SHEREHE
ZA MIAKA 50 YA UHURU WETU
Wakati tunajiandaa kusherehekea miaka 50 ya uhuru
wa taifa letu, nimekuwa nikitafakari tangazo la Haki Elimu, lililokuwa likirushwa kwenye luninga na
kwenye redio. Tangazo hili ambalo
lilikuwa na maneno tulia,
tafakari na chukua hatua, lilisumbua sana akili yangu. Inawezekana tangazo hili
lilisumbua pia akili ya watanzania wengine. Tangazo hili lilionyesha au
lilieleza kwamba kufuatana na takwimu za kitaalam na kiuchumi, uchumi wetu
unaendelea, na Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini hali hali
halisi inaonyesha maisha duni ya wananchi. Kwenye luninga zilionyeshwa picha za
nyumba mbovu, watu wenye afya na lishe mbaya, wamevaa nguo zilizochanika,
wamekata tamaa na kuduwaa kwa kusikia habari za maendeleo ya taifa lao. Mzee
Small, mwigizaji wa siku nyingi, alionekana akishangaa kwa kulinganisha yale
yanayotangazwa na redio kwamba uchumi unaendelea na hali halisi. Tangazo hili
ni muhimu sana wakati huu tunapoandaa sherehe za miaka 50 ya uhuru wetu. Ni
vigumu kukataa ukweli kwamba baada ya miaka 50 ya uhuru watanzania wengi bado
wanaishi maisha duni.
Mwaka huu mzima utakuwa ni mwaka wa kusherehekea.
Na kusema kweli sherehe zimeanza na
shughuli nyingine nyingi zimeandaliwa ili kuanza mapema kuonyesha yale
tuliyoyafanikisha ndani ya kipindi hiki kirefu cha miaka 50. Taasisi mbali
mbali zimeanza kuonyesha mafanikio ya miaka hamsini.
Ukweli kwamba watanzania wengi wanaishi maisha
duni, si kulenga kusema kwamba hakuna kilichofanyika baada ya uhuru. Wenye
mawazo finyu wanafikiri kwamba kuonyesha dosari za serikali yetu ni upinzani na
kwamba tunalenga kupotosha umma wa watanzania kwamba hakuna kilichofanyika
miaka hamsini iliyopita. Yamefanyika
mengi na bado mengine yanafanyika. Hoja inayojengwa hapa ni kwamba
ukilinganisha miaka hamsini na yale yaliyofanyika hadi leo, na hasa kwa
kuangalia maendeleo ya mtu mmoja mmoja, ni sawa na hakuna! Lakini hata
ukiangalia maendeleo ya taifa kwa ujumla,
bado kuna matatizo makubwa. Hatujafanikiwa kujijenga na kusimama imara
kwa kiburi kama taifa lililo huru na lenye rasilimali nyingi. Bado tunaomba
omba na kuamini kwamba kuna watu sehemu Fulani ya dunia hii watakuja na
kutuleta maendeleo. Tunasahau kwamba ili tuendelee ni lazima sisi wenyewe
tufanye kazi kwa bidii.
Sote tunaisubiri siku hiyo kwa hamu, siku ambayo taifa letu
lilipata uhuru miaka hamsini iliyopita.
Wengi wa walioshuhudia tukio hili miaka hamsini iliyopita ni marehemu. Wazee wa
leo ndo walikuwa vijana wakati tunapata uhuru. Tunasubiri kucheza, kuimba,
kunywa na kula wakati wa kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu. Lakini, je ni kweli kwamba uhuru wetu umekuwa uhuru wa kweli, uhuru wa
neema kwa kila Mtanzania, uhuru wa kuleta maisha bora na ukombozi wa kila
Mtanzania? Uhuru wa kujiamria mambo yetu sisi wenyewe? Je, si kweli kama
tangazo la Haki Elimu, linavyoonyesha kwamba kwa nje yanaonekana maendeleo,
lakini kwa ndani watu wanaishi maisha duni?
Kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana baada
ya uhuru. Hata na kule kuwa huru ni
mafanikio tosha. Lakini mafanikio ya kutuwezesha kufanya sherehe kubwa ya kula,
kunywa na kucheza, yanatiliwa mashaka. Taifa letu limeweza kudumisha utulivu na
amani, tumejenga mshikamano na aina Fulani ya uzalendo. Taifa letu limekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha na nchi nyingine za Afrika zinapata uhuru wake,
haya ni mafanikio makubwa sana .Mashule yamejengwa, mahospitali na huduma
nyingi za kijamii. Pamoja na mafanikio hayo yote, bado kuna ukweli unaosumbua,
kwamba baadhi ya watanzania bado wanaishi maisha duni. Na namba ya wale
wanaoishi maisha duni ni kubwa kuliko ile ya wenye neema!
Kwanini takwimu zinaonyesha uchumi kupiga hatua
wakati hali halisi inaonyesha kinyume? Kwa nini watanzania wanaishi maisha duni, wakati nchi yetu ina utajiri mkubwa?
Tatizo ni nini? Je ni kweli tusherehekee sikukuu hii ya uhuru wetu, au tutulie,
tutafakari na kuchukua hatua? Hatua gani? Elimu? Ukombozi wa fikira? Siasa safi
na uongozi bora? Ni lazima kuna tatizo mahali Fulani, na tatizo hili haliwezi
kutanzuliwa kwa kula kunywa na kucheza ngoma!
Baada ya miaka 50 ya
uhuru wetu, huduma ya maji bado si nzuri. Watanzania wengi hawajui kwamba dunia
ya leo maji yanamfuata mtu, na si mtu kuyafuata maji. Watu bado wanatembea
kilomita zaidi ya kumi kuyafuata maji. Watu hawa hawajui maji ya bomba, hawajui
maji ya ndani ya nyumba. Lakini mbaya zaidi hata na wale walio na maji ya
bomba, bomba hizo hazileti maji! Tunajionea kila siku kwenye vyombo vya habari
uhaba wa maji katika Jiji la Dar-es-Salaam na majiji mengine kama Mwanza,
ambalo siku za hivi karibuni limekumbana na mgawo wa maji.
Miaka 50 ya uhuru imepita na bado kuna watanzania
hawana mwanga nyakati za usiku. Hata bila kuongelea umeme, wako watu hawana
uwezo wa kununua mafuta ya taa! Leo hii wakati bei ya mafuta inapanda kwa
kisingizio cha thamani ya dola kushuka, serikali haina mpango wa kuwasaidia
wananchi kupata huduma ya mafuta ya taa. Wananchi hawa wanatumia mwanga wa jua,
hivyo inawalazimu kupata chakula cha usiku kabla ya jua kuzama, ili waweze
kutumia mwanga wa jua!
Miaka 50 ya uhuru
imepita na bado hakuna kitu hata kimoja ambacho tunakishughulikia vizuri na kwa
kujitosheleza. Hatujaweza kushughulikia kilimo chetu na kujitosheleza kwa
chakula. Tunaimba Kilimo kwanza wakati hakuna mpango wa wazi kueneleza kilimo
cha umwagiliaji. Hatuwezi kuendesha kilimo kwanza kwa kutegemea mvua; tabia
nchi inabadilika na ukame unaishambulia Tanzania. Ili kilimo chetu kifanikiwe
ni lazima kuwa na mfumo wa umwagiliaji unaoaminika. Hatujaweza kuishughulikia
elimu yetu na kuiendesha bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi. Hatujaweza
kuendesha viwanda vyetu na kufanya uvumbuzi mbali mbali. Hatujaweza kuendesha
hospitali zetu bila misaada kutoka nchi za nje. Hatujaweza hata kuendesha
serikali yetu bila kutegemea misaada na ruzuku kutoka nchi za nje. Labda mimi
ni kipofu, lakini ninatafuta ni kitu gani, hata kama ni kile ambacho hakina
kisingizio cha pesa za kigeni, ambacho tunakishughulikia kikamilifu kwa
kujitegemea, ni kipi? Kama hakipo, ni kwa nini tunataka kusherehekea? Kwanini
tunataka kutumia pesa nyingi kula na kunywa, eti tunasherehekea sikukuu ya
uhuru wetu?
Kuna haja ya kutulia,
kutafakari na kuchukua hatua kama tunavyoelezwa na tangazo la Haki Elimu. Kuna
mambo mengi ya kujiuliza juu ya uhuru wetu. Inatosha tu kuwa na uhuru wa
bendera na kuendelea na ukoloni mambo
leo? Inatosha tu kuwa huru na watu kuendelea kuishi maisha duni? Inatosha tu
kuwa huru na kuendeleza mifumo ya kikoloni? Inatosha kuwa huru na kuendelea
kupokea misaada kutoka nchi za nje? Tunaimba utandawazi kwamba dunia imekuwa
kijiji; wenzetu kutoka nchi za magharibi na Amerika wanaingia kwenye kijiji
hiki kwa uhuru bila ya kusumbuliwa,
lakini sisi tukitaka kuingia kwenye kijiji hiki ni lazima kupitia kwenye mchujo
wa hali ya juu. Wakati Afrika inaelekezwa kufungua milango yake yote kwa
kisingizio cha utandawazi; wao wanaifunga milango yao yote kwa kuogopa kwamba
sisi tukiruhusiwa kuogelea kwenye kijiji hiki cha utandawazi tutasambaza
ugaidi.
Mwalimu Nyerere,
alijitahidi sana wakati wa huru kubadilisha mifumo. Alileta falsafa ya Ujamaa
na Kujitegemea na wakati anakaribia kutoka madarakani, alisukuma kwa nguvu zote
demokrasia ya vyama vingi. Wakati Mwalimu, anakazana kuleta falsafa mpya, bado
mifumo mingine ilibaki ni ya kikoloni. Katiba yetu ilifanyiwa marekebisho
kutoka ile ya mkoloni. Bunge letu liliendeshwa na bado linaendeshwa kwa mifumo
ya kikoloni. Rais wa nchi alipewa madaraka makubwa na jambo hili bado
linaendelea. Mfano hadi leo hii Rais, ndiye anayemteua Jaji Mkuu, Rais ndiye
anayeteua Tume ya uchaguzi nk. Mfumo wa
serikali ya kikoloni, ulikuwa umesukwa, kwa namna ya wakoloni kujilinda na
changamoto ya wananchi, ulikuwa ni mfumo wa kuwasaidia kutawala kikoloni,
kutawala bila demokrasia. Baada ya
uhuru, baada ya kumfukuza mkoloni, tulichukua mfumo ule ule wa kujihami,
mfumo ule ule wa kuwaogopa wananchi, mfumo wa kuogopa changamoto za wananchi.
Wakati wa mkoloni,
kufikiri kinyume na serikali ulikuwa ni usaliti. Wale wote waliofikiri kinyume
na serikali ya mkoloni, walionekana kuwa magaidi. Leo hii tuko huru. Hakuna
mkoloni, lakini kuna dalili zote za kutaka watu wote wawe na mawazo yale yale, watu wote wawe wa chama kilele kile,
kinyume na hapo ni usaliti. Tunawezaje kusherehekea kwa pamoja wakati uhuru wa
baadhi ya watanzania unanyimwa pumzi?
Ni kweli tuko huru. Kwa
maana ya kumfukuza mkoloni na kuendesha mambo yetu wenyewe. Lakini kwa maana
yenyewe ya neno Uhuru, bado tuko chini ya mkoloni maana hata mbali na kuishi
maisha duni fikira zetu bado zinatawaliwa. Hili linajionyesha kwenye mijadala
inayoendelea kama ule wa kutumia lugha ya kingeni kufundishia. Watu walio huru
hawawezi kujadili kutumia lugha yao au
kutoitumia! Ukikuta mtu ameweka mjadala wa kuitumia lugha yake au kutoitumia,
utambue kwamba mtu huyo au watu hao wana matatizo mengi kichwani. Mtu huru hawezi
kujivuna kuongea lugha ya kigeni; atajivuna kuongea lugha yake au hata kuongea
lugha za kigeni.
Mbali na baadhi ya
watanzania wanaoishi maisha duni, kuna kundi jingine la watanzania wasioipenda
nchi yao. Watu hawa wanapora mali ya nchi na kuiwekeza nchi za nje, au
wanajilimbikizia wao na familia zao hawa si sehemu ya mafanikio, bali ni sehemu
ya ukoloni mambo leo. Ni dhambi kubwa watu hawa, waporaji wa mali za taifa
kusherehekea pamoja na watanzania wanaoishi maisha duni. Uhuru wa waporaji ni
tofauti na uhuru wa wazalendo walalahoi.
Hili tangazo la Haki Elimu, litusaidie kuona
kwamba, pamoja na uhuru wetu, pamoja na mafanikio yetu, bado kuna mambo mengi
ya msingi ambayo ni lazima kuyashughulikia kama taifa. Yapo mambo mengi ya
kushughulikia ili kuleta uhuru kamili wa taifa letu. Tunahitaji kutulia,
kutafakari na kuchukua hatua
Badala ya kufanya sherehe kubwa na kutumia
pesa nyingi kwa kula na kunywa, ni vyema
watu wakafanya mikutano ya majadiliano. Taifa liingie kwenye
majadiliano. Ni lazima tuangalie sababu inayopelekea watu wengi kuendelea
kuishi maisha duni. Ni wakati mzuri wa kuanza kufikiria kutengeneza katiba mpya
na mifumo mipya inayoendana na Uhuru wetu. Tusherehekee kwa kuzama katika
fikara!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment