WABUNGE WA CCM WANAISHI
TANZANIA IPI?
Sina uhakika kama kwenye
makala hii nitaandika kitu ambacho sijawahi kuandika siku za nyuma au ambacho
wenzangu hawajakiandika; kwa vile bado tunajenga nyumba yetu na itachukua miaka
mingi kuikamilisha haijalishi kama ninarudia yale yale! Ujenzi huu unahitaji
kila aina ya mchango na kwa vile nyumba yenyewe ndio bado na msingi uliojengwa
unabomoka; na watu wenyewe hawataki kusikia; tutaendelea na wimbo ule ule hadi
masikio yao yatazibuka!
Sina tatizo tena na
wabunge wa CCM kukisifia chama chao. Hata wakishinda wanakisifia na kukesha
wakikisifia; ni chama chao; ni mkombozi wao; anayekulisha, akakutunza na
kukuweka salama huyo ndio mfalme wako. Utaimba sifa zake na kumtukuza. Na wala
hakuna jipya; wataimba, watasifia na mengine mengi, lakini ni lazima wataingia
kwenye mnyororo wa historia wa kumpanda na kushuka na wakati mwingine kupotea
kabisa. Hili tuliache maana lina wakati wake wa kulijadili au litajadiliwa na
wale watakao kuwa wanajifunza historia ya nchi hii siku zijazo.
Sina lengo la kuwalaumu
wabunge wa CCM kwa utamaduni wao wa kuunga mkono hoja asilimia miamoja huku
wakiorodhesha matatizo chungu nzima ambayo yanasababishwa na Serikali
inayoongozwa na chama chao; huu pia ni utamaduni wa chama chao ambao katika
hali ya kawaida unazua wasi wasi juu ya namna yao ya kufikiri na kuyaona mambo.
Labda wana matatizo la kuzitambua rangi, kwao nyeupe ni kijani, na nyeusi ni
njano; inawezekana kabisa kwamba macho yao hayawezi kuona rangi nyingine zaidi
ya kijani na njano.
Labda niwakumbushe
wasomaji wangu kwamba hatuandiki na kufanya uchambuzi wa jinsi mambo
yanavyokwenda katika taifa letu kwa lengo la chuki binafsi; kumchukia mtu,
kukichukia chama ama kukipigia debe chama Fulani. Inaweza kuwa tafsiri ya
msomaji, lakini si lengo! Tunalenga katika kujenga utamaduni wa kukubali
kukosolewa, utamaduni wa kuambizana ukweli hata kama ukweli wakati mwingine
unauma; tunajaribu kuona kama watanzania tunaweza kuwa na mwelekeo hata kama tunatumia
njia tano tofauti, tufike tunakotaka kwenda.
Hoja yangu ya leo
ni AMANI. Kwenye Bunge la bajeti
linaloendelea kule Dodoma, akisimama mbunge wa CCM, baada ya Litania ya
kukipongeza chama chake kwa ushindi wa kishindo, kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Jakaya
Mrisho Kikwete, Kumpongeza Mheshimiwa Spika mwanamke wa kwanza kukalia kiti
hicho, kuwashukuru wapiga kura kwa kuchagua kati ya mbivu na mbichi, kuishukuru
familia: mme, mke, watoto, wajukuu nk, wanageukia AMANI. Kwamba kuna watu
wanataka kuivunja Amani ya taifa letu. Kwamba kuna watu wanashinda wanazunguka
nchi nzima kwa lengo la kutaka kuvunja amani. Hata kama hawataji jina, lakini
kila Mtanzania anafahamu wanachotaka kusema.
Wabunge wa CCM
wanapoteza muda mwingi wakieleza jinsi watu wenye nia mbaya watakavyo vuruga
amani ya Tanzania; wakati mwingine mtu anaweza kufikiri wako kwenye bunge la
Afrika ya mashariki, wanatoa taarifa kwa Waganda, Wakenya, Wanyarwanda na
Warundi wasioishi Tanzania. Wabunge wa CCM, pia wanakemea “vurugu”
zinazojitokeza Bungeni, ambazo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na Spika na
wenyeviti wake ambao wameamua wazi wazi kukibeba na kukipendelea chama chao cha
CCM. Spika anaposhindwa kulisimamia bunge kwa kanuni zilizopo , na kwa mujibu
wa katiba yetu; kwamba Bunge si mali ya chama, bali bunge la taifa zima
anategemea nini kama si vurugu na uvunjifu wa Amani?
Swali langu ni je ni
nani anataka kuivunja AMANI ya Tanzania? Hawa wabunge wa CCM wanaishi Tanzania
ipi? Maana swala la amani si la ushabiki wa chama; swala la amani linatugusa
sote. Kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda usalama na amani katika taifa letu.
Ndio maana uongo na uzushi wa wabunge wa CCM hauvumiliki. Wanataka kutulisha
kasumba kwamba kuna mtu mwingine mbali na CCM anayetaka kuvuruga amani ya taifa
letu? Nilishaandika miaka ya nyuma kwamba kama kuna kitu kitakachovuruga amani
ya taifa letu ni Chama Cha Mapinduzi. Niwepo kulishuhudia hili nisiwepo, lakini
historia itafanya kazi yake.
Tukiziangalia nchi
zilizotuzunguka, nchi ambazo amani ilipotea na kupigana vita ya wenyewe kwa
wenyewe, damu ikamwagika na maisha ya watu kupotea, chanzo chake ni nini? Ni
kugombania madaraka, ni kugombania rasilimali, ni kugombania ardhi, ubaguzi na
ushawishi wa kibeberu. Mfano wa Rwanda, Burundi, Uganda, DRC, Somalia; na vita
nyingine mbaya iliyo mbele yetu ni kugombania maji na chakula; tunawahitaji
viongozi wenye upeo na karama ya uongozi kuepusha janga hili kubwa. Maana hili
likitokea hakuna nchi ya Afrika itakayobaki na amani.
Kama amani ya Tanzania
itapotea; na dalili zinaanza kujitokeza; haitasababishwa na maandamano
yanayoendelea ya kuzunguka nchi nzima na wala hayatasabahishwa na vyama vya
upinzani. Tutapigana na kuuana tukigombania madaraka, tukigombania rasilimali,
tukigombania ardhi, maji, chakula na kushinikizwa na ushawishi wa kibeberu.
Haya yakitokea ni nani
wa kulaumiwa? Ni nani kinara wa kugombania madaraka katika taifa letu? Ni nani
anashindwa kutunga sera nzuri za kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na
rasilimali za nchi hii? Ni nani anashindwa kutengeneza sera nzuri za kulinda
ardhi yetu? Ardhi inaporwa na kuuzwa kwa wageni! Ni nani anatengeneza mikataba
mibovu ya uwekezaji kiasi kwamba rasilimali zetu zinasombwa na kupelekwa nje
kwa bei ya kutupwa? Ni nani anazalisha umasikini mkubwa ndani ya taifa letu? Ni
nani anaongoza ajenda ya ubaguzi katika taifa letu? Bila njano na kijani wewe
si mwenzetu! Hata kama umesoma, hata kama una ujuzi wa hali ya juu; bila njano
na kijani utabaguliwa! Nani anaongoza kuwasujudu na kuwaabudu mabeberu kiasi
cha kulamba hata viatu vyao?
CCM ni chama kilicho
madarakani miaka yote hii 50 ya uhuru wa taifa letu; pia ni chama kisichotaka
kuondoka madarakani. Na ndani ya miaka hamsini kimejenga utamaduni wa
kugombania madaraka. Tumeshuhudia na bado tunaendelea kushuhudia vita ya
kugombania madaraka ndani ya chama hiki; tumeshuhudia mtandao na makovu yake;
sasa kuna kuvuana gamba na nguvu za watu wachache wenye fedha na ushawishi
mkubwa ndani ya chama cha CCM. Hoja yangu ni kwamba vita ya kugombania madaraka
ikiibuka katika taifa letu, itakuwa na sura mbili: Kuna vita ya CCM wao kwa
wao, na kuna vita ya vyama vingine kutaka kuiondoa CCM madarakani. Hili
likitokea wa kulaumiwa ni nani?
Serikali iliyo
madarakani ndiyo yenye wajibu wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha
wananchi wote. Hili halifanyiki! Rasilimali zinawanufaisha wachache na kuwaacha
wale wanaoishi pembezoni wakitaabika kwenye umasikini usiopimika. Hawa
wakiamuka na kuanza kudai usawa katika kugawana rasilimali, si patachimbika?
Hili likitokea wa kulaumiwa ni nani?
Ardhi inauzwa, ardhi
inaporwa na serikali imekaa kimya. Watu wakisimama na kuchukua silaha
kuipigania ardhi yao, ni nani wa kulaumiwa? Tuliyoyashuhudia Nyamongo, Manyara
na Loliondo; ni uchochezi wa vyama vya siasa
au ni wananchi wenyewe kugundua kwamba serikali yao inawasaliti?
Leo hii kilio cha
watanzania wote ni kupata katiba mpya. Lakini mchakato unavyoendelea ni wa
kuirekebisha na kuiwekea viraka katiba ya zamani. Na hili la katiba tutake
tusitake kama likiendeshwa kinyume na matarajio ya wengi ni lazima
patachimbika. Na hili likitokea utakuwa ni uchochezi wa vyama vya siasa au ni
makosa ya chama kinachotawala ambacho kinaziba masikio na kutufanya tuamini
kwamba nchi hii ni mali ya CCM?
Chama ambacho
hakijaingia madarakani hakiwezi kuwa chanzo cha kuvunja amani. Vyanzo vyote vya
uvunjifu wa amani vinatengenezwa na serikali; sina haja ya kutoa mifano maana
sote tunaishi Tanzania; labda wabunge wetu wa CCM wanaoishi kwenye kivuli cha
Tanzania. Ninasema wanaishi kwenye kivuli
kwa maana kwamba hawana uwezo wa kuviona vitu kwenye uhalisia wake.
Mbali na kushindwa kuyaona hayo niliyoyataja hapo juu inashangaza kuwasikia
baadhi ya wabunge wa CCM ambao sote tunajua hawakushinda uchaguzi, na wao
wanajua kwamba waliupora ushindi; bado wanaendelea kutamba kwamba walishinda
kwa kishindo na wananchi wanajua kuchagua mbivu na mbichi.
Kuna ushahidi wa kutosha
kwamba kuna baadhi ya wa bunge wa CCM ambao hawawezi kwenda kwenye majimbo yao
ya uchaguzi na kufanya mikutano ya hadhara. Na wao wenyewe wanajua fika kwamba hawakubaliki; kuna wengine walitumia
fedha kuwanunua watu ili wapitishwe bila kupingwa; lakini leo hii ukiitisha
kura ya ndiyo na hapana yatakuwa kama yale ya Nyamagana. Inashangaza wabunge
hawa wanasimama ndani ya Bunge na kujigamba kwamba walishinda kwa kishindo.
Hizi ni dalili nzuri za kuilinda amani?
Kama wabunge wetu wa CCM
wanaishi ndani ya Tanzania yetu hii, tunayoijua na kuifahamu vizuri; tunawaomba
waache tabia yao ya kuwajengea hofu watanzania ili wavichukie vyama vya siasa;
waache kusema uongo; wajifunze kusema ukweli na hasa wafanye jitihada za
kusahihisha makosa ndani ya chama chao. Wajifunze mambo mapya na kuachana na
mawazo mgando. Waone wenzao wa vyama vya upinzani wanavyotembea na wakati.
Wakati wa Waziri wa Fedha anawasilisha hotuba yake kwa mtindo wa kizamani wa
kulamba karatasi hadi mate yanakauka, mwenzake wa upinzani aliwasilisha hotuba
yake kwa mtindo wa doti komu, teknolojia mpya ambayo haikulazimishi
kubebana na makaratasi na mikoba. Vile vile
Waziri Mkuu aliwasilisha hotuba yake kwa mtindo ule ule wa kuyalamba
makaratasi, lakini mwenzake wa upinzani alitumia teknolojia mpya.
Hili la serikali kuwa
nyuma ya teknolojia wakati upinzani unakimbizana na teknolojia linaweza
kuonekana ni dogo, lakini lina ujumbe mzito. Maana yake ni kwamba Serikali yetu
imezeeka, haiwezi kutembea na wakati, haiwezi kutusaidia kupambana na dunia hii
yenye kwenda kwa kasi ya kutisha; kuzilinda rasilimali zetu ni lazima tuwe
tayari kupambana na dunia hii inayokwenda kasi; vinginevyo tutapotea na
kumezwa! Mtu anayelamba karatasi huwezi kumlinganisha na yule anayebofya tu
mambo yakajipa! Wabunge wa vyama vya upinzani wamekaa ki doti komu;
Wakisimama kuchangia, si kulaumu tu wala kusifia, wanatoa hoja nzito,
zilizofanyiwa utafiti, zenye uzalendo na zinazotoka kwa wananchi na hii ndiyo
njia ya kujenga amani ndani ya taifa letu. Je wabunge wetu wa CCM hawaoni
ukweli huu? Wanaishi nchi gani? Tanzania hii au Mwezini?
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment