UHAKIKI WA KITABU: WANAWAKE WA TANU, Jinsia na
Utamaduni katika Kujenga Uzalendo Tanganyika: 1955-1965.
1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA
Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Wanawake wa
TANU, Jinsia na Utamaduni katika kujenga Uzalendo Tanganyika: 1955-1965 na
kimetafsiriwa na Kurahisishwa na Elieshi Lema.Mchapishaji wa kitabu hiki ni
E&D kwa niaba ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP). Kitabu hiki kimepatiwa
namba ifuatayo katika sekwenzia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 – 600 –11- 5.
Kimechapishwa mwaka 2005 kikiwa na kurasa 116. Na
anayekihakiki sasa hivi katika safu hii
ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. UTANGULIZI
Kitabu hiki ni tafsiri rahisi ya TANU WOMEN Gender
and Culture in Making of Tanganyika Nationalism, 1955- 195, kilichoandikwa na
Susan Geiger, na kuchapishwa na Heinemann, James Curry, E.A.E.P, Mkuki na
Nyota, 1997.
Susan Geiger, alikiandika kitabu hiki katika lugha
ya Kiingereza na katika mtindo wa kisomi ambao kwa kiwango fulani unawazuia
watu wa kawaida wasiweze kupata maudhui yaliyomo. Mbali na ugumu wa lugha na
mtindo wa kisomi wa kitabu hiki, ni kwamba hakipatikani na kujulikana kwa wengi
hapa Tanzania. Hivyo tafsiri rahisi ya kitabu hiki inakifunua kwa watanzania
wote. Jambo la kuomba kwa Mwenyezi Mungu, ni kuwajalia watanzania moyo wa
kupenda kusoma vitabu.
“Historia ya maisha ya wanawake inachukua
nafasi kubwa katika mpangilio wa kitabu. Tathmini ya mwandishi inakuwa kama uzi
uliounganisha maudhui ndani ya kitabu, lakini chachu ya maelezo yaliyomo
yanabaiki ni yale ya historia ya wanawake wanaharakaiti wenyewe” (Utangulizi wa kitabu,
viii).
Kitabu hiki kimegawanywa kwenye sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inayoongelea Kuvunja Ukimya, na ina sura tatu. Sura ya
kwanza inachambua Wanawake na Siasa Wakati wa Ukoloni. Sura ya pili inaangalia
Itikadi za Kikoloni na Uhalisi wa Maisha ya Mijini na Sura ya tatu inaongelea
juu ya Wanawake Waafrika Walioishi Dar-es-salaam.
Sehemu
ya pili ya kitabu hiki, inajikita juu ya Wanawake na Ujenzi wa Uzalendo. Sehemu
ina sura tano. Kwa maana nyingine inabeba sura ya nne hadi ya nane ya kitabu
hiki. Sura ya Nne inamjadili Bibi Titi Mohamed, na harakati zake za kisiasa
ndani ya Dar-es-salaam. Sura ya tano inamwangalia Bibi Titi Mohamed, na harakati
zake za kisiasa nje ya Dar-es-salaam. Sura ya sita inawaangalia wanawake wa
TANU walivyoinuka kutoka Gizani, hawa ni wanawake walioshi Dar-es-salaam na
walishirikiana na Bibi Titi Mohamed, katika harakati za kisiasa na ukombozi wa
taifa letu. Sura ya Saba inaelezea juu ya wanaharakati wanawake wa TANU wa
Kilimanjaro na Moshi Mjini na sura ya nane ni juu ya wanaharakati wanawake wa
TANU kutoka Mwanza.
Sehemu
ya tatu na ya mwisho ya kitabu hiki inajadili juu ya Uzalendo na Harakati za
Wanawake Baada ya Uhuru.Hapa kuna sura tatu. Yaani sura ya tisa hadi ya
kuminamoja za kitabu hiki. Sura ya tisa inayaangalia maisha ya Bibi Titi
Mohamed, wakati wa Uhuru na Baada ya Uhuru.Sura ya kumi inaelezea jinsi kitengo
cha Wanawake wa TANU, kilivyobadilishwa kuwa Umoja wa Wanawake na Sura ya
mwisho, inaongelea juu ya Lucy Lameck.
Katika
aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki, lakini baada ya
kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu chenyewe.
III.
MAZINGIRA YANAYOKUZUNGUKA KITABU
Kuna
ukweli usiopingika kwamba wanawake walishiriki kikamilifu katika harakati za
ukombozi wa Taifa letu. Walipambana bega kwa bega na wanaume. Na katika
mazingira mengine walikuwa mstari wa mbele kuliko wanaume:
“ Nilipokuwa Mbunge, nilipigania haki
sawa, nikijua kwamba wanawake walitoa mchango mkubwa kwa TANU.Kama haikuwa kwa
juhudi za wanawake, uhuru ungekuwa mgumu kupatikana kwa sababu wanauwe walikuwa
waoga” (Mahojiano ya Bibi Titi, Uk, 107).
Bibi
Titi, anaelezea jinsi wanawake walivyokuwa mstari wa mbele kujiunga na TANU,
ili kupigania UHURU wa taifa letu:
“
Tuliwapata wanawake 40 katika kilabu ya pombe, tukawachukua ofisi ya TANU,
Wanaume walisikiliza hotuba za Nyerere lakini waliogopa, waliogopa kweli,
lakini wanawake walijiunga. Waliunga mstari katika ofisi ya TANU
Wakinuua
kadi. Wanaume walipeleka wake zao kuwanunulia kadi. Mimi nilificha kadi mia
tatu na hamsini za watu walioogopa kuziweka ndani ya nyumba zao. Wanawake
hawakuwa na woga hata kidogo….”
(Mahojiano ya Bibi Titi Uk 37).
Baadhi
ya wanawake hawa ndoa zao zilivunjika. Walichagua siasa, walichagua harakati za
kulikomboa taifa lao, na kuzitelekeza familia zao. Walifanya biashara na
kutumia pesa na mali zao katika harakati. Zaidi ya hapo, wanawake hawa
wazalendo ndio waliojenga uelewa wa ni nini maana ya utaifa hapa Tanganyika,
Utamaduni wa wanawake na hasa vikundi vya ngoma na matumizi ya lugha ya
Kiswahili vilichochea moyo wa kizalendo na kuwaunganisha watu. Akina mama hawa
hawakuwa wasomi, lakini walikuwa wapambanaji na wenye upeo mkubwa kuelekeka uhuru
na kujitawala kwa nchi yetu. Mfano wa akina Mama hawa ni Bibi Titi Mohamed na
akina mama wengine wa Moshi, Mwanza, Kagera na Dar-es-salaam.
Pia
kuna ukweli usiopingika kwamba baada ya Uhuru, wanawake hawa, akiwemo na Bibi
Titi Mohamed, waliwekwa pembeni. Kwa makusudi au kwa bahati mbaya walitupwa nje
ya historia ya mapambano.
Ukweli
mwingine usiopingika, ni kwamba nguvu za wanawake hawa zilitambuliwa na
ziliogopwa. Tutaona jitihada zilizofanywa baada ya Uhuru, kuvunja nguvu za
kitengo cha wanawake wa TANU, na kuunda Umoja wa Wanawake.Pia,kifo cha BAWATA,
ni ushuhuda mwingine.
Pia
kuna aina Fulani ya mgongano wa Wanawake wasomi na wale waliokuwa na elimu
duni. Wasomi walikuwa wakristu, na kwa vyovyote walisimama upande wa wakoloni
wakristu waliokuwa wakitawala. Inawezekana kwa kutotaka, lakini kwa woga wa
kupoteza kazi zao. Wanawake wa elimu
duni walikuwa waislamu na hawa ndo walikuwa mstari wa mbele katika harakati.
Baada ya uhuru, kisomo kilikuwa kigezo. Inawezekana wasomi walichukua nafasi na
wale wa elimu duni wakatupwa nje, lakini hii si sababu tosha ya kufuta kabisa
juhudi za akina mama hawa katika historia ya taifa letu.
Wanahistoria,
wanasayansi wa siasa na wataalamu wengine wamepuuza kwa kiwango kikubwa mchango
wa wanawake wanaharakati wa Tanganyika katika mapambano dhidi ya wakoloni.
Hatuwasikii akina mama hawa. Baada ya Uhuru waliwekwa pembeni na kusahauliwa
kabisa!
CCM,
chama kilichotokana na TANU, hadi leo hii uongozi wake wa juu ni wa wanaume
watupu! Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Kama sikosei na mtu
anayeshikilia mfuko wa chama ni mwanaume! Marais wa awamu zote nne ambao
wanatoka CCM ni wanaume. Hatujapata Waziri Mkuu Mwanamke! Watu wengi
walitegemea kwamba Mwanamapinduzi kama Rais Jaka Kikwete, angeweza kumchagua
Mwanamke kuwa Waziri mkuu, lakini na yeye ameendeleza mtindo ule ule wa
kuwazika wanawake wa TANU!
Si
kweli kwamba wanawake wa Tanzania, hawana uwezo wa kuongoza, na si kweli kwamba
wanawake wa Tanzania, hawana kisomo. Profesa Anna Tibaijuka, anawika kwenye aga
za kimataifa. Dr.Asha Rose Migiro, ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa kuwa Naibu wake. Wanawake wenye uwezo kama ule Bibi Titi Mohamed, na
ambao wamesoma wapo na wamejaa tele! Tatizo ni nini? Wanawake wako wapi?
Inawezekana
wanawake walizikwa kwa kauli ya Bwana Mgonja? :
“ Akizungumza kwenye mkutano siku ya
pili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Bwana Mgonja, alizumgumza katika njia
iliyofifisha ari ya siasa kwa wanawake na kuimarisha mamlaka ya serikali.
Wakati Kitengo cha Wanawake kilikuwa kinahamasisha wanawake wajiunge katika
harakati za kujenga taifa, Mgoja aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto
watakuwa wamelea taifa zima. Aliwasifu wanawake Kwa juhudi zao katika kupigania
uhuru, lakini Kwa sasa walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba
visima na kupanda miti pamoja na kushiriki katika kisomo cha watu wazima…”
(Uk.110).
Je,
kukivunja kitengo cha Wanawake wa TANU, na kuunda Umoja wa Wanawake, ndo chanzo
cha kuwafunika wanaharakati hawa? ; “Tarehe
2 Novemba, mwaka 1962, Mheshimiwa Nyerere
aliagiza kwamba vyama vyote vya wanwake Tanganyika vivunjwe; yaani YWCA,
Baraza la Wanawake Tanganyika na UMCA, ili viungane kuunda Umoja wa Wanawake
Tanganyika (UWT).Umoja wa Wanawake ulikuwa tofauti na Kitengo cha wanawake cha
TANU…. Wakawakusanya wanawake pamoja na
kuwafundisha usafi, upishi, malezi ya watoto… elimu yawatu wazima na ususi…Vitu
vyote hivi havikuwepo katika Kitengo cha Wanawake cha TANU.Hatukuwa na muda wa
kufanya vitu hivi…”(Mahojiano na Bibi Titi uk 106).
Inawezekana
kwamba UWT, ndo kilikuwa kitanzi cha Wanawake wa TANU? Swali linabaki palepale!
Wako
wapi Wanawake? Wako wapi wanawake wa TANU, waliopigana kuleta uhuru wa taifa
letu. Utafiti wa Susan Geiger, ulilenga kulijibu swalihi hili. Mwana mama huyu
ambaye ni marehemu alikuwa msomi mwanaharakati aliyefundisha masomo ya Kiafrika
na yale ya Jinsia katika Chuo Kikuu cha Minnesota/Twin Cities, huko Marekani
kwa muda wa miaka mingi. Alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa mwalimu wa
kujitolea katika miaka ya 1960. Baadaye aliendelea kurudi Tanzania, katika
nyakati tofauti katika kipindi chote cha maisha yake. Susan alifariki mwaka 2001.
Kazi
yake kubwa ya utafiti ilikuwa juu ya historia ya uchifu wa Wachagga. Utafiti
huo ndio uliokuwa chimbuko la kujipatia Shahada ya Udaktari wa Falsafa. Baadaye
alianza utafiti wa wanawake wanaharakati wa Tanganyika. Wanaharakati hawa walijulikana kama Wanawake
wa TANU. Susan alikuwa mwanaharakati; Akiwa kiongozi wa wanaharakai wa jinsia,
Susan alipigania suala la nafasi ya mafunzo ya jinsi ili mafunzo hayo yatolewe
katika ngazi zote za jamii. Alishiriki kikamilifu katika harakati za mapambano
hata nje ya vyuo vya masomo.Susan alikuwa chachu ya vikundi vya mshikamano
ambavyo viliunga mkono harakati za ukombozi katika Bara la Afrika huko Marekani.
Baada
ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. MUHTASARI WA KITABU
Kitabu
hiki ni ushuhuda wa kitaalamu (Utafiti) kwamba Wananchi wa Tanganyika
walijipatia uhuru wao kutoka kwa Waingereza mwaka 1961 kupitia mapambano
yaliyoongozwa na jumuiya yenye nguvu chini ya uratibu wa chama cha TANU.Na
kwamba Wanawake wazalendo walikuwa ni viongozi mashuhuri katika medani zote
kwenye ngazi mbalimbali.
Kitabu
hiki kinauliza maswali kadhaa:
-
Ni kwa nini utaifa wa Mtanzania ulichukua sura
mpya baada ya uhuru kuliko ilivyokuwa katika nchi nyingime?
-
Je, tunauelezeaje ukweli kwamba, licha ya
tabia, utaifa wa Tanganyika umebaki kuwa alama tu ya utambulisho kwa wanawake?
-
Je, ukiangalia ukweli kuwa utaifa na utamaduni
katika Tanganyika vilikuwa kazi zilizoendeshwa na wanawake wa TANU, matokeo ya
kazi yao ni yapi?
-
Je, tuaneulezeaje ukweli kuwa utaifa hapa
Tanzania haukujengwa na kikundi cha wanamapinduzi au haukuwa ni matokeo ya kuibuka kwa matabaka kutaka kudhibiti dola?
Hata
hivyo swali la msingi ni: Wako wapi wanawake? Hili ni swali muhimu kwa kila
mtanzania. Susan Geiger, kwa utafiti wake anachangia jibu la swali hili katika
kitabu chake.
Sehemu
ya kwanza (uk.1-23), yenye sura ya kwanza hadi ya tatu ina ujumbe muhimu wa
Kuvunja Ukimya. Sehemu
hii ya kwanza inalenga kujibu maswali yafuatayo:
-
Kwanini
wanawake waliitikia wito wa TANU kwa hamasa kiasi hicho? Walijipanga vipi?
-
Wanawake
wapi walihamasika zaidi kisiasa? Shauku hiyo inaweza kuelezwa vipi?
-
Tukizingatia
vipingamizi vya kijamii na kiutamadanuni ambavyo vilizuia wanawake kushiriki
katika shughuli za umma, ni changamto zipi ziliandamana na kuibuka kwa uelewa
wa kisiasa miongoni mwa vikundi fulani fulani vya wanawake wa Tanzania?
Maswali yote haya yanajibiwa
kwa ufasaha katika sura hizi tatu. Historia ya Bibi Titi Mohamed, inaongoza
majibu ya maswali haya.
Sura ya pili inachambua
itikadi ya Kikoloni na Uhalisi wa maisha ya Mijini. Inaangalia jinsi wakoloni
walivyowaelewa na kuelekeza maisha ya wanaume na wanawake Waafrika.Ni kwamba
watawala wakoloni hawakuwaona wanawake Waafrika, isipokua tu pale matukio au
hali Fulani ilipolazimisha waonekane. Wakoloni waliwachukulia wanume kama
wazalishaji na wanawake kama tegemezi. Nyaraka za kikoloni zimejaa maelezo
yamawasiliano kuhusu matatizo na masuala ya haki za wanaume kudhibiti au kupata
huduma za ngono. Masuala haya yalijumuisha uzinifu- kwa kiasi gani wanawake
wazinifu waadhibiwe au kufungwa; kiasi gani cha pesa au mali kitolewe kama
mahari; faini gani itolewe kama adhabu ya kuwapa wasichana mimba. Masuala
yaliyohusu wanawake kama kulipa kodi, kupangiwa sehemu za kazi na mishahara kwa
walimu wanawake waafrika yalitazamwa kama vile yamo ndani ya mahitaji, haki na
wajibu wa wanaume na wale waliowategemea…uk 17.
Sura ya tatu, inachambua wanawake waafrika walioishi Dar-es-salaam.
Mwaka wa 1950, asilimia 90 ya wanawake walioishi Dar-es-salaam, walikuwa
Waisilamu na wasiojua kusoma walikuwa wanafikia asilimia 88. Wanawake wachache sana
walikuwa wasomi, ambao wengi wao walikuwa Wakristo. Kufikia miaka ya katia ya
1950, hili kundi la wanawake wachache wasomi, lilijumuisha wale wenye elimu ya
kutosha kuajiriwa kama walimu, watoa huduma hospitalini na mjini.
Wanawake ambao hawakujua
kusoma, walijipatia kipato kwa ukahaba, kupika pombe na kuuza samaki. Shughuli
nyingine za kujipatia fedha zilikuwa ni pamoja na kupasua na kuuza kuni,
kutengeneza na kuuza keki, kalimati, maharage, na nazi.
Makahaba walihitajika, kwani
asilimia 39 ya idadi ya wanaume Dar-es-salaam hawakuwa na wake. Wanaume
waliwaacha wake zao nyumbani ili waendelee kutunza mashamba na ardhi. Hivyo
wanawake waliofanya ukahaba, walifanya hivyo kwa uamuzi wa kiuchumi na wengi
wao walitumia pesa hizo kutunza familia. Mwaka
1956, asilimia 11.2 ya kaya zote Dar-es-salaam ziliongozwa na wanawake.
Kwa sababu kadhaa zilizoingiliana, ni wawawake wa Kiislamu wa
Dar-es-salaam wenye umri wa makamu, na ambao hawakusoma, ndio waliokuwa
wanaharakati. Harakati zao ndizo zilizoanzisha na kujaza ujasiri katika
uzalendo nchini Tanganyika.
Sehemu ya pili ya kitabu hiki (Uk31-82) yenye ujumbe: Wanawake na Ujenzi
wa Uzalendo, ina sura ya nne hadi ya nane na inalenga kujibu maswali yafuatayo:
-
Kwa
nini wanawake hawa walipenda siasa za kizalendo?
-
Walitarajia
kupata au kufanikisha nini?
-
Mchango wao kwa Utaifa, kukua na kuendelea
kwa TANU ulikuwa nini?
Maswali yote haya yanajibiwa kwa ufasaha katika sura
hizi tano. Katika sura hizi tunaelezewa juu ya harakati za Bibi Titi Mohamed,
Dar-es-salaam na nje ya Dar-es-salaam, juu ya wanawake kuinuka kutoka gizani,
juu ya wanawake wanaharakati wa Kilimanjaro na Moshi mjini na wanaharakati
kutoka Mwanza.
“Kambona aliporudi nilianza kuwapanga
wanawake katika idara. Tulianza kukutana katika ua wa ofisi ya TANU lakini
haukutosha, kwa hiyo tukawa tunakutana Anartoughlo.Tukachagua viongozi wetu… Bi
Kaundime kutoka Temeke, Asha binti Waziri, Temeke na Binti Kaundime, mwingine
Saada binti Kipara.Hawa ndio wanawake waliokuwepo. Kulikuwa na wengine
Kinondoni, Magomeni, Buguruni na Kigamboni… Tulitembea nyumba hadi nyumba,
usiku na mchana, tukingoja mlangoni na
kuwasihi wafike kwenye mkutano kesho
yake.Tulitembea kila mahali…” (Mahojiano ya Bibi Titi,
uk.37).
Na
Bibi Titi, nje ya Dar-es-salaam tunasikia yafuatayo:
“
Safari yetu ya kwanza tulikwenda Tanga, Januari 1,1956. Tuiokwenda ni Bwana Mkubwa,
mimi na Rajabu Diwani… Tulikwenda Tanga na Korogwe, tukazunguka mkoa mzima kwa
muda wa siku ishirini na moja, kisha
tukarudi Dar-es-salaam.Kamati Kuu ilipokaa iliamua kwamba ninao uwezo wa
kusafiri peke yangu… unajua, nchi hii ni kubwa, tusingeweza kusafiri pamoja
kila wakati. Kwa hiyo, mimi nilikwenda upande wangu na Bwana Mkubwa wake. Siku
hizo ilikukwa ni mimi na yeye tu tuliweza kufanya hivyo… Nilisafiri sana, na
sio kwa niaba ya wanawake tu, hotuba zangu zote ziligusa wanawake na wanaume na
nilifuatana na wanaume katika safari hizi. Niliweza kusafiri kwa miezi mitatu
mfululizo. Ningeweza kuwa Mwanza, halafu nikaenda Musoma ambapo ningepata
telegramu iliyonitaka niende Dodoma.Nikiwa Dodoma napata telegramu nyingine
kwenda Mbeya…” (Mahojiano na Bibi Titi. Uk
39-41).
Sura
ya sita inatufunulia wanawake mashujaa walioshirikiana na Bibi Titi Mohamed kwa
upande wa Dar-es-salaam.Hawa ni akina: Tatu Mzee, Halima Hamisi, Salima Ferouz,
Mashavu binti Kabonge, Binti Kipara, Mwasaburi Ali na Fatuma Abdallah.Wako na
wengine wengi, lakini hawa ndo waliweza kufanya mahojiano na Susan
Geiger.Mahojiano yao yanatoa mwanga wa kile kilichotendeka. Kwa vile waliongea
wao na kuna ushuhuda wa kihistoria kubainisha ukweli wao, hakuna sababu yoyote
kutilia mashaka maelezo yao. Wanawake wote hawa walijitoa muhanga, walitumia
mali zao hadi wengine ndoa zao zikavunjika. Salima Ferouz, alieleza kwenye
mahojiano yake na Susan Gieger:
“Niliuza
vitumbua kupata fedha ya kununua kadi. Nilijiunga kwasababbu nilitaka uhuru na
kuondokana na utumwa…. Ukoloni ulikuwa mgumu. Tuliwekwa ndani, au tuseme
tuliolewa. Unakaa ndani na kuletewa kila kitu… kinachoendelea nje hukijui,
hujui kinachoendelea duniani. Kwa hiyo tulifikiria, kama tusipopata uhuru sisi,
watoto wetu wataupata, lakini tufanye kazi tuondokane na utumwa… Sisi wanawake
tulikuwa na nguvu…. Tuliongoza njia kwa sababau ya uonevu wa watoto wetu na
jinsi tulivyowekwa ndani…” (Uk. 55).
Wakati
anahojiwa Bi Salima Ferous, alikuwa mwanamke mzee mwenye majonzi, ambaye afya
yake ilikuwa dhaifu, na ni wazi alikuwa hakumbukwi tena na chama
alichokitumikia kwa uaminifu kuleta Uhuru wa taifa letu. Wengi wa wanawake hawa
hawakumbukwi wala kutajwa popote pale!
Sura
ya Saba, inawaelezea wanaharakati wa Kilimanjaro na Moshi Mjini.Hawa walikuwa
tofauti na wale wa Dar-es-salaam.Hawa walikuwa wasomi na wengi wao walikuwa
wakristu. Wanawake hawa ni Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim, Zainabu
Hatibu, Morio Kibabo, Violet Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga,
Natujwa Daniel Mashamba, na Lucy Lameck. Maelezo ya Elizabeth Gupta,
yanaonyesha jinsi wanawake walivyokuwa mstari wa mbele katika harakati:
“
Kazi yetu ilikuwa kuimba. Tuliposhinda uchaguzi, nikaingia idara ya usalama na
ulinzi. Ilikuwa kazi ngumu. Tulikuwa tunalinda nyumba moja huku Nyerere,
amelala nyumba nyingine. Wakoloni walipotuona tunalinda nyumba, wao walijua
kwamba Nyerere yuko ndani. Tulikuwa tukijificha kwenye magunia, askari wa
kikoloni wakipita wanafikiri ni magunia ya mkaa…Nilisaidia kujenga ofisi ya
chama ya Mabogini, ilikuwa nyumba ya Abdi Nuru aliyoitoa kwa chama. Nyumba
yingine likuwa ya Bi Muhogo, alitoa chumba kimoja ambacho nilikikarabati
mwenyewe… nilitoa mali na rasilimali zangu kwa TANU…” (UK,73).
Sura
ya nane, inawaelezea wanaharakati wanawake wa TANU kutoka Mwanza. Hawa ni akina
Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili
Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa na Chausiku Mzee. Mahojiano yanaonyesha
jinsi wote hawa walivyoshiriki kikamilifu katika mapambano ya kuleta uhuru wa
taifa letu. Bi Chausiku Mzee, anakumbuka maandamano ya Geita na Mwanza:
“…Tulipigwa
mabomu ya machozi na wote tulifungwa. Baada ya hapo, tuliweza kufungua tawi la
TANU Geita, halafu tukaenda Maswa, Ngudu, Shinyanga, Tabora mpaka Bukoba. DC
alikuwa akituvuruga, mwishowe tukafanyia mikutano mbugani, akapeleka polisi
kutufuata…”(Uk 93).
Sehemu
ya tatu ya kitabu hiki (Uk 95- 113) inayoelezea juu ya Uzalendo na Harakati za
Wanawake Baada ya huru inazo sura tatu, sura ya tisa hadi ya kumi na moja na
zinalenga kujibu maswali yafuatayo:
-
Kwa nini Bibi Titi alisukumwa nje ya nuru ya
harakati za kisiasa baadaya uhuru? Ukimya uliofuata unatoa changamoto gani kwa
wanaharakati?
-
Ajenda ya waanawake wa TANU ya kuendeleza
harakati za kisiasa baaada ya uhuru ilibadilishwa na kufanywa ya ustawi wa
jamii. Ni kwa nini?
-
Wanaharakati
wa jinsia katika Tanzania ya leo wanajifunza nini kutokana na harakati za
kisiasa za wanawake wa TANU?
Maswali haya yanajibiwa
vizuri. Katika sura hizi tunaelezwa maisha ya Bibi Titi Mohamed, wakati wa Uhuru
na Baada ya uhuru, jinsi kitengo cha wanawake wa TANU, kilivyobadilishwa kuwa
Umoja wa Wanawake na mwisho tunapata historia fupi ya Lucy Lameck, mwanamke
aliyefanikiwa kuwa Mbunge na naibu waziri.
Wakati wa Uhuru Bibi Titi Mohamed, alikuwa upande wa
kulia wa Mwalimu Nyerere. Kufuatana na wachambuzi wa mambo wakati wa Uhuru,
Nyerere Na Bibi Titi Mohamed, ndio waliojulikana sana nchi nzima. Ingawa Bi
Titi hakuwa msomi, alichaguliwa kuwa mbunge na kupata nyazifa serikalini.
Baadaye alipoteza kiti chake cha Ubunge.Alifanya kosa la kudai ushikishwaji na
kuhoji baadhi ya vipengele vya Azimio la Arusha.Alihoji wazi bila kificho. Matata yalianza. Alijitoa kwenye uongozi wa chama baadaye aliusishwa na
mapinduzi. Aliwekwa kizuizini miaka michache na baadaye alisamehewa na Mwalimu
Nyerere.Nyota yake ilizimika! Lakini hii haina maana ya kufuta kumbukumbu zote
alizozifanya.
Mbali
na pigo hili la Bibi Titi Mohamed, wanawake wa TANU, walipata pigo jingine la
Kitengo chao ndani ya chama kugeuzwa kuwa Umoja wa wanawake.Kitabu kinaelezea
vizuri pigo hili na kwamba malengo ya Umoja wa wanawake yalikuwa tofauti kabisa
na kitengo cha wanawake wanaharakati.
Wanaume waliogopa nguvu za wanawake. Hawakutaka
wanawake waendelee kujiingiza kwenye siasa. Na hadi leo hii, serikali inakuwa
makini kwa vikundi vya wanawake. Ilipoanzishwa BAWATA ya Profesa Anna
Tibaijuka, serikali iliifutilia mbali kwa kisingizio kwamba umoja huo ulikuwa
unaelekea kujiiingiza katika siasa.
V. TATHMINI YA KITABU.
Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini
ya kazi hii aliyoifanya Susan Geiger.
Mwanzoni nilidokezea kwamba hii ni tafsiri
iliyorahisishwa, lakini kwa kiasi kikubwa ujumbe na ukweli unaobebwa na kazi
hii ya Susan Geiger, unabaki palepale. Elieshi Lema, aliyefanya tafsiri,
hakuongeza wala kupunguza ukweli wa utafiti. Njia alizotumia Susan Geiger za
kukusanya habari au takwimu za kitabu hiki ni za kipekee. Chanzo chake kikubwa
cha kupata habari na tathmini kilikuwa wanawake wanaharakati wenyewe. Kwa
kupitia utafiti uliofanyika, walipewa nafasi ya kuelezea maisha yao wenyewe
kama walivyoishi ndani ya jamii. Hizi ni simulizi zao pamoja mkusanyiko wa
matukio mengine ya historia. Wanawake wanaharakati walijieleza, jinsi
walivyoshiriki mapambano.
Sambamba na hili la kuwahoji wanaharakati, inaonyesha
Susan Geiger, alifanya utafiti wa kina kwenye nyumba za makumbusho ya mambo ya
kale hapa Tanzania na huko Uingereza.Nyaraka muhimu za Serikali ya kikoloni
hapa Tanganyika zilipatikana huko na katika vyanzo vingine vya habari. Alisoma
na kazi yingine zilizoandikwa kuhusu harakati za ukombozi katika taifa letu.
Kwa kuunganisha yote hayo aliweza kutoa kitu chenye uhakika, kinachoonyesha
ushiriki wa wanawake katika mapambano ya uhuru wa taifa letu.
Hivyo nianze tathmini hii kwa kumpongeza Susan
Geiger, kwa kazi yake nzuri ya kutufumbua macho na kutukumbusha historia yetu.
Kitabu hiki ni muhimu sana. Pia pongezi ziwaendee Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP) kufikiria kufanya tafsiri ya kitabu hiki. Ni matumaini yangu kwamba,
watu wakisoma, wataanza kujiuliza maswali mengi juu ya wanawake wa TANU.Wako
wapi akina mama hawa? Je, wamekufa na ushupavu wao au ushupavu huu
wameurithisha kwa wanawake wengine? Je maneno ya Bibi Titi, yanachukuliwa vipi
na wanawake wa Tanzania, hasa wale walio mstari wa mbele kutetea haki za
wanawake? :
“ Ingawa wanawake wanasema kwamba
hawajaendelea, mimi ninayewafahamu tangu wakati ule, naona kwamba wameendelea
sana, kwasababau serikali inataka kuwasaidia. Tatizo liko wa wanawake viongozi,
siyo kwa wanawake kwa ujumla” (Mahojiano ya Bibi Titi Uk.104). Inawezekana Bibi
Titi, aliyasema haya katika uzee wake? Kwamba alishaanza kupoteza kumbukumbu na
moyo wake wa ushupavu? Au inawezekana kuna ukweli katika maneno yake?
Pili, nikubaliane na hoja iliyotolewa kwenye
utangulizi wa kitabu hiki: “ Tunaamini kwamba vikaragosi vya wakoloni
vimejitokeza tena hivi leo kutokana na kuwepo kwa sera za soko huria na
kudhihirika kwa nguvu mpya za ubeberu. Tanzania inaweza kujikuta ina “uhuru wa
bendera” hasa ukitilia maanani kwamba uchumi wake sasa unamilikiwa na mashirika
ya watu wengi wa kigeni….”.
Hii ni kweli. Ukiangalia wimbi la uwekezaji na hasa
uwekezaji unaogusa ardhi, dalili za kuwa na wanahakarti kama wanawake TANU,siku
zijazo halikwepeki kamwe! Ni kama
inavyosemwa kwenye utangulizi wa kitabu hiki:
“ Muda mfupi baada ya Uhuru, Serikali ilipitisha sera ya ardhi
ambayo ilitambua umiliki wa ardhi kuwa wa
jamii na kuwazuia wageni wasimiliki
ardhi. Sera hii ya ardhi imekuwa ikipigwa vita na wawekezaji tangu miaka
ya 1980, na hatua kwa hatua, Serikali imekuwa ikiruhusu matumizi ya ardhi kwa
wageni katika sekta za kilimo, utalii, uchimbaji wa madini na mabenki
yanayowekeza hapa nchini. Hivyo basi, suala la ardhi limeanza kuibuka upya na
wanaharakati pamoja na jamii katika sehemu mbalimbali wameanza kujipanga upya
ili kulipinga.” (Utangulizi xi).
VI. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha, ninapenda kuwashauri watanzania
kukisoma kitabu hiki cha Wanawake wa TANU. Pia ninapendekeza, Serikali itafute
namna ya kuwaenzi wanawake hawa. Wale ambao bado wako hai, wapatiwe matunzo.
Wale waliokufa, kifanyike kitu cha kumbukumbu. Si vibaya hata kama familia zao
zitapatiwa kitu cha kumbukumbu.
Kuna haja ya dunia kuacha tabia ya kuwatumia
wanawake katika harakati na baadaye kuwatelekeza na kuwaweka pembeni. Ukisoma
kitabu cha Wanawake wa TANU, unapata picha ya Maria Magdalena wa kwenye Biblia,
pamoja na wanawake wale wote waliomtumza Yesu.Luka, anaandika kwamba wanawake
hawa, walitumia pesa zao na mali zao kumhudumia Yesu.Na walikwenda naye popote
alipokwenda na kuhudumia umati wote uliomfuata Yesu.Lakini kwenye kumbukumbu ya
Kanisa, wanatajwa Mitume wanaume peke yao na wanawake hawatajwi!
Maria Magdalena, alikuwa karibu na Yesu, alimhudumia
na alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia ufufuko wa Yesu, lakini katika kumbukumbu
za kanisa, ametupwa pembeni!
Yote
haya yanasababishwa na mfumo dume! Mfumo unaopenda madaraka kuliko kitu
chochote kile! Mfumo ambao umeleta vita na maafa makubwa hapa duniani.
Tunapofikiria amani ya dunia hii, na amani ya taifa letu la Tanzania tufikirie
kuirudia mifumo inayowashirikisha na wanawake, kama ile mifumo ya wanawake wa
TANU.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment