TAMASHA LA JINSIA NI JUKWAA HURU LA MAJADILIANO.

Tarehe 13.9.2011, litafunguliwa tamasha la kumi la Jinsia kwenye viwanja vya TGNP Mabibo Dar-es-Salaam na litaendelea hadi tarehe 16.9.2011. Tamasha hili limekuwa na litaendelea kuwa jukwaa huru la majadiliano. Kwa muda mrefu tamasha hili limekuwa likibeba mada kuu ambayo ni : Jinsia, demokrasia na maendeleo. Kila tamasha limekuwa na mada husika kutokana na mada hii kubwa; mwaka huu tamasha litajikita katika kujadilia Ardhi, nguvu kazi na maisha endelevu.

Tamasha hili linafanyika wakati tunasherehekea miaka 50 ya uhuru wetu; wakati ambapo tunashuhudia uporaji wa kutisha wa ardhi yetu, tunashuhudia wawekezaji wa kila aina, lakini pia tunashuhudia makundi mengi ya kutetea uhuru wa  watanzania kuendelea kudhibiti rasilimali zao. Tamasha hili linakuja wakati kuna vuguvugu la kuandika katiba mpya ya taifa letu.

Kwa vile hili ni jukwaa huru , tunategemea watu wengi watajitokeza kujadili na kupanga mikakati ya kuliendeleza taifa letu. Ni wazi mada yenyewe ya ardhi, nguvu kazi na maisha endelevu inalenga kwa kiasi kikubwa kugusia kuboresha  uchumi wa taifa letu la Tanzania.

Ili kuboresha uchumi wetu. Kuna haja kubwa ya kuiboresha kwanza elimu yetu na kuwaandaa vijana wetu waweze kuukabili ulimwengu huu unaobadilika kila siku ya Mungu. Jambo hili linahitaji msimamo wa kitaifa. Ni lazima liwe jambo ambalo litaheshimiwa na wanasiasa wote. Vyama vyote vinavyotengeneza sera na kujiandaa kuingia madarakani ni lazima vizingatie kitu hiki. Bila elimu bora, bila kuwaandaa vijana vizuri ni vigumu kujikwamua kiuchumi. Elimu ipewe kipaumbele na yeyote aliye na nia njema na taifa letu la Tanzania.

Kuna hatari kubwa ya kuwa na taifa dhaifu lenye hali mbaya katika nyanja zote yaani kiuchumi, kisiasa na kijamii endapo kijana wa sasa hakuandaliwa ipasavyo kushika nafasi za kusimamia masuala hayo. Aidha kijana huyu anapaswa kuandaliwa kwa kupewa elimu bora itakayombadilisha fikra na mtazamo wake kimaisha ili kumwezesha kupambana na changamoto muhimu za kimaisha kikanda na kidunia. Haya yote yanafanikiwa endapo tu kijana ataandaliwa kupata elimu.

Serikali iliyo madarakani na zile zilizopita zimejitahidi kiasi Fulani kufuata katiba kuhusu elimu: “ Serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa ya kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi kati ngazi zote za shule na vyuo vingine vya mafunzo” (Katiba, ibara ya 11(3) ).
 Tatizo linalojitokeza ni mfumo na ubora wa elimu inayotolewa. Baada ya uhuru elimu iliendelea kutolewa kwa kufuata mfumo wa kikoloni. Wakati wa ukoloni watu walielimishwa kuwatumikia wakoloni. Ilikuwa inaandaliwa nguvu kazi. Hawakuwa na haja ya kuandaa watafiti, wagunduzi na watu wa kuliendeleza taifa letu. Mitaala iliyotengenezwa ilikuwa ikilenga kumfundisha mtu katika mtindo wa kukariri tu. Au kufanya kazi kama roboti.

Kutokana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia yanayojitokeza hivi sasa kijana ndiye mwenye nafasi kubwa ya kujifunza na kuweza kuonyesha ujuzi wake katika taifa hivyo kuleta maendeleo nchini na uvumbuzi katika nyanja mbali mbali. Mambo ya kujiuliza ni kwamba je, kijana huyu ana nafasi gani ya kupata ujuzi, kuuendeleza na kuutumia? Mitaala yetu ya shule za msingi na sekondari inasaidiaje kumwandaa kijana kupambana na hali ya sasa hivi?

Ni bahati mbaya kwamba mpaka leo hii mitaala yetu yote bado ni kama ile ya wakati wa wakoloni! Mfumo bado ni ule ule wa kumfundisha mtu kukariri. Kinachohitajika kwa sasa hivi ni kutengeneza mitaala mipya ambayo italenga katika kutoa elimu ya kumkomboa mtu kifikira mtu akawa na uwezo wa kuhoji na kufanya utafiti hadi kuelekea uvumbuzi wa vitu mbali mba na kuchangia kukua haraka kwa uchumi na maendeleo ya taifa letu la Tanzania.

Bado kuna uhaba wa walimu na maandalizi yao siyo mazuri. Pia walimu hawana motisha wa kufundisha maana walio wengi wanafanya kazi katika mazingira magumu na wakati mwingine mishahara yao inacheleweshwa sana. Shule nyingi majengo yake yamezeeka. Ingawa wakati huu serikali inafanya jitihada ya kukarabati mashule kupitia mpango wake wa (MMEM): Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Misingi, bado kazi ni kubwa na katika maeneo mengine pesa za mradi huu zimepotea. Na mpango mzima hauonyeshi jinsi ya kujiendeleza. Majengo ni lazima kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara.

Elimu ya Tanzania ilianza kuingia matatani mnamo mwaka 1974, ilipoamuliwa kwamba kufikia mwaka 1977 kila mtoto mwenye umri kati miaka 7 hadi 13 awe ameanza shule ya msingi. Mfumo huu wa elimu uliitwa (UPE) Universal Primary Education. Mwanzoni mfumo ulionyesha mafanikio makubwa hasa kwa wingi wa idadi ya watoto wa kuanza shule ya msingi. Kati ya mwaka 1974 hadi 1978 idadi ya watoto wa kuanza darasa la kwanza iliongezeka kwa kiasi cha asilimia 254%, kutoka watoto 248,000 hadi 878,321. idadi ya watoto waliokuwa katika shule ya msingi ilipanda kutoka 1,228,886 mwaka 1974 na kufikia kilele cha 3,553,144 mwaka 1983. wakati huo Tanzania ilifikia asilimia 98% ya kuandikisha watoto wa kuanza darasa la kwanza.

Vijana waliomaliza darasa la saba walichukuliwa haraka katika vyuo vya ualimu. Walipewa mafunzo ya haraka na kurudi kufundisha. Walimu hawa wa UPE walichangia kiasi kikubwa cha kuzorota kwa elimu katika taifa letu. Sasa baada ya zaidi ya miaka 20 tangu mfumo huo ulipoanzishwa walimu watatu kati ya kumi ndio waliofuata mafunzo halisi ya ualimu. Walimu wa UPE ni zaidi ya asilimia 47% ya walimu wote wa Tanzania. Ingawa sasa hivi wanajiendeleza lakini hawafanikiwi kushinda mitihani kwa kiwango kinachotakiwa.

Kosa la kuwaandaa walimu aina ya UPE, limefanyika tena. Vyuo vya walimu hivi sasa vimejaa vijana ambao wengine wameghushi vyeti na wengine walikuwa wanafanya kazi kwenye mabaa. Matokeo yake ni kuzalisha walimu wengi wasio na uwezo wa kufundisha. Elimu yetu itaendelea kushuka. Watoto wanamaliza darasa la saba bila kujua kitu. Wengine hawawezi kuandika jina lao. Ni ndoto kwamba hali ilivyo sasa hivi mtoto aweze kujiajiri baada ya kumaliza darasa la saba na sekondari. Elimu yetu haiwezi kutusaidia kujenga Uchumi wa nchi yetu.

Wataalamu wanatuelezea kwamba Uchumi wa Tanzania umekuwa ukibadilika mwaka hadi mwaka. Kubadilika huku kwa uchumi kumetokana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakijitokeza ndani ya nchi na nchi nyingine duniani. Tanzania sio kisiwa katika dunia hii ambacho kitapitwa na mabadiliko hayo, hivyo nayo imeathiriwa kwa namna moja au nyingine.

Tunapozungumzia uchumi tuna maana ya mfumo mzima wa uzalishaji mali, matumizi (consumption) na ugawaji/usambazaji wa mazao hayo pamoja na huduma. Uchumi unazungumzia pia kudhibiti rasilimali, kugharamia mapato na matumizi ya jamii, biashara na viwanda. Kwa maana hiyo uchumi wa dunia umekuwa unabadilika hasa kwa kuongezeka kwa ushindani katika masoko ya dunia pamoja na kuongezeka kwa kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Nchi ambazo zitashindwa kwenda sambamba na mabadiliko hayo zina hatari ya kuathiriwa vibaya na kuzidi kuachwa nyuma kimaendeleo.

Tushiriki tamasha hili la jinsia ili tuibue yale ya kutusaidia kufikia  maendeleo endelevu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment