VURUGU ZA MAFUTA NI UCHOCHEZI WA CHADEMA?

Msomaji wangu mmoja amenitumia ujumbe mfupi kwenye simu yangu ya kiganjani: “Makala zao hazina tija, maana unaegemea upande mmoja”. Hakufafanua zaidi ni upande gani ninaegema katika makala zangu; na kama ninaegemea upande mmoja kwa mabaya ama mazuri. Kama ni mwelekeo wa kukipendelea chama Fulani, basi angesema wazi kuliko kuniacha hewani. Msomaji wangu amenipatia mtihani mkubwa; angenifafanulia upande ninaouegemea ningejitahidi si kujitetea bali kujenga hoja ya kuonyesha kwamba kuegemea upande mmoja kama kunajitokeza ni matokeo yasiyokwepeka; si upendeleo wala ushabiki; si kumchukia mtu binafsi na wala si kukichukia chama chochote cha siasa; ni hali halisi! Ninachojua ni kwamba msomaji wangu aliponituma ujumbe huo kwenye simu yangu ya kiganjani, nilikuwa nimeandika makala juu ya Wabunge wa  CCM kuendelea kuimba wimbo wa: “ CHADEMA ni wachochezi, CHADEMA wanahatarisha amani ya taifa letu, maandamano ya CHADEMA yataleta vurugu”. Nakumbuka katika makala ile nilijaribu kuelezea vizuri ni vitu gani vinaweza kuleta vurugu katika taifa letu. Nilitaja ufisadi, rushwa, ufa mkubwa kati ya walionacho na wasiokuwanacho, watoto wa mitaani wanaoachwa waendelee kuishi mitaani na kuanzisha familia za mitaani, hawa siku watakaposimama kudai haki zao, kudai ardhi na haki nyinginezo itakuwa ni vurugu na uvunjivu wa amani usiotarajiwa na wengi, uporaji wa ardhi, siasa mbovu (Uchwara), uchu wa madaraka, ukabila, udini na mengine kama hayo.

Ni vigumu kuandika juu ya mambo haya yanayotishia amani ya nchi yetu bila kuitaja serikali iliyo madarakani. Ni vigumu kuandika juu ya mambo haya yanayotishia amani ya taifa letu bila kukigusa Chama Cha Mapinduzi. Na kwa vile mambo haya ni mabaya na hakuna namna nyingine ya kuyapamba yakapendeza, ni lazima mwandishi utaonekana kuangukia upande mmoja.

Utaandika nini kifurahishe juu ya tatizo la umeme? Kwamba kuma mgawo wa usiku na mchana? Kwamba kazi zinasimama na wenye mahoteli makubwa wanatishia kufunga biashara? Kwamba serikali imeamua kukopa mabilioni ya fedha ili kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura? Kwamba Katibu mkuu wa Nishati na Madini, aliyekuwa akichangisha fedha ili kuipitisha bajeti ya wizara yake amesafishwa na sasa ni mtu asiyekuwa na hatia? Tumesikia kwenye vyombo vya habari kwamba bei ya umeme itapanda. Na hili likitokea maana yake ni maisha ya wananchi kuendelea kuwa magumu. Bei ya umeme ikipanda; bei ya bidhaa itapanda! Bei ya unga itapanda,  bei ya kusaga itapanda na kila kitu kinachozalishwa kwa kutegemea umeme kitapanda. Bei ya bidhaa mbali mbali ikiendelea kupanda hivyo, ni lazima ugumu wa maisha uwalazimishe watu kufanya yasiyotarajiwa. Ingawa watanzania ni watulivu kiasi cha kutoguswa na ugumu wa maisha, lakini kamba ikikazwa zaidi ni lazima wabadilike. Na hili  likitokea, utakuwa ni uchochezi wa CHADEMA?

Utaandika nini kifurahishe juu ya mikataba mibovu? Kwamba  wale wote walioipitisha mikataba mibovu wanaendelea na kazi zao bila kuwajibishwa? Kwamba familia zao zinaishi kwenye neema kubwa? Atakaye andika ya kuvutia juu ya mikataba mibovu ni msaliti na ni adui wa umma. Ingekuwa ni mikataba mibovu lakini vitua vinaonekana, mtu anaweza kujaribu kusifia. Sasa ni mikataba mibovu; hakuna linaloonekana! Richamond haikufanikiwa kuwasha umeme, usafiri wa reli umekufwa kwa sababu ya mikataba mibovu, Shirika la ndege la Tanzania limekuwa kwa sababu ya mikataba mibovu; wanachimba madini na kutuachia mashimo kwa sababu ya mikataba mibovu na mengine mengi.

Utaandika nini kipendeze juu ya kuingiza bidhaa bandia katika taifa letu? Kwamba Tanzania tunaongoza kwa kuingiza bidhaa bandia kwenye soko letu? Kwamba hata baadhi ya dawa ni bandia? Kwamba tumefikia hatua ya kuagiza samaki wa mionzi kutoka Japan? Tuandike tusifu matendo ya kinyama ya kulenga kuangamiza kizazi chote?

Utaandika nini kipendeze juu ya kuuza Ardhi? Serikali yetu imeuza ardhi, kiasi kwamba siku chache zijazo tutakuwa na watu wasiokuwa na ardhi. Tumesikia Rais wetu akitangaza kusitisha zoezi la kuuza ardhi kwa wawekezaji; kwamba wawekezaji wanaotaka kununua ardhi ni lazima wawe na ubia na wananchi. Hili ni tangazo na msimamo wa kusifiwa. Lakini limekuja wakati si wake; limechelewa wakati namba kubwa ya wawekezaji wana tayari hati miliki ya miaka 99. Ukweli ni kwamba badala ya kusifia tamko la kusitisha kuuza ardhi, ni lazima tusimame na kupaaza sauti zetu kwamba kuu za ardhi ni dhambi ya mauti. Ni kulenga kuwa na taifa ambalo watu wake hawana ardhi. Bila ardhi hakuna uhuru, bila ardhi hakuna maisha. Tunajua kwamba uchumi wa Tanzania unategemea kilimo kwa kiasi kikubwa; hivyo ni muhimu wananchi wetu kuwa na uhakika wa ardhi. Sote tunajua kwamba hakuna vita mbaya kama ile ya kugombea ardhi. Tunataka tusitake ni lazima hili litokee maana dalili za mvua ni mawingu Na hili likitokea, tutasema kwamba ni uchochezi wa CHADEMA.

Utaandika nini kipendeze juu ya uchimbaji wa madini? Kwamba kule Geita kila siku ya Alhamisi ndege inaruka ikiwa imebeba madini yenye dhamani ya milioni mianane; wakati watu wa Geita wanaendelea kuishi kwenye umasikini; wana tatizo la maji safi na salama; hawana nyumba bora na salama; barabara za vumbi na watu wanakufa kwa magonjwa yanayotibika?; Kwamba wanachimba madini na kutuachia mashimo? Kwamba wanachimba madini na kutuharibia mazingira?

Utaandika nini kipendeze juu ya Tatizo la Mafuta lililokumba taifa letu zaidi ya majuma mawili sasa? Kwamba wafanyabiashara wana uwezo kuipatia serikali masaa 24? Au kwamba makampuni yanayouza mafuta yana ushirikiano mkubwa na vigogo wa serikalini? Kwamba serikali imetangaza tatizo la mafuta kupungua na kuisha kabisa wakati bado kuna tatizo la mafuta? Tumeshuhudia vurugu kubwa wakati wa tatizo la mafuta. Barabara ya Mandela wananchi waliifunga na vijana walitishia kukichoma moto kituo cha Oil Com cha Barabara ya Mandela, ili kushinikiza kituo hicho kufungua na kuanza kuuza mafuta:

Je vurugu hizi ambazo zilionekana wazi ni hatari kwa usalama wa taifa letu ni uchochezi wa CHADEMA? Je ni maandamano ya CHADEMA ndio yalipelekea wauza mafuta kuvutana na serikali na kusababisha vurugu kubwa na mateso makubwa kwa wananchi? Wale wanaofikiri tunakibeba chama cha CHADEMA, wanasema nini juu ya vurugu hizi za mafuta?

Sote tunafahamu kwamba hakuna upungufu wa mafuta zaidi ya wafanyabiashara ya mafuta kuyaficha ili wasiyauze kwa bei ya hasara iliyotangazwa na Serikali. Hapana shaka kwamba na serikali inafahamu swala hili, lakini kwa vile serikali ina uhusiano wa karibu na wafanya biashara hawa, hakuna litakalofanyika zaidi ya wananchi kuendelea kuteseka. Katika hali kama hii, ni mtu gani kama si msaliti wa watu wake mwenyewe, asimame na kuisifia serikali kwa kazi nzuri? Unaweza kusifia kwa kutafuta sifa; kwa kutafuta mkono kwenda kinywani, lakini ukweli wenyewe ni kwamba hukumu yako inakuwa mbele yako; kama hutahukumiwa leo historia itakuhukumu.
Hivyo mtihani mkubwa mbele yetu ni je; usimame na kusema kwamba Mbuzi ni kuku, au nyeusi ni nyeusi badala ya kusema nyeusi ni nyeupe? Je tugeuze uongo kuwa ukweli ili tuonekane hatuegemei upande mmoja? Tusingependa kusema jambo hata mmoja ambalo ni hasi kwa serikali yetu; tunalipenda taifa letu na tungependa kuimba sifa tupu; lakini kama sifa hizi hazipo tuimbe nini? Kwamba serikali inatekeleza wajibu wake, si wimbo wa sifa bali ni wimbo wa wajibu! Kila serikali yoyote ile duniani ni lazima itoe huduma za  -kijamii kwa watu wake. Na serikali ikitimiza wajibu huo hakuna tena ulazima wa kuisifia na kuitukuza. Labda kwa kuisifia kwa kutimiza wajibu wake.

Utaandika nini kipendeze juu ya Serikali kupambana na matatizo ndani ya taifa letu? Tumeshuhudia jinsi Serikali yetu ilivyoshindwa kupambana na tatizo la Umeme. Serikali ya awamu ya nne, imekuwa ikijichanganya juu ya tatizo hili tangia ilipoingia madarakani. Mikataba ya Richmonda na Dowans ni ushahidi tosha wa kushindwa kwa serikali yetu kupambana na matatizo ya umeme. Tatizo la umeme limedumu majuma mawili bila serikali kutoa tamko. Je tatizo jingine linalokuja kwa kasi serikali yetu itakuwa na uwezo wa kupambana nalo? Njaa inakuja; tuandike nini cha kufurahisha juu ya tishio hili? Tunaweza vipi kukwepa kuegemea upande mmoja juu ya swala hili la upungufu wa chakula? Serikali yetu imejipanga vipi kupambana na  tatizo hili? Tuandike na kusifia kwamba serikali yetu ina chakula chakutosha kwa miaka mitatu ijayo?

Utaandika nini kipendeze juu ya uwajibikaji? Ni matukio mangapi yametokea katika Taifa letu , lakini hatujashuhudia mawaziri wakiachia ngazi? Mabomu kulipuka na kutoa uhai wa wananchi ni nani amewajibishwa au amewajibika yeye mwenyewe? Tatizo la umeme na sasa tatizo la mafuta ni mtu gani amewajibika au kuwajibishwa? Tuandike na kusifia nini katika eneo hili?

Serikali ikishindwa kutimiza wajibu wake ni lazima ishinikizwe kufanya hivyo. Hatuwezi kuiimbia nyimbo za sifa serikali inayoshindwa kutimiza wajibu wake. Baadhi yetu tunaojitokeza kuandika na kutoa maoni tunakuwa tunaishinikiza serikali kutimiza wajibu wake; n awala kwa hili hakuna mapenzi ya chama au kukichukia chama ni lengo zima la kujenga utaifa na mapenzi kwa taifa letu. Si kwamba tunapenda kuegemea upande mmoja; tunalazimishwa na hali ilivyo ili kutembea njia ya kuonya na kutoa ushauri.

Katika makala niliyoandika msomaji wangu akanihukumu kuegemea upande mmoja nilikuwa nikijenga hoja kwamba kama ikitokea amani ikavunjika katika taifa letu basi chanzo kitakuwa ni chama kilichoko madarakani. Wapinzani hawana nafasi yoyote ya kuvuruga amani ya nchi hii, labda ikitokea nao wakaingia madarakani siku moja. Kwa mazingira ya sasa, wapinzani hawana nafasi. Nguvu za wapinzani zinatokana na udhaifu wa chama kilicho madarakani.

Pamoja na ukweli kwamba Wabunge wa CCM wanajitahidi kutulisha kasumba ili tuamini kwamba CHADEMA ni chama cha vurugu ukweli utabaki pale pale kwamba amani ya taifa letu iko mikononi mwa chama Tawala; kulingana na Katiba tuliyonayo sasa hivi chama hiki hakiwezi kukwepa lawama kwa lolote linalotokea kwenye taifa letu.

Na,
Padri Privatus Karugendo

0 comments:

Post a Comment