweli ni kwamba hata wale waliouandaa
mpango huo si malaika; na si kweli kwamba kabla ya kuuandaa walizunguka nchi
nzima kuomba maoni ya wananchi juu ya mpango huo. Kuna wananchi wanaoishi
pembezoni na hasa wanawake; waliulizwa juu ya mpango huu? Mbona hatuoni vizuri
mikakati ya kuwanufaisha walio pembezoni ndani ya mpango wenyewe? Mheshimiwa
Mnyika, Mbunge wa Ubungo alihoji juu ya Barabara ya Morogoro ambayo hivi
karibuni itapanuliwa; mradi wa Mabasi yaendeayo kasi. Lakini ndani ya mpango wa
maendeleo wa miaka mitano haionyeshi kwamba zitatengenezwa barabara mbadala za
kuingia katikati mwa jiji wakati barabara ya Morogoro ikijengwa upya:
Msongamano wa magari utakaojitokeza wakati huo, haukutiliwa maanani na
waandaaji wa Mpango huo? Pia Mnyika alihoji juu ya huduma ya maji, wakati
mpango wa maendeleo wa miaka mitano unaongelea mpango mpya wa huduma ya maji,
bado mpango uliokamilika “ wa Wachina” bado maji hayajatoka! Hizi ni hoja za
msingi kuzipuuza ni kujitangazia hali ya hatari, kama si leo ni kesho. Maana
kama ni mpango wa maendeleo ya watanzania ni lazima watanzania wote
washirikishwe; yasiwe ni mawazo ya mtu mmoja, kwamba siku akiondoka basi na
mpango mzima unakufa; usiwe mpango wa chama kimoja kwamba siku kikiondoka
madarakani mpango mzima unakufa.
Mpango huu wa miaka
mitano kwa bahati mbaya au nzuri unakuja wakati Tanzania inasherehekea miaka
hamsini ya uhuru wake; lakini pia unakuja wakati tumeshuhudia mipango mingi ya
maendeleo na kukuza uchumi ambayo mafanikio yake yakama yanaonekana basi ni kwa
watu wanaoishi dunia nyingine na wala si hapa Tanzania. Ndio maana watu
wanakuwa na maswali mengi juu ya tumefanya nini ndani ya miaka hamsini. Kwamba
yaliyoshindikana ndani ya miaka hamsini yatawezekana ndani ya miaka mitano?
Kuuliza hivyo haina maana kwamba hatujafanya chochote ndani ya miaka hamsini;
kuishikia bango hoja hii kwamba kuna watu wanasema Serikali haijafanya chochote
ndani ya miaka hamsini ni kutaka kuipotosha hoja yenyewe:
Tanzania, imefanya mengi
ndani ya miaka hamsini: ukiachia mbali wimbo wetu wa taifa wa “Amani na
Utulivu”; kwenye michezo tunakuwa wa mwisho, tunaimba “Amani na Utulivu”,
uchumi wetu unadidimia, tunaimba “Amani na Utulivu”, kiwango cha elimu kinashuka
tunaimba “Amani na Utulivu”, kipindupindu, malaria na magonjwa ya
kusendeka yanatuteketeza hadi
tunakimbilia Loliondo tukiimba, “Amani na Utulivu”, rasilimali zetu zinachotwa
na wajanja wachache, tunaimba “Amani na Utulivu; Tulijenga Siasa ya Ujamaa na
kujitegemea; ikafa na tukaizika. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo
madarakani miaka yote hii? Tulianzisha mashirika ya umma yakafa na kuzikwa. Wa
kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulianzisha
maduka ya vijiji yakafa yote. Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani
miaka yote hii? Tulianzisha viwanda vikafa vyote na kuzikwa. Wa kuulizwa ni
nani kama si CCM iliyo madarakani miaka yote hii? Tulikuwa na sekondari nzuri
zikijulikana ndani na nje ya nchi, kama
vile Ihungo, Tabora Boys, Milambo na nyingine nyingi, ubora wa shule
hizi umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani? Chuo
Kikuukuu cha Dar-es-Salaam kilikuwa tishio Afrika nzima na duniani kote. Ubora
wa chuo hiki umekwenda wapi? Wa kuulizwa ni nani kama si CCM iliyo madarakani
miaka yote hii?
Ndani ya miaka hamsini
hatuwezi kutengeneza wembe! Hatujavumbua kitu chochote zaidi ya panya wa
kutegua mabomu! Tunanunua hata njiti za kuchokonoa meno kutoka nchi za nje.
Viongozi wetu wakiugua wanakimbilia nchi za nje na kule wanatibiwa na madaktari
wetu walioikimbia nchi. Ndani ya miaka hamsini tumezalisha madaktari wengi na namba kubwa imekimbilia
nchi za nje kutafuta maslahi zaidi. Ndani ya miaka hamsini tumenunua ndege ya
raisi wakati tunaomba msaada wa kujenga vyoo kwenye mashule yetu. Ndani ya
miaka hamsini tumenunua magari ya kifahari kwa viongozi wetu wakati tunaomba
msaada wa fedha za kuiendesha serikali yetu.
Ndani ya miaka hamsini
Tanzania bado tuna matatizo mengi. Wale maadui tuliowatangaza wakati wa Uhuru:
Ujinga, maradhi na umaskini, bado yametuzunguka. Ndio maana ninapendekeza
kwamba kuna haja wabunge wetu kutengeneza Jukwaa la majadiliano ndani ya
majimbo yao; wapate nafasi ya kuwasikiliza watu na kupokea maoni yao. Hii
itawasaidia kuondokana na utamaduni huu uliojengeka wa mbunge kuwasilisha maoni
yake binafsi na kuegemea zaidi kwenye chama chake badala ya kuegemea kwa
wananchi waliomtuma bungeni.
Wabunge wetu waige mfano
wa TGNP; huu ni mtandao a Jinsia Tanzania; ni shirika la kiraia na
kiuanaharakati, linalotetea mabadiliko ya -kijamii kwa mtazamo wa kifeministi,
ambayo yanalenga kwenye usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake, haki za
-kijamii, kufikia na kumiliki rasilimali kwa wanawake, vijana na makundi
mengine yaliyoko pembezoni. Dhana ya TGNP ni kujenga tapo la mabadiliko katika
jamii, ambalo litachangia kuwepo kwa jamii yenye mabadiliko, ambayo inatambua
na kuthamini masuala ya jinsia, demokrasi, haki za binadamu na haki za
-kijamii.
TGNP ilianzisha jukwaa
la majadiliano. Kila Jumatano jioni pale Mabibo – Dar-es-salaam kuna mijadala
inaendelea. Ni mijadala ya wazi
inayomkaribisha kila mtu. Wanajadilia maswala mbali mbali ya -kijamii na siku
hizi wanaendesha mijadala juu ya katiba mpya. Wabunge wetu wangekuwa
wanatembelea jukwaa hili ( Wabunge wengi wa Tanzania wanaishi Dar-es-Salaam)
wangeweza kupata mengi na kutambua mahitaji ya wananchi; pia wangeweza
kujifunza mbinu za kuanzisha majukwaa kama haya kwenye majimbo yao. Ni kupitia
kwenye majukwaa ya majadiliano tunaweza kuwa na uwakilishi wa kweli na wenye
tija kwa taifa letu.
Mbali na jukwaa la
majadiliano la kila Jumatano, TGNP, inaandaa pia matamasha ya jinsia. Kila
baada ya miaka miwili kuna tamasha la Jinsia pale Mabibo. Tamasha la jinsia ni
nafasi ya wazi kwa ajili ya watu binafsi, mashirika na mitandao, walio katika
mapambano yanayofanana, kubadilishana uzoefu,
taarifa, kujengana uwezo, kusherehekea mafanikio na kutathmini
changamoto zilizo mbele yao, kujenga na kuimarisha mitandao; na kupanga kwa
pamoja mikakati kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya -kijamii kwa mtazamo wa
kifeministi, kujengeana uwezo ili kuchangia katika mijadala ya wazi kuhusu
maendeleo ya jamii na binafsi.
Mwaka huu mwezi wa tisa
kuanzia tarehe 13 hadi 16, TGNP itaendesha tamasha la jinsia la kumi na mada kuu
ya tamasha hili itakuwa ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo: Ardhi, Ajira na
Maisha Endelevu. Ni Tamasha linalokuja wakati kumejitokeza wimbi kubwa la
uporaji wa ardhi. Serikali bado ina kigugumizi juu ya wimbi hili na baadhi ya
viongozi wa serikali wanashiriki wimbi hili la kupora ardhi. Hivyo ni wakati
mzuri wa kukutana na kujadiliana juu ya swala hili na mengine mengi. Haina
maana kukaa na kupanga mpango wa maendeleo wa miaka mitano wakati ardhi
inaporwa. Tunajua kwamba uchumi wetu
unategemea kiasi kikubwa sekta ya Kilimo; kama wananchi wetu hawana uhakika wa
ardhi yao; kama ardhi inaporwa na matajiri wakishirikiana na wageni; wananchi
watapata wapi ardhi ya kulima na kuzalisha? Hata hivyo ni muhimu kutambua
kwamba ardhi ndio uhai wa kila binadamu. Bila ardhi hakuna uhuru!
Ni bahati mbaya kwamba viongozi na wabunge wetu
wanalikwepa tamasha hili. Tamasha la jinsia la tisa, sikubahatika kukutana na
kiongozi yoyote kwenye tamasha hilo, hata viongozi wanaojulikana kuwa
wapambanaji na watetezi wa haki za binadamu na wapenda maendeleo ya Tanzania,
sikuwaona kwenye tamasha hili. Natumai mwaka huu viongozi wetu na wabunge
watafika kwenye tamasha hili la jinsia, maana kila mwenye akiri nzuri na kujali
uhai wa taifa letu anaona wazi kwamba sasa tunayumba, bila kuwa na majukwaa kama hili la TGNP na mengine mengi,
tunazama! Napenda kuwashauri viongozi wetu na wabunge kwamba matamasha kama hili la TGNP na mengine yanayoruhusu
mijadala ya wazi ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa letu. Ni muhimu
kuwasikiliza watu kabla ya kukaa na kuwapangia mipango ya miaka mitano. Unaweza
kufikiri wananchi wanahitaji maji, kumbe wao wanahitaji moto!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment