TAMASHA LA KUMI LA
JINSIA: MAFANIKIO NA CHANGAMOTO.
Tamasha la kumi la Jinsia, lililofunguliwa tarehe
13.9.2011 na kufungwa tarehe 16.9.2011 kwenye viwanja vya TGNP- Mabibo
Dar-es-Salaam, limefanikiwa kwa kiasi kikubwa likiwa limeibua changamoto nyingi
pia. Tofauti na matamasha mengine yaliyotangulia; tamasha hili lilikuwa ni la
kumi na limefanyika wakati tunasherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu. Hivyo
lilikuwa tamasha la kipekee.
Upekee wa tamasha hili
haukujikita tu katika kusherehekea miaka kumi ya tamasha na miaka hamsini ya
uhuru wa taifa letu, bali hata muundo wake ulikuwa wa kipekee: Tumezoea kuwa na
wageni rasmi kwenye sherehe zetu, na mara zote wageni hawa ni viongozi wa
serikali, viongozi wa kidini na viongozi wa mashirika. Tamasha la mwaka huu,
wageni rasmi walikuwa ni wananchi kutoka pembezoni. Wanawake na wanaume kutoka
pembezoni, kutoka vijijini ndio walikuwa wageni rasmi. Hawa ndio walioikalia
meza kuu, hawa ndio walionekana na kusikika kwenye vyombo vya habari. Sauti zao
zilisikika na kutoa ushuhuda kwamba Tamasha la jinsia ni Jukwaa huru la kila
mtu hata na wale walio pembezoni ambao
sauti zao hazisikiki katika mfumo wetu uliozoeleka. Sauti za wanawake
wanaoteswa na kunyanyaswa na kunyima fursa ya kumiliki rasilimali za taifa lao,
sauti za wafanyakazi wa majumbani, sauti za wananchi wanaoporwa ardhi yao,
kilio cha watanzania cha kutaka katiba mpya, sauti ya mashoga wanaotaka haki
zao za msingi ziingizwe kwenye katiba. Kuzipatia nafasi sauti za wale walio
pembezoni ni mafanikio makubwa ya Tamasha la kumi la jinsia.
Mada kuu ya mwaka huu
ilikuwa ni “ Ardhi, nguvu kazi na Maisha endelevu”, na mchokoza mada hii
alikuwa ni Profesa Dzodzi Tsikata kutoka Chuo Kikuu cha Ghana, huyu ni mwanaharakati
na mtetezi wa haki ardhi wa siku nyingi. Akichokoza mada hii iliyogusa hisia ya
washiriki wote na kuibua tatizo sugu la watanzania, alisema
“ Haijalishi unaongelea ukiwa ncha ipi ya
kidunia, iwe ni kaskazini au kusini mwa dunia, wale ambao mtaji wao ni guvu
kazi ndio wanaoathirika zaidi kwa kuiishi katika hali duni ambayo imekuwa
sehemu ya maisha yao. Wakati ambapo wamiliki wa mitaji mikubwa wamepata ulinzi
wa dhamana za mikopo ya kibenki na vyombo vingine vya kifedha, wafanyakazi
wamekosa uhakika wa ajira endelevu, kukosa ajira zenye hadhi, na kupoteza
makazi hifadhi ya jamii ya kudumu. Kiwango cha tatizo hili kwa ujumla wake
kinahatarisha maendeleo na demokrasia iliyopo”
Tatizo sugu la
watanzania lililojitokeza kwa nguvu kubwa kwenye tamasha hili na kuonyesha wazi
dalili za vurugu na machafuko siku za mbeleni kama hekima, busara na uzalendo
vitaendelea kuwa mbali na watanzania ni Ardhi na uwekezaji wa kigeni unaokuja
kwa kasi ya kutisha. Kilio cha uporaji wa ardhi kililitawala jukwaa la jinsia. Mchokoza
mada, Profesa Dzodzi Tsikata, alisema
“ Changamoto kubwa
inayowakabili wanawake katika ngazi ya jamii kote, mijini na vijijini, ni
kutokuwa na uhakika wa kufikia rasilimali muhimu kama vile ardhi, kunyonywa na
kunyanyaswa katika mahusiano ya ajira, mitaji na teknolojia ili kufanikisha
ndoto yao ya kuishi maisha bora. Changamoto nyingine zinahusiana na sera za
kiuchumi ambazo haziwasaidii, sera dhaifu za –kijamii, na kukosekana kwa
jitihada madhubuti katika kushughulikia athari za maisha duni. Changamoto hizi
zinafanya harakati za mapambano haya kuwa ngumu na hivyo kuendelea kufukarisha
wananchi kizazi hata kizazi”.
Ujumbe mzito ulitolewa
na wanawake kutoka Loliondo:
“ Ardhi ni uhai. Wanatufukuza kwenye ardhi
yetu, tutawazalia wapi watoto wetu? Hatuondoki
kwenye ardhi yetu liwalo na liwe” walisema akinamama hawa kutoka Loliondo.
Ushuhuda wa Loliondo unatia simanzi na kuzua maswali juu ya nia ya serikali
yetu; ukitilia maanani kwamba pamoja na unyama uliofanyika kule Loliondo, ardhi
iliyoporwa na wawekezaji ina bango linaoonyesha kwamba ardhi hiyo ni mali ya
watu wengine na ni kama nchi ndani ya nchi
“Hadi leo hii zimeundwa
zaidi ya tume 13 kushughulikia swala la Loliondo, la kushangaza ni kwamba tume
zote hizi haziweki ripoti zake wazi. Anayepewa ripoti ni mwekezaji, lakini
wananchi wanaachwa gizani. Serikali inawalinda na kuwatetea wawekezaji na
kuwatelekeza wananchi wake” Alisema mama kutoka Loliondo
Inasikitisha
tunapoelekea kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu, watu bado wananyanyaswa
kwenye ardhi yao. Mapendekezo ya wanawake wa Loliondo ni kwamba wakati umefika wa kuhakikishiwa usalama wao na kulindwa
na serikali yao, washirikishwe katika kuandika katiba mpya, wapewe fursa ya
kuitumia ardhi kwa maisha yao ya kila siku, maana bila ardhi hakuna maisha; na
kwamba anapokuja mwekezaji aje kwa unyenyekevu mkubwa, maana ardhi ni yao,
akija kwa mabavu wako tayari kupambana naye, maana sasa wamechoka. Hawataki
kuwa wakimbizi kwenye ardhi yao.
Martha Sumaye kutoka
mkoani Manyara alieleza kwamba: “Hivi
sasa kuna wanawake wanaoishi porini baada ya kuamua kuandamana kushinikiza
wakulima kutoka katika eneo la ziwa
Basutu. wakulima wamevamia eneo la wafugaji na
viongozi wa serikali wamekaa kimya juu ya mgogoro huo ambao unawaathiri
zaidi kina mama na watoto kwani hivi sasa hawana sehemu ya kuchota maji kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani”
Emmiliana Kimaro,
alielezea jinsi wanakijiji wanaoishi katika Msitu wa West Kilimanjaro eneo la
Ngaranairobi Kata ya Nduma, walivyotolewa kwenye maeneo yao na ardhi hiyo
akapewa mwekezaji “Kitendo
kilichofanywa na serikali kuchukua eneo la msitu huo wakati ndani yake kulikuwa
na wakazi wa kudumu bila kuwatafutia njia mbadala ya kuwahamishia wanakijiji
hao, ni ukatili uliovuka mipaka”. Alisema bi Kimaro na kuongeza
“Serikali ilitangaza
kuwa wanakijiji wa Ngaranairobi tumepatiwa ardhi ni uongo, waliomilikishwa ardhi na serikali ni
wanakijiji wa Ngurushani, na wengi wao ni wazee na ardhi waliyokabidhiwa ni
vipande vidogo. Naongea kwa masikitiko pia naomba mtandao huu unilinde kwani
kufichua siri iliyofichwa na serikali kwa muda lolote laweza kutokea hata hivyo
ukweli utabaki pale pale lazima kilio chetu jamii ikifahamu” alisisitiza Bi
Kimaro.
Ushuhuda kutoka Morogoro ni kwamba Serikali inapora ardhi na kuwagawia
wakoloni! Na kwamba sasa hivi ardhi imegeuka kuwa biashara kama ilivyo biashara
ya nguo au biashara nyingineyo. Sehemu za Mikese- Morogoro, ardhi imemegwa na
wananchi wamefukuzwa kwenye makao yao ili ardhi hiyo agawiwe Mwekezaji.
Aidha Anna Louchiro
kutoka Kilosa alieleza kuwa ni dhahiri watendaji wa serikali walio wengi
wamekuwa mstari wa mbele katika kutumia vibaya madaraka waliyopewa na hivyo
kusababisha migogoro mingi ya ardhi nchini.
Ushuhuda kutoka Ruvuma,
ni kwamba watu wanarubuniwa kutoa ardhi yao bure, kumbe baadaye serikali
inaiuza ardhi hiyo kwa bei kubwa.
Alex Japhet kutoka
Ruvuma alieleza kwamba sheria za ardhi ni dhaifu na hazina meno na hivyo
kuitaka serikali kuziboresha na kuzisimamia ipasavyo kwa maslahi ya Watanzania
wote.
Ushuhuda kutoka Mwanza,
ni kwamba ili kupata kiwanja mjini ni lazima kulipia fomu kwa shilingi 50 elfu,
na viwanja vyenyewe bei yake ni milioni tatu, tano hadi kumi. Swali ni je mtu
wa kawaida anaweza kupata kiwanja? Au
viwanja ni kwa ajili ya watu wenye fedha?
Margerth Ogongo,
mwanaharakati kutoka Zimbabwe, alielezea mapambano ya ardhi yanayoendelea
Zimbabwe na kuelezea jinsi walowezi walivyonunua ardhi kwa pesa kidogo,
walinunua eka moja kwa shilingi moja. Kwa njia hii waliweza kujilimbikizia
ardhi. Baada ya makubaliano ya kugawana ardhi kwa njia ya amani kushindikana,
walowezi walikataa kupunguza ardhi yao kuwapatia wananchi, matokeo yake ni
kwamba wananchi walikasirika na kuamua kuyavamia mashamba ya walowezi. Alitoa
ushauri wa wanawake wa Tanzania kusimama kidete kutetea ardhi, maana ni haki ya
kila mtu kuwa na ardhi, ili alime na kupata chakula na ili ardhi hiyo iyalinde
na kuyatunza maisha yake.
Ujumbe uliojitokeza
kwenye mada hii ni kwamba wananchi wamechoshwa na uporwaji wa ardhi unaoendelea
na sasa hivi wako tayari kwa lolote. Kama serikali haisikilizi na wabunge
wanakwenda kulala Bungeni, basi wananchi watahakikisha wanailinda ardhi yao kwa
gharama yoyote ile.
Ajira majumbani
ilijitokeza kuwa ni changamoto kwa washiriki wa tamasha la kumi; hoja
iliyojitokeza ni kwamba kazi za nyumbani si mbaya, tatizo linalojitokeza ni
kuwanyanyasa mabinti wanaoajiriwa kufanya kazi za nyumbani, kuwalipa fedha
kidogo na kuwaajiri watoto wadogo ambao hawana uzoefu wa kazi za nyumbani, kama
kutunza nyumba, kuwalea watoto na shughuli nyingine za siku kwa siku ndani ya
familia.
Michango ya mawazo
kutoka kwa washiriki ni kwamba wasichana wanaofanya kazi za ndani wanatendewa
mambo mabaya na wakati mwingine wanabakwa na kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Bwana Masege Mandoma, kutoka shirika la KIVULINI la Mwanza, alitoa ushuhuda
kwamba watoto wa kike wanaletwa Mwanza kufanya kazi za ndani na mawakala. Ni
kwamba mawakala hawa wanapanga na wazazi wao kwamba mshahara wote utakuwa
unatumwa nyumbani. Matokeo yake watoto hawa wanafanya kazi bila malipo. Pamoja
na mateso yote wanayokubana nayo kwenye kazi za majumbani, hawapati chochote
zaidi ya kupigwa, kulala njaa, kufanya kazi masaa mengi bila kupumzika na
wakati mwingine kufanyiwa vitendo vya kudhalilishwa. Kuna ushahidi wa binti wa
miaka kumi na miwili aliyepachikwa mimba wakati akifanya kazi majumbani.
Prisca Haule kutoka
Ruvuma, alitoa ushuhuda wa zaidi ya watoto wa kike 50 kuuzwa Msumbiji, ambako
pamoja na kazi za majumbani wanafanya kazi ya kupigwa picha za uchi. Serikali
inafahamu mtandao huu wa watu wanaowanunua watoto hawa kwa shilingi elfu
hamsini kila kichwa, lakini hakuna linalofanyika kukomesha biashara hii haramu.
Pia kuna ushuhuda
uliotolewa kwamba wanawake wanaofanya biashara ya kuwakusanya watoto wa kike
kutoka mikoani na kuwaleta kuwauza Dar-es-Salaam, ili wafanye kazi za ndani,
kuuza kwenye baa na kufanya bishara ya ngono wanafahamika, lakini serikali
haichukui hatua ya kukomesha biashara hiyo.
Changamoto iliyojitokeza
ni kwamba hata baadhi ya washiriki wa
tamasha wanawatumikisha watoto wa kike kwenye familia zao. Na mbaya
zaidi ni kwamba wazazi wanashirikiana na mawakala kuwauza watoto wao. Hii ni
changamoto kubwa kwa wanaharakati ambao wanajiweka mstari wa mbele kutetea haki
za binadamu na kupinga ajira kwa watoto, lakini bado wao wanafanya hivyo.
Nini kifanyike kuzuia
unyanyasaji huu: Msemaji kutoka Msumbiji, alitoa mfano wa nchi yake, kwamba wao
wameamua kuanzisha harakati za kumkomboa mtoto wa kike kwa kumpatia elimu. Wana
msemo: “Kumwelimisha mtoto wa kike ni kulielimisha taifa zima” Hata wale ambao
hawafanikiwi kusoma hadi vyuoni, wanawekwa kwenye makundi na kupatiwa mafunzo
ya kutetea haki zao. Anasema mfumo huu umeanza kupunguza wimbi la wasichana
wanaofanya kazi majumbani na unyanyasaji umepungua, maana hata kama msichana akifanya kazi za ndani anakuwa
anafahamu kazi zake vizuri na kutambua haki zake.
Imependekezwa kwamba
Tanzania, ni nchi tajiri, hivyo itoe elimu bure kwa wasichana. Lakini pia na
wazazi wabadilike, waache tabia ya kuwauza watoto wao. Wavumilie maisha magumu
na wasiwatumie watoto wao kama mitaji. Na wanaharakati wabadilike,
wasiwatumikishe watoto wadogo. Wale wenye watumishi wa ndani wasiwanyanyase:
Ushauri ni kwamba “Mabadiliko yanaanza na mimi ndio yanaenda kwa wengine”
Changamoto nyingine
iliyojitokeza kwenye Jukwaa la jinsia, ni kitendawili cha uchumi wetu kukua kwa
kasi wakati na umasikini ukiongezeka kwa kasi ya kutisha. Kigoda Cha Mwalimu,
waliandaa takwimu na kuelezea kitendawili hiki: Wakati dhahabu inachangia
asilimia 36 kwa mauzo ya nje, inachangia asilimia 3 tu kwa pato la taifa. Mauzo
ya dhahabu, fedha hazirudi ndani ya nchi ili kuendeleza mzunguko wa fedha, bali
zinawekwa kwenye mabenki ya nje na sheria inaruhusu! Na hili ndilo
litakalotokea kwenye uwekezaji wa kilimo unaokuja kwa kasi. Watalima si kwa
kuwalisha watanzania au kukuza uchumi wa Tanzania, bali watalima kuzalisha
chakula cha kuuza nje na fedha hizo zitawekwa kwenye mabenki ya nje.
Swala jingine
lililojitokeza kwa nguvu zote kwenye tamasha ni Katiba. Mchangiaji Magdalena
Rwebangila alisisitiza kwama maswala ya ardhi na mengine yote yanayoleta duku
duku kwa wananchi yaingizwe kwenye katiba. Naye Bwana Deus Kibamba
alitaadharisha “ Sasa hivi tuko kwenye wakati mgumu: Maana dola inawalinda na
kuwakingia kifua wale wenye fedha na wawekezaji badala ya kuwalinda kuwakingia
kifua wananchi wa pembenzoni. Na hii ni hatari kubwa tunapotaka kuandika katiba
mpya. Hivyo kuna haja ya kudai kwa nguvu zote kuingia kwenye mchakato wa
katiba”
Mecy, kutoa Kenya,
alitoa ushuhuda wake kwamba Kenya iliwachukua zaidi ya miaka 25 kutengeneza
katiba mpya.
“ Pamoja na juhudi zote
hizo, machafuko ya 2007, yalichangia kuharakisha upatikanaji wa katiba mpya.
Siwaombei watanzania kufika huko” Alisema bi Mercy na kuongeza “ Jambo la
kujivunia ni kwamba katiba ya sasa ya Kenya, imezingatia haki za wanawake.
Mafanikio hayo yalitokana na wanawake kushinikiza kwa nguvu zote kushiriki
mchakato mzima wa kuandika katiba mpya”.
Ushauri wake ni kwamba
mtandao ndio unasaidia harakati za kuunda katiba mpya, maana mtu mmoja mmoja,
au taasisi moja, au vyama vya siasa na
madhehebu ya dini haviwezi kujitosheleza kutengeneza katiba mpya, ni
lazima kuwepo na mtandao na watanzania wasichoke kuendelea kudai katiba mpya,
na kwamba elimu ya urai itasaidia sana kuchochea madai ya katiba.
Vicensia Shule, mhadhiri
kijana kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alichangia mada ya katiba kwa hisia
kali:
“ Tunasherehekea miaka hamsini ya uongo,
miaka hamsini ya kudanganywa, miaka hamsini ya kudharauliwa. Kwa vile
tumepumbazwa kwa miaka mingi wanaotusikia tunaongea juu katiba, wanatukejeli
kwamba tunataka kuingiza kila kitu kwenye katiba”.
Kwa maoni yake ni kwamba
kwa vile mfumo uliotufikisha hapa ulikuwa unatufundisha uongo na kutudanganya,
ulikuwa ni mfumo wa kutugawanya kiasi cha kunyosheana kidole na kubaguana kwa
rangi zetu, dini zetu, uwezo wetu na makundi yetu, ni lazima sasa tukae chini,
tujadiliane, na kukubaliana ni kitu
gani tunataka.
Mashoga nao walitoa
maoni yao na kutaka haki zao ziingizwe kwenye katiba mpya. Hapana shaka kwamba Jukwaa
la mwaka huu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibua sauti za wananchi walio
pembezoni.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment