TULIYATABIRI NA SASA
YAMETIMIA: KANALI FABIAN MASAWE NI MKUU WA MKOA WA KAGERA.
Baada ya uchaguzi mkuu
wa 2010, niliandika makala juu ya vurugu zilizotokea Karagwe na hatimaye Tume
ya Uchaguzi kumtangaza mbunge wa CCM mshindi kinyume kabisa na matarajio ya
wapiga kura wa Jimbo la Karagwe. Kwa faida ya wale ambao pengine hawakupata
kuisoma makala hiyo, na kwa vile yale niliyoyatabiri ya Mkuu wa Wilaya
kuzawadia Ukuu wa mkoa kwa kuhakikisha
majimbo yote ya Wilaya ya Karagwe, yanabaki CCM yametokea, narudia sehemu ya
makala hiyo:
“Naandika makala hii
kama wito kwa wapenda amani, demokrasia,
na watu wenye busara na hekima kushirikiana pamoja kulaani kitendo kilichotokea kule Karagwe cha jeshi la
polisi kuwapiga mabomu na risasi za moto wananchi waliokusanyika kwenye ofisi
ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karagwe, kusubiri majibu ya kura za mbunge wao.
Watu waliumizwa, walitishwa na wengine wamelazwa hospitali. Mbaya zaidi matokeo
ya uchaguzi mkuu yalitangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Haiwezekani
mwakilishi wa wananchi kutangazwa chini ya ulinzi mkali wa polisi. Hili ni
jambo la kulaani na kuonya kwamba hili halivumiliki. Viongozi wa dini wasikae
kimya, wajitokeza na kulaani wazi wazi, jinsi tulivyoshuhudia wakijitokeza
kukemea udini katika uchaguzi Mkuu, ndivyo hivyo hivyo wajitokeze na kukemea
serikali kutumia vyombo vya dola kupora haki ya wananchi ya kujichagulia
mwakilishi wampendaye.
“Watu wamepigwa mabomu
na risasi za moto na wengine hadi leo hii wako hospitali. Serikali imetumia
jeshi la polisi kushinikiza Tume ya Uchaguzi katika Jimbo la Karagwe,
kumtangaza mshindi wa CCM Bwana Gosbert Blandes. Wananchi, waliopiga kura
walikusanyika kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa wilaya ya Karagwe, baada ya kuitwa
kusikiliza matokeo. Na kufuatana na watu walivyopiga kura, walikuwa na imani ya
kutangazwa mgombea wa upinzani. Kwa kuogopa hilo Serikali iliagiza jeshi la
polisi kutoka mkoani Bukoba , kuja Kayanga, kuwatisha na kuwatawanya wananchi waliokuwa
wakisubiri matokeo. Na mbaya zaidi ni kwamba baada ya kuwatawanya wananchi hao,
jeshi la polisi lilivuka mipaka na kuingia sokoni Kayanga na kuwapiga mabomu ya
machozi watu waliokuwa sokoni wakijifanyia shughuli zao. Ni unyama kama
tunaoushuhudia kwenye nchi zinazotawaliwa kidikteta.
“Habari tulizozipata
kutoka Karagwe, ni kwamba baada ya kuwatawanya watu, kesho yake jeshi la polisi
lilizingira Ofisi ya Mkurugenzi na matokeo ya uchaguzi kutangazwa chini ya
ulinzi mkali. Baada ya matokeo mshindi aliyetangazwa Bwana Gosbert Blandes,
alisindikizwa kwa ulinzi mkali kupanda ndege kuondoka Karagwe, na baada ya siku
moja, alionekana Karagwe, akisindikizwa na polisi kuelekea kijijini kwao. Kwa
nini mwakilishi wa wananchi, asindikizwe kwa ulinzi wa polisi?
“Kuingilia uhuru wa watu
kumchangua mwakilishi wanayempenda ni kitu kisichovumilika. Kama wanavyosema
watu wa Karagwe, kuingilia uhuru wa uchaguzi wao ni sawa na kuibaka demokrasia.
Wananchi hawa wameporwa haki yao na
jambo hili ni la kupigia kelele. Ni jambo la kulaani. Watu wa Karagwe wana
matatizo chungu mbovu hivyo wanahitaji mwakilishi wa kuweza kuyatambua matatizo
yao na kuyawasilisha Bungeni. Karagwe kuna matatizo ya barabara na hasa kipindi
cha mvua, kuna matatizo ya kutokuwa na dawa kwenye vituo vya afya, kuna shida
ya kutokuwa na walimu kwenye sekondari za kata, kuna tatizo la bei ya Kahawa
kuendelea kushuka, kuna tatizo la maji kiasi kwamba watu wanasafiri zaidi ya
kilomita kumi kutafuta maji, kuna tatizo la kusambaza umeme vijijini, kuna tatizo
la nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari, kuna tatizo la ujenzi wa
nyumba bora na za kisasa, Wabunge waliotangulia walishindwa kuwasaidia watu
kupunguza matatizo hayo. Hata mbunge huyu aliyetangazwa kwa mtutu wa bunduki,
kwa kipindi alichokaa Bunge, ameshindwa
kuyawasilisha matatizo ya Karagwe. Alisikika Bungeni, wakati Tembo walipoivamia
Karagwe. Vinginevyo akiwa Bungeni anajielekeza kwenye matatizo ya Jimbo la
Ubungo maana yeye na familia yake wanaishi Ubungo. Watoto wake hawasomi kwenye
sekondari za kata na mke wake hafahamu matatizo ya maji wanayoyapata wanawake wenzake wa kule Karagwe.
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita Bwana Gosbert Blandes, hakuonyesha kuguswa na matatizo ya Karagwe. Hata kwenye kura za maoni ndani ya chama cha CCM ilijionyesha wazi kwamba wanachama wenzake hawakuridhishwa na utendaji wake, alifanikiwa kupita kwa mbinu na kutumia fedha kuwahonga wapiga kura. Kuna ushahidi wa kuaminika kwamba hata uchaguzi mkuu wana CCM walio wengi hawakumpigia kura Bwana Blandes, walifuata wito wa “Usichague chama, mchague mtu” kwa vile watu wa Karagwe wana hamu ya maendeleo baada ya kuachwa nyuma kwa miaka mingi, walikuwa na hamu ya kumchagua mbunge wa kusukuma mbele maendeleo ya Jimbo lao bila kuangalia anatoka chama gani.
“Uchaguzi umekwisha na
tutaanza kusikia majigambo ya CCM kwamba wameshinda kwa kishindo. Majivuno haya
yana msingi gani wakati majimbo mengine kama Karagwe, ushindi umelazimishwa kwa
mtutu wa bunduki? Inawezekana hili limetokea maeneo mengi, maana kila jimbo lililochelewesha
matokeo, mshindi ameibuka kuwa wa chama cha upinzani. Kama mwelekeo ni “ Hakuna
aliyeshinda na aliyeshindwa” na ule unafiki wa “Ushindi ni wa watanzania wote”
majigambo ya ushindi wa kishindo
yanatoka wapi? Mipango ya kujipanga upya ili kuyakomboa majimbo yaliyonyakuliwa
na wapinzani yanatoka wapi? Kama si kugombania fito kwa nini tusijifunze sote
kukubali kushindwa?
Kuna uzushi mwingine
tunaousikia, au ni uvumi? Kwamba wakuu wa wilaya wamepewa ahadi ya kupandishwa
kuwa wakuu wa mikoa kama watahakikisha majimbo katika wilaya zao hayachukuliwi na wapinzani. Hivyo ni kazi
yao kufanya wawezavyo ili CCM ipate ushindi hata kama kura zinasema vinginevyo.
Hili likitokea kwa Karagwe, kwamba watu wameporwa haki yao ya kumchagua
mwakilishi wanayempenda, wamepigwa mabomu na kuumizwa ili Mkuu wa wilaya apate
Ukuu wa mkoa, laana hii itamwandama huyu mkuu wa Wilaya ya Karagwe hadi vizazi
vijavyo”
Wakati nikiandika makala
hiyo sote tulifikiria ni uzushi au uvumi tu, maana Rais wa nchi anayewapenda
watu wake, hawezi kukubali kuzima uhuru wao wa kuchagua kwa kumpandisha mtu
cheo. Kumbe haukuwa uzushi wala uvumi ni
ukweli ,maana sote tumeshuhudia aliyekuwa Mkuu wa wilaya wakati wa
uchaguzi Mkuu wa 2010, Kanali Fabian Masawe, ameteuliwa kuwa mkuu wa mkoa, na
kama matusi vile kwa watu wa Karagwe, ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkowa wa Kagera,
ili ahakikishe hakuna upinzani mkoa wa Kagera.
Hapana shaka kwamba watu
wa Karagwe, watakuwa wameliona hili; Kanali Masawe, amewatumia kupanda cheo.
Aliuzika uhuru wao wa kujichagulia mtu wanayemtaka, ili yeye afufuke akiwa na
cheo kikubwa na labda baada ya kuhakikisha ameua kabisa upinzani Mkoani Kagera,
apande zaidi ya hapo? Ni wakati wa watu wa Karagwe kusema hapana!: Wasimame
pamoja na kusema: Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumeibiwa kura zetu kiasi cha
kutosha, tumeporwa ushindi wetu kiasi cha kutosha, sasa tunataka mapinduzi!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment