UCHAGUZI MDOGO WA IGUNGA NI KIPIMA JOTO?

Mtu muhimu anayeweza kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi mdogo wa Igunga, ni Rostam Aziz mwenyewe. Na huu ni mtihani mkubwa kwa ndugu yetu huyu. CCM itakuwa inapima uaminifu na mapenzi yake kwa chama chake; hivyo CCM inatarajia Rostam, kufanya kampeni na kumnadi mgombea wa chama chao. Tunavyojua nguvu ”fedha” na ushawishi wa Rostam, akikubali kuwa mtiifu kwa chama chake, CCM inaweza kushinda kule Igunga.

Mtihani mwingine alionao Rostam, ni sisi watanzania tunaotaka kuupima uzalendo wake na mapenzi yake kwa taifa letu. Yeye mwenyewe ametutangazia sisi na kuitangazia dunia nzima kwamba CCM inaendesha Siasa Uchwara. Na sababu kubwa ya yeye kujiuzulu ni kushindwa kuvumilia siasa uchwara. Hatua ya kujiuzulu ni kuonyesha wazi kwamba CCM haiwezi kuiwakilisha Igunga na haina uwezo wa kuliongoza taifa. Maana kama chama kinaendesha siasa uchwara kitaweza vipi kuliongoza taifa? Ndio maana tunamsubiri kwa hamu Rostam kupanda jukwaani na kuanza kumnadi mgombea wa CCM. Tutamdharau na kumuweka kwenye kapu la maadui wa taifa letu. Ujumbe utakuwa wazi kwamba Rostam Aziz ni adui wa wana wa Igunga kwa kutaka mwakilishi wao atokane na chama chenye siasa Uchwara.
Vyama vya upinzani navyo vina mtihani mkubwa kule Igunga. Inawezekana navyo vikamsimamisha mtu ambaye si mwana wa Igunga; mtu ambaye haguswi na kuyaishi maisha ya wana wa Igunga. Lakini changamoto kubwa kwa vyama hivi vya siasa ni ushirikiano. Kama vyama hivi vingeungana na kumsimamisha mngombea mmoja; ni wazi kabisa kwamba vingekuwa na uhakika wa kukishinda kiti cha Igunga. Bahati mbaya ni kwamba vyama hivi vinatofautiana kwa misimamo. CUF, wanaibeza CHADEMA, na CHADEMA inaibeza CUF kuishi katikati; mguu mmoja upinzani na mguu mwingine serikalini; vyama vikianza kubezana ni vigumu kuunda ushirikiano. Mzee Mrema, yeye anaonyesha wazi kwamba alichokitaka ni Ubunge, ili apate posho za kupeleka Jimboni kwake, zaidi ya hapo hana muda wa kuunda ushirikiano wa vyama vingine vya siasa. Hivyo kila chama kinapambana kivyake kwa manufaa ya chama na wala si manufaa ya taifa letu, maana kama ni manufaa ya  taifa basi vyama vyote vya upinzani vingeugana na kuhakikisha kiti cha Igunga kinaingia upinzani.

Kuna sababu nyingi za vyama vya upinzani kukitaka kiti cha Igunga. Kuongeza mbunge mmoja, ni kuongeza nguvu ya sauti ya upinzani Bungeni. Lakini pia vyama vya upinzani vikishinda Igunga ni ujumbe tosha kwamba wananchi sasa wamekichoka chama cha Mapinduzi na dalili nzuri kwa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.

Kuna sababu nyingi pia za CCM kutaka kukirudisha kiti cha Igunga: Hawataki kupunguza kiti hata kimoja Bungeni, Hawataki watanzania kuamini kwamba Igunga ni Rostam, na Rostam ni Igunga, kwa maana kwamba bila Rostam hakuna CCM Igunga, hawataki watanzania kuamini kwamba zoezi la kujivua gamba limekidhoofisha chama, hawataki kushindwa Igunga, maana uchaguzi mdogo wa Igunga ni kipima joto kuona kama CCM bado inakubalika na inaweza kuiingia kwenye uchaguzi wa 2015 kwa kujiamini.

Lakini pia kwa vile CCM inakitaka kiti hiki kwa gharama zozote zile inaweza kutumia mbinu chafu za kukipata kiti hiki. Ni kiasi cha serikali kuagiza kwamba ni lazima kiti cha Igunga kirudi CCM. Hii inatosha maana dola ina nguvu zote! Usalama wa taifa utafanya kazi yake; ingawa inasikitisha kuona usalama wa taifa unafanikisha uchaguzi mkuu kwa upande wa CCM na kushindwa kudhibiti vitu vya hatari kama samaki wenye mionzi walioingizwa kwenye taifa letu; Tanzania tunaongoza kwa kuingiza bidhaa bandia hadi dawa bandia ambazo ni hatari kwa afya za binadamu wakati usalama wa taifa wapo. Sote tunakumbuka ushindi wa kura moja kule Shinyanga; ulikuwa ni ushindi wenye utata mkubwa, lakini kwa vile tume yetu ya uchaguzi si huru, msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mtumishi wa serikali, alitangaza ushindi wa CCM, wa kura moja kule Shinyanga, tunakumbuka pia uchaguzi mkuu uliopita bunduki na mabomu ya kutoa machozi yalitumika kutangaza ushindi wa CCM kwenye baadhi ya majimbo, tunakumbuka mbinu ya kununua shahada ili kuhakikisha wanaojitokeza kupiga kura ni wachache na ni wanachama wa CCM. Sasa hivi kuna ugumu wa maisha, hivyo kuwanunua wapiga kura ni rahisi sana. Haitashangaza kusikia fedha nyingi zinatumika kununua shahada. Inaaminika kwamba uchaguzi mdogo wa Busanda, wakati ule shahada ilipanda dau hadi laki tatu! Inawezekana kabisa mwaka huu shahada ikanunuliwa laki tano. Fedha ya kufanya mambo haya machafu ipo siku zote; Ingawa kwenye bajeti wizara nyingi zimepangiwa fedha kidogo kwa kisingizio kwamba “Kasungura” ni kadogo, utashangaa fedha zinapatikana wakati wa uchaguzi  mdogo; utashangaa jinsi CCM itakavyowasafirisha wasanii wa kila aina kwenda kwenye kampeni kule Igunga. Ukiwauliza CCM, fedha hizo zinatoka wapi, watasema wao wana wafadhili wao. Swali langu kubwa ni je kwa nini wafadhili wa CCM wasichangie na miradi ya maendeleo na kuchangia fedha za kuendesha serikali? Kwa nini wachange tu fedha za kununulia kura? Hawa ni wafadhili au wanakuwa na lao jambo? Wanakichangia chama ambacho kesho na keshokutwa kitawapatia tenda na kuwauzia rasilimali za taifa kwa bei ya kutupwa?


Mbali na uvumi kwamba Rostam Azizi, alikuwa akitoa misaada mingi Kule Igunga, bado kuna matatizo mengi ambayo yanahitaji mbunge makini, mzalendo na asiyekuwa na ushabiki wa vyama vya siasa. Matatizo kama barabara, maji, shule, ugumu wa maisha na mengine mengi yapo kwenye Jimbo la Igunga. Wao wanajua matatizo yao na kumjua mtu anayeweza kuwawakilisha vyema  Bungeni. Hakuna haja ya kuwashinikiza, kuwashawishi na kuwanunua. Vyama vya siasa na hasa vile vya upinzani vifanye kazi ya kuelezea sera zao. Sera za CCM zinajulikana, maana ndicho chama tawala. Sasa hivi kiko kwenye mchakato wa kujivua gamba. Kila kikitoa gamba hili linazaliwa jingine. Tumesikia gamba jipya la kuuza UDA, na jinsi tunavyoukaribia Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga yatajitokeza magamba mengine. Ugumu wa maisha, kupanda kwa bei ya mafuta, sukari na bidhaa nyinginezo ni sera ya Chama cha Mapinduzi. Hivyo uchaguzi mdogo uchaguzi mdogo wa Igunga ni Kipima joto na ni changamoto kwa wananchi wa Igunga. Hata hivyo kumchangua mwakilishi wao ni jukumu lao na haki yao ya msingi, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuwaingilia.

Na,
Padri Privatus Karugendo.




0 comments:

Post a Comment