UPORAJI WA ARDHI NA USALAMA WA CHAKULA
Kofi Annan, amelalamika
kwamba mwaka 2010 peke yake, ardhi yenye ukubwa sawa na Ufaransa limeuza katika
bara la Afrika. Na huu ni uuzaji uliofanyika ndani ya mwaka mmoja. Hali ilivyo
ni kwamba uuzaji huu utaendelea. Ni wazi Kofi Annan, anatumia lugha ya
kistaarabu kusema kwamba Ardhi imeuzwa, lakini maana yake ni kwamba ardhi hii
inaporwa na viongozi wa Afrika na kuuzwa kwa wawekezaji wa nje ambao wanapewa hati
mili ya miaka 99 au wananunua moja kwa moja.
Wakati ardhi ya Afrika
unauuzwa na kuporwa tunaambiwa kwamba idadi kubwa ya binadamu wanaokabiliwa na
uhaba wa chakula wanaishi katika nchi ambazo bado ni maskini .Kwa mujibu wa
taarifa zilizotolewa na Shirika la Chakula na Kilio la Umoja wa Mataifa –FAO,
dunia hii na watu wapatao milioni 925 wenye njaa; kati yao asilimia 98 wanaishi
katika nchi zinazoendelea na wengi wa hao ni familia za wakulima maskini
wanaomiliki ardhi chakavu au maeneo ambayo huathiriwa na mafuriko au ukame wa
mara kwa mara. Aidha, takwimu zinaonyesha kwamba mtu mmoja kati ya watano
hamiliki ardhi anayoitumia.
Theluthi mbili la
wahenga wa njaa huishi sehemu za vijijini, hasa barani Asia na Afrika. Idadi
kubwa ya watu hawa hutegemea kilimo, hawana vyanzo vingine vya kujipatia riziki
na ustawi wao. Kwa sababu hii maisha yao ni tete, hawana uhakika. Wengi wao
wanahamia mjini kwa lengo la kusaka ajira, hivyo miji inafurika watu maskini na
makazi yaliyojengwa kiholela.
Kwa maana nyingine ni kwamba
umiliki wa ardhi ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula. Na si ardhi
tu, bali ardhi nzuri na yenye rutuba. Tumesikia kwamba asilimia kubwa ya watu
maskini wanamiliki ardhi chakavu. Ardhi yenye rutuba wanauziwa wawekezaji ambao
wanaitumia kufuatana na mahitaji yao.
Chalinze, Bagamoyo, Ruvu
Basin, Rukwa na Zanzibar, Waarabu watakuja kulima mpunga kwa kushirikiana na
JKT. Na hapa “Kushirikiana” ni lugha ya kistaarabu, katika hali halisi ni
uporaji ule ule, maana mikataba kama hii inakuwa ni siri kama ilivyo mikataba
ya madini na uwekezaji mwingine. Wakulima wetu ambao wengi wao hawana hati
miliki ya ardhi yao, watatolewa kwenye mashamba ili kuupisha mradi mpya wa
kilimo cha Waarabu. Ni uporaji ule ule wa ardhi unaoendelea katika taifa letu.
Tumesikia yanayotokea
kule Manyara, wananchi wakipambana na wawekezaji kugombania ardhi, tunayasikia
pia ya Kilombero na kule Kagera, Misenyi, wakubwa walitaka kuwafukuza wananchi
kwenye ardhi yao ili wao watengeneza maeneo ya ufugaji. Uporaji wa ardhi unaendelea
sehemu zote; vijijini na mijini. Bila kufuata sheria na kuwa na viongozi walio
makini na wazalendo, kuna hatari ardhi kumilikiwa na watu wa chache au kujikuta
tunatumbukia ndani ya ukoloni wa kujitafutia wenyewe.
Juzi, ITV, walionyesha
kipindi maalumu cha sakata la Nyamongo. Hadithi ni ile ile, ardhi imeporwa na
wawekezaji wa mgodi wa dhahabu. Wananchi wanabaki kuwa watumwa ndani ya nchi
yao. Hawana ardhi ya kulima chakula na hawana ardhi ya kuchimba madini. Watu
hawa wameishi miaka yote wakichimba madini na kuuza ili kupata kipato cha
kuendesha maisha yao. Sasa “Uwekezaji” huu unaofanywa katika mfumo wa uporaji,
umewalazimisha wananchi wa Nyamogo, kuishi katika hali ya umasikini na utumwa.
Tumeshuhudia jinsi Jeshi la Polisi, lilivyo simama kidete kuwalinda wawekezaji
wa Nyamongo na kuwaua wananchi wa Tanzania.
Hoja ninayojaribu
kuijenga kwenye makala hii ni kwamba tunaendelea kuuza ardhi wakati
tukishuhudia tishio kubwa la uhaba wa chakula. Wanaoinunua ardhi yetu wanaweza
kuamua kuifanyia chochote wanachotaka; wanaweza kulima mazao ya kuzalisha
mafuta badala ya mazao ya chakula; wanaweza kuamua kuitumia ardhi hiyo kufugia
wanyama na kuwafukuza wananchi wote wanaoishi maeneo hayo.
Mwaka 2008, tulishuhudia
uhaba wa chakula ulioikumba dunia yote. Na uhaba huu wa chakula utaendelea,
maana kuna mabadiliko ya tabia nchi, lakini pia na uhaba wa ardhi utachangia
kiasi kikubwa tatizo hili. Ndio maana inashangaza kuona pamoja na tishio lililo
mbele yetu bado tunakubali kuiuza ardhi
yetu kwa wageni.
Tangu tupate Uhuru,
taifa letu limeshindwa kufaidika na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo. Tulikuwa
usingizini kwa muda mrefu hadi mwaka 2007/08 tulipozinduka kutokana na kimbunga
cha uhaba wa chakula duniani kote. Tumeibuka na wimbo wa Kilimo Kwanza; wimbo
ambao unatuelekeza kwenye kilimo cha mashamba makubwa – mashamba ya wawekezaji
wa nje badala ya kuwaendeleza wakulima wadogo wadogo ambao wamekuwa uti wa mgongo
wa kilimo kwa miaka yote.
Hapa Tanzania sehemu
kubwa ya chakula tunachokula huzalishwa na wakulima wadogo ambao wastani wa
mashamba yao ni kati nusu hekta na hekta tatu. Wanawake ndio wazalishaji wakuu
wa mazao ya chakula na ya kuuza. Na kuna ukweli usiopingika kwamba akina mama
ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula katika nchi zinazoendelea. Hata hivyo,
mila, desturi na mifumo ya -kijamii haiwatendei haki. Kwani wanawake ndio
wanaoathiriwa zaidi na njaa na umaskini kuliko wanaume. Mwanamke mjamzito
asiyepata chakula anachostahili, hupungukiwa damu na kudhoofika. Matokeo yake I
kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo sana na ukuaji wa mashaka.
Mahitaji ya wanawake
wakulima ni mengi, yakiwemo fursa ya kuchangia mawazo wakati wa kupanga nini
kifanyike na jinsi gani kifanyike, umiliki wa rasilimali hasa ardhi, ushiriki
wao katika kutunga sera na kufanya maamuzi yanayohusu utendaji kazi. Katika
masuala haya, mara nyingi wanawake hupewa fursa ndogo ya kuhusishwa, au
hawahusishwi kabisa. Na wimbi hili jipya la uporaji wa ardhi linafanyika bila
kuwahusisha wanawake. Kesho na kesho ukitokea uhaba wa ardhi kutokana na uporaji
huu, mwanamke ndiye wa kwanza kuteseka maana kwa kiasi kikubwa hadi leo hii ndiye msingi wa usalama wa chakula
katika ngazi ya kaya. Hakuna usalama wa chakula bila kumiliki ardhi!
Hivyo kilimo kwanza
kingelenga kuendeleza wakulima wadogo wadogo na hasa akina mama wanaohangaika
usiku kucha kuhakikisha kuna usalama wa chakula katika ngazi ya kaya. Wakulima
wakubwa hawa wanaokuja kwa mgongo wa uwekezaji hawawezi kutuhakikishia usalama
wa chakula katika ngazi ya kaya. Watakuja kuchimba madini, watakuja kulima miti
ya mbao, watakuja kulima mazao ya kuzalisha mafuta na watakuja kutengeneza
mbuga za kitalii. Usalama wa chakula katika ngazi ya kaya unabaki mikononi mwa
wakulima wadogo. Hivyo ni jukumu la serikali yetu kuhakikisha wakulima wadogo
wanaendelezwa na kulindwa na hii ni pamoja na kukomesha wimbi hili la uporaji
wa ardhi.
Na
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment