SAKATA LA POSHO NI KIPIMA JOTO KWA WABUNGE WETU.
Inawezekana kabisa
kwamba Mheshimiwa Zitto ana ajenda yake binafsi ya kuibua hoja hii ya kufuta posho za wabunge na watumishi
wengine wa serikali; Inawezekana analenga uchaguzi mkuu wa 2015; kwa mwanasiasa
tena kijana kama yeye kuwa na malengo ya mbele si dhambi; na kama ajenda
yenyewe si ya kuliangamiza taifa letu. Lakini pia inawezekana kabisa kwamba
Mheshimiwa Zitto, ana nia njema ya kuibua hoja hii. Si kweli kwamba leo hii
Zitto ameibuka kuwa tajiri kiasi cha kuzikataa posho; anazihitaji posho lakini
ziwe za haki na zisiwe mzigo mkubwa kwa walipa kodi masikini wa Tanzania. Kwa
vile hatuko ndani ya moyo wa Zitto Kabwe, hatuwezi kusema kwa uhakika lile analoliwaza
yeye zaidi ya kuiweka hoja yenyewe kwenye mizani, kuipima, kuijadili na
kuichambua kwa kina. Tuiangalie hoja yenyewe bila kujali aliyeiibua; tuiangalie
hoja yenyewe bila kujali imetoka kambi gani.
Hatuwezi kusema kwamba
hii ni hoja ya Zitto Kabwe na kwamba anaitumia kujitafutia umaarufu, maana
tumeshuhudia sote kwamba hoja hii imeungwa mkono na wabunge wote wa CHADEMA na
baadhi ya wabunge wengine kutoka vyama vingine hata ndani ya CCM. Wabunge
makini wa CCM, wanajua fika kwamba wakicheza na hoja hii wanakwenda na maji;
kwamba haitapitishwa Bungeni ni wazi; maana wabunge wa CCM ni wengi na kwa
utamaduni wao waliojijengea wa kukitanguliza chama chao badala ya kulitanguliza
taifa ni lazima waipinge hoja ya Zitto na kuipitisha bajeti ambayo haina tija kwa
watanzania. Hata hivyo ukweli daima utabaki kuwa ukweli na historia ni mwamuzi
mzuri.
Wengine wanataka
kuipotosha hoja yenyewe. Zitto Kabwe, hajasema kwamba wabunge wasipate mshahara
na posho zao za kuwawezesha kula, kunywa na kulala pale Dodoma; au posho za
kumwezesha mbunge kufanya kazi zake ndani ya jimbo lake. Ugomvi wake ni posho
za nyongeza ambazo mbunge anazipata wakati akitekeleza majukumu yaliyo ndani ya
wajibu wake kama mbunge; majukumu ambayo
ndio yanampatia mshahara wake wa ubunge.
Ugomvi wa Zitto ni posho
wanazozipata watumishi wa serikali wakiwa wanatekeleza majukumu yao. Kwa nini
kwa mfano Mkuu wa Wilaya anapofungua warsha, semina kongamano au shughuli
nyinginezo ndani ya wilaya yake apokee
bahasha? Hiyo posho ni ya nini wakati mkuu huyo wa wilaya anakuwa akifanya kazi
yake ndani ya wilaya yake? Mkuu wa wilaya ana mshahara wake na marupurupu
mengine ndani ya ofisi yake; kwa nini basi aongezewe na posho nyingine
nyingi? Au Katibu mkuu wa wizara anapoendesha
mikutano, warsha au semina ndani ya wizara yake kwa nini apokee bahasha wakati
kazi anazozifanya ni kati ya kazi zinazomfanya apokee mshahara wa Katibu mkuu?
Ipo mifano mingi ya watumishi wa serikali kupokea posho wakati wakifanya kazi
ambazo ni wajibu wao na habari za kuaminika ni kwamba baadhi ya watumishi wa
serikali wanapa posho kubwa zaidi ya mishahara yao .Na baadhi ya posho hizi
zinawekwa kwenye bajeti ya serikali.
Ugonjwa huu wa posho na
bahasha umegeuka kuwa kansa ya taifa letu. Huwezi kuitisha mkutano, hata kama
unahusu maendeleo ya watu wenyewe; ukawapata washiriki wa kutosha kama
hukuandaa posho na bahasha. Inashangaza kuona hata yale mashirika (kutoka
mataifa ya nchi zilizoendelea ya Ulaya na Amerika) ambayo yako mstari wa mbele
kuhimiza maendeleo kuletwa na wananchi wenyewe wanaweka kifungu cha posho na
bahasha kwenye bajeti zao. Serikali yenyewe inaweka bajeti ya posho na bahasha!
Hii ndiyo hoja ya Zitto,
na kusisitizwa na Mheshimiwa Mbowe na watu wengine walio makini kwamba posho
hizi zikishughulikiwa ipasavyo, zikapunguzwa au kufutwa kabisa, serikali
itaokoa zaidi ya trilioni moja inayoweza kuelekezwa kwenye shughuli nyingine za
ujenzi wa taifa letu. Kama nilivyosema mwanzoni mwa makala hii, hoja inaweza
kuwa imelenga sehemu Fulani; umaarufu na mbio za urais wa 2015; vyovyote vile
bado ni hoja ya msingi ambayo ni lazima watanzania wengi wenye uchungu na nchi
yao wataibeba na kuikumbatia. Kama CCM walifikiri CHADEMA ni maandamano na
kuzunguka nchi nzima wakitukana; wamepotea njia. Maana hoja ya posho si ya
kubeza; bila wabunge wote kuchukua hatua hiki ni kitanzi kitakachowakumba
wengi.
Kwenye bajeti
tuliyosomewa juzi, tumesikia kwamba serikali itapunguza posho. Lakini
hatukuwaambiwa posho hizo zitapungua kutoka kiasi gani hadi kiasi gani. Na wala
hatukuambiwa kwamba mwaka uliopita serikali ilitumia kiasi gani cha fedha kama
posho na sasa inatarajia kutumia kiasi gani. Bahati nzuri au mbaya wakati
bajeti inaandaliwa hoja ya posho ilikuwa haijaibuliwa; vinginevyo mtu makini
angejipanga jinsi ya kuwasilisha hoja hii ndani ya bajeti. Vinginevyo ni kusoma
mambo mengi kwenye hotuba ya bajeti yasiyokuwa ya msingi na kuyaacha ya msingi.
Mheshimiwa Waziri wa
Fedha, alisoma hotuba ya bajeti masaa mawili na dakika kumi na tano. Ni kazi nzito na ya kuchosha
ukizingatia na asubuhi yake alikuwa amesoma hotuba nyingine ndefu ya hali ya
uchumi. Lazima tumpongeze kwa kazi hiyo ya kuchosha. Bahati mabaya ni kwamba
alijichosha kwa mambo mengi yasiyokuwa na maana, ambayo watu wangeweza
kujisomea. Baada ya kuvisambaza vitabu vya bajeti, kuna umuhimu gani kuisoma
bajeti nzima? Muhimu ni mchango wa wabunge kwenye bajeti hiyo; na wanaweza
kufanya hivyo baada ya kuisoma na kuielewa yote; hawafanyi hivyo kwa
kuisikiliza ikisomwa na mheshimiwa waziri. Na tumezoa kwamba hotuba hii ya
bajeti na bajeti za wizara moja moja zinawekwa kwenye magazeti yote kama
tangazo ili watu wengi wazisome; ingawa kuna shinikizo la serikali kukataza
matangazo haya ya bajeti kuwekwa kwenye vyombo vya binafsi bado hitaji hili ni
la muhimu sana. Magazeti ya serikali ni machache na usambazaji wake ni mdogo
kulinganisha na magazeti ya makampuni binafsi. Hili likitokea, la kuzuia
matangazo ya bajeti kuwekwa kwenye magazeti ya makampuni ya watu binafsi,
tutaamini kwamba serikali haina nia njema ya kusambaza habari kwa wananchi wake.
Masaa mawili yote aliyoyatumia waziri wa fedha kusoma hotuba ya bajeti
yalipotea tu kwa vitu visivyohusiana na bajeti ya wananchi! Waziri angeweza
kuwasilisha bajeti hiyo kwa dakika kumi na tano tu. Wananchi wanataka kujua
tumezalisha nini mwaka uliopita, tumetumia kiasi gani, tumebakiza kiasi gani?
Na mwaka unaoanza tutazalisha nini, tutatumia kiasi gani na tutabakiza kiasi
gani. Ngonjera nyingine ni mfumo wa kuwasilisha bajeti ambao tumeurithi kutoka
wapi? Bila kubadilisha mfumo huu tutabaki kuwa watu wa porojo na maneno bila
kufikia maendeleo ya kweli.
Inawezekana Mheshimiwa
Zitto Kabwe, alishutuka kuona serikali inasema kupunguza posho wakati bado kuna
mabilioni ya shilingi yametengwa kwa ajili ya posho bila maelezo ya kina kwamba
posho hizi zitatolewa kwa misingi ipi na kwa nani? Labda hili lingeelezwa
vizuri kwenye hotuba ya bajeti, asingeibua hoja hii ya posho ambayo imepandisha
joto ndani ya Bunge na kutishia kuleta mgawanyiko.
Tunataka tusitake hoja
hii ya posho ni kipima joto kwa wabunge
wetu. Tumekuwa tukilalamika kwamba baadhi ya wabunge wetu wanaingia Bungeni
kutafuta posho na wala si kuwawakilisha wananchi waliowatuma; tumekuwa tukisema
kwamba uwakilishi wa kweli ni ule wa mvuvi kumwakilisha mvuvi, mkulima
kumwakilisha mkulima; mfugaji kumwakilisha mfugaji; mwanakijiji kumwakilisha
mwanakijiji mwenzake na mtu wa mjini kuwawakilisha wenzake wa mjini. Kinyume na
hapo ni usanii wa kutafuta posho; tumeliandika hili na kulieleza kwa kina;
wengine walifikiri ni uzushi, ila sasa baada ya mheshimiwa Zitto kuliweka
bayana na yeye kutangaza na kuandika barua kwa Spika akiomba posho zake zifutwe
ukweli umejionyesha wazi.
Wabunge wengi wamekuja
juu na kulalamika, hawataki posho zao ziguswe na hasa wakati huu ambapo ndio
tumetoka kwenye uchaguzi mkuu. Baadhi yao walitumia fedha nyingi kwenye
uchaguzi na wanatafuta njia za kurudisha fedha hizo; kwa hesabu tulizozipata za
Mbunge kuondoka na zaidi ya shilingi 150,000 kwa siku, inatia matumaini kwamba
Mbunge anaweza kufanikiwa kuyalipa madeni yake. Hata Mheshimiwa Augustine
Mrema, ambaye walio wengi tuliamini ni mpambanaji na mtetezi wa wanyonge;
ukiachia mbali harakati zake za miaka ya nyuma, juzi juzi hapa tumeshuhudia
kwenye vyombo vya habari alivyokuwa akiwachachafya watumishi wa Halmashauri za
wilaya juu ya matumizi mabovu ya fedha za umma; naye amesimama kupinga posho
zisifutwe akisema kwamba Zitto alizikuta posho na ataondoka na kuziacha!
Huu ni wakati mzuri wa
wananchi kuwapima wabunge wao. Je wanaguswa na posho zao tu au wanaguswa na
mambo mengine ndani ya bajeti tuliyosomewa juzi. Wataipitisha bajeti kwa
kushangilia au watahoji vipengele vyote?;
Tumeambiwa kwenye bajeti
iliyosomwa juzi kwamba serikali itapunguza safari za viongozi nje na ndani ya
nchi. Je mwaka jana safari hizi
zilikuwa ni ngapi na zilitumia fedha kiasi gani? Na mwaka huu zitapungua kutoka
ngapi hadi ngapi? Tumesikia kwamba serikali itapunguza semina, warsha na
makongamano; ni maneno kama yale ya bajeti ya mwaka jana. Je mwaka jana semina
zilikuwa ni ngapi na zilitumia fedha kiasi gani? Tumeambiwa kwamba serikali
itaacha kununua magari ya kifahari; je mwaka jana ilinunua mangapi na mwaka huu
inatarajia kununua mangapi?
Hoja inayojengwa hapa ni
je wabunge wetu watakuja juu kuhoji baadhi ya mambo yaliyokwenda tenge kwenye
bajeti kama walivyokuja juu na kuonyesha mshikamano wakati wa kutetea posho
zao? Wabunge watapiga kelele bei ya sukari ishuke? Watapiga kelele bei ya
mafuta ishuke? Watapiga kelele ili mwananchi wa kawaida kijijini auze kahawa
zake, korosho zake na pamba yake kwa bei nzuri na kuiweka fedha yake mfukoni?
Jinsi wabunge wanavyopiga kelele kuiweka posho yao mfukoni ndivyo wananchi
wanavyopiga kelele kuuza mazao yao kwa faida na kushuka kwa gharama ya bidhaa
muhimu katika matumizi ya siku kwa siku kama vile mafuta ya taa, sukari, mchele
na usafiri. Ndio maana nikasema hoja hii ya posho ni kipima joto. Ndio wakati
wa kutambua wabunge wanaowawakilisha wananchi na wabunge wanaoyawakilisha
matumbo yao. Na dawa yao ni moja tu! Ni kuwanyima kura kwenye uchaguzi mkuu wa
2015.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment