TWAWEZA KULIJENGA TAIFA
BILA UAMINIFU?
Hali ilivyo sasa hivi
katika taifa letu la Tanzania, mtu anaweza kujiuliza uaminifu maana yake nini?
Na je, ni kwa nini mtu awe mwaminifu? Anaogopa nini? Anawajibika kwa nani?
Kipimo cha uaminifu wake nini? Je uaminifu ni wa watanzania wote au kuna baadhi
ya watu ambao ndio lazima wawe waaminifu. Uaminifu ni wa maskini tu au na
matajiri nao ni lazima wawe waaminifu?
Je umasikini unachangia kiasi gani watu kukoswa uaminifu? Je ukosefu wa huduma
muhimu katika jamii yetu unachangia kiasi gani watu kutokuwa waaminifu?
Bila kuyaangalia yote
haya na kuyafanyia kazi ni ndoto kuongelea uaminifu. Mtoto umleavyo ndivyo
akuavyo! Pia tunakumbushwa kwamba: "Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala
mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake.
Ni wazi kwamba watu hawachumi tini kutoka miti ya michongoma, wala hawachumi
matunda ya mizabibu kutoka mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina
bora iliyomo moyoni mwake, na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa
maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake" (Luka 6:43-45).
Tunataka tusitake,
hatuwezi kulijenga taifa bila ya kuwa na uaminifu. Tumeanza kunyosheana vidole
ju ya madawa ya kulevya; hata viongozi wa dini ambao katika mazingira ya
kawaida ndio wangekuwa mstari wa mbele kufundisha, kulinda na kuutetea
uaminifu, wameshukiwa kufanya biashara hii haramu. Tunapiga kelele juu ya mikataba
mibovu, tunapiga kelele juu ya mafisadi na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa
letu. Tunapiga kelele juu ya uporaji wa ardhi na uwekezaji unaoelekea
kutuingiza katika dimbwi la ukoloni mambo leo. Yote haya yanasababishwa na
uaminifu mdogo miongoni mwetu. Mataifa yote yaliyoendelea duniani, yamefikia
hatua hiyo kwa kujenga uaminifu imara
miongoni mwa wananchi wake.
Watanzania walio wengi
wamekulia katika mazingira ya udanganyifu, rushwa na uzembe. Tunaelekea
kusherehekea miaka 50 ya uhuru wetu tukiwa tumetanguliza udanganyifu na uzembe.
Matatizo mengi tuliyo nayo yanatokana na udanganyifu na uzembe. Tuna tatizo la
umeme kwa sababu ya udanganyifu na uzembe, tuna umasikini wa kutisha kwa sababu
ya udanganyifu na uzembe. Katika serikali ya awamu ya pili, ya tatu na sasa hii
ya nne tabia hizi zimejionyesha wazi na
kufumbiwa macho. Watu wachache wamefanya kazi kwa uaminifu na kwa bidii kubwa,
lakini asilimia kubwa ni udanganyifu, rushwa na uzembe. Mitihani inanunuliwa,
vyeti vinanunuliwa na watu wanapata mafanikio
ya haraka maishani ( wanajenga majumba, wanakuwa na magari, wanakuwa viongozi
wa juu serikalini, wana kuwa na viwanda, pesa nyingi hadi mabilioni) bila
kusoma, walau kuwa na digrii moja au cheti na wakati mwingine bila hata
kumaliza sekondari. Hadi kuna msemo
kwamba mafanikio maishani si kusoma!
Hata
hivyo uaminifu ni neno pana na linazua maswali kuliko majibu. Mtu mwenye
uchokozi anaweza kutoa maoni kwamba hata na majambazi wana uaminifu mkubwa
miongoni mwao. Ikiwa na maana kwamba mtu akiongelea uaminifu ni bora kutoa
maelezo ya kina. Jambazi akikamatwa, anakubali kuteswa na wakati mwingine
kuyapoteza maisha yake bila kuwataja majambazi wengine. Huu ni uaminifu wa
kiwango cha juu! Mtu anayechota pesa za
serikali ili kukiendeleza chama chake cha siasa, anakuwa anakoswa uaminifu
katika serikali, lakini ni mwaminifu katika chama chake. Mtu anayechota pesa za serikali ili
kuwasomesha watoto wake, jamaa zake na kuleta maendeleo katika wilaya yake,
anakuwa anakoswa uaminifu serikalini, lakini ni mwaminifu kwa familia yake na
kabila lake.
Uaminifu unahitaji
malengo, kipimo na uwajibikaji. Ni lazima mtu ajiulize ni kwa nini anatakiwa
kuwa mwaminifu, na kwa nani? Kwa familia yake, kwa kabila lake, kwa dini yake
au kwa taifa lake, na je ni kipimo gani kitatumika kuupima uaminifu wake. Na ni
lazima uwepo mfumo wa kumsaidia mtu kutekeleza malengo, kukumbushwa malengo na
kupimwa mara kwa mara. Mtu akiachwa peke yake ni lazima atangulize uaminifu
unaolenga katika kumletea manufaa yake
binafsi. Kwa vile watanzania wameachiwa bila kuwa na chombo cha kuwakumbusha,
kila mtu anajijenga binafsi badala ya kulijenga taifa letu.
Majambazi, wana mifumo
yao ya kulinda na kukuza uaminifu miongoni
mwao. Wana viongozi, wana viapo, wana nafasi za kukutania kufanya
mikutano na majadiliano na wana waganga wao wa kuwafanyia zindiko na matambiko.
Majambazi wana kipimo cha kupima uaminifu wa kila mshirika. Anayeshindwa kipimo
hicho anakwenda maji! Hivyo na sisi
kama tunataka kuendelea kama taifa ni muhimu kuwa na mfumo wa kupima uaminifu
wetu.
Wakati nikitafakari
swala zima la uaminifu katika taifa letu la Tanzania, nimekumbuka yale tunayoelezwa katika Biblia kuhusu Anania na Safira. Hawa ni mme na mke
walioishi kwenye jumuiya za kwanza za Kikristu zilizokuwa zimejiwekea malengo,
kipimo na uwajibikaji:
" Jumuiya yote yote
ya waamini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu
chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa
navyo........ Hakuna mtu ye yote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na
mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo,
zikagawiwa kila mmmoja kadiri ya
mahitaji yake".(Matendo ya Mitume 4:32-35).
" Mtu mmoja aitwaye
Anania na mkewe Safira waliuza shamba lao vile vile. Lakini, mkewe akiwa
anajua, Anania akajiwekea sehemu ya fedha alizozipata na ile sehemu nyingine
akawakabidhi mitume. Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani
ameungia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu
ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba? Kabla ya kuliuza lilikuwa mali
yako, na baada ya kuliuza, bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo, kwa
nini ,basi, uliamua moyoni kwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu,
umemdanganya Mungu". Anania aliposikia hayo, akaaguka chini, akafa. Watu
wote waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.....Baada ya muda wa saa
tatu hivi, mke wake, bila kufahamu mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani( neno mle
ndani, ni kutaka kumaanisha, mahali pa kukutania, mkutano wa jumuiya,
nafasi ya majadiliano, kukumbushana malengo na wajibu) Petro akamwambia,"
Niambie Je, kiasi hiki cha fedha ndicho mlichopata kwa kuuza lile
shamba?" Yeye akamjibu,
"Naam, ni kisi hicho". Naye Petro akamwambia, "Mbona umekula
njama kumjaribu Roho wa Bwana?........ Mara Safira akaanguka mbele ya miguu ya
Petro, akafa...... Kanisa lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo,
waliogopa sana" ( Matendo ya
Mitume 5:1-11).
Wataalamu wa Biblia
wanatuelezea kwamba kifo cha Anania na Safira, hakikuwa kifo kama tunavyojua
sisi mtu kufa akazikwa kaburini. Ni kwamba walitengwa na jumuia ya waamini.
Ukosefu wa uaminifu katika Jumuiya za Kikristu za mwanzo kulimaanisha kifo.
Kutengwa na jumuiya kulilinganishwa na kifo. Woga wa kutengwa na jumuiya
kuliwafanya watu kuwa waaminifu wakati wote. Kila mtu aliujua wajibu wake wa
kutanguliza jumuiya kabla ya kuyatanguliza maisha yake binafsi. Walisali
pamoja, walionyana, walikumbushana, walitiana nguvu.
Kabla ya uaminifu kwa
jumuiya nzima, kila mtu alichunguza uaminifu katika moyo wake. Kila mtu
alijipima kwa kipimo cha Anania na Safira. Ni kiasi gani mtu alijiamini yeye
mwenyewe. Anania na Safira, walitaka watoe nusu ya mali yao, kwa kisingizio cha
kutoa kila kitu walichokuwa nacho. Na kwa vile jumuiya nzima iliamua kwamba
hawa hawakuwa waaminifu kwa jumuiya hayo, walitengwa! Kwa msemo wao wa kiimani,
walikufa!
Mfano huu wa Anania na
Safira, unaweza kutusaidia sisi watanzania. Je, sisi tuna malengo gani? Kipimo
chetu cha uaminifu ni kipi? Anayekoswa uaminifu anafanywa nini? Tunakutania
wapi ili kuonyana, kukumbushana malengo
na kutiana nguvu? Ni nani anaogopa kutengwa na jamii akifanya mambo ya
udanganyifu? Tunaogopa nini? Ni yapi yaliyojaa mioyoni mwetu?
Ni muhimu kukumbushana
kwamba hatuwezi kujenga uaminifu miongoni mwetu kwenye majukwaa, kwenye luninga au kwenye magazeti, kwamba huwezi
kujenga uaminifu bila ya kuwa na malengo, mfumo na kipimo. Huko nyuma lengo letu lilikuwa ni kujenga Ujamaa na
Kujitegemea. Kila aliyekwenda kinyume na sera ya ujamaa, alionekana kuwa mtu
asiyekuwa mwaminifu. Sasa hivi hatujengi ujamaa, na hakuna mwenye uhakika
tunachokijenga ni kitu gani. Wengine wanasema Utandawazi, wengine wanasema kazi
yao au malengo yao ni kujenga barabara, wengine wanasema soko hulia, wengine wanaingia ubia na wawekezaji ,
wengine eti ni mlengo wa kulia, wengine eti ni mlengo wa kushoto na wengine
mlengo wa kati, wengine wanasema ubinafsishaji. Sasa hivi ni vurugu! Hatuna
kipimo!
Mtu, akipora pesa za
serikali, akajenga hekalu, watu wanamshangilia. Huyu anaonekana kama shujaa.
Kila Mtanzania, anataka awe kama yeye. Mazingira kama haya hayawezi kujenga
uaminifu. Tume ya Warioba, ilifichua watu na mazingira yanayosababisha ukosefu
wa uaminifu (rushwa), hakuna kilichofanyika! Kwanini basi " Bongo land"
isimaanishe ubazazi? Watu wana macho na akili. Wakiona kiongozi anaanzisha
ubazazi, nao wanafuatisha! Na tunatembea kifua mbele tukijitangaza kwamba sisi
ni “Bong land”: ukitaka bidhaa bandia karibu “Bongo land”, ukitaka kutajirika
haraka, kuchota na kujiondokea, karibu “Bongo land”, ukitaka kushuhudia
viongozi wa watu masikini wanaoogelea kwenye utajiri mkubwa karibu “Bongo
land”.
Watu wengi , wametajwa
mara nyingi kuogelea kwenye dimbwi la udanganyifu. Hakuna kinachofanyika! Na la
kushangaza zaidi wale wote wanaotajwa kuwa wadanganyifu ndo wanajiweka mstari
wa mbele kutaka kuliongoza taifa letu la Tanzania na kuonyesha wazi wazi kwamba
hii ni "Bongo land", Kama huu si ubazazi ni kitu gani? Kuna haja
ya kuweka wazi malengo ya kitaifa na kutengeneza mifumo ya kutekeleza malengo
hayo. Wengine wanafikiri kwamba tunahitaji pia katiba ya nchi itakayokuwa
inaelezea wazi hatua za kumchukulia mtu anayevunja uaminifu wa kitaifa. Katiba
inayowapatia wananchi uwezo wa kuwakataa viongozi wala rushwa. Katiba
inayoruhusu wagombea binafsi, jambo ambalo linaweza kuleta ufanisi wa kisiasa
katika Taifa letu maana kuna watu wanapenda kulitumikia taifa letu lakini
hawapendi ukiritimba wa vyama vya siasa.
Katiba itakayo toa mwanya wa kuunda
tume huru ya uchaguzi, ili wananchi wawe na uhuru wa kuichagua serikali
yenye sera ya kujenga uaminifu wa
kitaifa. Tunahitaji kuwa chombo katika ngazi zote kuanzia vijijini hadi
taifani cha kuweza kukumbusha, kujadiliana, kutiana nguvu na kupima uaminifu wa
kila Mtanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment