TUTAANDAMANA KULINDA
HISTORIA YA TAIFA LETU.
Waziri Kombani
anawashangaa wale wanaotaka kuandamana kupinga Serikali kuuza jengo la Mahakama ya Rufani. Kwa maoni yake, nina wasi wasi kusema ni maoni ya
Serikali, maana serikali isiyolinda na kutetea historia ya taifa lake haifai
kabisa kuwa madarakani, ni kwamba jengo hilo halina hadhi ya kutumiwa na majaji
wetu, hivyo liuzwe na serikali ijengewe jengo jingine lenye hadhi ya majaji
wetu.
Hoja inayochefua zaidi
na kutilia mashaka uzalendo na uwezo wa kufikiri wa Waziri Kombani, ni pale
alipolieleza Bunge kwamba Serikali imempata mbia ambaye yuko tayari kulinunua
jengo hilo na “Kutujengea jengo jingine la mahakama ya rufani”. Alisema hivi:
“Jamani pale wanapokaa majaji wetu ni aibu tupu, hapafai ndiyo maana hivi sasa
tunafanya mazungumzo na mbia, ili ajenge jengo la kisasa kwa makubaliano ya
kumuachia pale”.
Kwa nini serikali yetu itegemee mahitaji ya wabia
na wawekezaji? Ina maana akijitokeza mbia anayetaka kutujengea Ikulu ya Kisasa,
tukubali kuuza majengo ya kihistoria ya Ikulu yetu ya sasa? Akijitokeza
mwekezaji anayetaka kujenga mji wa kisasa Ubungo na Tabata ,tuwaamishe wananchi
wote wa maeneo hayo ili kumpisha mwekezaji? Akijitokeza mwekezaji anayetaka
kukausha sehemu ya Bahari ili kujenga mji wa kisasa tukubali wazo hilo kwa
sababu atakuwa anatusaidia kujenga majengo ya kisasa? Ujinga gani huu wa
kuiishi kwa kutegemea matakwa ya wengine? Na mbaya zaidi kumtegemea mtu
anayekuja kutengeneza faida? Kwa nini serikali kama inaona jengo la Mahakama ya
rufani halina hadhi ya majaji wetu, isijenge jengo jipya? Hatuna uwezo wa
kujenga Mahakama ya rufani mpaka tupate mbia? Mbona tunajenga barabara wenyewe?
Mbona tumejenga Chuo cha Dodoma wenyewe na bado serikali ina mpango wa kufanya
mambo mengine mengi? Ni bora Waziri Kombani ,angetueleza kwamba Serikali
ilipitiwa kutaka kuuza jengo hilo na sasa imesitisha mpango huo badala ya hizi
porojo za kuingia ubia na mwekezaji na kwamba mbia huyu “Atatujengea Mahakama
ya rufani ya kisasa”
Labda ni kutokuelewa au
kuonyesha kwamba Mawaziri wetu hawako pamoja wa wananchi. Wale wanaotaka
kuandamana lengo lao ni kutetea jengo la kihistoria kuuzwa na kubomolewa.
Kwamba jengo hilo halina hadhi kwa Majaji wetu si hoja. Serikali ina uwezo wa
kujenga jengo jipya lenye hadhi kama ilivyojenga majengo mengine mengi. Hoja ni
kwamba jengo la kihistoria lisivunjwe. Hatuangalii kama jengo hilo ni shule,
hoteli, hospitali au mahakama. Duniani kote watu wanalinda historia ya majengo yao,
historia ya utamaduni wao na historia ya mambo mengine yote yanayotunzika. Hii
ndiyo hoja na ndiyo maana watu wako tayari kuandamana ili kulinda na kutetea
jengo hili la kihistoria.
Kumezuka wimbi la
kuyabomoa majengo ya zamani na kujenga majengo mapya na kisasa na hasa kwenye
jiji la Dar-es-Salaam. Sura ya Jiji la Dar-es-Salaam, inaanza kubadilika.
Itakuwa vigumu kwa vizazi vijavyo kuwa na picha ya jinsi Dar-es-Salaam
ilivyokuwa. Baadhi ya watu wanashangilia kwamba majengo haya mapya ni
maendeleo, na wengine wanashangilia kwamba sasa jiji linapendeza. Inategemea
uzuri unapimwa kwa vigezo gani; kama kutizama juu na kuyaona maghorofa badala
ya kuliona anga, nyota na mwezi, ndio uzuri, basi wanaoyafurahi majengo hayo
wana haki. Lakini ndugu zetu ambao wamekuwa na utamaduni wa kujenga majengo
marefu kwa miaka mingi, wanasema uzuri wa Jiji ni kusimama ukatizama juu ukaona
anga, nyota na mwezi na kufurahia maajabu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Sasa
hivi ukiwa katikati ya Jiji la Dar-es-Salaam, anga, nyota na mwezi vinaanza
kupotea! Kinachoonekana ni haya maghorofa yenye vioo!
Tukiliacha hili swala
uzuri, kuna hoja nyingine ya hizi fedha zinazojenga majengo haya yanayofumuka
ndani ya Jiji la Dar-es-Salaam zinatoka wapi? Je ni fedha za wabia? Na kama ni
fedha za wabia kuna usalama? Hawa wanaojenga majengo makubwa kwa fedha nyingi
hivyo si kesho na keshokutwa watataka kumiliki na ardhi yetu? Si watataka
kututawala? Kama majengo haya yanajengwa kwa fedha yetu sisi wenyewe kama
ambavyo ningetaka mimi mwenyewe kuamini, iweje bado tunalia kuwa kwenye
umasikini? Iweje tunafikiri kujenga majengo makubwa hivyo kabla ya kuwa na
uhakika wa mfumo wa kusambaza maji, kabla ya kuwa na barabara za uhakika
kuingia na kutoka kwenye Jiji letu la Dar-es-Salaam? Lakini pia tunaweza vipi
kufikiria kujenga majengo kwa gharama kubwa wakati watanzania wengi hawa nyumba
bora na salama? Watanzania wengi hawana huduma ya maji, hawana shule nzuri,
hawana hospitali na wengine hawana uwezo wa kupata milo miwili kwa siku?
Tukitaka kuwa na vitu
vipya na vya kisasa kwa gharama ya kupoteza vile vya zamani, basi taifa letu
halitakuwa na historia. Na taifa lisilokuwa na historia yake, basi hilo ni
taifa mfu! Lakini pia tunaanza kujenga utamaduni wa hatari sana, huu wa
kuendesha maisha yetu kwa kutegemea wawekezaji. Hawa jamaa wanakuja kwa lengo
la kutafuta faida na wala si lengo la kutusaidia kujenga taifa letu.
Kwa nini mtu atujengee
Mahakama ya Rufani? Kwa vile anatupenda sana? Kwa vile ni ndugu yetu? Kwa vile ana uchungu na maendeleo yetu? Mbona
bei ya mafuta inapanda, thamani ya dola inapaa, wakati shilingi yetu inazama na
bei ya mazao yetu ya biashara inakwenda chini siku hadi nyingine? Wa kulijenga
taifa hili ni sisi watanzania na wala si hao wawekezaji. Wa kulinda historia
yetu ni sisi wenyewe na wala si wageni kutoka nje.
Majengo ya kizamani
yamejengwa kwa ufundi wa aina yake, na ufundi huu haupatikani tena! Vifaa vingi
vilivyojenga majengo ya zamani ni vifaa vya hapa hapa kwetu. Ujenzi wa sasa
hivi unategemea sana vifaa kutoka nje ya nchi. Hivyo ujenzi wa sasa hivi ni
biashara; hata na mbia huyo anayesema atatujengea Mahakama ya Rufani kwa
makubaliano ya kubomoa jengo letu la kihistoria, analenga biashara zaidi ya
msaada. Vifaa vya ujenzi vitaagizwa kutoka nje na kuvinufaisha viwanda vya nje
na kujenga uchumi wa nchi zao. Hakuna mtu wa kutoa msaada katika dunia hii ya
soko huria, utandawazi, ubepari na ubeberu. Kwa maana hiyo katika zama hizi za
upole wa njiwa na ujanja wa nyoka, tunahitaji viongozi wenye kuona mbali si
hawa wa aina ya Mama Kombani.
Hivyo ni bora Waziri
Kombani na wengine wa aina yake kutambua kwamba Maandamano ya kupinga kubomolewa
kwa Jengo la Hoteli ya Forodhani yako pale pale. Kukubali kubomolewa jengo hili
ni mwanzo wa kukubali kubomoa kila kitu; tutabomoa mashule yetu ya zamani,
tutabomoa mahospitali yetu, tutabomoa majengo ya kihistoria ya Mkemia mkuu,
tutabomoa Ikulu yetu hadi tutabomoa na uhuru wetu! Tuna wajibu wa kuilinda
historia yetu kwa gharama yoyote ile; historia yetu ni urithi wetu na tuna
wajibu kwa kurithisha urithi huu kwa vizazi vijavyo.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment