“VURUGU” BUNGENI NI KOSA
LENYE HERI?
Kwenye miaka ya
themanini nchini Ujerumani, niliishi na jumuiya ya watu waliokuwa na theolojia ya kushangilia makosa. Mwanzoni
theolojia hii ilinichanganya na kunipunguzia kiwango fulani cha imani yangu.
Baada ya kuishi miaka mitatu ndani ya jumuiya hii na kuielewa theolojia yao,
niliipenda na kuikumbatia na imenijenga kiimani hadi leo hii. Nilikuwa
nimelelewa kwenye utamaduni na theolojia ya kulaumu makosa na kunyosheana
vidole. Mtu akikosea, analaumiwa,
anazomewa ananyoshewa kidole, anaadhibiwa na wakati mwingine anatengwa na
jumuiya husika. Hawa ndugu zangu Wajerumani, mtu akikosea; anashangiliwa na
kupongezwa kwa kuisaidia jumuiya kugundua kasoro zake. Waliamini kwamba mtu
mmoja kwenye jumuiya hawezi kufanya makosa bila kusababishwa na mazingira
yanayomzunguka. Maana yake ni kwamba kosa la mtu mmoja linaweza kuwa lina
mnyororo wa matukio yanayowagusa watu wengi ndani ya Jumuiya.
Wajerumani hawa, au
niseme wanajumuiya hawa, maana ni jumuiya ambayo pamoja na kuwa nchini
Ujerumani ilikuwa na watu wa mataifa mbali mbali, waliamini kwamba kila tukio
lilikuwa na fundisho. Liwe tukio baya au zuri kwao ni fundisho. Walijitahidi
kutafakari kila tukio na makosa ya wanajumuiya kwao yalikuwa ni makosa yenye
heri. Waliamini kwamba uhai wa jumuiya yao ulikuwa unasimama juu ya matukio,
yawe ya watu binafsi, ya jumuia nzima, ya taifa au ya dunia nzima. Na kwao kila
tukio; baya au zuri ni sherehe!
Mtu akikosa uaminifu
kwenye ndoa yake, badala ya kumhukumu
na kumlaani, wanampongeza kwa kuwasaidia kuonyesha mapungu yaliyo kwenye
Jumuiya yao. Hawakai wakatulia mpaka watafute chanzo cha mtu huyo kuisaliti
ndoa yake. Hatimaye, wanagundua kwamba wote wanashiriki kosa hilo; hivyo kwa
pamoja wanatafuta njia za kuisaidia ndoa hiyo. Wakifanikiwa; wanasherehekea na
kufanya ibada ya kumtukuza Muumba wao. Mfumo huu wa kuyashangilia makosa na
kuyatumia kujisahihisha, kuchukuliana, kuvumiliana, kukamilishana na kupiga
hatua kwa pamoja ndani ya jumuiya ya watu wenye mapungu yanayokamilishana
kujenga kitu imara zaidi ulitumika kwa makosa yote yaliyokuwa yakijitokeza
kwenye jumuiya yao; kutowajibika, udanganyifu, ubinafsi, uchoyo, ubaguzi,
upendeleo nk.
Si lengo langu kuelezea
kwa kirefu juu ya theolojia hii ya kuchukuliana, kusameheana, kuvumiliana na
kukamilishana, bali ni kutaka kuona kama sisi watanzania tunaweza kujifunza
kitu kutokana na theolojia hii ya Kosa lenye heri? Je tunaweza kuyatumia makosa
yanayojitokeza kwenye taifa letu, kugundua kasoro tulizonazo kama taifa? Je
makosa haya hayatokani na mazingira ambayo kila Mtanzania anayachangia?
Ingawa binafsi siamini
kama Bunge letu lina “Vurugu”, au hata kama vurugu hizi zipo ni makosa,
ninalazimika kulijadili hili maana watu wanataka kulipotosha. Wasomi,
wanaharakati na viongozi wastaafu kama vile Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Warioba,
wamesikika wakilalamika kwamba Bunge letu la sasa lina vurugu na wanataka hatua
za haraka zichukuliwe kurudisha heshima za
Bunge letu. Vurugu hizi ni ile hali iliyojitokeza ya Wabunge wa Upinzani
kuhoji mambo mbali mbali na Spika kuonyesha wazi upendeleo wa chama chake na
kupelekea malumbano na mivutano hadi baadhi ya wabunge wa upinzani kufukuzwa
kwenye vikao vya Bunge.
Tumesikia wengine
wakilalamika kwamba walifukuzwa bungeni kwa kosa la kuwasha taa za vipaza sauti
bila kuruhusiwa na kubishana na kiti. Wabunge kusinzia Bungeni, viti vya Bunge
kuwa wazi na hoja nyingi kupitishwa kwa “Ndiyo” mamoja na kasoro nyingi
zinazojitokeza kwenye hoja hizo, si makosa na wala hakuna mtu anapiga kelele
juu ya kasoro hizi.
Sina uhakika Kanuni za
Bunge zinasema nini juu ya idadi ya wabunge inayohitajika ili kikao kiendelee.
Tunashuhudia viti vingi bungeni vikiwa wazi; au Mbunge akisha orodhesha jina
lake asubuhi, hata asipoendelea na vikao vyote, akaingia mitaani kula nyama
choma, kufanya shughuli nyingine za kutumwa na Spika au kujituma yeye mwenyewe
anahesabika yuko Bungeni? Posho inaingia mfukoni na wananchi wanajisikia
kuwakilishwa? Maamuzi muhimu yanapopitishwa bila Mbunge huyo kuwepo au kura
ndiyo na siyo zinapopigwa na kupitisha
maamuzi muhimu, wananchi wa jimbo lake wanakuwa wamewakilishwa kiasi gani? Kama kuna “Vurugu” ndani ya Bunge
letu, ni wabunge kutohudhuria vikao vya Bunge. Kama kuna “Vurugu” ndani ya
Bunge letu ni wabunge kupitisha hoja kwa ushabiki wa vyama vyao vya siasa bila
kuzingatia maslahi ya taifa zima la
Tanzania. Na hayo ndiyo ya kulalamikiwa!
Lakini kwa vile msemo
wetu wa Kiswahili unasema kwamba wengi wape, basi tulijadili hili la Wabunge wa
upinzani kubishana na Kiti, na Kiti kuonyesha upendeleo wa wazi wazi kwa chama
kinachotawala kama Kosa lenye heri.
Sote tuna
vibanzi. Kila mtu kwa nafasi yake. Tusiwanyoshee wabunge kidole wala kuwalaumu.
Tunapenda sana kulaumu. Ni watanzania wangapi wangefanya kinyume kama wangepata
nafasi ya kutuwakilisha Bungeni? Ni wangapi wangeongea bila woga wa kupoteza
viti vyao? Bila woga wa kupokonywa nafasi zao za kugombea kupitia vyama vyao
vya siasa? Ni watanzania wangapi wanayatanguliza maslahi ya taifa mbele? Kama
ni kila mtu kujihoji, kama ni kila Mtanzania kujipima, kasoro ni nyingi. Kasoro
ni nyingi na makosa ni mengi. Labda
tungeliangalia kosa la wabunge kwa namna tofauti. Mtizamo ambao ni
tofauti kabisa na kulaumiana na kunyosheana kidole. Kuna kitu kinaitwa kosa lenye
heri. Hili ni kosa ambalo kutokana nalo watu wanajifunza, watu wanajisahihisha
na kupiga hatua kubwa katika shughuli zao kinyume na kabla ya kosa kutendeka.
Ukweli ni kwamba, kosa linapotendeka, ni kwamba kunakuwa na kasoro fulani
katika jamii husika. Hivyo kosa hilo linasaidia kufichua mengi. Yaliyofichika
yakifichuliwa, na kama hayo yaliyofichika ni mabaya, basi hekima inaongoza na
njia pya zinatafutwa, na jamii inasonga mbele kwa kujiamini zaidi. Ndio hapo,
kosa linageuka kuwa lenye heri. Kwa maana kwamba bila kosa hilo, labda hatua
nzuri zaidi isingefikiwa.
Hii haina maana kwamba
walichokifanya wabunge ni kizuri au haina maana kwamba mimi ninawatetea. Kama
ni kuwatetea mimi ningekuwa mtu wa mwisho! Maana yake ni kwamba wametufumbua
macho. Wametusaidia kuziona kasoro zilizokuwa zimefichika. Watu walihisi tu,
lakini sasa wameona kwa uwazi zaidi kwamba Spika wa Bunge kutoka kwenye chama
tawala au chama cha siasa si vizuri.
Hili la wabunge ni
tatizo kama yalivyo matatizo mengine makubwa katika jamii yetu. Mfano wale
wanaowapora maiti wakati wa ajali katika barabara zetu, wengine wanaiba nyaya
za umeme na transfoma, wengine wanahujumu TTCL, wengine wanachimbua mabomba ya
maji na kuharibu mtandao wa maji, wengine wanaiba alama za barabarani kwa
kutumia vyuma kutengeneza nondo za madirisha na majiko ya mkaa, wengine
wanakata misitu kiasi tabia nchi inabadilika, wengine wanapora raslimali bila
kuangalia mahitaji ya kizazi kijacho, wengine ni majambazi wanaiba na wakati
mwingine kutoa roho za watu. Ni matatizo mengi!
Sote tuna vibanzi!
Unyonge wa wabunge hauna tofauti na
unyonge wa watanzania walio wengi. La msingi ni je, tunajifunza nini kutokana
na unyonge wetu? Ukiona mtu anakata tawi la mti alilolikalia, ujue mtu huyo ana
matatizo makubwa na anahitaji msaada. Ukiona mtu anabomoa nyumba yake ya
kuishi, anatoa milango anauza, anatoa madirisha anauza, ujue mtu huyo ana
matatizo makubwa na anahitaji msaada.
Kama kweli sote tuna
vibanzi, ni lazima tujenge jamii inayojifunza na kupiga hatua kutokana na
matukio mbali mbali. Na kawaida jamii iliyo hai ni ile inayokua na kuendelea
kusonga mbele kutokana na matukio mbali mbali. Ni ukomavu wa tukio baada ya
tukio. Ni lazima tujenge jamii inayotafakari na si jamii ya kulalamika kila
wakati.
Je, ni kweli wabunge
wetu wanafahamu kazi yao? Na je, wananchi wanafahamu kazi za mbunge? Je,
wanawahitaji wabunge? Kwamba tuwe na wabunge, ulikuwa ni uamuzi wa wananchi?
Kama kuna waliowafanyia uamuzi kwa vile ndio kwanza tulikuwa tunajitawala, sasa
inawezekana wananchi wakapata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya Bunge? Au juu ya
kuwa na wabunge na wabunge wa aina gani? Wa kujitegemea au wakutoka kwenye
vyama? Mbunge ni wa kupika pilau na kugawa kanga au ni mwakilishi wa wananchi
katika Bunge? Dhana nzima ya uwakilishi inaeleweka vizuri? Je, watanzania
walipewa nafasi ya kuamua ni jinsi gani wangependa kuwakilishwa? Mifumo yote
tuliyonayo imejadiliwa na nani? Maana kama watu wangepewa nafasi ya kutoa maoni
juu ya mifumo mbali mbali, isingewezekana wakakubali kupokea pombe, kanga na pesa
kutoka kwa mbunge. Wao ndio wana shida, wanataka kumtuma mwakilishi Bungeni,
badala yao kupokea kanga, sukari na pesa kutoka kwa Mbunge, wao wangekuwa
wanatoa sukari, kanga na pesa kwa mbunge, ili akubali kuwawakilisha.
Hivyo hili la wabunge ni
lazima kuliangalia kwa upana wake. Si jambo la kufanyia mzaa na si jambo la
kupuuzwa. Bunge ndicho chombo cha kutunga sheria. Bunge, Serikali na Mahakama,
nchi inasimama. Kama Bunge halina
uwezo wa kuyaangalia matatizo ya nchi hii na kuyatafutia ufumbuzi , basi
kuna tatizo kubwa katika jamii yetu, kuna tatizo kubwa ambalo kama tukibweteka,
litatutafuna sisi na vizazi vijavyo.
Kosa lenye heri limeweka
mbele yetu ukweli kwamba hapa Tanzania, chama ni kikubwa kuliko Bunge, chama ni
kikubwa kuliko serikali. Tumejifunza kwamba wabunge wa chama tawala
wanatanguliza chama chao kabla ya kuangalia na kuwakilisha matatizo na hoja za
wananchi waliowapigia kura. Je, hii ndio misingi ya demokrasia na utawala bora?
Ni lazima kuendelea na mfumo huu ambao unakitukuza chama kuliko hata Katiba ya
nchi? Tujifunze na kuchukua hatua.
Tukianza mchakato wa
kutengeneza katiba mpya ni lazima Kosa lenye heri litatuongoza: Tutahakikisha
Katiba yetu inatamka wazi wazi bila utata wowote nafasi ya Bunge, nafasi ya
vyama vya siasa na nafasi ya serikali. Tutahakikisha Katiba inatamka wazi bila
utatata wowote juu ya nani awe Spika wa Bunge letu; Kwamba asitoke kwenye vyama
vya siasa: awe Mtanzania msomi, mwadilifu, mzalendo, mwenye hekima, mwenye
msimamo, anayeongozwa na kanuni za
Bunge, sheria na kuiheshimu Katiba ya nchi.
Ndio maana hoja
ninayoijenga leo hii ni kwamba yale tunayoyaona kama “Vurugu” Bungeni, tuyachukulie kama “Kosa” lenye heri.
Yatusaidie kugundua kasoro tulizonazo kwenye taifa letu, kujisahihishe,
tuchukuliane, tuvumiliane na kukamilishana. Tanzania ni yetu sote!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment