TUNA TATIZO KUBWA KAMA TAIFA
Nimekuwa nikiandika juu
ya swala hili kwa miaka mingi kwamba tuna tatizo kubwa kama taifa; tunashindwa
kulinda mali zetu, madini yetu yanaibwa, ardhi yetu inaporwa, tunauza shahada
zetu za kupiga kura na kukubali kuwachagua watu wanaotupatia sukari na kanga
wakati wa uchaguzi, tunamchagua mkulima kuwawakilisha wafugaji, tunamchagua
mvuvi kuwawakilisha machinga, tunamchagua mzee kuwawakilisha vijana,
tunawachagua wanaume kuwawakilisha wanawake, tunashindwa kuipenda lugha yetu,
tunaukataa utamaduni wetu, tunakataa ngozi yetu nyeusi na kukazana kujichubua, tunazikataa nywele
zetu na kukazana kuvaa za bandia, tunashindwa kufanya kazi masaa yanayotakiwa
na kutaka tulipwe mshahara kwa kazi ambazo hatufanyi; waandishi na wachambuzi
wengine wa maswala ya -kijamii wameandika pia juu ya swala hili na kuonyesha
kwamba watanzania tuna matatizo makubwa kama taifa; kwa maneno mengine namna
yetu ya kufikiri ina matatizo. Maendeleo ya taifa letu yanakwama kwa kushindwa
kuwa na fikra pevu; tunadaganywa, tunapumbazwa na kubakia kuwaabudu na
kuwasujudia watu badala ya kuliabudu na kulisujudia taifa letu la Tanzania.
Inawezekana nimekuwa
nikiandika uzushi na labda mimi ndo nina matatizo ya kufikiri; inawezekana pia
kwamba na waandishi wengine waliokuwa wakiandika juu ya swala hili na bado
wanaandika juu ya swala hili wana matatizo
vichwani mwao. Vyovyote vile ukweli unabaki pale pale kwamba Watanzania
tuna tatizo kubwa; tunahitaji dawa ya kututibu vinginevyo tunaelekea kubaya
kama taifa:
Tunaweza kuacha mengine
yote ya nyuma, na kuchukua mfano wa hivi karibuni wa Mheshimiwa Rostam Aziz,
kujiuzulu nafasi za uongozi katika chama chake cha CCM na kuachia kiti chake
cha Ubunge wa Igunga. Tumeshuhudia kwenye vyombo vya habari baadhi ya watu wa
Igunga wakilia na kuzirai; hili nalo ni tatizo kubwa, maana kwa nini watu walie
na kuzirai mtu kuacha kiti cha Ubunge, na kuacha kulia na kuzirai kwa matatizo makubwa waliyonayo
watanzania? Tuna matatizo makubwa ambayo kama si kulia na kuzirai basi mtu
atasimama na kupambana kiume; atapigana kufa na kupona akitetea uhai wa taifa lake kuliko kumlilia mtu mmoja ambaye
wala si kitu si lolote kwenye uhai wa taifa letu; Sina haja ya kuyataja
matatizo ya watanzania, maana sote tunaishi ndani ya taifa hili na matatizo
yetu ya umasikini, njaa, magonjwa na ugumu wa maisha kwa ujumla tunayafahamu
sote. Hata hivyo kulia na kuzirai kwa watu wa Igunga si msingi wa hoja yangu
ninayotaka kuijenga kwenye makala hii. Walio mlilia Rostam Aziz, wanajua
wenyewe watakayoyakosa: Kupanda kisiasa kwa kutumia nguvu za fedha, kutupiwa
kanga na sukari na vijisenti ambavyo havimsaidii mtu kujitegemea.
Hoja yangu ya kuonyesha
kwamba tuna tatizo kubwa kama taifa ni je, Huyu Rostam Aziz ni nani?
Amelifanyia nini taifa hili kiasi ajiuzulu, magazeti yote yamwandike Rostam
Aziz, na vyombo vyote vya habari viimbe habari za Rostlam Aziz, kuachia ngazi.
Yangeanika magazeti yake ya Habari Coporation, ingeeleweka, lakini magazeti
yote ya Tanzania kuandika juu ya Rostam Aziz, inaacha alama ya kuuliza.
Alivinunua vyombo vyote vya habari viandike habari zake? Alilipia habari yake
kama matangazo kwenye vyombo vyote vya habari? Habari yake ina uzito gani katika maisha ya Mtanzania wa kawaida
anayeshuhudia bei ya sukari na mafuta ya taa ikipanda kila kukicha? Ina maana
kwamba tukio la Rostam Aziz, ndizo habari ambazo watanzania wanataka kusikia?
Tuna watu wengi waliolifanyia taifa letu mambo mengi, tuna watanzania waliokuwa
mawaziri, waliokuwa mabalozi, wanakufa, na hakuna gazeti lolote au chombo
chochote cha habari kinachoandika au kutangaza historia ya maisha yao.
Rostam Aziz ni nani
asimame na kusema; kwa kejeli na kiburi kwamba CCM, chama kinachotawala,
kinaendesha siasa “Uchwara” na siasa za “Ovyo” tusisikie karipio la aina yoyote
kutoka kwa viongozi wa serikali? Ina maana viongozi wetu wanakubali kwamba
wanaendesha siasa “Uchwara”? Wanakubali kwamba wanaendesha siasa za “Ovyo”. Ni
nani huyu mwenye uwezo mkubwa wa kuitukana serikali – na viongozi wakafyata
mkia? Ni wazi tuna tatizo kubwa kama
taifa!
Rostam Aziz, alikuwa
kwenye mtandao; anajua vizuri maana ya kugombania madaraka; anajua jinsi
alivyoendesha mapambano ya kuingia madarakani kwenye uchaguzi wa 2005, ndivyo
na watu wengine wanavyoendesha mapambano ya kuingia madarakani 2015; anashangaa
nini? Yeye na wenzake walianzisha utamaduni wa kuingia madarakani kwa nguvu za
fedha; kura zinanunuliwa, watu wananunuliwa na uongozi unanunuliwa. Katika
mfumo wa kuuuza na kununua kuna kupata faida na kupata hasara; kuna kutajirika
sana na kuna kufilisika; amefilisika ni lazima akubali ukweli huo. Yeye anajua
vizuri kwamba mtandao uliwachafua watu wengi, uliwaumiza watu wengi, ulizima
ndoto za watu wengi. Leo hii anasema vyama vya upinzani na vyombo vya habari
vina ajenga ya kuchafuana na kuunga mkono siasa “Uchwara”. Leo hii anatumia
vyombo vya habari na watu wa Igunga kutuonyesha kwamba ameonewa, kutuonyesha
kwamba watu wa Igunga walimpenda sana? Kama tunayakubali hayo, ndio hivyo tuna
matatizo katika vichwa vyetu; kufikiri kwetu na kuyaona mambo kuna dosari kubwa.
Rostam Aziz, anatwambia kwamba yeye ni
Mfanyabiashara wa kimataifa. Je anafanya biashara gani? Hizo biashara zake
zinalinufaisha taifa letu? Analipa kodi? Tukienda TRA, tutapata takwimu zake za
kulipa kodi? Amewaajili watu wangapi? Mbona hatujamuona kwenye umoja wa wafanya
biashara wa Tanzania? Mbona hatujaona matangazo ya makampuni yake kama
tunavyoona IPP, Precision Air na makampuni mengine mengi yanayotangaza biashara
zake kwenye maonyesho ya biashara kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere kama
yaliyofungwa hivi majuzi?
Tunachokijua ni kwamba
amekuwa akitajwa kwenye kashifa zote za ufisadi ndani ya taifa letu. Ametajwa kwenye EPA na kampuni yake ya
Kagoda, ametajwa kwenye Richmond na Dowans. Kwa nini atajwe yeye? Ni kuonewa?
Ni kuonewa wivu? Yeye ni nani kiasi aonewe na kuhusishwa na kila aina ya
ufisadi? Hawezi kukana uhusiano wake wa karibu na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,
hawezi kukana uhusiano wake wa karibu na Rais Dkt Jakaya Kikwete, hawezi kukana
uhusiano wake na Mheshimiwa Edward Lowassa. Hawezi kukana uhusiano wake wa
karibu na chama chake cha CCM; na kama hiyo ni kweli, hawezi pia kukana yale
yote anayohusishwa nayo.
Rostam Azizi, anasema
siasa “Uchwara” zimevuruga biashara zake na kuigusa familia yake. Lakini kwenye
vyombo vya habari tunamshuhudia
akisimama peke yake na wanachama wa CCM wa Igunga bila familia yake kuwa upande
wake wa kulia. Hiyo familia yake iko wapi kama hatuioni Igunga kwenye Jimbo
lake la uchaguzi, itakuwa wapi? Na sisi tunaendelea kumlilia mzalendo huyu
ambaye familia yake hatuioni na hatuna uhakika kama familia hii inashiriki na
kuguswa na hali yetu ya maisha? Ndo maana kwa maoni yangu ninaona tuna tatizo
kubwa kama taifa! Tunapumbazwa na kukubali kupumbazwa!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment